Thursday, 1 September 2016

MIUJIZA YA MWEZI WA AUGUST.

Mwezi wa August

1. Wiki ya kwanza ilishuhudia safari ya kurudi nyumbani kwa Maalim Seif huku kukiwa na kelele za IGP kutaka kumkamata. Alipokewa na akafurahiwa kwa kurudi zake salama pamoja na kuyaeleza mafanikio ya safari zake. Magazeti na ulimwengu ulikuwa hai kutazama hatima ya kamata kamata na hasa kauli ya IGP kwenye vyombo vya habari. Vile vile zikaanza kauli za Dodoma, viongozi wakishindana nani wa kufika mwanzo na kwa staili gani, kama hadithi ya mfalme Suleiman na ndege wake hudhud, ni masuala ya kasi hata kwenye giza, makofi kwa mkuu wa kusomesha namba hata zisizo na thamani kama sifuri ilivyo.

2. Wiki ya pili ikaja kauli ya kwamba "asichezewe" JPM, na watakaojaribu watakiona. Hii ilikuwa ni majibu yake kwa waliosukumwa na madai ya haki yao ya kuendesha siasa kama katiba inavyosema badala ya amri ya Rais iliokuwa na khofu ya kurudisha siasa za mfumo wa chama kimoja. Kipindi hiki kikabebwa na UKUTA, ambao uliwapanga serikali, chama, na hata taasisi marafiki na chama tawala kulaani haki ya "kuendesha siasa katika nchi ya demokrasia ya vyama vingi". Miongoni mwao kukawa na msajili, sheikh wa Dar, baadhi ya maaskofu, polisi na wenginewe bila ya kumsahau Mwenyekiti wa bodi ya parole. Vile vile ikaja kauli ya kufyetua tu watoto na serikali ipo itasomesha bure, kama vile watoto wanahitaji elimu pekee. Tafiti zikaja na makubwa kwamba asilimia 70 ya watoto wanaishi katika umasikini. Baadae ikatolewa tafsiri pana kwamba serikali bado inasimama na sera ya uzazi wa mpango, na kufyetua ni utani tu kwa wazaramo na wasukuma. Alau hakuna utani na makabila mapya "wazanzibari" hasa wa fyokofyoko.

3. Wiki ya tatu kikaja kifo cha Mzee Jumbe, Rais wa pili wa Serikali ya Zanzibar, Makamo Wa Rais wa Muungano mstaafu na mmoja wa viongozi aliebeba makubwa katika siasa za Zanzibar. Lililokuwa kubwa zaidi ya yote ni namna ya maziko yake yalivyosimama kama alivyousia mwenyewe (Mungu amraham). Na ndio kipindi cha figisu figisu ikafika wakti mpasuko ukagonga nafsi ya siasa za Zanzibar baada ya Makamo wa kwanza Mstaafu kuukata mkono wa aliemuona ni dikteta aliekamata watu wake (alieitwa nduli hakuwapo) akapiga waliompinga, akawa ni sehemu ya vitisho vya kukamatwa kwake. Kama ilivyo ada, mara hii taasisi rafiki za chama ndizo zilizokuja juu, na kelele zikaanza kwa Mwenyekiti wa bodi ya parole na kumalizika kwa Naibu wa chama alieitaka serikali imzuie Maalim Hamad kushiriki katika sherehe za kitaifa. Eeeh mfano maziko, au pengine sehemu yoyote atayokuwapo mflame wa asilimia 92.

4. Wengine hawakuwa nyuma kama kauli mpya kwa mwenye mkoa wa Dar akizuia watu kuingia mkoani kwake bila ya kazi maalum na kwa kutembea halkadhalika kwa muda maalum. Mwenye mkoa anaamini kwa kauli na amri, anaamini ndie mwenye jeshi na polisi wa mkoa na ni kama Chechnya na Urusi (namuita Ramzan Kadyrov, mtafute utanifahamu). Ule utani wa kizaramo na kisukuma ukaisha, aliekuja kwa mwenge anazuia wengine kufika kwa mwenge. Wa visiwani nao watahesabiwa vipi? Wana muda upi wa kukaa katika himaya mpya ya mfalme wa Dar hasa na maamrisho yake ya kuzuia wahamiaji bara seuze wa visiwani. Tulijiuliza tungesema sisi ingekuwaje!

5. Wiki inayofuata yake, yakaja mauaji makubwa ya polisi na ndio kauli za wapambe wapya wa uimla zilipopaa zikihimiza askari kupiga kwanza, kuuwa kwanza halafu wenye kelele wamtafute mbishi wa haki za binaadamu, Kadyrov wa Dar. Kwa mara ya kwanza inayoitwa tume ya haki za binaadam, ikatoa tamko na kulalama ikimkemea Rais wa Mkoa, na kumpigia makofi wa nchi aliesema yale yale dhidi ya haki za binaadam. Vile vile kukawa na furaha ya miaka 50 ya ndoa ya Mkapa, kiongozi aliefurahia ndoa yake na mwenzake ya miaka 50 ikitajwa kuwa ni ya miujiza kutokana na madhehebu ya imani tafauti, si muislam na mkristo bali mlutheri na mkatoliki. Sisi tulianza 1964, kwa ulazima mpya, tukachanganya shia na sunni, wahindi na waswahili nk. Mwadham wetu kayabashiria miujiza haya ya Che Nkapa, ya kwetu sijui angesema nini?

6. Wakati akipongezwa kwa kudumu kwa ndoa yake, wengi walisahau namna alivyoweza kuharibu ndoa za wengine na kuweka vizuka kwa mauaji ya mwaka 2001. Unajuwa wangapi wamepoteza baba zao? Waume zao? Kaka na dada zao? Alau wangetimiza miaka 15, Bronze jubilee? Ndio dunia ya leo, mwenye nguvu hupongezwa kwa sifa za miujiza hata akiwa karoa damu za wengine wanyonge kwa kumpinga tu. Halkadhalika golden jubilee hii ikawakutanisha JPM na EL, kwa kile kilichotajwa kuwa ni miujiza kupokezana mikono. Magazeti yakaamka na kichwa cha habari cha EL muungwana, wengine wanauliza kwani kaibiwa mara ngapi, wetu mara nne, uungwana na kikomo chake.

7. Kubwa zaidi likaja la Profeseri wa Uchumi, bingwa anaeheshimika na kupendwa kiasi kwamba alijizulu mwaka mzima na kuamua kufuta azma yake baada ya mwaka akidai kwa nguvu kiti chake. Mnyonge huyu mwenye unyenyekevu wa hali ya juu na imani kubwa ya maadili ghafla akapinga njia ya uchaguzi kurudi kwake na kuiona haki yake ya uenyekiti ikiwekewa ngumu na hivyo akavunja yote yenye mantik kuhakikisha hapotezi kilichomstahili. Matokeo yake ni fujo, na mvutano, kuharibika kwa mkutano mzima na mwishowe kusimamishwa kwa uanachama wa watu 10 akiwemo mwenye  dhana ya haki yake ya uenyekiti na waliomfuata miongoni mwa viongozi. Figusu lipo kwa mrajis wa vyama, anaeonekana kulivalia njuga lisiharibike.

8. Likaja sakata la kamata kamata la viongozi wa CDM akiwemo Mbowe na wote waliokuwa katika meza kuu akiwamo EL. Wakati wenye kujenga Ukuta wakiweka mchanga na saruji sawa kwa ujenzi, na wavunja Ukuta wakifanya mazowezi makubwa hadharani, kama vile wakijitayarisha kushiriki katika mapigano DRC, Somali au Darfur, kumbe ni Dar, Mwanza, Mbeya tena kusimama na haki ya uhuru wa vyama vingi. Hatimae na Jeshi likaingizwa kati, moshi wa Afrika ya Magharibi ya kina Sani Abacha ukipaliliwa kuni kidogo kidogo, demokrasia mpya, tafsiri mpya ni ya mwendo wa kasi tu. Tumevuka kutoka kule wapigwe tu, tumechoka mpaka sasa tusimchezee kiongozi wa malaika, yeye hachezeleki.

9. Tumefunga mwezi kwa mkurupuko mwengine, kwamba Rais anakusudia kubadili pesa ili kuwakomoa wale wanaoweka pesa zao ndani ili zisitumike. Sifikirii kama kuna tajir anaeficha fedha ya madafu (natumia nukuu ya JK), hivyo hata ukibadilisha pesa haitasaidia kuwakomoa wanaobana matumizi na kuficha pesa zao kutokana na mazingira ya khofu muliowajengea. Zaidi wataumia wanyonge kwa "inflation" na inafurahisha kuwa na serikali inayoondosha vitafunio kwa sababu ya kupunguza gharama lakini ikaingia katika gharama mpya ya kubadili noti kwa sababu tu ya kukomoa walioweka za kwao majumbani. Tujitayarishe sasa na ongezeko la soko la walanguzi hasa kwenye mabadilishano ya fedha. Namtazama malaika mwengine wa Rwanda,Kagame "role model" anavyoisukuma nchi hii kidogo kidogo katika korokoro (abyss) baya kama alivyofanikiwa kwa DRC.

10. Na visiwani kukafanyika mahafali ya "diaspora" mwenye nchi akafungua na tai na suti zikatinga. Kutoka Next, Topman, hata za TK max, wengine wa mamtoni wakafika na Boss, Armani, ili mradi ni shangwe na vigeregere kwa wazalendo wapya wanaofaidika na demokrasia, uhuru wa haki, uhuru wa chaguzi kwa wanaemtaka bila ya bughdha tena hata wepesi wa kulalama kwa kubaguliwa hata wanapokosea, huko walipotoka. Lakini kule kwao wanasema "bado mapema, bado kwanza" wakipiga makofi kwa kufutwa chaguzi huru, wakibeba ubaguzi kwa wengine, wakisubiri tunda la utajiri wa urahisi kwa vile nje kunataka nguvu kazi, ndani kunataka unyenyekevu kwa wenye nguvu. Hata zile dharau za kuitwa diaspora wakimbizi imekufa, ni mwendo wa kasi tu.

Sisi tunasema "Aluta continua" tusubiri miujiza ya mwezi ujao.

No comments: