Monday, 4 February 2013
Wafalme wa Kibongo au wa kiafrika !
Uteuzi wa viongozi waliokataliwa na wapiga katika uchaguzi uliopita wa mchujo, bilashaka uliwaacha wengi wakijiuliza, taifa letu limebadirika kuwa mpokezano wa Kifalme nini? Sote tulishuhudia ukiukaji wa sheria kama ilivyofafanuliwa na Katiba yetu mpya. Katiba imeeleza wazi kuwa viongozi wa vyama vya kisiasa wanahitajika kuteua wawakilishi katika jamii ndogo zilizotengwa, walemavu( kama vile waliopooza, bubu, vipofu, watoto mayatima, akili punguani n.k) na Wakenya maskini hohehahe waliosahauliwa na serikali. Wananchi wa Kibera na Mathare wanahitaji mwakilishi wao wa kutetea wapate vyoo, maji safi, usalama na zahanati. Badala yake, viongozi wa vyama hivi vya kisiasa hawakufanya hivyo. Walivunja sheria bila kujali na kuwapuuza Wakenya hawa. Katiba inafafanua makundi ya watu wanaopaswa kuteuliwa. Raila Odinga, Uhuru Kenyatta, na Mudavadi hawaoni hayo. Kukosa vyoo Kibera, kwa miaka hamsini, nani ajuaye hivyo zaidi ya mkaazi wa mtaa huo?
Baada ya Wafrika kuchoshwa na kupinga himaya za wakoloni, Usultani na Kifalme kuanzia miaka ya 1950 hadi mwishoni wa miaka ya 1960, Afrika imeshuhudia kwa muda mfumo mpya wa makundi ya jamaa mmoja kushikilia nyadhifa serikalini bilahata kuwa na haya nyusoni. Sote tunayakumbuka yaliyotokea katika mataifa ya Kiarabu kule Mashariki ya Kati na pia Kaskazini na Magharibi mwa Afrika. Katika mfumo wa upepo mpya wa mageuzi katika mataifa hayo, waliokuwa marais wa nchi za kama vile Libya, Misri, Tunisia na sasa hivi Syria, walitumia nchi zao kama maliyao binafsi. Mataifa mengine kama vile Uganda, Zimbabwe, Botswana, na Swaziland wanaendeleza sera kama hizo tu.
Katika mataifa hayo na mengine mengi katika Bara la Afrika, ikiwemo Taifa letu la Kenya, viongozi hao wanawatunukia watoto wao, wake zao, ndugu, shemeji, na jamaa zao madaraka makubwa serikali. Wengi wa viongozi hawa, wanapokaribia kustaafu au kung'atuka uongozini, wanaanza kutengenezea jamaa zao mazingira ya kushika hatamu huku wakiwaacha wananchi wa nchi zao kupandwa na mori. Kwa mfano, Rais Joseph kabila wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo(DRC) alichukuwa hatamu za urais baada ya babake kuuliwa na walinzi wake hapo 2001. Rais Faure Gnassingbe wa Togo naye aliridhi urais wa nchi hiyo baada ya babake Gnassingbe Eyadema kuitawala kwa karibu miaka arubaini.
Nchi ya Botswana hakuwaachwa nyuma katika mtindo huo. Rais Luteni Jenerali Ian Khama alinyakuwa madaraka kutoka kwa baba yake mzazi, Sir Seretse Khama, baada ya kuingoza nchi hio tangu mwaka wa 1966 ilipopata uhuru. Baada ya Muammar Gadaffi kuitawala nchi ya Libya kwa miaka 42, alimtayarisha mwanawe Saif Al-Islam Gadaffi kuchukua madaraka ya nchi hio. Katika serikali ya Gadaffi, zaidi ya nusu ya mawaziri wake na viongozi wa juu taasisi za kiusalama, zilishikiliwa na jamaa na familia yake. Katika nchi ya jirani ya Uganda, mwanawe Rais Yoweli Museveni, Luteni Kanali Muhoozi Kainerugaba Museveni, ndiye kamanda wa kikosi maalum kinachomlinda yeye.
Bila shaka, kasheshe za viongozi zilizofuata baada ya uteuzi ya uchaguzi wa mchujo uliofanywa nchini zinaonyesha waziwazi mtindo huo huo wa kuwateua jamaa na marafiki zao mamlakani. Kwa mfano, Askofu Margaret Wanjiru tayri amemtayarisha mwanawe Steve Kariuki kung'ang'ania ubunge katika mchuano wa eneo jipya la Mathare. Wakati Ramadhani Kajembe anawania kuwa Senata wa kisiwani Mombasa, mwanawe Seif Kajembe anawania kiti cha bunge cha eneo la Jomvu. Mwanawe huyu alimshinda shemejiye Badi Twalib Badi katika teuzi ya ODM. Mwenyekiti wa ODM Bw Henry Kosgei, amemuweka mwanawe Alex Kimutai Kigen kutafuta cheo katika eneo la Umgwen, wakati babake naye anatafuta Useneta. Wote wataka yote wapate yote.
Yasitoshe hayo. Wakati mkongwe Ole Ntimama amekatalia pale pale kung'eng'ania kiti cha Ubunge cha Narok, bintiye mpenda ubishi, Lydia Masikonte, naye ameteuliwa kuwawakilisha wanawake wa eneo hilo. Naye Julius Ole Sunkuli hakuwa na haya alipomtarajia mkewe awawanie ubunge wa Kilgoria, ingawa alibwagwa chini chini mchana wa jua kali. "Mkewe" Mzee Mwai Kibaki, Bi Mary Wambui, sasa atawania kiti cha ubunge kilichowachwa wazi na "Mumewe" mstaafu. Ingawa Mzee Kibaki mkimya kuhusu uhusiano wake na mwanamke huyu, ambaye inasemekana ana watoto wengine wanne, ingawa umma wanajua tu yule mmoja wa kike, malialionayo Bi Wambui yafumbuwa vitendawili hivyo! Kwani haya yote yakatoka wapi? Mbona anawaficha watoto hao wengine? Mbona uhusiano wao na baba Jimi ni siri siri? Na Mzee mkimya tu.
Kwa upande mwingine katika Bonde la Ufa, bintiye aliyekuwa bunge wa Molo, Laikipia Magharibi na Nakuru Kaskazini, Bi Susan Kihika, sasa ameteuliwa kuwa mwakilishi wa wanawake katika eneo lao. Wengine ni Alice Mbodze Maitha, mkewe wa aliyekuwa waziri marehemu Karisa Maitha. Dadake Tobiko, Ann Tobiko, atawakilisha wanawake wa Kajiado. "Kamwana" Uhuru Kenyatta, naye anamshinikiza shemejiye Beth Mugo, awanie uongozi hata baada ya yeye kustaafu katika ulingo wa siasa. Abdulswamad Hariff Nassir, Mwanawe "mpende msipende" nyinyi wakati wa KANU, atawania ubunge huko Mvita. Na mwishowe, dadake Raila, Ruth Adhiambo Odinga na nduguye, Dkt Oburu Odinga, shemejiye Washington Jakoyo Midiwo, hata baada ya kukataliwa na wapiga kura, waliteuliwa wapate kujenga himaya za Kifalme katika familia ya Odinga. Katika nyumba yao, wanabalozi wawili, Waziri Mkuu, wabunge na waziri. Wakenya ni wapunbavu kweli?
Katiba yetu mpya inaposisitiza uteuzi wa watu kutoka jamii ndogondogo, wanawake, walemavu na vijana waliotengwa tangu uhuru katika serikali, inaelewa kwamba viongozi walishindwa kabisa kutatua matatizo yao. Jamii hizi ndogo ni kama vile Warendille, Gabra, Daasanach, Hamar Koke, Karo, Nyagatom, Mursi, Surma, Elmoro, na zinginezo. Viongozi wetu hawajajifunza na matukio yaliowapata Marais wa Libya, Misri, Tunisia na kwingineko. Wanaendelea kutumia raslimali zetu kama milki zao, au mashamba yao. Wanapowateua ndugu na dada zao, wake na watoto wao, jamaa na marafiki zao, wazichukue vyeo vya walevu, wanyonge na maskini wa kutupwa, bila kupesa mboni za macho yao, wanauchokara mzinga wa nyuki. Wakenya ni watu wavumilivu. Lakini tamaa hizi zao, ubinafsi huu wao, uhasama wao, umefika kilele. Tunafahamu kinachowafanya wafanye hivyo: wapatwe kuwasilishwa na watu kutoka jamaa zao iwapo hawatachaguliwa Machi 4. Wanahitajika kulindwa. Mali, kashfa, na uporaji wao wa mali ya umma wahitaji zaidi ya marafiki: ila tu wake zao, watoto wao, ndugu na dada zao. Mfumo wa tawala za kifalme....Mmmmm! La hasha! Wagonje matokeo yajayo, watapatwa na mshtuko wa roho!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment