Friday 24 July 2009

Mizengo pinda unamtisha Nani Zanzibar haikuhusu

Mizengo Pinda unamtisha nani ? Zanzibar si nchi ,, isiwe na chochote , imekukosa nini Zanzibar leave us alone.

Wazanzibari Mkitaka mjaribu muone kama kuna urahisi katika jambo hilo," alijibu Pinda kwa mkato!

Waziri Mkuu Pinda atoa onyo kwa viongozi Z'bar wakivunja Muungano


Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ametadharisha kutokea madhara makubwa iwapo muungano utavunjwa kutokana na kauli za baadhi ya viongozi wa Zanzibar.

*ASEMA UKIVUNJIKA UPANDE MMOJA UTASAGA MENO

Habel Chidawali, Dodoma


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameonya uwezekano wa Muungano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kuvunjika endapo malumbano kuhusu gesi asilia na mafuta yaliyoanza sasa yataendelea na kuonya kwamba baada ya hatua hiyo upande mmoja utapata shida.


Pinda anatoa onyo hilo bungeni jana, wakati tayari viongozi wawili wa ngazi za juu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) walishatoa msimamo rasmi wa kutaka suala la mafuta na gesi asilia liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano.


Viongozi hao ni Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yussuf Himid ambaye alitoa msimamo wake wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2009/10 katika Baraza la Wawakilishi Mjini Zanzibar.


Naye Naibu Waziri Kiongozi Zanzibar, Ali Shamhuna, amewahi kutoa kauli kama hiyo akidai kuwa suala la mafuta ni la Zanzibar peke yake, Bara hawahusiki nalo.


Pinda alitaka Watanzania kuangalia jambo hili ili kujua nani ataathirika zaidi endapo jambo hilo litafanyika.


Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nzega, Lukas Selelii aliyetaka kujua sababu za viongozi wa juu akiwamo Rais Jakaya Kikwete kuwa kimya kuhusu jambo hilo ambalo linaonekana kuuweka Muungano katika hali tete.


Akijibu swali hilo, Pinda wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo bungeni jana, alieleza wasiwasi wake kuhusu jambo hilo akisema kuwa likitokea lazima kuna upande ambao utaathirika, bila ya kutaja ni upande gani.


"Kama kuna uwezekano jambo la mafuta na gesi asilia kuondolewa katika Katiba ya Muungano ambako liliiingizwa mwaka 1968 itakuwa ni jambo la heri, lakini sio kuvunja Muungano,” alisema na kuongeza:


"Tumekuwa tukipata tabu sana na kusumbuliwa na kauli zinazotolewa na baadhi ya wenzetu. Mara tunaambiwa kuwa ni wezi wa mchana, wakati mwingine tunaambiwa kuwa ni wakoloni.... Ahaa jambo hilo linasikitisha sana..., ipo siku muungano utavunjika na ikifikia hatua hiyo, nina hakika upande mmoja wa muungano utaathirika.”


Katika swali lake Selelii alimtaka Waziri Mkuu aeleze ukimya wa viongozi wa juu akiwemo Rais wa Jamhuri pamoja na Rais wa Zanzibar kuhusu jambo la mafuta ambalo linaonekana kuuweka Muungano katika hali tete.


"Mheshimiwa Waziri Mkuu, kumekuwa na maneno ambayo yanaonekana kuuchokonoa Muungano kutoka kwa baadhi ya wabunge pamoja na Baraza la Mapinduzi Zanzibar ambapo sote tuliapa kuulinda na Katiba yake; lakini viongozi wa juu mmekuwa kimya sana, hamuoni kuwa hivi ni viashiria vya kuvunja Muungano?”alihoji Selelii.


Akijibu swali hilo, Pinda alitumia baadhi ya maneno ambayo yalitolewa katika hotuba ya Rais Jakaya Kikwete Juni 26, mwaka huu akisema: "Hata rais alishasema na kukemea juu ya jambo hilo".


Pinda aliongeza: "Rais alishasema kuwa mafuta hayajapatikana na huenda yasipatikane kabisa. Kiongozi wa nchi alionya juu ya malumbano hayo na kuagiza kuwa yaachwe mara moja".


Alifafanua kuwa ilishaundwa tume ya wataalumu kutoka nje ili kuangalia uwezekano wa namna bora ya kuzishauri serikali mbili juu ya kugawana pato litakalotokana na mafuta na kwamba, tume ilishawasilisha taarifa yake ndani ya serikali tangu Juni 23 mwaka huu.


Kiongozi huyo wa serikali bungeni alisema kuwa ana wasiwasi mkubwa na hata wakati fulani anajiuliza juu ya muungano huo kama utavunjwa, kitu gani kinaweza kutokea hasa kwa upande wa pili.


Alisema tume iliyoundwa ambayo iko chini ya ofisi ya Makamu wa Rais inafanya utaratibu mzuri wa kuangalia masilahi kwa pande zote mbili ndani ya Muungano ili kutoa nafasi sawa.


Hata hivyo, akijibu swali lingine lililohusu Muungano, Waziri Mkuu alionekana kuwa hasira baada ya kujibu swali lililohusu Katiba ya Muungano ambalo alilijibu kwa mkato tena kwa hasira.


Swali hilo liliulizwa na Yahaya Issa mbunge wa Chwaka (CCM) aliyetaka

kujua juu ya Zanzibar kuingizwa katika ushirikiano wa Kimataifa.


Issa alisema kuwa kutokuingizwa Zanzibar katika ushirikiano wa Kimataifa ni njia moja wapo ya kuinyanyasa Zanzibar kwa kuwa jambo hilo halipo ndani ya Katiba, hivyo upande huo wa pili wa nchi ni kama unakandamizwa.


Akijibu swali hilo, Pinda alisema Katiba ya Muungano ndio mwakilishi wa nchi ya Zanzibar pia, hivyo upande huo wa pili wa Zanzibar utaendelea kuwakilishwa na Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa siku zote.


"Mkitaka mjaribu muone kama kuna urahisi katika jambo hilo," alijibu Pinda kwa mkato.


Jibu hilo la mkato lilionekana kutokuwaridhisha wengi na wabunge wengi walipigwa butwaa, kwani hawakulitegemea.


Wakati huo huo, Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohamed amepinga majibu ya Pinda, akidai kuwa chokochoko za Muungano zilianza tangu wakati wa hayati Karume na Mwalimu Nyerere.


Alisema katiba ya Muungano ndiyo kikwazo kikubwa kwa kuwa iliongezwa vipengele ambavyo havikuwepo awali.


"Kuongezwa kwa vipengele hivyo kulitokana na Katiba ya muda ambayo ilikuwa imepanga kuwa kabla ya mwaka kumalizika, baada ya muungano, kuwe na katiba ya kudumu, lakini haikutekelezwa badala yake ikakamilishwa baada ya miaka 7,” alisema Rashidi.


Aliyataja mambo yaliyoongezwa katika kipindi hicho kuwa ni pamoja na suala la mafuta ambalo mwanzo halikuwepo.


Aliongeza kuwa jambo lingine linaloyumbisha Muungano ni pamoja na kuondolewa kwa wadhifa wa Rais wa Zanzibar katika nafasi ya makamu wa rais wa Muungano.

Alisema hakuna usawa wa kimasilahi kwa nchi hizo mbili kutokana na upande mmoja kupata masilahi zaidi ya upande wa pili.


Mohamed alikanusha vikali kuwa Muungano ukivunjwa upande mmoja utaathirika akisema kama ni hivyo basi Karume na Nyerere waliwadanganya wananchi waliposema tuungane kwa masilahi ya pande mbili.


Alionya kauli hiyo iachwe mara moja na kisha akasema muungano ukivunjika pande zote zitatikisika.

No comments: