Thursday, 26 November 2015
UTAMU WA VINGORA NA UPOFU WA DEMOKRASIA ZANZIBAR
*Hoja ni kutokuwa tayari kuachia madaraka, sio uchaguzi kuharibika
Tarehe 25 Oktoba mwaka huu wazanzibari na watanzania kwa jumla waliingia katika mchakato wa kuwachagua viongozi wao kwa utaratibu wa kidemokrasia na kisheria kama ilivyowekwa kwa mujibu wa matakwa ya katiba zote mbili, ile ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Viongozi waliochaguliwa ni madiwani, wajumbe wa Baraza la wawakilishi kwa upande wa Zanzibar, wabunge, Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Hakuna asiefahamu namna uchaguzi wa Zanzibar unavyoandaliwa na unavyoendeshwa tokea kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa Tanzania. Katika chaguzi zote zilizowahi kufanyika, vitendo vya hila, wizi, njama, mbinu chafu na ubabe ndio misingi mikuu inayotawala katika kuendesha chaguzi hizo. Chama tawala CCM kimekuwa kikishirikiana vyema na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na vyombo vya ulinzi na usalama, polisi, jeshi na vikosi vya SMZ katika kuunda mtandao mzuri na imara wa kuuhujumu uchaguzi kwa malengo ya kuisaidia CCM iendelee kubaki madarakani.
CCM Zanzibar imekuwa ikitumia wakati mwingi na kutumia fedha nyingi kubuni na kuratibu vyema hujuma dhidi ya uchaguzi huru na wa haki kwa kuvitumia vyombo vya dola na Tume ya uchaguzi (ZEC). Hujuma hizi na hila hizi huanzia tokea hatua ya maandalizi ya orodha ya wapiga kura, mchakato wa kampeni, siku ya upigaji kura na hata utangazwaji wa matokeo. Hakuna hatua hata moja katika hizo ambayo haiandaliwi hujuma na mbinu lukuki za wizi kwa malengo ya kuisaidia CCM.
Daftari la wapiga kura la ZEC ni chafu huku uchafu huo ukitumika kama moja ya jitihada zai kuiokoa CCM isishindwe. Tuchukulie mfano mdogo tu wa matokeo ya uhakiki wa daftari la kupigia kura kwa shehia moja tu ya Mwanyanya, jimbo la Mtoni, wilaya ya Magharibi A Unguja uliofanywa na Chama cha CUF katika eneo hilo. Matokeo ya uhakiki wa daftari la shehia hiyo moja yamebaini wapiga kura 455 sio wakaazi halali wa shehia hiyo, wapiga kura 22 ni wafu, wapiga kura 11 ni watoto wadogo walio chini ya umri na wapiga kura 2 waliandikishwa zaidi mara moja. Jumla ya kura za mamluki katika shehia hii moja ambazo zipo katika mahesabu ya CCM ni 510. Hii ni shehia moja tu fanya mahesabu hayo kwa shehia zote za Zanzibar zilizobaki.
Orodha chafu ya wapiga kura huandaliwa kwa utaratibu mrefu wa kuvishirikisha vyombo na taasisi nyingi za serikali ambazo ni Ofisi ya vitambulisho vya mzanzibari mkaazi, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), JWTZ, jeshi la polisi, vikosi vya SMZ na vijana maharamia wa CCM waliopewa mafunzo maalum ya kufanya hujuma kwa kutumia silaha za kienyeji kama mapanga, marungu na nondo maarufu kama mazombi. Ulimwengu mzima ulishuhudia jinsi ZEC ilivyokuwa ikiandaa orodha ya wapiga kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25. ZEC na washirika wake hao kwa kufuata maelekezo ya CCM waliweza kuandaa daftari chafu la wapiga kura. Wapiga kura wasio wakaazi wa maeneo husika, wageni wasio wazanzibari na watoto walio chini ya umri wa kuandikishwa walichukuliwa kwa magari ya JWTZ na kupelekwa katika kambi za JWTZ ikiwemo kambi ya Chukwani ambako walipatiwa vitambulisho vya mzanzibari mkaazi kinyume na sheria ili kukidhi sharti la kuweza kuingizwa katika orodha ya wapiga kura ya ZEC.
Vitendo hivyo haramu vinavyokwenda kinyume na sheria vilifanywa huku vikishuhudiwa na kila mtu kwani magari ya JWTZ yalikuwa yakipita katika ofisi za CCM mchana kweupe na kusomba watu na kuwapeleka katika kambi za jeshi kupatiwa vitambulisho. Ushahidi wa picha na video za uharamia huo zilienezwa mitandaoni na Tume ya Uchaguzi haikutoa kauli yeyote. Wananchi walijaribu kupinga mamluki hawa wasiweze kuandikishwa kama wapiga kura, hata hivyo nguvu kubwa ya vyombo vya dola ya polisi na vikosi vya SMZ ilitumika kulazimisha mamluki hao kuandikishwa kama wapiga kura hata ilipobidi kuwafyatulia watu risasi za moto.
Pamoja na kuingiza maelfu ya wapiga kura batili ndani ya Daftari la wapiga kura, bado CCM haijiamini kushinda uchaguzi. Utaratibu mwengine wa kuwanyima wapiga kura halali fursa ya kuandikishwa kama wapiga kura hufanyika. CCM kwa kutumia viongozi wa serikali za mitaa maarufu kama masheha na ofisi za usajili wa wazanzibari wakaazi kwa pamoja huhakikisha wanawanyima kuwaandkishwa na kuwapatia vitambulisho vya mzanzibari mkaazi wale wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa CUF kwa malengo ya kuweka sawa hesabu zao. Mamlaka mbili hutumika kisheria kuweza kuwapatia watu vitambulisho vya mzanzibari mkaazi. Masheha ambao hutambua na kutoa barua za utanmbuzi kwa wahusika na ofisi za usajili wa wazanzibari ambao hufanya usajili. Sheha huhakikisha anatoa barua za utambuzi kwa idadi maalum tu ya wafuasi wa CUF ambao kwa maagizo ya CCM ndio inayopaswa kuwemo katika orodha ya wapiga kura bila ya kuathiri hesabu za Chama hicho. Idadi hiyo ikifika masheha hukataa kutoa barua zaidi za utambuzi kwa wafuasi wa CUF kwani kufanya hivyo ni kuhatarisha kura za CCM. Baadhi ya wafuasi wa CUF hutumia njia mbali mbali mbadala ili kuona wanafika katika ofisi za vitambulisho ili waweze kusajiliwa. Sheha anapokataa kukupa barua ya utambulisho huwezi kuipata pahala pengine popote.
Baadhi ya watu hufanikiwa kupenya moja kwa moja katika ofis za usajili na kufanikiwa kusajiliwa. Hata hivyo kusajiliwa huko ni jambo moja na kupatiwa kitambulisho ni jambno jengine. Kabla ya watu hao kupatiwa vitambulisho vyao masheha huitwa na kuwakagua picha za wakaazi wa maeneo yao ili kubaini kama wamo wafuasi wa CUF na wakibainika kuwa ni wafuasi wa CUF vitambulisho vyao huzuiwa na wahusika huambiwa njoo siku fulani lakini siku hiyo huo haifiki tena. Kuna mamia ya wafuasi wa CUF ambao waliweza kufika moja kwa moja na kufanikiwa kusajiliwa katika ofisi za usajili wa vitambulisho hivyo lakini mpaka uandikishaji wa wapiga kura wa awamu ya mwisho unawadia hawakupewa vitambulisho vyao vya mzanzibari mkaazi na hivyo walikosa kuandikishwa kama wapiga kura. Inakadiriwa kiasi cha wafuasi wa CUF 40,000 walinyimwa vitambulisho vya mzanzibari mkaazi Unguja na Pemba na hivyo kukosa sifa ya kuandikishwa kama wapiga kura.
Kama hiyo haitoshi pamoja na kufanikiwa kuandikishwa kama mpiga kura unaweza hapo hapo ukakosa kupiga kura kwani njama na uchafu wa ZEC huwa haujamalizika. Unaweza kuorodheshwa kama mpiga kura na kupewa kitambulisho cha mpiga kura, hata hivyo siku ya upgaji kura jina lako likakosekana katika orodha za wapiga kura zilizobandikwa vituoni wiki moja kabla kwa ajili ya uhakiki au unaweza kukosekana katika orodha ya wapiga kura iliyokabidhiwa kwa maafisa wapigishaji kura siku ya upigaji kura. Mamia ya wafuasi wa CUF kwa makusudi majina yao yalikatwa na kutoonekana siku ya kupiga kura na hivyo walikosa haki yao ya kupiga kura pamoja na kwamba waliandikishwa kama wapiga kura.
Je kuna kuharibika kwa uchaguzi zaidi ya hivi inavyofanywa Tume yenyewe ya Uchaguzi kwa maagizo ya CCM na usimamizi wa Jecha na Mkurugenzi wake mapema sana tokea hatua za maandalizi? Katika hatua ya uandikishaji wapiga kura kwa mfano, CUF imekuwa ikiwasilisha katika Tume ya Uchaguzi barua za malalamiko na vielelezo vyenye ushahidi wa wazi dhidi ya njama zote na hujuma zote hizo zifanywazo na ZEC kwa kushirikiana na CCM lakini ZEC kwa kuwa hawakufanya hayo kwa bahati mbaya wamekuwa wakiyapuuzia mbali mbali malalamiko na kuendelea mbele na mchakato bila ya masawazisho yeyote ya msingi. Pamoja na uchafu wote huo katika Daftari, Jecha hajawahi kusikika akitangaza zoezi la uandikishaji limeharibika. Hakuwahi kusikika akifuta zoezi la uandikishaji baada ya kukabidhiwa ushahidi mpaka wa picha na video za wageni, watoto wadogo na wasio wakaazi wakipewa vitambulisho vya mzanzibari mkaazi ndani ya ofisi za JWTZ na kusajiliwa kusiko halali katika orodha ya wapiga kura. Hakuwahi kusikika kufuta zoezi chafu la uandikishaji na kusema limeharibika litarudiwa upya, hakuwahi. Hakuwahi kwa sababu hapa huwa anaisaidia CCM.
Sasa tuone kuharibika huku kwa uchaguzi wa Zanzibar kunakotajwa na CCM na Jecha. CUF mara zote imekuwa ikifanyiwa hujuma hizi hizi za wizi na hila katika chaguzi zote zilizotangulia lakini mara hii imekuwa na mkakati imara wa kisayansi wa kuzitambua na kuzikabili hujuma hizo na mwisho wa siku njama na wizi kushindwa kufua dafu. CCM wanadhani CUF ilikurupuka tu na kuingia katika uchaguzi wa 2015. CUF iliingia katika uchaguzi wa 2015 siku ya pili tu baada ya Dr. Shein Kuapishwa Novemba 2, 2010. Mkakati imara wa kisayasni uliotengenezwa vyema baada ya kutumia uzoefu wa miaka yote na kuusoma vyema mfumo mzima wa wizi na hujuma za kuichaguzi wa CCM ndio uliotumika kuielekeza CUF katika uchaguzi Mkuu wa 2015 huku ukisimamiwa na Timu imara yenye weledi, uzoefu na umakini mkubwa. CUF kwa kutumia mkakati wao huo waliweza kuikabili vyema kila hatua ya kiuchaguzi na kuugeuza wizi na hujuma zilizokuwa zinapangwa na kuzipindua biru. Kwa mfano wakati CCM wamewekeza matarajio makubwa kwa maelfu ya wasio wazanzibari na watoto wadogo walioweza kuwaandikisha kama wapiga kura wao, CUF imekuwa ikijikita na kampeni ya kisayansi kwa wapiga kura hao mamluki ili wasiwapigie kura CCM na bila shaka yeyote CUF ilifanikiwa.
Mtaji mwengine muhimu wa kuisaidia CCM ni hujuma dhidi ya mawakala wa CUF. CCM kwa kutumia nguvu yake ya usalama wa taifa na fedha hufanikiwa kwa kiwango kikubwa kupachikiza mawakala feki katika mfumo wa mawakala wa CUF na kuwanunua kwa fedha nyingi. Hila hii kwa asilimia 100 halikuweza kupata nafasi katika uchaguzi wa Oktoba 25. Hakuna wakala yeyote alieweza kununulika na hivyo CUF iliweza kusimamia kura zake zote kwa mafanikio. CUF iiweza kukusanya ushahidi wa fomu kutoka katika vituturi vyote vya kupigia kura nchi nzima Unguja na Pemba kwa ukamilifu. Hili limekuwa pigo kubwa kwa CCM kwani hawakuweza kucheza na matokeo halali ya kura zilizopigwa vituoni.
Ukweli unabaki katika hoja ile ile ya msingi yaani CCM Zanzibar imeshindwa vibaya katika uchaguzi kwa kuangukia pua huku ikidhani mtandao wake, mfumo wake na vyombo vyake vingeweza kubadili hujuma na wizi wa uchaguzi kuwa ushindi na hivyo kuisaidia kwa mara nyengine. CCM haikuyafahamu matayarisho ya CUF na hivyo kukwaa kisiki. CCM imeshindwa huku ikiwa haikujiandaa kisaikolojia. Haikuwa na matayarisho ya uwezekano wa kushindwa na haikuwa na matayarisho ya kushindwa. CCM katika mipango yake na hesabu zake chafu za wizi wa uchaguzi haikuweza kuzingatia kwamba pia na mpinzani wake, CUF ya 2015 nayo inazo hesabu zake ambazo zinapangwa vyema kuzifelisha hesabu za wizi za CCM kisayansi na kwa ufundi wa hali ya juu kabisa. CCM imekuwa ni kama panya mjanja na mpevu alenaswa mtegoni huku watu wanamuangalia wakimcheka.
Katika makala hii sipendi kupoteza kurasa kujadili hoja za ZEC za kufuta uchaguzi wa Zanzibar kwa kuwa suala hilo limeshajadiliwa sana na kwa kina huku hoja za CCM baada ya kutamkwa tu na jecha akisaidiwa na CCM hapajawahi kutolewa hoja za kuzitetea au ushahidi wa kuzijenga. Kuhusu hilo ni wazi kwamba sio ZEC wala Mwenyekiti wake hawakuwa na mamlaka ya kikatiba wala ya kisheria kufuta uchaguzi. Hoja zilizotolewa na Jecha na kufuta uchaguzi zote hazina mashiko na ni za kuandikiwa na mtu asie na uhakika wa anachokiandika. Nimeipenda hoja moja tu ya Jecha kwamba uchaguzi Pemba ulivurugika. Hoja hii ndio kabisa imekosa kusimama kwakuwa wananchi wa Pemba ndio waliofanya kazi ya ziada kuunusuru uchaguzi huo usiharibike baada ya kukamata kura feki na kuwakamata maafisa wa UMAWA kutoka Unguja waliopelekwa Pemba kuuchafua uchagzui wakidai wao ni mawakala wa Chama cha TADEA. Jitihada hizi za wananchi wa Pemba kuutakasa uchaguzi na uchafu uliopangwa kufanyika siku ya kupiga kura ni za kupongezwa na kila mpenda demokrasia na uchaguzi huru na wa haki. Huu ndio uchaguzi wa Pemba ambao CCM na Jecha kwa kinywa kipana wanauita UCHAGUZI ULIOHARIBIKA kuwa tu jaribio la kuuchafua lilifeli na hivyo CCM haikubebeka.
Hapo juu nilisema kwamba CCM sio imeibiwa ushindi ila imeshindwa bila ya kujiandaa kushindwa na kuwa tayari kushindwa. Haikuwa tayari kushindwa na kukabidhi serikali kwa alieshinda. Ushahidi mwingi sana upo kwamba CCM haikuwa tayari kukabidhi serikali. Moja ya ushahidi huu ni pale Mgombea wake wa urais wa Zanzibar aliposhindwa kutoa kauli ya kukubali kushindwa pindipo ikitokea hivyo. Mgombea wa urais kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kwa kinywa kipana alitamka hadharani wakati wa kampeni kwamba pindipo ikitokea kushindwa kihalali katika uchaguzi huu, atakubali kushindwa huko na atampongeza alieshinda. Pia Maalim Seif alimtaka mgombea mwenzake wa CCM, Dr. Ali Mohammed Shein kutoa kauli kama hiyo ya kiungwana na ya kuonyesha ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia lakini Dr. Shein alishindwa kutoa kauli kama hiyo pamoja na kukumbushwa mara kadhaa. Hii ndio siri ya kuharibika kwa uchaguzi. Kutokuwa tayari kushindwa. Watawala waliopo madarakani wamelewa na utamu wa madaraka waliyonayo hivyo hawawezi kuyakosa hata kama wananchi wamewakataa.
Suala la CCM Zanzibar kutokuwa tayari kung’oka madarakani halikuanzia na mchezo wa kuigiza wa Jecha Salim Jecha bali limeanzia mbali na kusisitizwa mara kadhaa na watawala na viongozi wa CCM kwa kauli na vitendo. Ishara ya watawala wa CCM Zanzibar kutokuwa tayari kung’oka madarakani ilianza kuonyeshwa tokea kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini. Wakati ilipowasilishwa hoja ya kubadilishwa kwa mfumo wa chama kimoja na kwenda katika mfumo wa vyama vingi, Rais wa Zanzibar wa wakati huo Dr. Salmini Amour maarufu kama Komandoo aliiambia wazi Halmashauri Kuu Taifa ya CCM hivi;
“sisi CCM upande wa Zanzibar vyama vingi hatuvitaki wala hatuko tayari kuvipokea na ingelikuwa sio huu Muungano na kwamba suala hili ni la Muungano kamwe vyama vingi visingeingia Zanzibar”.
Kauli hii haikutoa muelekeo mwema na msingi mzuri kwa demokrasia ya vyama vingi ndani ya Zanzibar na hivyo mchakato wote wa kidemokrasia ndani ya Zanzibar tokea zama hizo ulianza safari ya nuhsi na ulijengewa msingi na msimamo wa kibabe na kidikteta.
Kama kauli hiyo ya Komandoo ni ya zamani na hivyo haiakisi vyema maendeleo ya kisiasa ya zama hizi kwa kupitiwa na wakati hebu tuangalie kauli za viongozi wakubwa wa serikali na wa CCM zilizotolewa hivi siku za karibuni zikishadidia na kusisitiza kuwa kwa hali yeyote ile CCM Zanzibar haitayawachia madaraka kwa chama chengine chochote hata kama CCM itashindwa katika uchaguzi. Mmoja wa viongozi hao ni aliekuwa mwakilishi wa jimbo la Magomeni, Marehemu Salmin Awadh Salmin ambae alitamka wazi wazi kupitia mkutano wa hadhara kwamba CCM haiko tayari kukabidhi madaraka kwa chama chochote kupitia utaratibu wa kupiga kura hata ikibidi kuua. Alisema huku akisisitiza kwa kuwatisha wananchi kwa vifaru vya jeshi vinavyotembea barabarani kwamba ni nguvu kubwa za serikali ya CCM ambayo haitaondoka madarakani kupitia uchaguzi.
Kiongozi mwengine maarufu kwa kauli za kibabe Asha Bakari, wakati wa vikao vya Bunge Maalum la Katiba alitamka hadharani kwamba CCM Zanzibar haina mpango wa kuachia madaraka kwa utaratibu wa kura. Alisema;
‘….nchi hii ni ya kimapinduzi. Na mie namwambia Jussa sasa, hatuitoi, hatuitoi, hatuitoi, labda watupindue. Serikali ya kimapinduzi haichukuliwi kwa karatasi (kura). Hilo nawatanabahisha na uwezo huo (wa kupindua) hawana maana sisi ndio wenye madaraka”.
Kauli hizo zinazokwenda kinyume na misingi ya demokrasia na utaratibu wa kikatiba na wa kisheria wa vyama vingi vya siasa zimekuwa zikitolewa mbele ya masikio ya umma bila kificho huku viongozi wakuu wa Chama kutozikemea kauli hizo jambo ambalo linadhihirisha na kuonyesha kuwa zimepata baraka kutoka juu na hivyo ni kauli halali za Chama.
Katika kuonesha anapigilia msumari hoja yangu kuwa hizi ni kauli kauli rasmi za Chama ni ilekauli aliyoitoa Rais Mstaafuwa awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi wakati wa ufungaji wa kampeni za CCM Zanzibar katika viwanja vya Kibandamaiti aliposema;
“….mapinduzi yalifanywa na watu wa Unguja na sio watu wa Pemba, ingelikuwa yamefanywa Pemba angalau nao (Wapemba) wangeujuwa uchungu wake. Lakini kwa uungwana wa waliofanya Mapinduzi (watu wa Unguja) wakaamua kuwakaribisha kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa…”
Mzee Mwinyi akaendelea kwa kuyapamba maneno yake kwa wimbo ufuatao;
“…Msegeju ana ng’ombe, nami nina ng’ombe zangu…..anambia tuchanganye, sitaki, kwaheri nakwenda zangu…”
Mzee Mwinyi anakusudia wapemba (anaojidanganya eti ndio CUF pekee) wameshafanyiwa ihsani ya kuingizwa katika serikali ya umoja wa kitaifa hivyo hawastahiki tena kutaka serikali nzima eti kwa kuwa wao hawakushiriki Mapinduzi ya Zanzibar. Kwanza sijui Mzee mwinyi anakusudia wapemba gani hao maana hawa waliopo hivi sasa Mapinduzi wanayasoma vitabuni. Hivi kama kila CUF ni mpemba je wale wafuasi wa CUF waliopigwa risasi kule Kae Makunduchi kwa kupinga mamluki wasiandikishwe pia ni wapemba? Au Mzee Mwinyi kakusudia mababu wa wapemba? Hata hivyo bado vitabu vya historia vinatwambia kwamba katika uchaguzi wa mwisho kabla ya Mapinduzi Julai, mwaka 1963 ushindi wa Chama cha ASP Pemba ulikuwa ni asilimia 43 dhidi ya ZNP/ZPPP. Hii ikimaanisha karibu ya nusu ya wapemba waliunga mkono ASP. Ni aibu Mzee kama huyu kuwagawa watu badala ya kuwaunganisha tena kwa kutumia ngano za kale. Tunaposikia yeye ni mmoja wanaoshiriki mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa Zanzibar baada ya uchaguzi wa Oktoba 25 lazima tujiulize ni aina gani ya busara anayosaidia kupitia mazungumzo hayo.
Ukiwacha kauli hizo za viongozi, CCM pia ina utaratibu mwengine wa kupaza sauti na kutoa misimao yake inayoikusudia kwa umma. Utaratibu huu ni ule wa kutumia ubao wa maskani Kuu ya CCM hapa Zanzibar maarufu kama KISONGE. Nathubutu kusema ubao wa kisonge ni mdomo wa CCM kwani tokea wameanza kuandika kauli za kichochezi, kibaguzi na matusi hakujawahi kusikika kauli ya Chama ya kukemea machapisho ya ubao huo. Hivyo basi machapisho ya maskani ya kisonge ni matamko halali ya Chama na yanazo baraka zote katika Chama. Ubao wa kisonge umekuwa ukiandika na kurejea mara kadhaa kwamba CCM kamwe haitakuwa tayari kuachia madaraka kwa namna yeyote ile. Miongoni mwa machapisho yake mengi ni hivi karibuni imewahi kuchapisha kwa maandishi makubwa kwamba “HATUTOI NCHI HATA KAMA TUTAKUFA SOTE”.
Ukiunganisha yote hayo yaliyoelezwa huko juu unapata picha ya wazi kwamba hoja ya CCM ni kutokuwa tayari kuwachia madaraka Zanzibar pamoja na kushindwa vibaya katika uchaguzi na sio kuharibika kwa uchaguzi kama wanavyodai. Watawala hawa wamelewa na utamu wa madaraka wanayoyashikilia kwa muda mrefu sasa ambayo yanayowanufaisha wao, watoto wao na koo zao na sio wananchi. Wananchi walio wengi mara zote katika chaguzi zote tokea ule wa kwanza wa 1995 wamekuwa wakiukataa utawala huu wa CCM usiowanufaisha bila ya sauti zao hizo kuthaminiwa na kuheshimiwa. Oktoba 25 walirejea tena kauli yao kwamba wamechoka na utawala wa CCM usiowajali wananchi wake, unaowabagua wananchi wake na inaowanyanyasa na kuwatesa wananchi wake. Sasa wananchi wanasema basi inatosha, ni lazima kauli hii sasa iheshmiwe na si vyenginevyo.
Binafsi nina mashaka na juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika kulitafutia ufumbuzi suala hili la mkwamo wa kisiasa wa Zanzibar na haki kuonekana imetendeka. Hivyo tunaiomba jamii ya kimataifa kuliingilia kati suala hili kwa nguvu kubwa na kulipa mazingatio makubwa. Jamii ya kimataifa imekuwa ikishuhudiwa kuchelewa sana na kupoteza jitihada kubwa bila ya mafanikio mazuri kwani udikteta wa watawala huwa tayari umeshaitumbukiza nchi katika machafuko na mauwaji.
Jamii ya kimataifa haina budi kuviona mapema viashiria hivi vya uvunjifu wa amani na kuiingiza nchi katika umwagaji wa damu kunakofanywa na watawala wa CCM Zanzibar na kuhakikisha hali hiyo inaepushwa kwa gharama yeyote. Kuna kila dalili kwamba CCM Zanzibar inadhamiria kuipeleka nchi katika maafa makubwa hivyo jamii ya kimataifa ihakikishe inatumia njia zake za kidiplomasia kuzuia hali hii na ikibidi kutumia nguvu ili kunusuri vifo vya watu wasio na hatia hususan wanawake na watoto. Wazanzibari wamechoka kumwagwa damu zao kulinda matumbo ya wachache.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment