ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema Dk. Willibrod Slaa ametekwa na mke wake Josephine Mushumbusi na haiwezekani kumtoa. Gwajima amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wandishi wa habari katika Ukumbi wa Landmark Hotel, Ubungo akijibu tuhuma zilizotolewa na Dk. Slaa Septemba 1 mwaka huu.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari Dk. Slaa alimshambulia Gwajima kwamba, ndiye aliyekuwa mshenga na aliyefanya kazi kubwa ya kumuunganisha mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa na viongozi wakuu wa chama hicho.
Dk. Slaa alienda mbali zaidi kwa kusema, mshenga huyo (Gwajima) amabye ni rafiki wa karibu na Lowassa alimfuata na kumwambia “maaskofu 30 kati ya 34 wamehongwa ili kumkubali Lowassa,” na kuongeza;
“Aliona ni sifa kwa viongozi wa dini tena maaskofu kuhongwa. Kama ni kweli maaskofu hao watubu.”
Akijibu tuhuma hizo Gwajima amekiri kuwa na urafiki wa karibu na Lowassa kabla na baada ya kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hata hivyo amesema Dk. Slaa pamoja na kumshambulia Lowassa lakini ameondoka Chadema kutokana na shinikizo lililofanywa na mkewe Mushumbusi ambaye ‘ndiye anayemtawala.’
“Nimeamua kuitisha mkutano huu kwa makusudi ili kujibu tuhuma nzito alizitoa Slaa juu ya wachungaji maana tukikaa kimya ni hatari kwa waumini wetu kwa kuwa kitendo alichofanya ni cha uchonganishi kwa waumini wetu” amesema na kuongeza;
“Slaa ni muongo na hakuna ukweli wa alichokisema. Slaa ni rafiki yangu lakini amenikosea sana kwa sasa sio rafiki tena bali ni rafiki mkosefu.”
Gwajima amesema Dk. Slaa hakukosea kumwita mshenga na kwamba, limemsaidia vitu vingi ikiwemo kumuunganisha yeye na Lowassa pamoja na kumtafutia walinzi na mpishi nyumbani kwake.
“Kweli mimi ni mshenga maana namjua vizuri sana Slaa kuanzia nyendo zake, chumbani kwake hadi jikoni kwake maana mshenga hutumiwa na mtu asiyejua kitu,” amesema.
“Mimi ni kweli ndiye nilieshiriki kumleta Lowassa ndani ya Chadema tena baada ya yeye kuniomba niwaunganishe naye. Slaa alishiriki vikao vyote hadi dakika za mwisho hadi tarehe 26 mwezi wa saba mwaka huu ambapo Chadema ilimkaribisha rasmi Lowassa na yeye akiwepo”.
Amesema, Slaa alishiriki katika shughuli zote za kumpokea Lowassa Chadema lakini hali ilibadilika baada ya kurudi nyumbani kwake ambapo alikumbana na matatizo makubwa kutoka kwa mke wake ndipo alianza kubadili msimamo wake.
Akielezea hali ilivyokuwa nyumbani kwa Slaa Julai 26 mwaka huu mlinzi wa Slaa aliyetambulika kwa jina moja la Kornel amesema, saa 6:30 baada ya kurudi nyumbani katibu huyo alikumbana na vurugu za Mushumbusi na kusababisha alale ndani ya gari.
“Baba (Slaa) aliporudi alikuta mlango umeshafungwa na tulipojaribu kugomga mlango haukufunguliwa, baada ya kulazimisha ndipo alipofungua huku akiwa na begi la nguo mkononi na kuanza kumfukuza huku akimwambia rudi ulikotoka,” na kuongeza;
“Baada ya mimi kumbembeleza kwa muda mrefu ilipofika saa 7 usiku ndipo aliamua kumfungulia mlango lakini ilikuwa kwa shariti la kutorudi Chadema na kuwa endapo Lowassa atapokelewa basi yeye ajiuzulu.”
Hata hivyo, Gwajima amesema, baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa walinzi, aliamua kukutana na mke wa Slaa na kuzungumza naye kwa lengo la kumwacha aendelee na kazi za ukatibu mkuu.
“Mimi nilishajiandaa kuwa first lady na nilishaandaa biashara zangu huko nje za nchi hivyo siwezi kubadili msimamo wangu.
“Mke wake Slaa ana viashiria vyote vya matendo ya kishetani. Ni dhahiri kuwa yawezekana Slaa anayofanya yote sio akili zake, anamuendesha vibaya. Sasa kwa mfano angeteuliwa kuingia Ikulu, ingekuwaje nchi hii?” amehoji Gwajima.
Wakati Dk Slaa anatangaza kustaafu siasa Septemba Mosi, alimwita kiongozi huyo wa Kiroho kuwa ni mshenga wa Edward Lowassa kwa Chadema na kusema kuwa askofu huyo alimwambia kuwa wapo maaskofu 30 wa Katoliki wamehongwa na Edward Lowassa.
Licha ya kukanusha tuhuma hizo, Akofu Gwajima amesema kuwa kuna watu wanawatumia Dk Slaa na mchumba wake, Josephine, na kuwaonya waache kutumika.
Pia Askofu Gwajima ametoa tuhuma kwa Usalama wa Taifa kuwa wanatumika pamoja na Dk Slaa.
“Mimi najua wapo Usalama wa Taifa ambao wanamlinda Dk Slaa lakini nawaomba sana Usalama wa Taifa walinde nchi ikae kwa amani, wasijiingize kwenye siasa au kulinda kikundi flani’’ alisisitiza Gwajima.
Aidha askofu huyo amesema kuwa kama Dk Slaa atajitokeza kumjibu kwenye vyombo vya habari, na yeye atajitokeza kuelezea mambo aliyoyafanya Dk Slaa Afrika ya Kusini akiwa na vijana wa Usalama wa Taifa siku chache kabla ya kutangaza kuachana na siasa.
Kiongozi huyo wa Kiroho amewataka wananchi waangalie ni mtu yupi anayefaa na wasije wakagawanywa na harakati zinazoendelea.
No comments:
Post a Comment