Jaji Warioba.
VURUGU zilizoambatana na ngumi kurushwa zimetokea hivi punde katika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam wakati aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba alipokuwa akitoa mada kwenye mdahalo wa kujadili umuhimu wa kuielewa kwa kina Katiba inayopendekezwa kama ilivyopitishwa na Bunge Maalum la Katiba. Vurugu hizo zimezuka baada ya watu waliokuwa na mabango kuvamia ukumbuni hapo na kusababisha baadhi ya watu Kukimbia ovyo.
Huu ndio ulikua Ujumbe wa Warioba huko nyuma baada ya ccm kulazimisha katiba ya vijisenti.Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba aliesema Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba imeondoa mambo manne muhimu yaliyokuwa kiini cha kupata Katiba ya mageuzi. Akiyataja mambo hayo muhimu ambayo ni maadili ya viongozi wa umma, madaraka ya wananchi, mgawanyo wa madaraka na muungano. “Tutakutana mtaani. Tume tutaendelea kutetea rasimu yetu na wao wawaeleze wananchi kwa nini wameondoa maoni yao yaliyokuwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba,” aliongeza kwa ufafanuzi Jaji Warioba.
Na Huko Zanzibar Wasomi watakiwa kuunga mkono harakati za kupinga Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa .
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ametoa wito kwa wasomi wa vyuo vikuu na taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar kuunga mkono harakati za kupinga Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayopendekezwa kwa sababu Katiba hiyo haiwakilishi maoni yaliyotolewa na wananchi Tanzania, na haiinufaishi Zanzibar ndani ya Muungano.
Maalim Seif ametoa wito huo jana hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar, alipokuwa akizungumza kwenye Kongamano lililojumuisha wawakilishi kutoka vyuo vikuu na taasisi za elimu ya Juu 13 zilizopo Zanzibar, lililojadili nafasi ya Wasomi katika kuleta Mabadiliko na Maendeleo Zanzibar.
Amesema mabadiliko katika nchi yoyote huletwa na vijana wakiongozwa na wasomi na kwa namna hiyo hata Zanzibar ambayo asilimia 65 ya wananchi wake ni wenye umri chini ya miaka 35, itaweza kuleta mabadiliko makubwa, iwapo vijana wataaluma watachangamka na kuongoza harakati za kuleta maendeleo ya nchi yao.
Akizungumza katika kongamano hilo ambapo vijana 380 wa taasisi hizo walijiunga na chama cha CUF na kukabidhiwa kadi zao hapo hapo, alisema jambo kubwa lililopo mbele ya Wazanzibari na Watanzania wote kwa sasa ni kuipinga Katiba inayopendekezwa na kuing’oa CCM mwaka 2015.
“Vijana wasomi nyinyi ndio wenye maamuzi kwa nchi yenu, mkiamua mnataka kitu gani ndicho kitakacho kuwa, tushirikiane kupige kampeni ya Hapana kwa Katiba inayopendekezwa yenye maslahi CCM na sio ya wananchi”, amehimiza Maalim Seif.
Katibu Mkuu huyo wa CUF, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema amepata moyo na kufarajika sana kuona vijana wa Zanzibar wana ari kubwa ya kutetea nchi yao, kuliko ilivyo kwa wazee na kila siku zinavyo kwenda, kasi ya vijana kudai Mamlaka ya Zanzibar inazidi kuimarika.
Maalim Seif amesema historia inayonesha harakati zinazosimamiwa na kuongozwa na vijana mara zote hupata mafanikio makubwa na ndio maana hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliongoza vyema TANU hadi kuleta Uhuru wakati huo ambapo alikuwa ni kijana shababi.
Alieleza kuwa mbali na Mwalimu, hata Waziri Mkuu Mstaafu Dk. Salim Ahmed Salim alipewa Ubalozi nchini Misri na marehemu Mzee Karume akiwa na umri wa miaka 22 na alifanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa, mbali na yeye (Maalim Seif) pamoja na vijana wengine ndani ya CCM ambao waliweza kukitikisa chama hicho na kuleta mabadiliko makubwa wakiwa vijana.
Amesema katika kipindi hichi cha kuelekea kwenye kura ya maoni, pamoja na uchaguzi mkuu wa mwakani, vijana hao hawatakiwi kulala na wanahitajika kuungana na wote wanaoendesha kampeni ya Hapana, kama vile UKAWA dhidi ya Katiba inayopendekezwa.
“Kama kweli mnataka Mamlaka kamili ya Zanzibar, tambueni Katiba inayopendekezwa inaitoa roho Zanzibar na kwa kweli ni koti la Muungano linalozidi kuibana Zanzibar, tuungane pamoja kupiga kampeni ya Hapana ili isipite”, amesema.
Katika risala yao iliyosomwa na mwanafunzi, Hafidh Ali Hafidh, wanafunzi hao walisema walifarajika sana baada ya Rais Jakaya Kikwete kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba, lakini baadaye wamefadhaishwa sana na yaliyotokea kwenye Bunge la Katiba kwa kupitisha Katiba ambayo ni kinyume na waliyoyataka wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar.
“Tulipatwa na wasi mkubwa baada ya kuona baadhi ya wenzetu wa Zanzibar waliokubali Serikali tatu Zanzibar, walipofika Dodoma wamebadilika na kufuata Sera ya chama chao”,wamesema.
Wamesema kwamba kitendo walichokifanya wana CCM hao ni uhalifu mkubwa na ni ubaguzi mkubwa ambao hawakubaliani nao na Katiba wanayoipendekeza haifai na wao watakuwa mstari wa mbele kuendesha kampeni ya Hapana.
Hafidh amesema kwa Katiba inayopendekezwa hatma ya Zanzibar imewekwa katika Kuti Kavu na sasa inadhihirika wazi wapo baadhi ya watu wanataka Zanzibar ifutike kabisa katika ramani ya Dunia, jambo ambalo Wazanzibari wazalendo hawatalikubali.
“Wenzetu hawa wamezowea vya kunyonga kamwe vyakuchinja hawaviwezi, tutaitetea Zanzibar kwa vyovyote itakavyo kuwa, tutapita kila kona kuhamasisha vijana waikatae Katiba hiyo inayojali maslahi ya wachache”, wamesema katika risala hiyo.
Miongoni mwa wageni waliokaribishwa kuzungumza katika Kongamano hilo ni Mshauri wa Mikakati Katibu Mkuu wa CUF, Mansour Yussuf Himid ambaye amesema Wazanzibari hawako tayari kuona Zanzibar yao ikitupwa katika debe la taka, na sasa umefika wakati wananchi wawachague viongozi wenye uzalendo, wasio tetereka na ambao si madadali wa Zanzibar.
Naye mjumbe wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, Ismail Jussa Ladu amesema wimbi la mabadiliko linaloikumba Zanzibar na Tanzania nzima hakuna wa kulizuia na wala watu wasipite kuwadanganya wananchi.
Jussa ambaye pia ni Mwakilishi wa CUF wa jimbo la Mji Mkongwe amesema Wazanzibari walio wengi walidhani viongozi wa CCM watakubali kuleta mabadiliko kwa njia za kistaarabu baada ya wananchi kutoa maoni yao na kuratibiwa na Tume ya Mbadiliko ya Katiba, lakini ni kinyume chake kwa vile wameyapiga teke maoni hayo.
Amesema Wazanzibari hawawezi kukubali kuporwa heshima na hadhi ya nchi yao ambayo kwa miaka mingi nyuma imekuwepo, hadi kufikia hatua ya kuwa ni Himaya (Empire), lakini heshima hiyo imkuwa ikifutwa kidogo kidogo hadi sasa kuelekea kuwa Zanzibar ni kama vile Manispaa tu
No comments:
Post a Comment