Sunday, 25 January 2009

CUF WAMJIBU KIKWETE

Hasira za Wapemba kwa CCM Zinatokana na Kufeli kwa Chama Cha Mapinduzi"
Wapendwa Wanahabari,
Kufuatia ziara yake ya hivi majuzi kisiwani Pemba, Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mhe. Jakaya Kikwete, amenukuliwa akiwaambia Watanzania wa kisiwa cha Pemba kwamba huenda upinzani usiingie kabisa madarakani, na kwa hivyo ni vyema wakashirikiana na Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho kilichopo sasa madarakani.
Licha ya kuwa kauli hii ni ya kisiasa ambayo inaweza kutafsiriwa kwa muelekeo huo tu – kwani huyu ni mwenyekiti wa CCM ambaye kwa vyovyote asingetarajiwa kukitabiria chama chake kuondoka madarakani au kukiri kwamba kuna chama chengine ambacho kinaweza kuchukua nafasi ya CCM – sisi Kurugenzi ya Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma ya The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi) tunaona kuwa kuna haja ya kuitolea ufafanuzi.
Kwanza, kumekuwa na tabia ya viongozi wa ngazi za juu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuyatafsiri matatizo ya kisiwa cha Pemba kisiasa tu bila ya kuzingatia hali halisi ya kiuchumi ambayo wananchi wa kisiwa hicho wamekuwa wakipambana nayo.
CUF tunaposema kwamba hali ya maisha ni ngumu, ni kwa kuwa serikali zilizopo madarakani zimekisusa kisiwa cha Pemba na kukitenga kabisa kimaendeleo.
Serikali hizi, ambao zinaongozwa na CCM, zimekuwa zikifanya hivyo kama ni njia ya kuwakomoa wakaazi wa kisiwa hicho ambao tangu kuanzishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi, mwaka 1992, wamekuwa wakionesha wazi msimamo wao wa kuipinga CCM.
Kwa hivyo, wakaazi wa Pemba wataendelea kuzipinga serikali zilizopo si kwa sababu ya chuki wala fitina, bali kwa sababu serikali hizo zimeshindwa kukidhi (have failed to deliver) matashi yao.
Pili, kwa kuwa Rais Kikwete na wenzake wanajuwa hasira walizonazo wakaazi wa kisiwa cha Pemba dhidi ya serikai hizi zilizoshindwa kuinua hali ya maisha ya mkaazi wa kisiwa hicho – kama vile pia zilivyoshindwa kwa wengine – basi wanatafuta kisingizio cha kuzielezea hasira hizo, kwamba eti ni viongozi wa vyama vya upinzani.
Huko ni kuwadhalilisha wananchi hao kwa kuwaona kama kwamba wenyewe hawana uwezo wa kuchanganua na kufahamu hasa lilipo tatizo lao, ambalo ni serikali za CCM zilizofeli, mpaka wachanganuliwe na viongozi wa upinzani. Hasira za wananchi wa Pemba ni muakisiko wa kufeli kwa CCM, na si chenginecho.
Tatu, ni vibaya kwa Rais Kikwete kutumia uzinduzi wa miradi ya maendeleo kuwasimanga wananchi wa kisiwa cha Pemba, kwani kwanza miradi hiyo inajengwa kwa kodi zao au kwa misaada ya wahisani ambayo huko ilikotolewa ilitolewa kwa ajili ya wananchi hao, na si kinyume chake.
Kama alivyosema mwenyewe, Serikali kujenga miundombinu ni jukumu lake na wala Rais Kikwete asijenge picha kwamba anawafanyia hisani wananchi wa huko; na hivyo akapata sababu ya kuwasimanga.
Mwisho, ikiwa kweli Rais Kikwete ana dhamira ya kuisaidia Zanzibar kuondokana na ule aliouita ‘Mpasuko wa Kisiasa’ anapaswa kuliangalia suala hili kwa uadilifu. Kuendelea kwake kupiga mifano ya watu ‘waliogomewa’ kupata huduma za kijamii kutoka kwa wenzao lakini asigusie kabisa sababu halisi zilizopelekea hao waliogomea kugomea, ni kuwabagua watu na ni kuendeleza mpasuko.
Tunakusudia kusema, ikiwa Rais Kikwete anaongelea kisa cha mwanachama wa CCM kususiwa biashara yake na wana-CUF, kwa mfano, basi pia na azungumzie kuwa mwana-CCM huyo aliyesusiwa ndiye aliyeshiriki kuwabaka watoto wa wana – CUF, kuiba mali zao na kuwaletea makundi ya Janjaweed kuwavunjia nyumba zao. Je, Rais Kikwete yuko tayari kuueleza ukweli huu pia?
Imetolewa na
Salim Bimani
Naibu Mkurugenzi,
Directorate of Human Rights and Public Relations
The Civic United Front (CUF)
Party Headquarters
P.O. Box 3637
Zanzibar
Tanzania
Tel. (+)255 (0)777 414 100 / (+)255 (0)777 414 112
E-mail: cufhabari@yahoo.com
Weblog: http://hakinaumma.wordpress.com
Website: http://cuf.or.tz

No comments: