1. Wajumbe wengi(asilimia 81) kati ya wale
201 walioteuliwa na Rais Kikwete ni viongozi na wanachama waandamizi wa CCM.
Tukavumilia na kukaa kimya.
2. Kwenye kutengeneza kanuni za Bunge Maalum
CCM walipambana kila kukicha kupitisha kanuni zitakazotetea MFUMO wao -
tukatumia nguvu kubwa kuwazuia lakini tulifanikiwa kidogo sana -...Tukakaa
kimya.
3. Katika kuanza kuzitumia kanuni, Mwenyekiti wa Bunge Maalum kwa
shinikizo la wazi la CCM alikiuka kanuni bila aibu, ikapangwa kuwa hotuba ya
Jaji Warioba ianze ili aje Rais wa nchi baadaye, jambo hili ni kinyume kabisa na
kanuni. Suala hili likaleta mvutano mkubwa sana tukaamua KUJIFANYA HATUTAKI
MAKUU, tukaliacha - Tukakaa kimya.
4. Jambo hili lilipokubalika, CCM
wakamshinikiza Mwenyekiti wa Bunge Maalum amnyime jaji Warioba muda. Mwenyekiti
akatangaza kuwa atampa dkk 60 tu, tukakataa, siku jaji Warioba alipokuja
kuwasilisha tukalikwamisha ili aongezewe muda, baada ya mashauriano ya baadaye,
ikakubaliwa apewe saa nne.
5. Baada ya uwasilishaji wa Rasimu wa Warioba,
Rais Kikwete alikuja na kuivunjavunja na kuweka misimamo ya chama chake dhidi ya
maoni ya wananchi yaliyomo kwenye rasimu ya katiba. Tukamsikiliza Rais kwa
nidhamu kubwa na kuvumilia hatua yake ya juu ya kupinga hadharani rasimu ya
katiba ambayo imetokana na maoni ya wananchi ambayo ameyakusanya baada ya
kuiunda tume ya Warioba. Tukakaa kimya.
6. Ikumbukwe kuwa hata kwenye
kuchagua Mwenyekiti wa Bunge la Katiba CCM walipigania nafasi hiyo na kushinda.
Nafasi ya Makamu Mwenyekiti pia waliipigania wakachukua. Tukakaa
Kimya.
7. Jana Mwenyekiti wa Bunge la Katiba aliteua kamati za uandishi
na kamati ya Kanuni. Kamati zote hizi mbili, kila moja, mwenyekiti na makamu
mwenyekiti walioteuliwa wote ni viongozi wa CCM, Tukakaa kimya. Wenyeviti wa
kamati hizi wote wanaingia kwenye kamati ya uongozi ya Bunge Maalum. Tumekaa
kimya.
8. Juzi CCM walipokutana kwenye kikao cha wajumbe wa CCM waliamua
kuteka kamat zote 12 zitakazojadili sura za Rasimu ya Katiba.
Jana
tulipokwenda kwenye uchaguzi wa viongozi wa kamati, wateuliwa wote wa CCM
walishinda akiwemo HAMAD RASHID na Dr. Francis Michael ambao pia wamejivika joho
la kusimamia maoni ya wananchi huku ukweli halisi ni kuwa wapo ili kusmamia
matwaka na Maslahi ya CCM.
Ikumbukwe kuwa, wenyeviti wa kamati hizi 12,
wote ni wajumbe wa kamati ya Uongozi ambayo ndiyo dira itakayoongoza kila jambo
linaloletwa katika bunge Maalum.
9. Leo, Mwenyekiti wa Bunge Maalum
ameteua wajumbe watano ili kuingia kwenye kamati ya uongozi kama kanuni
zinavyoelekeza. Jambo la ajabu ni kuwa, kati ya nafasi hizo 5, nafasi 4 zote
amewateua wajumbe ambao ni viongozi waandamizi wa CCM akiwemo mwakilishi wa
walemavu Amon Mpanju.
Mjumbe mmoja wa walemavu amesimama na kupinga
uteuzi wa mwakilishi wao palepale.
Prof Lipumba amesimama na kukataa
uteuzi huo, ameeleza si wa haki hata kidogo. Ameeleza alijiunga na siasa ili
kutafuta haki za wananchi na umoja wa kitaifa na si vinginevyo. Lipumba amesema
kuwa hawezi kutumika kama mhuri.
Kama CCM wana nia njema wasingehodhi
nafasi zote katika mchakato wa katiba.
10. Hoja kubwa ya CCM kuchukua
nafasi zote za uongozi wa bunge maalum ni "eti" wao ni wengi. Hoja ya ajabu sana
hii! Kama hoja ni nani au kundi gani lina idadi gani basi nafasi hizi
zingegawanwa kwa mantiki hiyo. Vyama visivyo CCM peke yake vina wajumbe zaidi ya
130, kama hoja ni wingi vyama hivi peke yake vingepewa nafasi 5 kwenye kamati ya
uongozi. Badala yake tumepewa nafasi 1 tu a Prof. Lipumba ambayo ameikataa kwa
sababu si nafasi ya haki.
11. Tuko hapa kwenye Bunge Maalum kutafuta
katiba ya wananchi wa Tanzania, hatuko hapa kutafuta katiba ya chama chenye
wabunge wengi kuliko vyama vingine kama anavyosema Mwenyekiti wa Bunge Maalum
Samwel Sitta. Ili tupate katiba ya watanzania wote lazima chama chenye wabunge
wengi kitambue wingi wao, na kiutumie wingi huo kuunganisha makundi muhimu yenye
idadi ndogo ili kutafuta katiba yenye maridhiano na inayokubalika na makundi
madogo na makubwa ndani na nje ya Bunge Maalum.
12. Michakato mingi ya
kutafuta katiba mpya inaonesha kuwa vyama vilivyoko madarakani huwa ni chanzo
kikubwa cha kuvuruga mchakato wa katiba. Na sbb kubwa ya kuvuruga mchakato
husika huwa ni chama dola kutaka kuhodhi na kulinda maslahi yake dhidi ya
maslahi ya wananchi. Pamoja na uzoefu huu, bado CCM hawataki kujifunza, wanataka
kushinda bila kujali wananchi watapata nini.
ANGALIZO;
Masuala
hayo 12 yanaonesha wazi kuwa CCM hawana kabisa nia ya kuona nchi inapata katiba
inayokidhi matakwa ya wananchi. CCM wanataka kuchukua kila kitu, wanataka kupata
kila kitu, wanataka kuhodhi kila kitu, hawajali wananchi wamesema nini.
Wasidhanie kuwa tulioko hapa Dodoma ni watoto wadogo, tutachukua hatua,
hatua stahili kwa wakati muafaka. Idadi yao na wingi wao havina maana katika na
juu ya maslahi ya taifa na matakwa na maoni ya wananchi.
MWISHO;
CCM
watambue kuwa TUTAKULA nao sahani moja, hatutatumiwa kuwa mhuri wa Maslahi ya
chama chao na kwamba katiba mpya siyo hisani yao, ni matakwa halisi ya
watanzania na serikali na chama kinachoongoza dola lazima kitii maoni ya
wananchi na matakwa ya misingi ya kdemokrasia, na kwa sababu mchakato huu
umeshaanza lazima ufike mwisho. "Jini likitoka kwenye chupa, halirudi"(hadithi
za Alfu Lela Ulela).
No comments:
Post a Comment