Monday, 12 October 2020
WITO WA UPIGAJI KURA SIKU MBILI ZANZIBAR
KURA YA MAPEMA : TUZUIE JAHAZI LISIGONGE MWAMBA ?
Na Ally Saleh (LLB Hons)
Utangulizi
Nataasaf kuandika makala hii najua kutakuwa na hoja ya imani yangu ya kisiasa, lakini napenda wananchi wenzangu wajue nimeamua kuandika makala hii kwa nafasi yangu kuwa ni Mzanzibari yaani mwananchi na ambaye natanzwa sana na hali inavyoelekea kuhusiana na suala hili la Kura ya Mapema.
Naandika ili tuwepo ambao tulijaribu kunasihi juu ya utekelezaji wa sheria hii wakati pakiwa na dalili kadhaa wa kadhaa juu ya utata uliozonga suala hilo, lakini pia kukiwa na ishara za mivutano, na kwa hivyo makala hii pengine itakuja kukumbukwa kwa chanya au hasi kutegemea matokeo yatovyokuwa.
Binafsi sioni matokeo mazuri na kama naweza kutoa tathmini yangu mwanzo wa makala hii basi nikuomba Tume ya Uchaguzi Zanzibar na kuinasihi isiendelee na suala hili, na hoja zangu nitaziandika kwenye makala hii.
Kwanza matumizi ya kipengele cha Kura ya Mapema hakikuwekwa kuwa cha lazima, bali ni hiari ya ZEC kukitumia au la. Maana yake sheria ikisema hivyo, chombo kilichopewa kazi kama hiyo, hulazimika kupima wingi wa faida kuliko hasara.
Kwangu naona kuna hasara zaidi, au uwezekano wa hasara kuliko faida itayopatikana. Na ugumu wa faida ni kuwa hapajakuwa na taarifa za uwazi sana, za kujitosheleza, za kufanya kila mtu aamini kuwa uwazi umetosha, na kwa hivyo kuna donge la shaka, halijapatiwa maelezo.
Itoshe tu kuwa upande mzima wa siasa Zanzibar yaani Chama cha ACT Wazalendo hawana imani na matumizi ya kipengele cha Kura ya Mapema, wakati upande wa pili wa Chama cha Mapinduzi ukiwa kimya kabisa, ambapo wengi wetu tunaamini ni kwa kuwa ni wanufaika watarajiwa wa kura hio.
Kama shaka imegawika kiasi hicho, na kipengele si cha lazima kutumika, ila ZEC imehiarishwa kwa kupima faida zaidi na sio sio hasara zaidi, kwa nini ZEC inachagua upande wa kukitekeleza?
Maana kama ni kusimamia vyema uchaguzi ZEC ilipaswa ihakikishe kuwa kila hatua inachukuliwa ili kila mwenye haki ya kupiga kura kwa kufika umri na kuwa na sifa, anapata fursa hio.
Ukiuliza hilo ZEC inasema si wajibu wao. Kama si wajibu wao, wanapataje nguvu ya kufanya makisio ya wapiga kura bila wapiga kura hao wawe ni wale ambao wanasifa zilizowatangulia kupiga kura, na wale wapya wanaopaswa kuingia katika daftari.
Kwa maana nyengine haiingii akilini kuwa wajibu wa ZEC ni kukaa tu kuongojea taasisi ya Zan Id ndio ifanye kazi hiyo, na watu wachache watakaoletwa kwao wakiwa na Zan Id iwe ndio hao hao wanaoandikishwa kupata Kadi za Kupigia kura, bila ya ZEC kujiridhihisha ndio kiwango cha nchi kiidadi.
Uhusiano wa ZEC na taasisi ya Zan Id sio wa hiari, bali ni wa lazima.
Malalamiko kila pembe
Hivi sasa kuna malalamiko makubwa sana kuwa watu wengi, ACT Wazalendo wanakisia kuwa wanafika hata 50,000 hawakuweza kupata Zan Id na kwa hivyo wamekosa kupata Kadi za Kupigia Kura. Hii ni idadi kubwa kudaiwa kwa mujibu wa idadi ya wapiga kura tulionao Zanzibar.
Mtu anaweza kuona hio ni chumvi ya ACT Wazalendo, wasiokwisha malalamiko na ulalalamishi, au kuwa waliokosa ni wananchama wa ACT Wazalando peke yao. Juzi katika mkutano wa Mgombea Urais wa CCM huko Bumbwini, kijana mmoja wa CCM alilamika hadharani kuwa hata vijana wa CCM wamekoseshwa Zan Id na kwa hivyo watakosa kupiga kura.
Ni dhulma kubwa kwa nchi yoyote ile kufanya hila kuzuia raia wake wasipige kura.
Ndio maana watu wengi hawaelewi kuwa ACT Wazalendo haipigii kelele wanachama wake tu, lakini pia ACT inasemea wapenzi wake na hata wananchi kwa jumla kukoseshwa haki ya Zan Id ambao ndio msingi wa kupiga kura kwa sheria ya nchi hii.
Lakini pia kumekuwa na malalamiko kuwa wapiga kura wakongwe, labda chaguzi mbili au tatu nyuma nao hawakupewa vitambulisho vya Zan Id msimu huu, maana lazima tuuite msimu, na kwa maana hiyo nao pia wamekosa fursa ya kupiga kura. Wengi tunajua letu linatiwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kwa hivyo inawezekanaje kumuengua mpiga kura ambaye amepiga chaguzi mbili au tatu na bado hajapoteza sifa….ila sifa ilipotezwa dhidi yake ni ya kukoseshwa Zan Id na sio kuwa amebadilisha uraia, au amekuwa mgonjwa wa akili na kadhalika.
Hili nalo ZEC hawakupaswa kulinyamazia kimya. Jee wametenda haki kuwakosesha kupiga kura watu wa kundi hili kwa sababu tu kuwa taasisi ya Zan Id haikuwapa vitambulisho? ZEC inyamaze tu, sidhani ina mantiki.
Ninachojaribu kuonyesha hapa kuna mambo ambayo yalikuwa ni ya wajibu wa ZEC kuyatekeleza ili kuongeza imani juu ya taasisi yetu hii ambayo ndio ina maana kusimami uchaguzi ili tupate uongozi wetu wa kisiasa.
Kwa maneno machache kabisa ni kuwa haki ya kupiga kura bado haijawa haki hapa kwetu Zanzibar na vyombo vinavyohusika kuona jambo hilo la kisheria na kikatiba linatimizwa ni ZEC na taasisi ya Zan Id kwa pamoja na umoja wao. Na tatizo bila shaka linaanzia hapo
ACT imepigwa sana
Kiukweli ACT haiwezi kusema imekuwa kila siku ikipigwa kwa matukio ya mijaku ya ZEC kwa sababu ACT ni chama kipya katika harakati za Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar. Hii ni mara ya kwanza.
Haikubaliki ACT wakisema, kwa dhana na wanaokataa, kuwa imefanyiwa vitimbi kadhaa kama Wapinzani wakati huo wakiwa Chama cha Wananchi CUF katika matukio ya kiuchaguzi kwa sababu ndio maana sasa wanaogopa hata wakiona ukuti baada ya kuumwa na nyoka.
Na iwe hivyo, kuwa CUF sio ACT, lakini hii mara ya kwanza tu ACT inayoshiriki kikamilifu Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar basi Wazalendo imeumizwa vibaya sana kwa kuenguliwa Wagombea Uwakilishi 10 ( kama namba ipo sawa) na Wagombea Ubunge 5 (kama namba ipo sawa) na Wagombea Udiwani kadhaa.
Wengi walitegemea, na pengine ilikuwa ni sehemu ya stratejia kuu kuu kuwa ACT Wazalendo inune, ivimbe, ifutuke na kujitoa katika Uchaguzi Mkuu au itie watu bararabarani na kuzua fujo na tafrani.
Kumbe hadi leo Serikali ya Zanzibar na CCM imekuwa ikiendelea kuzidiwa maarifa na Upinzani wa Zanzibar kwa kuwa mbele yao kila wakati na kwa kila jambo, na imekuwa ni wazi kuwa watunza amani wakuu wa Visiwa hivi ni Wapinzani na kabisa kabisa ni Maalim Seif Shariff Hamad.
Maana haifikiriki kabisa mkasa kama huu wa kupokwa majimbo 15 ya Uwakilishi na Ubunge kama wangekubali na hali ingekuwa baridi kama wanavyoiona sasa. Sote tunaamini pangezuka vagi na timbiwili ambalo halijawahi kutokea.
Ila ukweli walipofikishwa Wazalando patoshe kabisa. Na ndio maana viongozi wao wanasema jahara kuwa SASA BASI. Na hio ndio hofu yangu tukielekea kwenye Kura ya Mapema, ambayo wapinzani wana shaka nayo lukuki.
Kura ya Mapema
Tunajaua Kura ya Mapema ipo kisheria.
Tunajua Kura ya Mapama kisheria imehiarishwa na si ya lazima.
Tunajua Kura ya Mapema katika mazingira mengine ni ya lazima, lakini katika mazingira yetu haionekani kuwa ya lazima, kwa sababu ya masafa lakini, kwa sababu ya idadi yetu kama nchi, na kubwa zaidi kwa sababu ya kuwa na sheria mbili kinzani za kupiga kura kwa Mamlaka ya Zanzibar na ile ya Mamlaka ya Muungano.
Tuanze na hoja ya masafa. Wanasheria hupenda kusema ukitafsiri sheria ufikirie mtungaji alikuwa na maana gani. Na katika hili inaelekea wazi mtungaji (Baraza la Wawakilishi) alikuwa anajua kabisa kuwa eneo letu la Unguja na Pemba ukitoa Visiwa ni rahisi kufikwa ndani ya muda mdogo. Lakini pia aina yetu ya utawala ni ile ambayo tumeshusha mamlaka na kwa hivyo Watendaji wako kila ngazi. Kwa maana hio haukuonyeshi ulazima wa kupiga Kura ya Mapema kwa sababu watendaji wako karibu na eneo lao la kazi.
Pili, hakuna haja ya kukitumia kifungu hicho cha Kura ya Mapema kwa sababu idadi ya watu wetu ni kidogo sana na fursa ya Tume kuajiri kadri ipendavyo kukabili ukubwa wa suala hilo, ipo. Hapatakuwa na haja au ulazima wa Kura ya Mapema. Na ndio maana mtunga sheria alihiarisha na sio kulazimisha matumizi yake.
Jengine ni kuwepo kwa sheria zinazogongana au zisizokwenda pamoja. Sheria ya Uchaguzi ya Tanzania haina kipengele cha Kura ya Mapema. Sasa imekuwa haiingii kwenye vichwa na mantiki ya watu wengi, iwewe watendaji wanaopiga kura Oktoba 27 ili wawe huru kwa kazi Oktoba 28, basi wao wao tena kulazimika kupiga kura ya Vyombo vya Muungano vya Ubunge na Urais?
Kupiga kura ya Ubunge na Urais inaweza kuchukua dakika 4. Kupiga kura ya Uwakilishi, Urais wa Zanzibar na Udiwani inaweza kuchukua dakika 6 yaani jumla ikawa 10. Kuna sababu gani kura hizo zipigwe siku moja kabla? Na muda gani hapo unaookolewa uzuie mtendaji asipige kura zote mbili Oktoba 28?
Kwani mapema lazima iwe siku moja kabla? Mapema haiwezi kuwa saa 12 ya Okoba 28 ili wapiga kura wa kawaida waanze kupiga kura saa 1 asubuhi?
Ukweli ni kuwa hakuna kuamininiana. Na kwa sababu sheria hailazimishi siku moja kabla ila imehiarisha, mantiki inatuelekeza hakuna sababu ya kukazia sheria hiyo. ZEC haitakuwa haikutimiza wajibu wake ikiwa italazimisha kitu ambacho kimehiarishwa na mantiki ikiwa wazi kuwa kuna faida kutopiga mapema kuliko kupiga mapema.
Jahazi linakabili mwamba
Inawezekana ZEC na Serikali ya Zanzibar wanaona kuwa kauli za ACT Wazalendo kuwa zitawapeleka watu kupiga kura Oktoba 27 zinaonekana ni za kutishia tu, Wazungu husema Calling a bluff. Si ZEC wala SMZ wenye uwezo wa kujua udhati wa kauli hizo.
Au pia kwa kuwa zimetolewa hadharani na kwa nguvu zote, inawezekana tusijue wanachama wa ACT Wazalendo wamehamasika kiasi gani baada ya viongozi kuaminisha kuwa kura ya Okotba 27 haitakuwa na maslahi upande wao.
Upande mwengine SMZ na ZEC wanasimama kuwa taasisi hiyo ni lazima itimize wajibu wake wa kisheria nao ni kusimamia mfumo mzima wa upigaji kura ili kupata wawakilishi wa wananchi na Kura ya Mapema ni moja ya njia ya kupata lengo hilo. Tunakubali.
Lakini pia SMZ ina wajibu mkubwa sana wa kulinda amani na usalama wa nchi hii. Uchaguzi wenyewe tayari una joto kubwa, na joto kidogo la ziada litapeleka chombo chetu kielekea kwenye mwamba.
Binafsi, narudia tena binafsi, kwa sababu haya ni maoni yangu mimi mwenyewe kama Mzanzibari kuwa sioni pataharibika kitu ikiwa ZEC itaacha (set aside) huu utaratibu wa Kura ya Mapema. Hapatakuwa na chochote cha kupoteza. Najua ni ngumu kama taasisi, lakini ni rahisi kufanya maamuzi hayo kama taasisi kwa faida ya nchi.
Naamini itakuwa si udhafu bali ni nguvu na busara iwapo ZEC itauondosha utaratibu huo wa Kura ya Mapema kwa faida na maslahi ya nchi mpaka muda mwengine ambapo utaratibu mzuri na wa ushirikishwaji zaidi utakuwa umewekwa.
Maamuzi ya aina hii yanayoweza kufanywa na ZEC yatabaki katika kumbukumbu daima, na vyenignevyo maamuzi ya kuendelea na Kura ya Mapema yanaweza kubaki pia daima kwa njia ya majuto na masikitiko.
Tusisubiri tuone kitakuwa nini asubuhi ya Oktoba 27 au tuone watathubutu au hawatathubutu, pengine wakati huo tutakuwa tumechelewa sana. Tukisubiri pengine jahazi litakuwa lishafika mwambani na athari yake ni kupasuka vipande vipande. Hatulitaki hilo naamini.
#IwavyoZanzibariMoja
-
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment