Wednesday 17 February 2016

KOFIA TATU ZA JAJI AUGUSTINO RAMADHAN

Ni zaidi ya mwezi wa tatu sasa tangu kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanyika 25 Oktoba mwaka jana, tukio ambalo limevitia visiwa vyetu kwenye mtihani na wasiwasi mkubwa kuwahi kabisa kutokea. Hii ni kwa kuwa, kwa bahati mbaya sana, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, alitangaza kuufuta uchaguzi huo pamoja na matokeo yake baada ya kuwa ulishakamilika na matokeo yake yote kujulikana.
Baada ya hapo wakajitokeza wanasheria na wataalamu wabobezi wa sheria wa Tanzania Bara na visiwani Zanzibar kueleimisha na kutoa nasaha kwa ZEC, Jecha, wagombea  na hata serikali kwa namna mbalimbali. Wachache katika hao ndio wameonekana kuunga mkono tangazo la Jecha, lakini walio wengi wamepinga na kuelekeza njia za kufuatwa baada ya tukio hilo la kufutwa kwa uchaguzi.
Lakini bado watu walibakia na masuala mengi wakijiuliza kwamba kuna baadhi ya watu ambao ni viongozi, wengine ni wastaafu na wengine bado wamo katika serikali hawajasikika kauli zao juu ya tukio la kwanza la kufutwa kwa uchaguzi kinyume cha sheria na kisha la pili la kutangazwa kwa uchaguzi wa marudio wa hapo Machi 20 mwaka huu, ambako nako pia ni batili kwa kuwa kulizalikana na ubatili wa awali.

Na Ali Mohammed
Na Ali Mohammed

Miongoni mwa waliokuwa wakiuliziwa ni pamoja na Jaji Mstaafu Augostino Ramadhani, ambaye alikuwa ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba Mpya, mbali na nafasi nyengine alizozishikilia jeshini na sasa Rais wa Mahakama ya Haki za Binaadamu ya Afrika yenye makao yake makuu jijini Arusha. Juu ya yote, Jaji Ramadhani ni Mzanzibari halisi. Kimya chake, kwa hakika, kilikuwa na machungu makubwa kwa Wazanzibari wenzake wamjuwao na wanaothamini uzalendo na mchango wake.
Labda ni baada ya kuchokozwa sana na wadadisi katika vyombo vya habari, ndipo siku ya Jumatatu ya tarehe 15 Februari 2016 akatokea katika gazeti la Mtanzania na kauli yake ya kwanza iliyobeba kichwa cha habari kisemacho, “Jaji Ramadhani apasua jipu urais CCM” humo akielezea kutoridhishwa na mchakato mzima ulivyoendesha ndani ya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kumpata mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho. Jaji Ramadhani alikuwa miongoni mwa wagombea waliokatwa majina yao bila maelezo wala mjadala wowote. Mwenyewe anasema amepanga “kwenda kuonana na uongozi wa juu hivi karibuni kutokana na kutokukubaliana na baadhi mambo“ ndani ya chama hicho tawala.
Siku ya Jumanne ya tarehe 16 Februari 2016, gazeti hilo hilo likachapisha sehemu nyengine ya mazungumzo yao na Jaji Ramadhani, ambamo safari hii kichwa cha habari kikawa: “Jaji Ramadhan: Ninaumizwa na Zanzibar”. Ndani yake muna maelezo ya jinsi jaji huyo anavyoumizwa na hali ya Zanzibar iliyopo sasa, akimaanisha tangu kufutwa kwa uchaguzi na baada ya kutangazwa uchaguzi wa marudio, na akasema ameliweka suala hilo katika ratiba yake ya maombi maalum kanisani. Ikumbukwe kuwa mbali na uanasheria, huyu pia ni mchungaji wa kanisa la Anglikana la Zanzibar.
Jaji Ramadhani ametoa duku duku lake na kusema anaumizwa na mambo mengi sana na sababu zake za kuumizwa nayo ni Uzanzibari wake usio kuwa na shaka. Historia ya familia yake ina mizizi kwenye siasa za ukombozi za Zanzibar. Babu yake, Mzee Ramadhani, alikuwa ni miongoni mwa waanzilishi wa “African Association” ambayo baadaye iliungana na Shiraz Association mwaka 1957 na kuzaliwa Afro Shirazi Party (ASP) na kisha ASP kuungana na TANU ya Tanganyika mwaka 1977 na kuzaliwa CCM ya sasa.
Lakini katika malalamiko yake yote alisahau kueleza ni ipi nafasi yake katika kuutafutia ufumbuzi wa haki mgogoro huu wa Zanzibar unaomsitikisha. Labda Jaji Ramadhani amepitikiwa na hilo au yawezekana hakupenda kuziweka hatua zake hadharani.
Ingawa baada ya taarifa yake ya Jumatatu kuna watu wengi walimbeza wakiuliza siku zote alikuwa wapi, mimi nataka niwaaminishe katika kutafuta suluhu ya mgogoro wowote ule, basi hakuna kuchelewa. La muhimu ni kuwa na nia ya kweli na uthubutu wa utatuzi.
Niseme kwa mimi bado nampa nafasi kubwa Jaji Ramadhani na namuona ni miongoni mwa watu muhimu katika kusaidia kuutatua mgogoro huu unaoitafuna Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Imani yangu hio inajengeka kwa kuziangalia kofia tatu alizozivaa Jaji Ramadhani – uanachama wa daraja la juu ndani ya CCM, uchungaji wa Kanisa la Anglikana, na uwanasheria na urais wa  Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu.
Akiwa mwanachama wa ngazi za juu wa CCM, Jaji Ramadhani anatakiwa kutumia nafasi yake kama mwana chama maalum wa CCM ambaye aliyefikia kuaminiwa kupewa fursa ya kuwania uteuzi wa urais wa Muungano wa Tanzania, kuwakabili wanachama na viongozi wenzake. Akaye nao kitako na awaoneshe umuhimu wa kuheshimu maamuzi ya Wazanzibari ya tarehe 25 Oktoba ili nchi ikwamuke ilipo na isonge mbele.
Akiwa ni mchungaji katika kanisa la Anglikana, Jaji Ramadhani anatakiwa atoe elimu ya haki kwa waumini wake na awaeleze bayana kwamba kilichotokezea Zanzibar kwa kufutwa uchaguzi na kutangazwa uchaguzi vyote havikufanyika kwa haki na aendelee kuomba dua, kuwaombea viongozi walainike nyonyo zao ili watende haki kwa raia. Kanisa Anglikana ni kongwe visiwani Zanzibar na lina nafasi yake kwenye historia. Linaweza kutumia ushawishi wake wa kiimani kulainisha nyoyo ngumu za viongozi wa serikali na chama ambao hawaoni hawasikii kwa sasa, zaidi ya kuiingiza nchi kwenye machafuko kupitia kile wanachokiita uchaguzi wa marudio wa Machi 20.
Akiwa kama Jaji Mstaafu wa Tanzania awaelimishe wanasheria wasiotenda haki juu ya jambo hili, kwa kuwa wao ndio wanaowapotosha viongozi waliosalia madarakani kwa kuwapa tafsiri potofu. Na kwa nafasi yake ya urais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binaadamu, ahakikishe haki za binadamu katika ncha hii iliyoko ndani kwa bara la Afrika (Zanzibar) zinaheshimiwa. Kila siku tunasikia makundi yanayoitwa Mazombi yakishambulia raia wasio hatia na kuharibu mali za wananchi, huku vyombo vya kusimamia amani na kutoa haki vikiwa vinapuuzia na kuwanyima wananchi haki zao.
Hivyo, kwa kofia hizo tatu, Jaji Ramadhani anao uwezo wa sio tu kusemea katika magazeti, bali kuukabili ukweli kwa vitendo kule kwenyewe hasa uliko. Kwa sasa, wengi tunamuona kuwa bado hajafanya kitu kikubwa sana kuinasua Zanzibar yake anayoipenda – nchi ambayo imezikiwa wazazi wake – kama atajiona kuwa anafungwa mikono nyuma kuisaidia nchi hii na vizazi vyake
ZANZIBAR DAIMA

No comments: