Sunday 30 June 2013

MUKHTASARI WA ALICHOKIZUNGUMZA MAALIM SEIF LEO KITOPE HUKO ZANZIBAR JIMBONI KWA MHESHIMIWA SEIF IDDI





Wanaoweza kusoma alama za nyakati tumeona nguvu ya vijana Brazil , Turkey na Egypt hivi karibuni ila na Vijana wa Zanzibar hawako nyuma kudai mabadiliko leo vijana wa Zanzibar zaidi ya Miatano wamejitoa CCM na Kujiunga na CUF Kuamini chama hichi ndio pekee kitakachoweza kuirudisha hadhi ya Zanzibar.

Maalim Seif leo alicharuka huko Kitope maana kazungumza maneno mazito. Anasema baadhi ya wakubwa hawakutaka mkutano ufanyike lakini akampigia simu Balozi Seif Ali Iddi na kumwambia mkutano utafanyika iwe isiwe. Na kama mikono yao bado ina damu basi yeye atakuwa wa mwanzo kuuliwa kisha wanachama wake.

Pia akawashambulia mkuu wa mkoa na wilaya kwa kufanya ukereketwa na kukataa maridhiano. Maalim pia hakumuacha kiongozi mmoja wa juu kabisa mstaafu wa Jamhuri ya Muungano aliyemtaja kuwa anaharibu siasa za Zanzibar kwa kutopenda maridhiano.



Lakini Maalim kamcharukia pia Profesa Issa Shivji na misimamo yake juu ya muungano na kumshangaa alivyobadilika hivi karibuni kwa kukataa hoja ya MAMLAKA KAMILI na kuamua kuwatisha watu kwa kutaja mifano ya Yugoslavia na Soviet Union. Akauliza mbona hawatoi mifano kama ule wa Singapore kujitoa kwenye Shirikisho la Malaysia kwa usalama na kwa kubaki na ujirani mwema.

Maalim Seif akamnukuu Nyerere kwamba alisema siku yoyote iwapo Wazanzibari wataamua kwa khiyari zao wenyewe kuwa Muungano hauna maslahi kwao na wakaamua kujiondoa hatowapiga mabomu. Sasa Maalim anahoji mbona hawainukuu kauli hiyo?

Maalim Seif hakuacha kumsifu Mzee Mark Bomani ambaye ni mwanasheria anaeujua hasa muungano kama ilivyo kwa Mzee Moyo hasa pale Bomani alipopendekeza kwamba kwanza inapasa Wazanzibari waulizwe wanautaka muungano au la, na kama wanautaka basi mfumo gani? Maalim akauliza kwani muungano lazima uwepo hata iwe kunatumiwa vitisho kuulazimisha?

Na Maalim akaahidi yeye na wenziwe wakiwemo Kamati ya Maridhiano waliojitolea katika kutaka Mamlaka Kamili hawatasimama hadi kupatikane mamlaka kamili ya Zanzibar kitaifa na kimataifa.

Akasema Wazanzibari hawatoikubali rasimu iwapo hairjeshi kwenye Mamlaka ya Zanzibar mambo yafuatayo:

1. Mipaka inayotambulika ya Zanzibar na Tanganyika;

2. Mambo ya Nje;

3. Uraia na Uhamiaji; na

4. Sarafu na Benki Kuu.

Mwisho, Maalim Seif alimalizia kusema kuwa Zanzibar inaweza kupiga hatua kubwa za maendeleo na kubadilisha maisha ya watu wake kwa haraka iwapo itapata UONGOZI MAKINI WENYE DIRA.

Akasema dira yake yeye ni kuiona Zanzibar inakuwa "The London of East and Central Africa and the Indian Ocean" kwa maana ya kuwa kituo kikuu cha uchumi wa huduma za kifedha, mabenki na uchumi katika ukanda huu. Na akasema kufikia huko ni lazima tuwe na mamlaka kamili ili tuweze kusarifu sera zetu za ndani na nje kulingana na mahitaji yetu. Alitumia mifano ya Seychelles, Singapore na Qatar kama kielelezo cha maendeleo ya kiuchumi tunayoyataka kwa ajili ya Zanzibar mpya.

Katika mkutano huo wanachama wapya 435 wengi wao wakiwa vijana walijiunga na CUF wakiwemo waliorejesha kadi za CCM mmojawapo akiwa ni nguzo ya CCM jimbo la Kitope kutoka Shehia ya Mgambo anayeitwa Mzee Mabati.

No comments: