Hizi siasa si mchezo wa karata
Na Ahmed Rajab
SAFARI moja Mei 2001, Marehemu Kanali Muammar Qadhafi, kiongozi wa Libya wa wakati huo, alikuwa Uganda kwa ziara ya siku nne. Alipokuwa huko alisema maneno ya kumshajiisha mwenyeji wake Rais Yoweri Museveni asistaafu 2006 kama alivyotakiwa afanye kwa mujibu wa Katiba ya nchi yake ya 1995.
Katiba hiyo ilimruhusu Rais atawale kwa mihula miwili tu na Museveni alikuwa katika muhula wake wa pili. Lakini Qadhafi alimtaka Museveni aihalifu Katiba na aendelee kutawala kwa muda wote autakao.
Qadhafi kwanza aliyasema maneno hayo kama mzaha, huku akitabasamu. Kwa vile yalikuwa maneno aliyokuwa akiyaamini kwa dhati, aliyakariri kwenye mkutano wa kitaifa alipokihutubia chama cha Museveni cha National Resistance Movement (NRM).
Huku utundu ukimwenda kwenye macho yake, Qadhafi alikiambia chama hicho kimruhusu Museveni atawale kwa muda wote ataomudu. Alisema:
“Viongozi wa kimapinduzi hawapaswi kuwa na tarehe za kumalizika, kama vinywaji vya mikebe. Ndugu yangu Museveni alizaliwa mwanamapinduzi. Aendelee [kutawala] kwa muda wote ataokuwa na uwezo nao.”
Museveni alijifanya kama hakumsikia mgeni wake. Si kwamba hakumsikia lakini aliyaachia maneno hayo yaingie sikio moja na yatoke sikio la pili bila ya kuyatia maanani. Alikuwa na yake moyoni ambayo hayakupingana na ushauri wa Qadhafi.
Sasa tunajua kuwa Museveni alikuwa na mizungu yake na tuliitambua Julai 2005 pale Bunge la Uganda lilipopitisha mswada wa kukifuta kifungu cha Katiba chenye kumtaka Rais atawale kwa mihula isiyozidi miwili.
Wakati huo Uganda ilikuwa imegubikwa na mjadala mkubwa kuhusu suala hilo nyeti la mihula ya utawala wa Rais.
Haya maradhi ya viongozi wa Kiafrika kung’ang’ania madaraka ni maradhi sugu yaliyotapakaa kwingi Afrika. Kila sehemu ya bara letu kuna, au kuliwahi kuwako, walau kiongozi mmoja aliyefanya ukaidi na asibanduke madarakani. Wakishakikalia kiti cha urais hujaribu kuganda.
Wa karibuni aliyefanya ukaidi wa kukataa kubanduka, ingawa alishindwa katika uchaguzi, ni Yahya Jammeh wa Gambia. Wiki mbili zilizopita tuliandika makala chini ya kichwa cha maneno: “Kama si leo kesho, Jammeh yuko njiani (Raia Mwema, Toleo la Januari 12, 2017).
Tulijaribu kueleza yaliyojiri Gambia tangu uchaguzi wa Desemba Mosi, 2016. Mwisho wa makala hayo tulijaribu kutabiri yatayotokea na tuliandika:
“Utabiri wetu ni kwamba hata kama majeshi ya Jumuiya ya Uchumi ya Afrika ya Magharibi (Ecowas) hayatotimiza ahadi ya kuingia Banjul na kumng’oa madarakani Jammeh, siku za dikteta huyo zimekwisha.”
Mwisho wa utawala wa Jammeh ulikuwa usiku wa Ijumaa iliyopita alipotangaza kwenye televisheni ya taifa kwamba amekubali kumwachia madaraka Adama Barrow aliyemshinda kwenye uchaguzi wa Desemba, mwaka jana. Matokeo ya uchaguzi huo yalipotangazwa na Alieu Momar Njie, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi, Jammeh alifanya uungwana, akampigia simu Barrow na kumpongeza.
Siku mbili baadaye akabadili msimamo na akakataa kuyaacha madaraka. Alikuwa na njama zake za kuhakikisha kwamba kwa kutumia taasisi za dola, kama mahakama, Tume ya Uchaguzi na jeshi, matokeo hayo yatabatilishwa.
Haikuwa hivyo kama alivyotaka na hivi sasa Yahya Jammeh ni raia wa kawaida anayeanza maisha ya uhamishoni Equatorial Guinea.
Watu wengi wanajiuliza: “Ilikwenda kwendaje hata utawala wa Jammeh ukaweza kuzimwa na ule wa Zanzibar usiweze?”
Swali hilo limenifikisha nilikotaka kwenda. Nako ni kwenye tofauti baina ya Afrika ya Mashariki na Afrika ya Magharibi. Na hususan juu ya misimamo ya viongozi wa kanda hizo mbili kuhusu demokrasia.
Nchini Gambia Jammeh alijaribu kuyafuta matokeo ya uchaguzi uliokuwa halali na uliompa ushindi mpinzani wake. Watawala wa Zanzibar, kwa upande wao, walipong’amua kwamba mgombea urais wa upinzani, Maalim Seif Sharif Hamad, ndiye atayeibuka mshindi waliufuta uchaguzi mzima uliofanywa kihalali, kwa mujibu wa waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa na wa ndani mwa Tanzania.
Hamna shaka yoyote kwamba walioubatilisha uchaguzi wa Zanzibar wa Oktoba 2015 waliuiba uchaguzi huo. Hamna maneno mepesi, na ya mkato, ya kuelezea walichokifanya.
Walichofanya ni kuwapokonya wananchi haki yao ya kumchagua kiongozi wamtakaye. Kitendo cha kuubatilisha uchaguzi, cha kuharamisha kilichokuwa halali, kilikuwa kioja kikubwa.
Maajabu zaidi zilikuwa hatua za wakuu wa serikali ya Muungano za kuuvumilia na kuushadidia huo utundu wa kisiasa uliokuwa umefurutu ada.
Iko siku kimya chao kitawasuta na kuwasumbua. Ubaya wa mambo ni kuwa si kwamba walikaa kimya tu lakini kuna ushahidi kwamba walishiriki katika njama za kuhakikisha ya kuwa vyombo vya dola vinatumika kuwapa ushindi wenzao wa Zanzibar.
Wa mwanzo wa kulaumiwa ni Jakaya Kikwete, ambaye wakati huo alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), chama cha dola. Wa pili ni mrithi wake wa vyeo vyote hivyo viwili, Dkt. John Pombe Magufuli.
Jinsi walivyokuwa wakimzungusha Maalim Seif ni ushahidi wa kwamba hawakuwa na nia ya dhati ya kutenda haki katika sakata hilo.
CCM nayo inabeba lawama, hasa katibu wake mkuu, Abdulrahman Kinana. Yeye pamoja na marais hao wawili waliendelea na shughuli zao kama mshipa haukuwapiga. Ni tofauti kabisa na ya Gambia.
Yaliyojiri Gambia yamedhihirisha msimamo wa kijasiri na uliojaa uadilifu wa viongozi wa Afrika ya Magharibi. Kwa bahati mbaya viongozi wa ukanda wetu wa Afrika ya Mashariki hawakuonyesha kuwa na msimamo kama huo juu ya uchaguzi wa Zanzibar wa Oktoba, 2015.
Madhumuni yangu ni kuichukua mifano ya Gambia na Zanzibar, kuipima na kuilinganisha misimamo ya viongozi wa kanda hizo mbili za Afrika juu ya mifano hiyo miwili.
Kwa kufanya hivyo, leo sitokuwa na budi ila kuwasema marafiki na watu ambao, kwa jumla, ninawaunga mkono kwa mengi. Kweli lazima isemwe hata ikiwa ina uchungu wa shubiri. Haki lazima itetewe hata kama utetezi huo utakufanya ufarakane na wenzako. Ni kheri wakupige pande kuliko kukaa kimya ukawaacha wenye nguvu wawaonee wasio nazo.
Ukweli uliopo ni kwamba katika kanda nzima ya Afrika ya Mashariki hakuna kiongozi aliyechomoza kuwa sauti ya uadilifu, sauti yenye kukemea uvunjwaji wa Katiba, utumiwaji vibaya wa vyombo vya usalama dhidi ya raia wasio na silaha au vitisho dhidi ya raia wenye kugombania haki zao.
Yote hayo yametokea Zanzibar katika vipindi tofauti na hasa katika nyakati za uchaguzi au za baada ya uchaguzi lakini hapajawahi kutokea kiongozi hata mmoja wa Afrika ya Mashariki aliyepaza sauti yake kukemea vitendo kama hivyo. Wapo waliotamka kuhusu Burundi au Sudan Kusini lakini kuhusu Zanzibar ni kama wameitia gundi midomo yao isifunguke.
Pengine tunayoyataraji kutoka kwao ni mambo ambayo hawawezi kuyatekeleza. Hawawezi, kwa mfano, kuwa na msimamo wa uadilifu endapo wao wenyewe makwao wana taksiri za uadilifu. Kuna mambo ambayo viongozi kama Marais Paul Kagame wa Rwanda na Museveni hawastahili kuyafanya lakini wanayafanya. Na yale wanayostahili kuyafanya hawayafanyi.
Hawastahili kuyafanya wayafanyao kwa sababu hawa ni viongozi walioendelea, wasomi walioitalii historia na ni wanaharakati wa zamani wenye kujua lipi jema na lipi ovu katika uendeshaji wa nchi. Na sababu hizohizo ndizo zinazowafanya wastahili kuyafanya wasiyoyafanya.
Nina hakika kwamba ndani ya nyoyo zao wanatambua ya kuwa yaliyotendeka Zanzibar Oktoba 2015 ni uhuni wa kisiasa.
Ninajua pia kuwa wapo watu kadhaa walio karibu na Marais wa Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda, baadhi yao ni mawaziri na wengine ni washauri, ambao unapozungumza nao wanakwambia wanasikitishwa na yaliyotokea Zanzibar baada ya uchaguzi wa Oktoba 2015. Juu ya hayo, si wao wala marais wao walioonyesha ujasiri wa kuyatamka hayo hadharani.
Kinyume na viongozi wa ukanda wetu, viongozi wa Afrika ya Magharibi wameonyesha kuwa na moyo wa kuingilia kati katika nchi jirani pale panapozuka migogoro ya kidemokrasia au ya kikatiba. Hawachelei wala hawachelewi kutamka hadharani pale wanapowaona viongozi wenzao wa Afrika ya Magharibi wanafanya mambo ya kuaibisha.
Tukiiangalia hii kadhia ya Jammeh tu, na kabla ya hapo ya Blaise Compaoré wa Burkina Faso au Laurent Gbagbo wa Côte d’Ivoire, tunaona jinsi viongozi wa eneo hilo walivyokuwa imara kuitetea misingi ya demokrasia.
Halafu kuna taasisi mbili muhimu za kanda hizi mbili za Afrika, Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas) na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Jumuiya hizi zinatazamiwa kuwa ni miongoni mwa matufali makubwa ya kujengea Afrika iliyoungana kisiasa na kiuchumi na kuwa taifa moja.
Hiyo si ndoto; ni tumaini alilonalo kila mwanamajumui wa Kiafrika (pan-Africanist). Lakini tukiziangalia jumuiya hizo mbili tunaona kuwa ni wanyama wawili tofauti. Moja ni simba na nyingine ni kipanya.
Kuhusu kadhia ya Gambia, Jumuiya ya Ecowas imeonyesha kuwa ni simba kwa namna ilivyozicheza karata zake na kuonyesha musuli zake za kisiasa na za kijeshi. Kwa upande mwingine, kuhusu kadhia ya Zanzibar Jumuiya ya Afrika ya Mashariki imeonekana kama kipanya. Sauti yake haikusikika hata kidogo.
Tofauti hiyo inatokana na tofauti ya viongozi wa kisiasa wa jumuiya hizo yaani, tunarejea palepale, viongozi wa nchi wanachama na pia viongozi wa sekretarieti za jumuiya hizo.
Kuna maneno yaliyotamkwa na Jammeh Ijumaa usiku alipokuwa anasalim amri na kukubali kuyaacha madaraka ambayo inafaa watawala wetu nao wayazingatie. Alisema: “Nadhani hapahitajiki hata tone moja la damu limwagike.”
Siku chache kabla ya hapo mkuu wa majeshi ya Gambia, Jenerali Ousman Badjie alisema kwamba hatoyaamrisha majeshi yake yapigane na majeshi ya Ecowas kwa “jambo la upuuzi”, yaani njama ya kisiasa ya Jammeh ya kutaka kuselelea madarakani.Badjie alitambua kwamba angeendelea kumfuata Jammeh basi damu ingemwagika Gambia. Hizi siasa si mchezo wa karata. Ni suala zito lenye kuzihusu roho za watu.
Baruapepe: ahmed@ahmedrajab.com
No comments:
Post a Comment