Thursday 12 June 2014

Mikoa ya kanda ya ziwa wao ni Ukawa

Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ukiwa unaendelea na ziara zake mikoani, viongozi wa Chadema kutoka Kanda ya Ziwa wanasema wanaunga mkono umoja huo unaotetea maoni ya wananchi.Ukawa wanapinga Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba wakidai kuwa umetekwa na CCM ambao wamedai kuwa wamekuwa wakitumia wingi wao ndani ya Bunge kuchakachua maoni yaliyotolewa na wananchi.Viongozi wakuu wa Ukawa ambao wanazunguka mikoani wanatoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi ambao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa.Wenyeviti Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Ziwa kutoka mikoa ya Mwanza, Geita, Simuyu na Kagera wanasema wao wanaunga mkono Ukawa na kwamba hawatingishwi na propaganda zinazotumiwa na Chama Cha Mapinduzi CCM kutaka kuwanyamazisha.Kauli za viongozi wa Kanda ya Ziwa.
Kauli za viongozi hao wa Chadema wa mikoa ya Kanda ya Ziwa zinakuja siku chache baada ya kuenea kwa taarifa kwamba baadhi ya wanachama wa Chadema Kanda ya Ziwa, wanapinga kitendo cha viongozi wa juu wa chama hicho kususia Bunge Maalumu la Katiba.Wakizungumza mkoani hapa Wenyeviti wa Chadema kutoka Geita, Simiyu na Kagera wanasema uamuzi wa kutetea maoni ya wananchi ili kuhakikisha wanapata Katiba bora, upo sahihi na kwamba wao kutoka Kanda ya Ziwa wanaunga mkono harakati za Ukawa ili wanachi wapate Katiba wanayoitaka.
Kwa mujibuwa viongozi hao kitendo kinachotaka kufanywa na CCM cha kupora maoni ya wananchi ya wananchi siyo cha kistaarabu na kinaharibu Mchakato mzima wa Mabadiliko ya Katiba ulikwishaendelea vizuri.Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita Alphonce Mawazo anasema wametambua mbinu zinazotumiwa na CCM kuwahonga watu fedha ili wadhoofishe nguvu za Ukawa ili wasiendelee na vuguvugu la kudai Katiba ya Wananchi hivyo wamejipanga kukabilina na watu hao.Mawazo anasema viongozi wa Chadema Kanda ya Ziwa wapo pamoja na Ukawa na kwamba hakuna mtu anayepingana na Umoja huo, kwani una masilahi kwa Watanzania wote kwa jumla.“Naomba niwaambie wanachama na wanaukawa kwa jumla taarifa za Chadema Kanda ya Ziwa kupinga Ukawa ni propaganda zinazotengezezwa na CCM” anasema Mawazo na kuongeza:“Tumechoka kuvumilia mchezo huo sasa tunajipanga kuhakikisha tunawashughulikia watu wote wanaotumiwa kutaka kuvuruga Ukawa. Tunajua kuna watu wameanza kuogopa ndiyo maana wanatumia mbinu chafu kutodhoofisha Ukawa hivyo hatutakubali,” anasema. Anasema kila Mtanzania ana haki ya kudai haki ambayo itakuwa na masilahi kwa taifa zima, na siyo masilahi ya chama fulani, au watu wenye mrengo fulani.
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita anasema kamwe hawawezi kupinga Ukawa na kwamba hizo ni mbinu za CCM kutaka kupunguza makali ya Umoja huo.“Hakuna mtu hata mmoja ambaye ni mwanachama wa Chadema kutoka Kanda ya Ziwa ambaye anapinga Ukawa. Naomba Watanzania watambue kwamba Chadema na Ukawa ni nguvu moja na tutaendelea kudai Katiba ya wananchi hadi itakapo patikana,” anasema Lwakatare.Lwakatare alihoji mantiki ya wao kupingana na umoja huo ambao unaoungwa mkono na viongozi wakuu wa chama hicho ngazi ya taifa.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Simuyu, Mshuda Wilson anasema wao kama viongozi wa Chadema kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa wamesikitishwa na taarifa za wao kupinga Ukawa na kwamba harakati zao za kudai Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi zitaendelea.Anasema wanatambua kwamba wana maadui wengi ambao wanapinga harakati zao, lakini wamejipanga kukabiliana nao kwa njia zote ili kuhakikisha Katiba ya wananchi inapatikana.“Tunajua kwamba tuna maadui wengi na tumejipanga kukabiliana nao wote na kwamba tupo pamoja na Ukawa na tutaendelea kudai Katiba ya wananchi hadi itakapopatikana,” anasema.

No comments: