Tuesday, 22 April 2014

CCM INAPOKUA NA AJENDA YA KUPAMBANA NA UISLAMU.


P 7
Na Mohammed Said,

Imekuwaje leo Uislam wa Zanzibar unakuwa neno miaka 50 baada ya muungano? Kuna kitu hapa hakisemwi kwa kuwa kinatisha. Dunia nzima hivi sasa Uislam unakuja juu na huu ni ukweli usiopingika. Hapa kwetu Tanganyika Uislam umechukua sura nyingine pia. Kuna kitu Ulaya na Marekani wanakifahamu nacho ni ”Militant Islam.” Hili ni somo tosha linalojitegemea lakini hapa hatuwezi kuingia ndani ila itoshe tu kusema kuwa kuna Waislam wananyanyua silaha kuilinda dini yao. Kama hivyo ni sawa au si sawa hilo tuwaachie maulamaa waamue. Ili mtu aweze kuelewa kwa nini leo uhusiano kati ya Zanzibar na Tanganyika umefika hapa ulilipofika ni muhimu sana akaijua historia ya kweli ya muungano. Vinginevyo mtu atakuwa anatapatapa hana mahali pa kushika.


Mwaka 1964 wakati Tanganyika inaungana na Zanzibar, Tanganyikahaikuwa kama hivi sasa ilivyo. Suala la ”udini” halikuwapo katika siasa za Tanganyika. Uislam ulikuwa umetumika vilivyo kupigania uhuru wa Tanganyika bila ya kuuathiri Ukristo na hakuna aiyekuwa hajui nguvu ya Uislam. Nyerere mwenyewe aliingia madarakani mwaka 1961 na kuishika nchi akiwa amekaa juu ya mabega ya Waislam. Siasa zilizotamalaki wakati ule zilikuwa siasa za uzalendo wa Kiafrika. Dini katika uendeshaji wa nchi haikuwa na nafasi. Hii leo mambo yamebadilika sana.
Uislam Tanganyika ulianza kupigwa vita vya chini kwa chini mara baada ya uhuru hatimaye kufika mwaka 1968 vita hii ilikuwa ishafika kileleni katika mgogoro wa East African Muslim Welfare Society (EAMWS) na kuundwa kwa BAKWATA. Si siri tena kuwa Nyerere na Kanisa Katoliki walihusika sana na hatimae nguvu ya Waislam katika siasa za Tanganyika zikapotea kabisa pamoja na historia ya Uislam katika kupigania uhuru wa Tangayika. Hadi leo mashujaa waliopigania uhuru wa Tanganyika historia yao imefutwa. Imekuwa mwiko hata kuwataja katika vitabu vya historia.
Hivi sasa hisia za Uislam katika nchi yetu zinafukuta chini kwa chini na ndiyo maana tumekuwa na mauaji ya Mwembechai, Picha ya Ndege, na Kilindi na vijiji vya pembezoni mwake hivi karibuni na majuma mawili yalopita tu Waislam wamingiliwa msikitini (staili ya Mwembechai) na kupigwa na polisi. Kesi za masheikh zimekuwa maarufu Zanzibar na Tanganyika. Shuhudia hapa JF hamaki za kidini na wakati mwingine matusi baina ya Waislam wa Wakristo. Hizi ni dalili tosha kuwa mambo si shwari tena. Kitu cha kushangaza ni kuwa viongozi wetu wanajifanya hakunajambo, tuna amani.
Hii leo Zanzibar Karume akitajwa baadhi ya watu wanamlaani na halikadhalika Tanganyika Nyerere akitajwa baadhi ya Waislam wanamlaani. CCM Zanzibar katika chaguzi zote toka 1995 wamekuwa wakishindwa na hili linafahamika dunia nzima. Zanzibar wanachukua serikali kwa mtutu wa bunduki. Kitu cha kujiuliza ni hiki. Ni nani hawa wanaowanyima CCM Zanzibar kura? Jibu ni kuwa hawa ni wananchi na wengi wao wamezaliwa baada ya mapinduzi.
Wazanzibari asilimia 99 ni Waislam. Hii asilimia 99 leo inajua kuwa nchi yao imeungana na Tanganyika mbayo viongozi walioshika madaraka ni Wakristo na wana chuki kubwa na Uislam. Wazanzibari hawajasahau sakata pale walipojiunga na Organisation of Islamic Conference (IOC) mwaka 1993 na wala hawajasahau Aboud Jumbe alivyotolewa madarakani Dodoma kwa kuidai Zanzibar. Viongozi wa leo wa Tanganyika hawa hawapendezi Zanzibar kama walivyopendeza kwa wazee wao wakati wa muungano mwaka wa 1964. Viongozi hawa ndiyo hawa katika kundi la akina William Lukuvi wanaoingia kanisani na bila hofu kusema kuwa hawataki kuiona Zanzibar inakuwa nchi ya Kiislam. William Lukuvi alipopewa nafasi ndani ya Bunge Maalum la Katiba kujieleza bila hofu na kwa kibri cha hali ya juu akarudia maneno yale yale na kusema yeye si mnafiki atasema kile kilicho katika nafsi yake kuwa hawawezi kuiachia Zanzibar iwe huru isimamishe Uislam. Ile picha iliyozoeleka Zanzibar na Tanganyika hapo zamani ya kuwaona Karume na Nyerere wote wamevaa kofia za mkono (kofia za Kiislam) leo haipo.
Labda kitu cha kujiuliza leo ni kwa nini Nyerere aliacha kuvaa barghaishia iliyokuwa ikimkaa vyema? Viongozi wa Tanganyika leo wanaingia Zanzibar wamening’iniza misalabamizito ya dhahabu shingoni. Ilikuwa Wazanzibari watanabahi siku nyingi sana. Naomba nihitimishe kwa kunukuu maneno ya Dk. Harith Ghassany katika kitabu chake maarufu kuhusu Zanzibar, ‘’Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru’’:
‘’Inavoonyesha, bado haijawadhihirikia Tanganyika watawala kuwa baada ya miaka 50 kuwa ipo haja kubwa kwa Tanganyika kuubadilisha mtizamo wake juu ya Zanzibar na kuupinduwa msimamo mkongwe wa kuinyanganya na kuinyima Zanzibar haki zake kwa kukhofia kuwa ikiwachiwa huru Zanzibar itakuwa ni tatizo la kimataifa kwa Tanganyika. Au Zanzibar itakuja kutumiliwa au kutumika kama ni mlango wa kuuingiza ubeberu wa Kiarabu na wa Kiislamu Tanganyika na Afrika ya Mashariki na ya Kati. Wako wengi wenye kuhadaika na udogo wa Zanzibar ingawa athari zake wanaziona lakini wameamuwa kuukataa ukweli huo. Anasema Jalaluddin Rumi “Yatizame macho yako. Ni madogo lakini yana uwezo wa kuyaona mambo makubwa.” 

No comments: