MIMI ni miongoni mwa Watanzania wa ndani na nje ya nchi waliofuatilia kwa umakini mkubwa tukio la Jumamosi ya Mei 30, mwaka huu, kupitia matangazo ya vituo mbalimbali vya redio na televisheni nchini, vilivyotangaza moja kwa moja tukio la kuanza kwa Safari ya Matumaini ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta uliopo katikati ya Jiji la Arusha. Lilikuwa ni tukio la kihistoria lililovuta watu wengi sana, walioandaliwa kwa umahiri mkubwa na waandaaji wake, ili kuuonyesha umma wa Watanzania pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa ujumla wake, kwamba mwanasiasa huyo, ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Awamu hii ya Nne kabla ya kujiuzulu mwaka 2008 baada ya kuhusishwa na kashfa ya kampuni ya kufua umeme wa dharura, anapendwa na sehemu kubwa ya umma wa Watanzania.
Kwa hakika kabisa, kama kigezo cha mtu kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au kigezo cha CCM kufikia uamuzi wake katika uteuzi wa mgombea wake wa urais, ni umahiri wa kukusanya watu pamoja kutoka kila pembe ya nchi hii, basi Lowassa hana mpinzani miongoni mwa wapinzani wake wa ndani ya chama hicho wanaotangaza nia zao za kuutaka urais wa nchi hii. Binafsi, sina tatizo na wingi wa watu wale na aina ya wanasiasa wa ndani ya chama chake waliomsindikiza Lowassa katika tukio lile la kutangaza nia tu, ambalo mtu mwingine angeweza kuitisha mkutano wa waandishi wa habari na kutoa tamko la nia yake hiyo, sera zake binafsi na vipaumbele vyake.
Bali tatizo langu nililoliona katika tukio lile liko kwa Kingunge Ngombale-Mwiru, na hilo ndilo ninalokusudia kulijadili hapa katika makala haya!
Ndugu zangu, Kingunge Ngombale-Mwiru ni miongoni mwa wanasiasa wakongwe hapa nchini, ambao sisi wengine tuliwafahamu na kuwaamini kwamba siasa zao zinaongozwa na Itikadi ya Ujamaa au Ukomonisti, moja ya itikadi ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliikubali na kuiamini kwamba inaweza kuwaondoa Watanzania kwenye unyonge wao wa kifikra katika kukabiliana na umasikini, ujinga na maradhi.
Lakini hotuba ya Kingunge, aliyoitoa kwa niaba ya Wazee wa CCM katika Safari ya Matumaini hiyo ya Lowassa siku ile ya Jumamosi ya Mei 30, mwaka huu, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, imenifanya siyo tu nimwondoe kwenye kundi la wanasiasa wajamaa wa nchi hii, bali nishindwe kufahamu dhamira hasa aliyonayo mwanasiasa huyo mkongwe kwa chama chake, Tanzania hii na Watanzania kwa ujumla wao.
Kwa kifupi kabisa niseme mapema hapa, kwamba kama Kingunge alidhani hotuba yake ile imemjenga mtu wake Lowassa, atakuwa amejidanganya mwenyewe. Kwa maoni yangu, hotuba ile ya Kingunge amerahisisha sana jukumu la vyama vya siasa nchini vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuing’oa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu!
Ninazo sababu nyingi tu ni kwanini nafikia hitimisho hilo. Hata hivyo, kabla sijaeleza sababu hizo, naomba kwanza niwakumbushe wasomaji wangu kuhusu Kingunge na Lowassa wa mwaka 1995, halafu kwa pamoja tutafakari kama wawili hao ndio hawahawa wa mwaka 2015?
Ndugu zangu, mwaka 1995, Lowassa kwa mara ya kwanza alichukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama chake, CCM, kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza katika mfumo huu wa sasa wa vyama vingi.
Alifanya hivyo kimyakimya, kwa maana ya kutotangaza nia kabla ya kuchukua fomu kama alivyofanya safari hii. Yeye na ‘rafiki’ yake, Rais wa sasa Jakaya Kikwete, wote wakiwa mawaziri katika Serikali ya Mzee Ali Hassan Mwinyi, walipanda ndege moja kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa lengo hilo la kuchukua fomu bila mbwembwe.
Kama kawaida, mchakato wa vikao vikuu vya CCM, wakati huo Kingunge akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu, uliwadia. Lakini kabla ya kuanza kwa vikao hivyo, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alikuwa amekutana mahali fulani na Kingunge jijini Dar es Salaam na kunong’onezana kuhusu uadilifu wa Lowassa, mwanasiasa kijana tu wakati huo ambaye alikuwa ameamua kutaka kuongoza Taifa hili.
Mwalimu alikuwa anamwamini sana Kingunge, ama pengine kutokana na uelewa wake au kutokana na utiifu wake wa ‘ndiyo mzee’.
Kamati Kuu ilipoanza kikao chake na jina la Lowassa kuwasilishwa mbele ya wajumbe wa kikao hicho ili waweze kulijadili, mtu wa kwanza kusimama ndani ya kikao hicho kwa lengo la kuelezea sifa za Lowassa alikuwa ni Kingunge huyu huyu tunayemjua.
Ni Kingunge aliyewaeleza wajumbe wa Kamati Kuu jinsi Lowassa asivyofaa hata kujadiliwa na kikao hicho kutokana na utajiri mkubwa alionao wa fedha na mali nyingi, yakiwemo majumba ya kifahari wakati umri wake na muda wake wa utumishi wa umma, havifanani na utajiri wake huo.
Zipo taarifa ambazo Kingunge hajawahi kuzikanusha tangu wakati huo hadi sasa, za kwamba mwanasiasa huyu ndiye aliyewakumbusha wajumbe wenzake wa Kamati Kuu kufahamu kuwa CCM ni chama cha Wakulima na Wafanyakazi, chama mtetezi wa wanyonge, hivyo hakiwezi kuongozwa na kada wake mwenye utajiri usiokuwa na maelezo ni wapi ameupata.
Ni baada ya Kingunge kutoa hoja hiyo, ndipo Mwalimu alipopigilia msumari wa mwisho juu ya Lowassa kukosa sifa za kuongoza Taifa hili, si kwa kupitia tiketi ya CCM pekee kutokana na misingi yake, bali chama chochote cha siasa au hata kama angekuwa mgombea binafsi, hana sifa za kuwa Rais wa Tanzania.
Rafiki zangu wa karibu na Kingunge na Lowassa mwenyewe, waliwahi kunidokeza kuwa baadaye Lowassa alikuja akapata taarifa kwamba mjumbe aliyemmaliza ndani ya Kamati Kuu alikuwa Kingunge.
Lowassa baada ya kupata taarifa hizo alimtolea uvivu Mzee wake huyo na kumwendea, kabla ya kumtamkia kwamba “wewe Mzee ni mtu mbaya sana, siwezi kuongea na wewe tena katika maisha yangu”.
Inaelezwa kuwa baada ya Kingunge kuambiwa hivyo na Lowassa alikimbilia kwa Mwalimu kulalamika, ndipo Mwalimu akaamua kuingilia kati na kuwapatanisha, lakini kwa kumwelimisha zaidi Lowassa kuwa uamuzi wa kuondoa jina lake haukuwa wa Kingunge kama Kingunge, bali ulikuwa ni uamuzi wa vikao vya chama chake, na uamuzi wa chama lazima uheshimiwe!
Swali ni je, Lowassa huyu tunayeambiwa na Kingunge kwamba ndiye anayefaa kuongoza nchi hii kwa sasa, ni yuleyule wa mwaka 1995 aliyemsulubu ndani ya Kamati au ni mwingine?
Je, Kingunge huyu aliyewakumbusha wajumbe wa Kamati Kuu mwaka 1995 kwamba chama chao hakiwezi kumsimamisha kwenye nafasi ya urais mwanachama wake mwenye utajiri usioelezeka chanzo chake ni huyuhuyu tuliyemsikia wiki iliyopita pale Arusha akimfagilia Lowassa?
Ndugu zangu, sasa naomba mniruhusu nieleze ni kwanini hotuba ile ya Kingunge amerahisisha sana jukumu la vyama vya siasa nchini vinavyounda Ukawa kuing’oa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Katika hotuba yake hiyo ya kumsindikiza Lowassa katika Safari yake ya Matumaini, alizungumza mambo mawili ambayo dhahiri, kwa maoni yangu, yanainyima kabisa CCM sifa ya kuendelea kutawala nchi hii.
Kwanza, alisema nchi hii inakabiliwa na matatizo mengi sana ambayo yamekuwepo kwa miaka yote takriban 50 ya Uhuru. Pili, alisema CCM imemaliza orodha ya makada wake wote walioandaliwa na Chama kuongoza Taifa hili, na kwamba mtu pekee aliyebakia kwa sasa katika orodha hiyo miongoni mwa wote wanaotia nia ya urais ndani ya chama hicho, ni Lowassa.
Kingunge kupitia hotuba yake hiyo ameweka wazi kwamba marais wote waliopita chini ya utawala wa CCM wameshindwa kuyamaliza matatizo hayo, likiwemo tatizo la umasikini unaolikabili Taifa hili pamoja na wananchi wake, hivyo mtu pekee anayeona anaweza kumaliza matatizo hayo ni Lowassa.
Akasema CCM, katika mkakati wake wa kupata viongozi bora, huko nyuma chini ya uongozi wa Mwalimu kiliwapeleka makada wake kwenda kupata mafunzo ya kijeshi katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili waweze kuwa makada walioiva kisiasa, kiakili na kiukakamavu.
Kwa mujibu wa Kingunge, kada ya mwisho iliyobakia katika orodha hiyo ya makada wa CCM waliokuwa wameandaliwa kiuongozi kwa kupelekwa kupata mafunzo hayo ya JWTZ, ni kada ya kina Lowassa, Rais Jakaya Kikwete, Abdulrahman Kinana, Yussuf Makamba na wengine ambao hakuwataja katika mkutano huo uliokuwa umefurika watu wengi sana.
Akasema sababu hiyo ya Lowassa kubakia peke yake ndani ya CCM, katika orodha yote iliyoandaliwa na Mwalimu kuwa viongozi wa Taifa hili, ndiyo iliyomsukuma mwanasiasa huyo mkongwe nchini kumuunga mkono mkono mbunge huyo wa Monduli.
Ikumbukwe kwamba Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, aliwahi kutamka kwamba katika mfumo huu wa sasa wa vyama vingi, Rais wa Tanzania anaweza akatoka chama chochote cha siasa, lakini Rais Bora wa Tanzania lazima atatoka CCM.
Bila shaka Mwalimu alimaanisha kizazi hicho cha kila Lowassa, Kikwete, Kinana, Makamba na wengine ambao Kingunge hakututajia.
Swali ni je, kama Kingunge anasema orodha ya viongozi bora hao waliotamkwa na Mwalimu imehitimishwa na Rais Kikwete, na kwamba aliyebakia ni Lowassa pekee, sasa ndani ya CCM kuna kiongozi bora tena au kuna bora viongozi?
Kwanini Kingunge anawataka Watanzania wamalizie ‘makombo’ yaliyobakia katika hazina hiyo iliyoandaliwa na Mwalimu au na CCM, kwa kumchagua Lowassa kuwa Rais wa Tanzania?
Kama Kingunge anakiri hadharani kwamba Lowassa ndiye pekee aliyebaki katika hazina ya viongozi bora waliotajwa na Mwalimu, basi CCM inapaswa kupisha na kuondoka yenyewe kwa hiyari yake sababu haina tena kiongozi bora au Ukawa na wapenda mabadiliko wanapaswa kukiondoa kwa nguvu ya kura chama hiki!
Hakuna namna yoyote ambavyo Kingunge anaweza kuushawishi umma wa Watanzania ukubaliane na kauli yake hiyo ya kwamba Lowassa ndiye mwenye uwezo wa kumaliza matatizo ya umasikini, rushwa, ufisadi, ubovu wa huduma karibu zote za kijamii na kadhalika, yaliyoshindikana kuondolewa na Mwalimu, Mzee Ali Hasan Mwinyi, Mzee Benjamin Mkapa na sasa Rais Kikwete, akiwa ndani ya CCM hiyo hiyo!
Miaka 54 ya utawala wao, imethibitisha kwamba CCM imeiongezea nchi hii na Watanzania kwa ujumla wao matatizo mengi zaidi, kiasi cha Kingunge kukiri hivyo hadharani.
Nihitimishe makala haya kwa kukumbusha kwamba vya mlevi huliwa na mgema kama walivyokwishakusema wahenga wetu. Fedha zilizotapanywa katika tukio lile la Arusha, wenye nazo hawana uchungu nazo kwa kuwa walizipata kifisadi, sasa zinateketezwa kifisadi pia.
Lowassa huyu anayepigiwa debe na Kingunge kwa sababu ya njaa zake au kwa sababu ya kuvimbiwa na fedha za kifiadi hasafishiki kwa namna yoyote ile.
Aliiahidi dunia nzima nyumbani kwake mjini Dodoma kwamba ataelezea kilichomtokea mwaka 2008 pamoja na kashfa nzima ya Richmond wakati wa kutangaza nia yake hiyo mjini Arusha.
Sasa mbona hatukumsikia akitimiza ahadi yake hiyo wala kugusia mapambano ya rushwa na ufisadi katika vipaumbele vyake?
Angewezaje kuzungumzia mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi katika vipaumbele vyake wakati waliomsindikiza karibu wote pale Arusha wana harufu hiyo ya rushwa na ufisadi?
Dawa ya matatizo yote hayo yanayoikabili nchi hii, si kupeleka anaowataka Kingunge Ikulu, bali ni kuiweka kando CCM na kizazi chote cha Mwalimu, ili kizazi kipya cha sasa kiweze kuwaongoza Watanzania kwa kutumia mfumo wao mwingine mpya kabisa wa kisera na kimikakati.
Kingunge ameufumbua masikio umma wa Watanzania. Ni jukumu lao kuunganisha nguvu zao na wapenda mabadiliko wote nchini, na kazi hiyo ianze sasa endapo CCM imewachoka Watanzania na kutaka kuigeuza Ikulu yao kuwa pango la walanguzi na mafisadi papa na nyangumi!
No comments:
Post a Comment