Thursday 21 July 2016

*THE CIVIC UNITED FRONT* *(CUF- Chama Cha Wananchi)*


*21 JULAI, 2016*

*TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI*

Ndugu zangu waandishi wa Habari,


Awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na uzima wa afya na tukaweza kukutana hapa asubuhi hii ya leo. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu pia kwa kuijaalia nchi yetu kuendelea kubaki katika hali ya amani, na kuwajaalia wananchi wa nchi yetu kuendelea kubakia katika hali ya stahamala na uvumilivu mkubwa, licha ya kuwepo kwa matendo mengi ya makusudi wanayotendewa ili yawapelekee kusababisha uvunjifu wa amani na kuondoa utulivu uliopo.

Pili, nichukue fursa hii kukushukuruni nyinyi waandishi wa habari kwa kuitikia wito wetu na kuja kutusikiliza. Naamini mtatusikiliza kwa makini, hususan kutokana na uzito wa suala tulilowaitia na kwa kuzingatia hali ya nchi yetu, tunawaomba muwafikishie wananchi yale ambayo tutawaeleza.


Tumewaita leo hii ili kuzungumzia kwa kina kuhusiana na kauli za Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, na kutoa msimamo wetu juu ya mipango na mikakati ya Jeshi la Polisi dhidi ya vyama vya upinzani, hususan Chama Cha Wananchi CUF.


Juzi, Jumapili tarehe 17 Julai, 2016 wakati akihojiwa na Tido Mhando katika kituo cha televisheni cha Azzam TV na kukaririwa na magazeti kadhaa, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, amenukuliwa akisema kwamba wakati wowote kuanzia sasa, Jeshi la Polisi litamkamata na kumshitaki Katibu Mkuu wa CUF - Chama Cha Wananchi Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuwachochea wafuasi wake ili waichukie serikali iliyopo madarakani.


Baada ya kuitafakari kauli hiyo ya IGP, ni vyema tuweke bayana kwamba hatukustaajabishwa na tamko hilo, japokuwa tumesikitishwa mno kuona kuwa IGP Mangu, sasa ameamua rasmi kuwathibitishia watanzania kuwa Jeshi la Polisi ni Idara Maalum katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Msingi wa hoja za Chama Cha Wananchi CUF kutokustaajabishwa na tamko la IGP juu ya mpango wa Jeshi hilo kutaka kumkamata Maalim Seif Sharif Hamad, umetokana na kukubali kwake binafsi kuwa kibaraka wa CCM.


Mangu amekuwa akilitumia kwa muda mrefu Jeshi la Polisi kushiriki katika matukio mbali mbali ya kuhujumu demokrasia na kukiuka haki za binadamu kwa lengo la kukinusuru Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na anguko kubwa la kukataliwa na wananchi kama ilivyothibitika kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa 25, Oktoba 2015.


Utekelezaji wa mkakati wa kumkamata Maalim Seif Sharif Hamad, unaopigiwa debe na Ernest Mangu, ni sehemu ya muendelezo wa CCM kuvitumia vyombo vya Dola, ikiwemo Jeshi la Polisi, kubaka na kuminya demokrasia, kupunguza na hatimaye kuzima kabisa sauti za wananchi wanaodai kuheshimiwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015, ambao Maalim Seif Sharif Hamad alimshinda Dr Ali Mohamed Shein kwa kura 25,831.



Mambo yafuatayo ndiyo yaliyojificha nyuma ya mkakati huo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM):


Ni kumzuwia Maalim Seif asiendelee na jitihada zake za njia za amani zinazoendelea ndani na nje ya Nchi za kuhakikisha kuwa haki ya Wazanzibari kujichagulia viongozi wao inaheshimiwa. Ziara za Maalim Seif pia zina lengo la kuhakikisha kuwa baadhi ya viongozi wa kisiasa na viongozi wa vyombo vya dola wanashitakiwa katika Mahkama za Uhalifu za Kimataifa kwa makosa mbali mbali ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu.


IGP Mangu anayasema haya kwa kujua kuwa yeye ni sehemu ya watu waliohusika kubaka demokrasia kwa kumnyima Maalim Seif ushindi wake wa kuwa Rais wa Zanzibar, na baadae kuendeleza vitendo mbali mbali vya uvunjifu wa Haki za Binaadamu.
Itakumbukwa kwamba baada ya Maalim Seif Sharif Hamad kushinda Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015, Jeshi la Polisi, chini ya Ernest Mangu lilitumika kubaka demokrasia na kupindua maamuzi ya wananchi wa Zanzibar.


Kwa maelekezo ya Mangu, Jeshi la Polisi ndilo lililomteka na kumuweka kizuizini katika Makao Makuu ya Polisi-Ziwani Zanzibar, Makamo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, ambaye pia ni Jaji wa Mahkama Kuu, Mhe. Abdul-hakim Ameir Issa. Jaji Abdul-hakim kwa nafasi yake ndiye aliyekuwa akiongoza kikao cha Tume ya Uchaguzi cha kuhakiki matokeo na kuyatangaza siku ya Jumatano tarehe 28 Oktoba, 2015 wakati Mwenyekiti wa Tume akiwa amejificha kusikojulikana.


Hivyo juhudi hizi za Ernest Mangu zimelenga kujinusuru yeye binafsi, kama mtendaji mkuu wa Jeshi la Polisi, na kuwalinda wanasiasa waliojiweka madarakani kwa mabavu na kuendesha nchi kwa mkono wa chuma, kwa kukiuka haki za binadamu kwa kuvamia, kupiga, kutesa, kubaka na kuwaweka vizuizini kwa kuwabambikizia kesi raia wasio na hatia.


Kwa mfano, hivi tunavyozungumza Jeshi la Polisi limekuwa na utaratibu wa kukamata raia, kuwapiga kuwabambikizia kesi, kuwashikilia na kuwatesa katika vituo vya Polisi bila ya kuwafikisha mahakamani. Hadi sasa zaidi ya wananchi mia nne (400) wameathirika kutokana na hujuma za Jeshi la Polisi kwa kubambikiziwa kesi.


Imekuwa ni kawaida kwa Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwarundika katika vituo vya Polisi wanachama na viongozi waandamizi wa CUF kwa muda mrefu kinyume na matakwa ya Katiba na Sheria za nchi.


Katika baadhi ya matukio haya ya udhalilishaji wa wanachama wa CUF kunakofanywa na Jeshi la Polisi kulihusisha pia kuwakamata na kuwaweka ndani raia waliokwenda katika vituo hivyo vya Polisi kwa madhumuni ya kufuatilia na kujua khatma za ndugu zao wanaoshikiliwa katika vituo vya Polisi.


Khofu ya Ernest Mangu inatokana na kuona kwamba azma ya CUF ya kuwafikisha mahakamani vinara wote wa uminyaji wa demokrasia na uvunjwaji wa haki za binadamu ni halisi, ameamua kutumia mkakati wa kutaka kumkamata Maalim Seif Sharif Hamad kama njia ya kujipapatua ili kuhakikisha lengo la CUF halifanikiwi kwa kuwa yeye ni miongoni mwa wahusika wakubwa wa uhalifu dhidi ya ubinadamu.


Hakuna asiyejua kuwa Maalim Seif Sharif Hamad ni kipenzi cha wazanzibari na ndiye anayeshinda chaguzi kuu zote zilizofanyika Zanzibar ukiwemo huu wa tarehe 25 Oktoba, 2015.  Jaribio lolote la kumkamata na kumdhalilisha kwa kumuweka ndani na kumbambikizia kesi ni kulazimisha kuitumbukiza Zanzibar na Tanzania katika machafuko makubwa ambayo Maalim Seif amejitahidi muda wote yasitokee.


Kwa makususdi, CCM kwa kumtumia Ernest Mangu wameigeuza Zanzibar kuwa ni nchi ya Polisi (Police state). Inashangaza sana, kuona IGP akiwa na dhamana ya kusimamia uzingatiaji wa sheria za nchi katika utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka anayoiongoza, anashindwa kuchukua hatua dhidi ya watendaji walio chini yake kutokana na ukiukwaji wao wa taratibu na uendeshaji usiozingatia maadili ya taasisi hiyo.


Kwa mfano, mbali na kuwepo ukiukwaji mkubwa wa Haki za Binadamu unaofanywa na Jeshi la Polisi Zanzibar ikiwa ni pamoja na kukamata, kuwabambikizia kesi na kuwafungulia mashitaka raia wasio na hatia,ikiwemo Viongozi wa CUF, pamoja na lugha za vitisho, zinazotolewa na wasaidizi wake, IGP ameshindwa kuchukua hatua stahiki.


Hadi hivi leo, IGP Mangu ameshindwa kuchukua hatua, au kutoa tamko la kukemea, kuomba radhi au kumuwajibisha Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ya jinai (DDCI) Salum Msangi dhidi ya kauli za vitisho na kibabe alizozitoa kuhusiana na Mawakili wanaofika vituo vya Polisi kuwawakilisha na kuwatetea wananchi waliokamatwa kwa tuhuma mbali mbali.


Kwa kuwa IGP Ernest Mangu amejitwisha jukumu la kuwa sehemu muhimu ya kutekeleza mkakati wa wanaomtuma, kwa kutumia Mamlaka ya Dola ya Jeshi la Polisi, Chama Cha Wananchi CUF kinamtaka Ernest Mangu kufahamu kuwa Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi wote wa CUF hawatatishwa wala kurudishwa nyuma au kunyamazishwa kwa aina yoyote ya vitisho katika kudai haki ya ushindi wa Wazanzibari kutokana na maamuzi yao waliyoyafanya kupitia njia za kidemokrasia tarehe 25 Oktoba, 2015. Hivyo, CUF inamtaka Ernest Mangu kufahamu kuwa:


1. Tamko lake la kumkamata na kumfungulia mashitaka Maalim Seif Sharif Hamad halimshitui yeye binafsi, viongozi wenzake wala wanachama katika CUF. Imekuwa ni mazowea kwa Maalim Seif na wana CUF kukamatwa, kupigwa, kuteswa na kufunguliwa mashitaka bandia ili kuwavunjia heshima yao.

Maalim Seif Sharif Hamad, alishawahi kukamatwa na kuwekwa kizuizini 9 Mei 1989, hadi 30 Novemba 1991 bila ya hatia yoyote na kufanyiwa udhalilishaji mkubwa. Wakati huo, tunaamini kuwa Ernest Mangu hakuwa lolote wala chochote katika Jeshi la Polisi la Tanzania. Kukamatwa huko na kuwekwa kwake kizuizini hakukumvunja moyo bali kulimjenga na kumfanya kuwa mwanasiasa imara katika kusimamia aliyoyaamini.


2. Ni muhimu kwa Ernest Mangu kutambua na kutilia maanani kuwa Maalim Seif Sharif Hamad alishinda Uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na kwamba ushahidi wote wa vielelezo vya fomu za matokeo ya Uchaguzi huo, kwa kila kituturi cha kupigia kura, zipo na zimehifadhiwa kwa matumizi yoyote itakapohitajika.

Aidha, CUF inamtanabahisha Ernest Mangu kuwa kwa mujibu wa Sheria za nchi hii Maalim Seif Sharif Hamad ndiye kiongozi halali aliyechaguliwa na wananchi, na kwa hivyo Uchaguzi wowote mwengine, ikiwamo ule wa tarehe 20 Machi, 2016 ni batili na serikali iliyopo madarakani ni batili pia.


3. Mpango wa kuishawishi dunia kuwachukulia hatua wahusika wote wa ukiukwaji wa Haki za Binadamu na uvizwaji wa demokrasia uko pale pale, wala hautasitishwa kwa vitisho vyovyote ili kuhakikisha unyama dhidi ya raia wasio na hatia unakomeshwa, na uzingatiwaji wa Sheria za nchi unatamalaki katika uendeshaji wa nchi yetu.


4. CUF inamtahadharisha Ernest Mangu na viongozi wanaomtuma kwamba Zanzibar na wazanzibari tumechoshwa na figisufigisu hizi za Jeshi la Polisi kwani tunaamini *figisu figisu huzaa Timbwiri.*

*HAKI SAWA KWA WOTE*


*NAIBU KATIBU MKUU - CUF – ZANZIBAR*

No comments: