Monday 16 November 2015

NAFASI YA UMA KAMU WA KWAZA, YA RAIS ZANZIBAR YA ZUA BALAA CCM



Na Jabir Idrissa, Zanzibar

WAKATI wananchi hawajui hasa kinachojadiliwa kwenye vikao vya viongozi wakubwa waki wemo wastaafu Zanzibar, kuna fununu kuwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuna mvutano wa nani atashika wadhifa wa makamu wa kwanza wa rais wa kushiriki Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoundwa na Maalim Seif mara akishatangazwa mshindi wa uchaguzi uliokwisha.

Taarifa kutoka ndani ya serikali, chama hicho zimesema kwamba inaonekana jina la Balozi Seif Ali Iddi ni kama halipendezi kwa pande zote mbili – upande wa chama alicho cha CCM, wanamlaumu kauwa chama kwa mipasho yake na upande wa Maalim Seif ambaye yumo katika kupigania haki yake ya kuongoza Zanzibar kwa kuwa ametoa takwimu zilizothibitishwa ndani ya Tume ya Uchaguzi kuwa zimempa ushindi wa urais kufuatia kura zilizopigwa Oktoba 25, mwaka huu.

Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), amegombea wadhifa huo mara ya tano mfululizo, safari hii akiwa amefanikiwa kukusanya ushahidi wa wazi kuwa amechaguliwa na wananchi kwa zaidi ya asilimia 53.

Gazeti hili limefahamishwa na vyanzo vyake kwamba CCM baada ya kusalimu amri kuhusu kudai kuwa kimehujumiwa lakini kikipaisha malalamiko yake kinyume na utaratibu wa kisheria, viongozi wake wanahangaika kupata mtu atakayeshika umakamu wa kwanza, ule ambao Maalim Seif amemaliza kuutumikia kwa miaka mitano hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, ambayo mabadiliko yake ya mwaka 2010, ndiyo yaliyozaa utaratibu wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ikiongozwa na Rais na kusaidiwa na makamu wawili, mmoja kutoka chama kinachoibuka cha pili katika matokeo ya uchaguzi, safari hii itahitajika CCM ndio wateue makamu wa kwanza.

Katiba ya Zanzibar, Ibara ya 39(1), inasema “Kutakuwa na makamu wawili wa rais ambao watajulikana kama makamu wa kwanza wa rais na makamu wapili wa rais. Kifungu cha 3 inaelezwa, “Makamu wa Kwanza wa Rais atatakiwa awe na sifa za kumwezesha kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na atateuliwa na Rais baada ya kushauriana na chama kilichotokea nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya uchaguzi wa rais.”

Kama Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ambayo Mwenyekiti wake Jecha Salim Jecha, alitoa taarifa Oktoba 28 ya kufuta uchaguzi mzima, itarudi kazini na kukamilisha kazi ya kutangaza matokeo ya kura za urais za majimbo 23 yaliyobakia, 18 yakiweko kisiwani Pemba ambako CUF imepata zaidi ya asilimia 90 ya kura za urais, Maalim Seif atakuwa ametangazwa rasmi mshindi wwa uchaguzi mkuu wa 2015.

Oktoba 26, Maalim Seif aliwaambia waandishi wa habari kuwa alikuwa anaelekea kupata kura zinazofikia asilimia 52.87 dhidi ya asilimia 47.13 za Dk. Shein na kutaka Tume isicheleweshe utangazaji wa matokeo huku akimsihi rais Dk. Shein akubali kama ambavyo yeye alikubali kushindwa 2010 na kushiriki kuundwa serikali.

Vyanzo vya taarifa vimesema kwamba yapo majina yanayotajwa katika kutafuta mmoja atakayependekezwa kwa Maalim Seif, lakini jina la Balozi Seif halitajwi kuwa miongoni mwake hayo.

Kwa sasa gazeti hili linamtaja Amina Salum Ali, mwanasiasa aliyetumikia serikali kwa miaka mingi akiwa waziri wa fedha, na baadaye kupelekwa kuwa mmoja wa watendaji viongozi katika Ofisi ya Kamisheni ya Afrika, ndani ya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, kama anayefikiriwa kuchukua nafasi hii.

Zipo fikra kwa wanasiasa wawili-watatu wengine, akiwemo Omar Yussuf Mzee, mtaalamu wa uongozi wa fedha aliyeshika uwaziri wa fedha kwa miaka mitano katika serikali iliyomaliza muda wake kwa mujibu wa Katiba baada ya uchaguzi uliofanyika.

Jitihada za kuwapata Balozi Amina ambaye naye ni mtaalamu wa uongozi wa fedha aliyesoma nchini na India, na Omar, ambaye hajapata kugombea uongozi jimboni, baada ya kuwa ofisa mwandamizi serikalini, kupata kauli kama wanajua wanavyotajwa, zimeshindikana.

Mwandishi wa habari hizi ameuliza viongozi kadhaa ndani ya CCM kupata kujua ni kwanini hasa jina la Balozi Seif halitajwi katika hayo yanayofikiriwa wakati amekuwa makamu wa pili, kwa miaka mitano, nafasi iliyompa uzoefu wa kuongoza shughuli za serikali katika Baraza la Wawakilishi, lakini majibu ni “ameonekana hakumsaidia Rais.”

“Huyu amelalamikiwa sana kusema kweli kwa staili yake ya uongozi, isitoshe ameleta usumbufu mkubwa kisiasa kutokana na maneno yake majukwaani yaliyoonekana kama yamejenga chuki kwa wananchi kwa itikadi za kisiasa. Inasikitisha amejidhalilisha na amekiumiza chama wakati wa uchaguzi,” gazeti hili limemnukuu kiongozi mmoja katika makao makuu ya chama Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Lakini alipoulizwa ni kwanini CCM ihangaikie jina la anayeweza kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wakati chama hicho kinaendelea kushinikiza kufanyika kwa uchaguzi mpya, kiongozi huyo alisema, “Kuna habari za jambo la kweli na halali kisheria na habari za jambo lisilo kweli na lisilokubalika kisheria. Haya ni mambo tofauti.”

Hakutaka kufafanua usemi wake, lakini huenda akawa amelenga kuthibitisha kuwa pamoja na viongozi wa juu wa CCM kupigania uchaguzi mpya badala ya ule uliofanyika sambamba na uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wabunge, wanajua hilo halitafanikiwa.

Lakini zipo taarifa nyingine kuwa Balozi Seif Ali Iddi si katika majina ambayo Maalim Seif atakuwa tayari kuyateua kwa nafasi za uwaziri katika serikali atakayoiunda, kwa kuwa kama inavyosemwa na wasaidizi wake, “hayuko tayari kuwa na mawaziri ambao uadilifu wao na heshima (nidhamu) yao vinatiliwa shaka na umma.”

Kauli za Balozi Seif zimekirihisha wengi hasa pale alipoendeleza kumshambulia hadharani makamu mwenzake Maalim Seif na kuwasimana kivitisho masheikh wa Zanzibar, kwa kutoa mfano wa wale wapatao 20 waliokamatwa na kupelekwa Tanzania Bara kufunguliwa mashitaka ya tuhuma za ugaidi.

Katika moja ya mikutano ya kampeni aliyohudhuria, Balozi Seif alisema wazi kuwa kama “watu wa Uamsho wanataka kujaribu, waangalie yaliyowakuta wenzao wanaonyea ndooni, watakiona cha mtema kuni.”

Katika mkutano wa mwisho wa kampeni ambao hata Dk. John Magufuli alihudhuria mjini hapa, Balozi Seif alitamka waziwazi mashambulizi dhidi ya Maalim Seif akimdhihaki kwa majina kadhaa mabaya ikiwemo muongo, mnafiki na mpumbavu. Alisema Maalim Seif amekuwa akidai anaibiwa kura zake kama vile hana mawakala wa kuziangalia.

Leo, moja ya madai ambayo CCM inayataja kama malalamiko yake ya kushinikiza uchaguzi mpya, ni kudai imeibiwa kura zake kisiwani Pemba.

Katika serikali iliyomaliza muda wake Novemba 2, CUF ilipata mgao wa mawaziri saba.

No comments: