Tuesday, 5 April 2016

UNAFIKI WA WAJIITAO WAZALENDO WA CCM

Wahafidhina mambo leo wamejipa peke yao haki ya kuwa wazalendo wa nchi yetu. Ufuasi wao kwa chama tawala (CCM) na serikali zake wanaufananisha na uzalendo wa kweli kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na, kwa sisi wengine, kwa nchi tunayoitambua kuwa Zanzibar. Suala la Marekani kusitisha sehemu ya pili ya msaada wake wa kimaendeleo kwa serikali ya Rais John Magufuli limeurejesha tena mjadala huo. Tayari wameanza kampeni yao mitandaoni sio tu kudogosha athari za hatua hiyo ya Marekani, bali pia kuipotosha kwa kuichanganyisha kwenye vumbi la “uzalendo-butu”.

Ukweli ni kuwa ni wajinga tu ndio wasioweza kutafautisha kati ya nchi yao na watawala wanaoitawala nchi yao. Hao ndio wanaoamini kuwa watawala ndio nchi na nchi ndio watawala. Msemo “right or wrong, my country is first” hautaji watawala. Watawala wakikosea na ukiamua kutosimama nao, haimaanishi kuwa wewe unaisaliti nchi yako. Hapana. Ni kinyume chake. Ikiwa watawala wamekosea kwenye kuitendea vyema nchi yako kisha nawe ukasimama nao kuwatetea, wewe utakuwa ndiye MSALITI kwa nchi yako kama walivyo wao, hao watawala.
Hili la Marekani kuzuia awamu ya pili ya msaada wake kupitia kile kinachoitwa Millenium Challenge Cooperation (MCC) kwa Tanzania kutokana na uhuni wa serikali hiyo visiwani Zanzibar na pia sheria kandamizi dhidi ya uhuru wa kujieleza ni kosa la watawala. Kusimama na watawala kwa kujidai eti wewe ni MZALENDO ni UNAFIKI na USALITI kwa nchi yako. Na zaidi unapotumia msemo huo wa “iwe haki iwe batili, nchi yangu daima” ndio kabisa unazidi kupotoka.
Ni sahihi kusimama na utawala wa nchi yako pale tu utawala huo unapokuwa unatenda lililo sahihi na si sahihi kusimama nao ikiwa unachokitenda ni batili. Kwa la Zanzibar na hata hilo la sheria kandamizi ya uhalifu wa mitandaoni, watawala wametenda batili, na mzalendo wa kweli wa nchi yake hawezi kuunga mkono ubatili huo kwa jina la “east or west, my country is right”.
Waliotendewa na wanaoathirika na ubatili huo ni sehemu ya wananchi wenzako wa taifa unaloliita lako. Kwa Zanzibar, ni zaidi ya nusu ya watu wake ambao kila siku wanazidi kuumizwa na ubatili huo ili tu mtawala azidi kujihalalishia ubatili wake.

Kisha angalia KIWANGO CHA UNAFIKI kilichomo ndani ya hao wanaoendesha kampeni ya kulidogosha suala lenyewe: wanakuja na hoja ya UHALALI WA KIMAADILI kwa upande mmoja na ya DIPLOMASIA YA UTEGEMEANO kwa upande mwengine.
Huku kumoja wanaonesha kuwa Marekani yenyewe ina undumilakuwili na ubabe usio na msingi, kwa sababu inasaidia mabilioni ya dola kwa utawala wa Misri ambao ni kandamizi dhidi ya raia na si wa kidemokrasia na pia kwa Israel ambayo inasigina haki za Wapalestina, huku ikisitisha msaada kwa Tanzania kwa jina hilo hilo la kupinga ukosefu wa demokrasia na uwepo wa ukandamizaji.
Kwengine, wanaonesha kuwa kilichoathirika hasa ni sehemu ndogo tu ya mahusiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na taifa la Marekani na kwamba sehemu nyengine kubwa ya mahusiano hayo ipo na itaendelea kuwepo kwa kuwa kila upande unamuhitaji mwenzake. Hakika hata hiyo sehemu yenyewe ndogo wanayosema imeharibika (awamu ya pili ya MCC) wanasema itawaumiza zaidi wawekezaji wa Marekani kuliko wa Tanzania.
Sasa, kama kweli wanaichukulia Marekani kuwa ni hivi ilivyo kwenye hoja ya uhalali wa kimaadili, kwa nini basi wasiikatae moja kwa moja kwenye hoja ya pili ya utegemeano wa kidiplomasia?
Wanapotumia mifano ya Mwalimu Julius Nyerere kuvunja mahusiano na Ujerumani Magharibi na Uingereza kwa msingi wa kutetea mamlaka ya dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sera yake ya nje kuelekea uhuru wa mataifa ya Kiafrika, ndipo wanapovurunda kabisa. Kwa sababu, kama kweli Mwalimu Nyerere alikuwa na uthubutu huo, basi alithubutu KUKATISHA mahusiano yote ya kibalozi na mataifa hayo makubwa na sio kuchuja kuwa tutashirikiana hapa, kisha tutaachana pale.
Ingalitegemewa na Rais John Magufuli naye afanye hivyo hivyo, maana hoja anayojengewa na hawa washauri wake ni kuwa hapa yanayohusika na mamlaka ya taifa lake, madaraka ya urais wake na uhuru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini inavyoonekana hatofanya hivyo, kwa kuwa hoja yenyewe nzima imejengwa juu ya msingi wa unafiki, ukereketwa wa chama tawala na kutokuona mbali.

Neno la mwisho kwa kundi la wahafidhina-mamboleo ambao wananukuu msemo wa kizalendo unaosemekena kutolewa kwanza na Stephen Decatur baada ya chakula cha usiku baina ya mwaka 1816 na 1820: “Our Country! In her intercourse with foreign nations may she always be in the right; but right or wrong, our country!” na kisha kuhusishwa na na Carl Schulz mwaka 1972: “My country, right or wrong; if right, to be kept right; and if wrong, to be set right.” Munakosea. Munayasoma mambo nusu nusu kama ilivyo kawaida ya kundi la vichwa-mchungwa miongoni mwenu. Kuna msemo pia wa Thomas Paine pale mwaka 1791 aliposema: “The duty of the patriot is to protect his country from the government.” 
Munapaswa pia kujizowesha maneno mengine kama yale ya Rais Theodore Roosevelt hiyo hiyo Marekani, aliposema: “Patriotism means to stand by the country. It does not mean to stand by the president or any other public official, save exactly to the degree in which he himself stands by the country.”
Tuliochaguwa kuwaambia kweli watawala kuwa walichokifanya Zanzibar ni uhuni ambao ni hasara kwa taifa letu, tu wazalendo zaidi kwenye hili kuliko

No comments: