Ameandika Advocate: Othman Masoud
KAMARA KUSUPA NA MTAMBO WA KASUMBA JUU YA ZANZIBAR
Nimesoma katika Gazeti la An-nuur la tarehe 11- 17 Novemba, 2016, Makala ya Mwinjilisti Kamara Kusupa isemayo “Kabla ya kudai “Fungu Baraka” Ulizeni nani aliitoa Zanzibar UN? Makala hiyo imeshereheshwa na maneno “tusisahau kila zama na kitabu chake”. Mwandishi wa Makala hiyo ameeleza wazi kuwa nia yake ni kujibu Makala niliyoandika kuhusu umiliki wa Zanzibar wa kisiwa cha Latham (Fungu Mbaraka) na kusambazwa katika mitandao ya kijamii na magazeti mbali mbali.
Nitangulie kueleza kwamba baada ya Makala hiyo kuchapishwa na mitandao na magazeti mbali mbali nilipigiwa simu na Watanzania wengi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na takriban wote walishukuru kwa utafiti wa kina niliofanya na kuiweka bayana historia yetu katika suala la kisiwa hicho. Watanzania hao sio wa kwanza kukiri kwamba walikua hawajui historia hiyo. Hata viongozi wengi wa Serikali wakati nilipowasilisha utafiti huo walikiri kwamba walikuwa hawajui historia hiyo kwa kina kiasi hicho zaidi ya kujua tu kwamba kisiwa hicho kiko upande wa Zanzibar.
Katika Makala yake Mwinjilisti Kusupa ameeleza mengi na kutuhumu mengi ambayo yanaonesha kwamba yeye ameichukulia Makala yangu kuwa ya kisiasa, ya kiuchochezi na kwamba ni ishara ya kupinga Muungano. Fikra zake hizi potofu ndio zilizonifanya niweke kumbukumbu sawa. Aidha, fikra zake hizo potofu zina kila dalili kwamba Mwinjilisti Kusupa ni miongoni mwa mafundi waliobebea wa Mtambo wa Kasumba kuhusu Zanzibar. Unachojua Mtambo huo ni kupotosha kila kitu kuhusu Zanzibar kwa kutumia wino wa usultani na uarabu na kalamu ya Muungano.
CHANZO CHA MAKALA YA FUNGU MBARAKA
KWANZA, Mwinjilisti Kasupa anakiri kuwa haelewi madhumuni ya Makala yangu lakini badala ya kuuliza kama walivyofanya waungwana wengine walionipigia simu kutoka Kigoma, Simiyu, Iringa, Shinyanga, Arusha na Dar yeye ameamua kuchukua wino wake wa usultani na kalamu ya Muungano kuchakata Kasumba.
Napenda kumfahamisha kwa ufupi historia na madhumuni ya Makala hiyo. Mwishoni mwa mwaka 2011, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Zanzibar ilitoa leseni ya uvuvi kwa Kampuni ya Open Water Adventures LTD kwa ajili ya uvuvi wa “sports fishing” katika maeneo ya Zanzibar isipokuwa katika maeneo ya hifadhi ya bahari. Miongoni mwa maeneo ambayo Kampuni hiyo ilikusudia kuvua ni eneo la kisiwa cha Latham (Fungu Mbaraka). Kampuni hiyo waliomba kuthibitishiwa na Idara ya Uvuvi Zanzibar kuwa eneo la Latham sio sehemu ya hifadhi ya bahari. Idara ya Uvuvi iliwajibu kwa barua yao DFD/2124/II/Vol I ya tarehe 22 Sptemba, 2011 kwamba eneo la kisiwa cha Latham sio eneo la hifadhi ya bahari.
Kampuni hiyo ilipeleka wateja wake ambao ni raia wa nchi mbali mbali ikiwemo Marekani na Afrika Kusini kuvua katika kisiwa cha Latham tarehe 16 Novemba, 2011. Wakiwa katika kazi hiyo walikamatwa na watu ambao baadaye walikuja kufahamika kuwa ni maofisa wa Uvuvi wa Tanzania Bara na wakapelekwa Dar es salaam na kuwekwa ndani. Kampuni hiyo pamoja na kutaka ufafanuzi wa uhalali wa kitendo hicho kutoka Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ya Tanzania Bara lakini walijibiwa kuwa Wizara hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kutoa leseni za uvuvi na kwamba kisiwa cha Latham pia kimo katika mamlaka yao.
Baada ya tukio hilo ndipo hatua za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwasiliana na Serikali ya Muungano juu ya kadhia hiyo zilipochukuliwa. Ni kwa kupitia kadhia hiyo ndipo Serikali ya Muungano ilipoamsha rasmi mzozo wa umiliki wa kisiwa cha Latham kwani Waziri Mkuu Mizengo Pinda alieleza wazi kwamba kisiwa hicho kwa mujibu wa kumbukumbu za SMT ni cha Tanzania Bara.
Mzozo mwengine wa wazi baina ya pande mbili za Muungano kuhusiana na kisiwa hicho kisiwa ni katika suala la utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia. Ni wazi kwamba suala hili hasa ndio lilopelekea madai ya ajabu ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuhusiana na kisiwa cha Latham.
Kwa mujibu wa kifungu cha 2 cha Sheria ya Petroli iliyotungwa na Bunge ya mwaka 2015, mafuta na gesi asilia yatasimamiwa na vyombo vya SMT kwa upande wa Tanzania Bara na vyombo na taasisi za SMZ kwa upande wa Zanzibar. Na kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria hiyo mafuta na gesi vitachimbwa katika maeneo ya kijiografia ya Zanzibar na Tanzania Bara. Hata hivyo si sheria hiyo wala nyengine yoyote iliyofafanua maeneo ya kijiografia ya pande mbili za Muungano.
Kisiwa cha Latham mbali ya kuwa kituo kilichotumika kupima eneo la ukanda huru wa kiuchumi wa bahari kuu (baseline point) lakini kwa ugawaji wa sasa wa vitalu kinaviweka vitalu namba 7, 8 na kitalu cha Latham Kimbiji katika utatanishi mkubwa wa umiliki kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya Petroli. Hivyo kupatiwa ufumbuzi wa kitaalamu suala la umiliki wa kisiwa cha Latham sio suala la kasumba ya Kusupa, kwamba ni siasa, bali ni lazima kwa mujibu wa matakwa ya sheria zetu.
Jambo la pili muhimu naomba kumrejesha Mwinjilisti Kusupa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Tokea katika Mkataba wa Muungano suala la kuwepo pande mbili za Muungano na kuwepo Serikali mbili na kuwepo mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano ndio umekuwa mhimili wa Muungano. Ibara ya 4 ya Katiba ya sasa ya Muungano imeliweka jambo hilo bayana sana. Kama unatambua kuwepo mamlaka Zanzibar inayoongozwa na Serikali yenye mihimili yote mitatu ya dola, itawezekanaje usibainishe mipaka ya kijiografia ya eneo hilo la kiutawala. Ni kwa mantiki hiyo ndio mana hata Jimbo la uchaguzi, Kata, Shehia, Wilaya na Mkoa yote inayo mipaka ya kijiografia (territorial or geographical boundaries). Nashindwa kupima nadhari za Mwinjilisti Kusupa anapoona ni dhambi kueleza mipaka ya Zanzibar na anaposema kwamba kusema kwamba kisiwa cha Latham ni cha Zanzibar ni dalili ya kutaka kukitoa kisiwa hicho mikononi mwa Tanzania ili wapewe wageni wafanye wanavyopenda na kuidhuru Tanzania.
Jambo la tatu la kumtanabahisha Mwinjilisti Kusupa ni kuwa kwa mujibu wa Sheria za sehemu zote mbili za Muungano, mtu aliyefanya kosa Zanzibar iwe la jinai au madai hawezi kushtakiwa Tanzania Bara na kinyume chake. Hivyo, kwa mfano mtu akitenda kosa la jinai katika kisiwa cha Latham hoja ya mwanzo ni kuwa ashtakiwe katika Mahkama za upande upi na mamlaka ipi ina uwezo wa kumshtaki, DPP wa Zanzibar au wa Tanzania Bara. Hoja hii ipo pia
kwa mamlaka za Mahkama na za kiserikali kwa mambo ambayo si ya Muungano.
Ni vyema akina Kusupa wakaelewa kwamba hoja ya umiliki sio hoja ya kisiasa wala ya kizayuni bali ya kikatiba kwa mujibu wa Katiba zetu za Tanzania na ya kisheria kwa mujibu wa sheria zetu za Tanzania. Aidha, hoja ya umiliki wa Latham si ya akina Othman bali ni ya Jahmhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali ya Zanzibar mara kadhaa imetoa tamko la wazi na bayana ndani ya Baraza la Wawakilishi ambalo limekuwa likidai ufafanuzi wa umiliki wa kisiwa hicho. Katika maelezo yake, Serikali imekuwa siku zote ikiwatoa hofu Wazanzibari kuwa kisiwa hicho ni cha Zanzibar na hakuna anayeweza kukidai. Matamko ya karibuni yametolewa na waliopo sasa madarakani kupitia Bwana Mohamed Aboud na Bwana Issa Haji Ussi Gavu wote wametoa kauli hizo katika Baraza la Wawakilishi. Wote hao wawili ni mawaziri katika utawala uliopo Zanzibar na ambao naamini akina Kusupa hawana mashaka nao juu ya utii wao kwa TANZANIA. Mbali ya matamko hayo ndani ya Baraza la Wawakilishi, hivi karibuni, ndani ya Bunge la Muungano Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais Bwana Januari Makamba alijibu suali kuhusu kisiwa cha Latham. Kituko alichofanya ni kuwa alisema kuwa kisiwa hicho ni cha Muungano wakati aliulizwa kuwa jee kisiwa hicho kipo upande gani wa Muungano. Naamini kama angeulizwa kuhusu kisiwa cha Mafia asingesema kuwa kisiwa hicho ni cha Muungano. Waswahili wanasema “mwenye macho haambiwi tazama”. Kwa wenye macho wanaona bila kuambiwa kuwa kuna mgogoro baina ya pande mbili za Muungano. Lakini kama kawaida Tanzania ya zama za kitabu cha akina Kusupa kila kitu kinafichwa, kinapotoshwa na kupambwa kwa siasa za dahri na zama. Ni baada ya majibu hayo ndipo nilipoamua kuwaeleza ukweli Watanzania juu ya suala hilo. Hivyo, ni dhahiri mtambo wa kasumba wa akina Kusupa haufurahii na ukweli huo na wanatafuta kila njia kuzalisha kasumba za kupotosha ukweli.
HOJA YA MIKATABA YA ZAMANI NA MIPAKA YA WAKOLONI
Mwinjilisti Kusupa amepotosha kiasi cha kupotosha au niseme amejipotosha mno kuhusu suala la mikataba ya kikoloni na mipaka ya leo ya nchi za Afrika. Kwa fikra zake kwamba mikataba ya kikoloni iliyoigawa Afrika haina nafasi sasa hivi. Na haifai kutumika kujenga hoja. Ameenda mbali zaidi kwa kusema kuwa akina Othman hawana tofauti na wenye chachu ya kizayuni wanaotumia maandiko ya kale kuhalalisha anayofanya sasa hivi. Nasema amejipotosha kwa vile katika Makala hiyo anakubaliana na Tamko la OAU la 1963 kuhalalisha mipaka ya kikoloni. Suala ni kuwa jee Mwinjilisti Kusupa anajua kuwa mipaka ya kikoloni ilitumia maandiko ya kale zaidi kuliko 1898 wakati Zanzibar ilipotangaza rasmi kuwa Latham ni ya kwake? Aidha, Kusupa anajenga dhana kwamba ni mipaka ya Zanzibar tu ndiyo iliyoundwa na Sultani lakini ile ya Tanganyika ni ya kizalendo na imeakisi matakwa ya Watanganyika wenyewe.
Labda nimtanabahishe Mwinjilisti Kasupa tu kwamba kwanza mipaka ya eneo la Afrika Mashariki ambalo baadaye lilikuja kuwa Tanganyika kama nchi moja, ilianza hasa na utashi wa mtu mmoja, Carl Peters kinyume hata na matakwa ya viongozi wa nchi yake ya Ujerumani. Wanahistoria wanaelewa vizuri kwamba Kansela wa Ujerumani wa wakati huo, Bwana Otto von Bismark ambaye alikuwa na ushawishi mkubwa kwa mfalme wao William II hakuwa na hamu na sera ya makoloni Afrika. Ni baada ya ushawishi wa Carl Peters na wenzake na kuonesha kwa vitendo kuwa tayari wanazo sehemu wanazoweza kuzifanya makoloni Afrika ndipo ramani ya iliyokuja kuwa Tanganyika ilipoanza kuchorwa kuanzia tarehe 3 March, 1885 wakati Emperor William wa Ujerumani alipokubali kuyatambua maeneo yaliyopatikana kwa mikataba ya ghilba ya Carl Peters na machifu wenyeji. Maeneo yaliyotambuliwa yalikuwa manne tu nayo ni Usagara, Naguru, Useghu na Ukami [inawezekana maeneo hayo sasa yamebadili majina]. Kutambuliwa huko kulipata nguvu baada ya Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza Bwana Glanville, alipomueleza Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Count Herbert von Bismarck kwamba Uingereza inatambua maeneo hayo ya Ujerumani katika bara ya Afrika Mashariki. Wakati Tanganyika inaanza kuchorwa na Wajerumani Zanzibar tayari ilikuwa na mikataba ya kibalozi na Marekani, Uingereza, Italy, Ufaransa na Ubelgiji. Takriban nchi zote hizo zilikuwa na Balozi zao Zanzibar. Marekani kwa mfano chini ya Balozi wao ambaye alikuwa pia mfanyabiashara Bwana Richard Waters ilikuwa ikifanya biashara kubwa na Zanzibar wakati huo.
Ni baada ya hatua hiyo ya Mfalme William na hatua ya Uingereza kutambua mbegu iliyozaa Tanganyika ndipo Balozi wa Ujerumani aliyekuwepo Zanzibar Dr Gerhard Rohlfs alipomtaka Sultani naye atambue rasmi maeneo ya Ujerumani ya Bara. Sultani alipokataa ndipo mwezi wa August, 1885 kikosi cha Wanamaji cha Ujerumani kilipopelekwa Zanzibar kumtishia Sultani kuitambua mipaka ya Ujerumani Bara au watatumia nguvu. Hatua hii iliifanya Uingereza iingilie kati na kumshawishi Sultani akubali mipaka hiyo. [ingawa kumbukumbu zinaonesha Ujerumani na Uingereza shauri lao lilikua moja]. Tarehe 14 August, 1885 Sultani alikubali mipaka hiyo na Tume ya kuainisha mipaka ikaundwa na kuanza kazi Oktoba mwaka huo wa 1885. Hatimaye, baada ya Tume ya Mipaka kumaliza kazi ilipelekea Mkataba wa 1886 baina ya Uingereza na Ujerumani kuhusiana na kuainisha mipaka ya Ujerumani Bara na Mipaka ya Zanzibar. Ujerumani ilichukua takriban eneo lote ambalo leo ndio Tanganyika na Zanzibar ikabakishwa na ukanda wa pwani wa Bara wa maili 10 tokea Mto Ruvuma hadi Mto Tana.
Sina hakika kama Mwinjilisti Kusupa itapotokea mzozo wa eneo la Tanganyika ataukubali mkataba huo wa 1886 au kwake utakuwa ni uzayuni kutumia maandiko ya kale kuhalalisha haki yako ya sasa.
Baada ya mkataba huo wa 1886, Tanganyika ilikuja kuwekwa bayana zaidi na mkataba wa Heligoland- Zanzibar wa July, 1890. Mkataba huu pia ndio uliweka bayana zaidi mipaka ya Kenya na Uganda za leo.
Ukifatilia harakati na matokeo yaliyopelekea mkataba wa Heligoland ni wazi kuwa ulizingatia zaidi maslahi ya Wajerumani na Waingereza sio ya makabila kadhaa ambayo kwa wakati huo yalikuwa bado hayajawa nchi moja.
Ni baada ya kuondoka Kansela Otto von Bismark madarakani March, 1890 ndipo Waingereza walipoingia hofu kuwa Mfalme William atafuata ushawishi wa wafanyabiashara na wanasiasa wanaopenda Ujerumani iwe na sehemu kubwa ya makoloni Afrika. Ushahidi wa hofu hii ya wazi ya Waingereza ilioneshwa na jarida la TIMES la March 20, 1890 ambapo lilieleza kuwa Waingereza wengi wanapenda iwepo suluhu ya mipaka ya makoloni Afrika baina ya Uingereza na Ujerumani ili kuepusha ugomvi baina ya Uingereza na Ujerumani utaotokana na uchu wa makoloni wa Ujerumani baada ya Bismark kuondoka. Ni kutokana na hilo ndipo Sir Percy Anderson wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza alipotakiwa aende Berlin, Ujerumani kuanzisha mazungumzo na Serikali ya Kansela Leo von Caprivi aliyeshika madaraka baada ya Bismark. Kabla ya kwenda Berlin, Anderson alionana na Balozi wa Ujerumani nchini Uingereza Count Hatzfeldt na hatimaye akaenda Ujerumani May 3, 1890 na kuanza mazungumzo tarehe 5 May, 1890 na Dr. Krauel wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Ujerumani.
Mazungumzo hayo yalizaa majadiliano ya miezi 2 ambapo kila upande ukieleza kile inachotaka. Ujerumani ikikubali kuitoa sehemu ya ziwa Nyanza upande wa kaskazini lakini ikishikilia nayo kuachiwa ukanda wa Pwani uliopo chini ya Zanzibar na kisiwa cha Heligoland. Mjadala mkali katika Bunge la Uingereza wa May 22, 1890 unatoa ufafanuzi wa kutosha juu ya maslahi ya wakoloni kwa mipaka waliyochora. Hatimaye mkataba wa Heligoland- Zanzibar ulitiwa saini July 1, 1890 lakini ulihitaji kuidhinishwa na Mabunge ya Uingereza na Ujerumani. Mkataba huo ndio uliokuja kuiondoa Ruvuma, Mtwara, Lindi, Mafia, Dar es salam na Tanga na sehemu ya mwambao wa pwani wa Tanganyika kutoka mikononi mwa Zanzibar. Mjadala mkali katika Bunge la Uingereza wakati wa kujadili Mswada wa Sheria ya Kuiondoa Heligoland Uingereza (Heligoland Cessation Bill) uliofanyika July 3, 1890 na hotuba ya Kansela Leo von Caprivi katika Bunge la Ujerumani la Reichstag tarehe 28 Julai, 1890 ni ushahidi wa kutosha kwamba Afrika Mashariki iligaiwa kwa kuzingatia maslahi ya kiuchumi na kimkakati ya Wakoloni. Aidha, ni ushahidi kuwa mipaka ya Tanganyika na Zanzibar haikuwekwa na Sultani bali na Waingereza na Wajerumani. Ni ushahidi pia kwamba mipaka ya leo ni ajali ya kihistoria ambayo tumekuja kuikubali kama ilivyo na kuilinda kwa Katiba, Sheria na nguvu zetu za kijeshi kama tulivyofanya kule Kagera. Ni vyema pia akina Kusupa wasome kwa makini kitabu cha Map of Africa by Treaty kilichoandikwa na Sir Edward Hertslet ambacho ndicho kinachotumiwa kama rejea ya kuthibitisha mipaka ya Afrika katika Mahkama za kimataifa na Mabaraza ya Usuluhishi ya mipaka. Sina hakika kama Kusupa atawaita wanaotumia kitabu hicho ni Wazayuni kama anavyowaita akina Othman.
Jambo la mwisho kuhusu mikataba ya zamani na mipaka ya Afrika na dunia napenda kumtanabahisha Kusupa kuwa hata Sheria za kimataifa zimetambua Treaty law kama msingi mkuu wa kuamua mipaka baina ya nchi mbali mbali duniani. Na katika mikataba inayotambulika na Sheria za kimataifa ile mikataba ya zamani inapewa uzito wa aina ya pekee. Aidha, sheria za kimataifa zinatambua mipaka iliyowekwa wakati wa ukoloni kuwa ni msingi mkubwa wa uhalali wa mipaka ya sasa. Chini ya Kanuni ya Uti Possidetis, hata Mahkama ya Kimataifa ya ICJ mara kadhaa imeipa uhalali mipaka ya kikoloni katika kuamua migogoro ya mipaka Afrika, Amerika ya Kusini na Asia.
Kwa hili la Latham lipo jambo la ziada la kuzingatia. Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1963 ilieleza wazi kwamba mipaka ya Dola ya Zanzibar ni visiwa vya Unguja, Pemba na Latham. Katiba hiyo ndiyo iliyotumika na Zanzibar kuomba na kukubaliwa uanachama wa Umoja wa Mataifa. Aidha, wakati huo Tanganyika ilishatangulia kupata uhuru kwa angalau miaka miwili. Haikutokea hata siku moja Tanganyika kulalamika rasmi au kwa njia isiyo rasmi kwamba mipaka hiyo ya Zanzibar inaingilia Tanganyika.
Akina Kasupa wanapojaribu kutuuzia kasumba kwamba mipaka hiyo ni ya Sultani kwa vile tu inahusu Zanzibar kama kwamba ile ya Tanganyika na nchi nyengine za Afrika ni mipaka ya kizalendo ni kudhihirisha kwamba wanadhani Watanzania na hasa Wazanzibari hawawezi kupambanua ajali hiyo ya historia ambayo tumeihalalisha na madam tumeikubali na kuihalalisha ni lazima tuilinde kama tulivyoilinda Kagera bila kujali udugu wa Waganda na Watanzania wa Kagera. Aidha, ajali hiyo ya kihistoria kama tulivyobainisha imetambuliwa na sheria na Mahkama za kimataifa na pia Umoja wa Nchi Huru za Afrika na Tanzania ndio iliyokuwa kinara wa azimio hilo la OAU la kutambua mipaka ya kikoloni.
HOJA YA SULTANI NA UMILIKI WA ZANZIBAR
Kusupa anajaribu kutuuzia kasumba nyengine ya ovyo zaidi anaposema kwamba Latham ni ya Sultani sio ya Wazanzibari na hivyo hawawezi kuidai. Nasema hii ni kasumba ya ovyo kwa vile kwa ushahidi nilioeleza hapo juu Tanganyika sio tu kwamba ni ya Wajerumani lakini kwa ajali hiyo hiyo ya historia ilikuwa ya Zanzibar na ikachukuliwa kwa hila na nguvu na Wajerumani. Hivi kuna mtu yeyote wa Tanganyika au Mtanzania wa leo aliyehusika kuweka mipaka ya Tanganyika? Kama ni hivyo, msingi gani uliotumiwa na Tanzania kupigania Kagera? Na ni msingi gani unaotumika na Tanzania leo kudai eneo la ziwa Nyasa? Na ni msingi upi unaotumika leo na nchi za Afrika kuweka pasi za kusafiria ndani ya Afrika na vikwazo vya viza na vyenginevyo. Kusupa atueleze kama uzalendo, uafrika na udugu ndio chanzo cha umoja wa Afrika kipi kinachoipa Tanzania kuhofia Kenya kuhusu ardhi na kufanya kazi bila kizuizi. Ni vyema tukawa wakweli na kuzitendea haki taaluma na nadhari zetu. Ni vyema pia kuwa na heshima kwa wenzetu kwa kutowauzia kasumba za ajabu za uzalendo pori kiasi hichi.
Jambo jengine nnaloomba kuwatanabahisha akina Kusupa ni kuwa asiwatishie nyau Wazanzibar kwa Sultani kama kwamba ni jinni linaloishi kuimeza Zanzibar wakati wowote ule kutapokuwa na mabadiliko katika siasa za Muungano. Anachojaribu kueleza ni kasumba iliyochakaa mno.
Kwanza ni ukweli wa historia ambao akina Kusupa na hata wale walionunua na kutandika kasumba za akina Kusupa katika ofisi zao za mamlaka ya siasa Zanzibar kwamba baada ya suluhu ya Governor Canning ya 1860, Zanzibar na Kwanza ni ukweli wa historia ambao akina Kusupa na hata wale walionunua na kutandika kasumba za akina Kusupa katika ofisi zao za mamlaka ya siasa Zanzibar kwamba baada ya suluhu ya Governor Canning ya 1860, Zanzibar na Oman zilitengana rasmi kiutawala. Sultani wa Zanzibar hakuwa tena na mamlaka Oman na wala Sultani wa Oman hakuwa tena na mamlaka Zanzibar. Kilichobaki ilikuwa historia ya udugu sawa na vile Mmasai, Mjaluo, Mngoni, Mhindi, Muarabu au Mzungu wa Tanzania anavyojua kuwa asili yake ni pahala fulani na inawezekana ana udugu na watu wa pahala fulani. Ndio maana Sultani alipopinduliwa hakwenda Oman bali alikimbilia Uingereza. Hivyo kudai leo Sultani atarudi Zanzibar ni sawa na hadithi ya alfu lela ulela. Kwa sababu Sultani wa Zanzibar hayupo kimamlaka wala kiaila. Sultan wa leo wa Oman siye aliyekuwa Sultani wa Zanzibar na hivyo hana mamlaka ya kudai chochote Zanzibar wala hana sababu ya kufanya hivyo.
Pili, hata Sultani alipokuwepo Zanzibar ni ukweli wa kihistoria kwamba baada ya Mkataba wa kimahamia (Protectorate Treaty) wa June, 1890, Sultani alibaki pambo tu katika utawala. Dola na Serikali iliendeshwa na Uingereza. Waingereza walimleta Gerald Portal Zanzibar tarehe 6 Agosti, 1891, ambaye kwanza alipelekwa Misri kujifunza mila za kiarabu, ili kuja kuanzisha rasmi Serikali. Sultani mwenyewe akawekwa katika orodha ya kulipwa mshahara tu (Civil List). Waingereza ndio walioanzisha Mahkama za Kadhi 1897, Kamisheni ya Wakf mwaka 1907 na ndio waliotangaza kuwa Sheria za Kiislamu ndio zitakuwa Sheria mama za Zanzibar mwaka 1897. Mfumo wa Serikali ulioasisiwa na Gerald Portal ulibadilishwa mwaka 1906 baada ya Bwana Edward Clarke kuletwa Zanzibar akitokea London kuja kuangalia mfumo wa Serikali Zanzibar na namna ya kuuboresha. Mapendekezo ya Edward Clarke yaliidhinishwa na mfumo mpya wa Serikali uliasisiwa Julai 1, 1906. Chini ya mfumo huo Brigadier-General Rakes aliteuliwa First Minister, Bwana Peter Grain ambaye alikuwa Hakimu Mkazi aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza wa Zanzibar na Bwana C.E. Akers aliteuliwa kuwa Waziri wa kwanza wa fedha na biashara.
Nimetoa maelezo haya kwa kina ili akina Kusupa waelewe kwamba Serikali wala dola haikuendeshwa na Sultani. Mambo yote yalipangwa London, kuamuliwa London na kutekelezwa Zanzibar bila hata baadhi ya wakati Sultani kushauriwa. Ndio mana katika Serikali mpya ya 1906 hamkuwa na muarabu hata mmoja. Ushahidi mkubwa kuliko wote kwamba Zanzibar pamoja na Sultani mwenyewe ikiendeshwa na Uingereza ni pale mwaka 1913 pamoja na kuwepo mkataba wa umahamiya wa June, 1890 lakini Uingereza waliamua kuiendesha Zanzibar chini ya Ofisi ya Makoloni sawa na koloni jengine badala ya chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ambapo ndipo ilipostahiki. Aidha, mwaka 1962 Uingereza ilimteua Bw. Robertson kuandaa taarifa ya utaratibu wa kuiendesha sehemu ya pwani ya Kenya ambayo Uingereza ilikuwa imeikodi kutoka kwa Sultani tokea mwaka 1895. Mapendekezo yake ndiyo yaliyopelekea sehemu hiyo kurejeshwa kuwa sehemu ya Kenya kuanzia tarehe 5 Oktoba 1963, bila ya shaka kwa maslahi ya kiuchumi ya Uingereza.
Ni kutokana na ushahidi huo wa dhahiri ndipo kasumba za akina Kusupa zinapowasuta. Kama Sultani ndiye aliyekuwa na mamlaka Zanzibar ni vipi Uingereza ingetamalaki katika kila mamlaka ya Zanzibar.
HOJA YA ZANZIBAR KUTOKA KATIKA UN
Mwinjilisti Kusupa analeta hoja ya kituko kwamba eti Zanzibar ilitolewa katika UN kwa sababu Sultani wa Zanzibar angekuwa kikwazo kwa uhuru wa kweli wa Afrika. Hivi ni Sultani yupi huyo? Huyu ambaye tumemuonesha kwa ushahidi wa hapo juu kama hakuwa na mamlaka ya mambo yake mwenyewe na ya nchi yake awe na mamlaka ya kuzuia uhuru wa Afrika kiasi cha kuogopwa na mataifa makubwa? Huu ni uongo hadhir shahir ambao akina Kasupa wamekuwa wakiwauzia wale waliowatawala akili zao.
Sababu ya Muungano na hatimaye Zanzibar kutoka katika UN zimeelezwa kwa ufasaha na kwa ushahidi katika taarifa ya Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) ya mwaka 1967 ambayo iliondolewa katika kiwango cha taarifa ya Siri ya kitaifa mwaka 2007.
Taarifa hiyo imeeleza wazi kwamba kiini cha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni hofu ya mataifa makubwa juu ushawishi wa nchi za mashariki hasa China na Ujerumani Mashariki walizokuwa nao kwa Zanzibar. Aidha, imetaja wazi kuwa urafiki wa karibu sana wa akina Abdulrahman Babu, Ali Sultan Issa na hata Hassan Nassor Moyo na mataifa hayo ulileta uwezekano mkubwa wa nchi hizo kuitumia Zanzibar kueneza ukomunisti Afrika Mashariki na kuigeuza Zanzibar kuwa Cuba ya Afrika Mashariki. Imefafanua pia mbinu zilizotumika kumlazimisha Rais wa Zanzibar hayati Mzee Abeid Amani Karume kuingia katika mkataba wa Muungano. Napenda nimuhakikishie akina Kusupa na mafundi wenzake wa mtambo wa Kasumba kwamba Wazanzibari wengi hasa wa kizazi cha vijana wanaelewa vizuri historia hiyo ya Muungano na Zanzibar kutolewa katika UN. Weledi hawapati shida. Labda kimya chao kinawafanya akina Kusupa kuamini kwamba Wazanzibari wanaweza kuuziwa kasumba hiyo na wakalewa nayo mpaka milele. Nikubaliane na maneno ya Kusupa hapa kwamba KILA ZAMA NA KITABU CHAKE. Sasa ni zama za ukweli kujulikana. Lakini sio lazim kila ukweli utasemwa hadharani. Tabaan, kwa zama za sasa ukiuchokonoa ukataka usemwe hadharani utasemwa. Jitayarishe tu na ushujaa wa kuusikiliza.
HOJA YA ZANZIBAR NA MAADUI WA MUUNGANO
Mwinjilisti Kusupa ameonyesha dhahiri kuwa yupo jikoni katika mtambo wao wa kasumba. Anahusisha hoja ya umiliki wa Zanzibar wa Latham na maadui wa Muungano. Hii ni nyimbo ya kale na bahati mbaya pamoja na kuwa ya kale haikuingia katika “Zilipendwa” na wala haikuingia katika ule msemo wa zamani wa “Old is Gold”.
Moja kati ya nguzo za udhaifu wa Muungano ni akina Kusupa kugombana na ukweli na kuufanya Muungano kuwa roho yake ni siasa tena siasa za kale ambapo wananchi waliamini na kufata kila lisemwalo na viongozi wa siasa. Siasa ya wakati ambapo maoni ya umma yalifata taasisi za siasa. Zama hizi kitovu cha maoni ya watu na sera za umma sio tena siasa wala taasisi za siasa. Kitovu ni mawasiliano kwa vile watu wanaelewa mengi, taarifa zinasambazwa kwa haraka kuliko kasi ya siasa na taasisi zake. Wanaomiliki maoni ya watu na sera za umma sasa hivi ni wanaomiliki mawasiliano. Hivyo kasumba hizi za kina Kusupa ni lazim ziwekwe pembeni kama Muungano wa kweli na endelevu unatakiwa uwepo.
Kama kuna Muungano wa kale ambao uliundwa kwa njia za mashauriano na ridhaa ni ule wa Uingereza na Scotland ambao ulianza mwaka 1603 wakati James Stuart aliposhika ufalme wa nchi mbili za Scotland na Uingereza lakini nchi hizo bado zikaendelea kuwa nchi mbili tofauti kwa zaidi ya miaka 104. Pamoja na juhudi kubwa za Mfalme James Stuart kuziunganisha nchi hizo kwa matamko ya kifalme lakini hakufanikiwa. Ni hadi mwaka 1707 wakati Mabunge mawili ya Scotland na Uingereza yalipoidhinisha Mkataba wa Muungano. Hata hivyo, Muungano huo umekuwa katika majaribu mara kadhaa na hadi sasa umo katika majaribu. Muungano huo umevuuka majaribu kwa watu kuwa huru na wakweli kujadili udhaifu wa Muungano wao na kurekebisha kasoro zake sio kwa kuuza kasumba zilizochoka na kuwaita wabaya wanaokosoa Muungano.
Kwa miaka 52 sasa ya uhai wa Muungano, kumekuwa na kutuhumiana na kutiliana shaka baina ya nchi mbili zinazounda Muungano huu. Hakuna kuaminiana. Ukisoma historia ya Muungano, utaona mvutano ulianza mapema sana mwaka ule ule wa 1964 kuhusiana na Sera ya Mambo ya Nje (Foreign Policy) ya Muungano kuhusu uwepo wa Balozi za Ujerumani Magharibi iliyokuwa ikitambuliwa na Tanganyika na Ujerumani Mashariki iliyokuwa ikitambuliwa na Zanzibar. Mwaka 1965 kukaibuka mvutano mkubwa kuhusiana na uanachama wa Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki. Na tokea wakati huo, tumekuwa hatumalizi mwaka bila ya mvutano kuhusiana na uendeshaji wa Muungano huu.
Ni maoni ya wengi kwa upande wa Zanzibar kwamba sababu kuu ya mizozo na mivutano hiyo isiyokwisha ni msingi wenyewe wa Muungano na jinsi ulivyoanzishwa kama nilivyogusia kwa ufupi sana hapo juu. Bado wapo akina Kusupa kadhaa wanaodhani kwamba Muungano ni nyenzo ya kuidhibiti Zanzibar hasa kwa sababu ya imani ya dini ya wazanzibari walio wengi. Sina haja ya kuwataja kwa sababu tumepata fursa ya kuwasikia wakiyasema hayo hadharani kadamnasi. Wapo pia wanaodhani kuwa kwa sababu ya udogo wake, Zanzibar ni tegemezi tu wa Bara na itaendelea kuwa hivyo. Tumeshindwa kujifunza historia na yanayotokea ulimwenguni. Singapore ilifukuzwa kutoka katika Muungano na Malaysia mwaka 1965 ikiwa hahe hohe; fukara, haina mbele wala nyuma kiasi cha kumfanya aliyekuwa Waziri Mkuu wao wa mwanzo kuangua kilio. Miaka chini ya 30 baadae Singapore ilikuwa ngome ya uchumi wa Malaysia hasa katika kuuza bidhaa zake nje na soko la fedha. Wakati wa mtikisiko wa fedha (currency crisis) si siri kwa vile yapo maandiko ya Mshauri wa Waziri Mkuu Mahathir Bwana Sulong Wong katika kitabu chake “Notes to the Prime Minister” yanayobainisha ni kiasi gani Singapore ilisaidia ringeti ya Malaysia isianguke. Aidha, tukiwauliza Wachina hii leo, hawafichi kwamba Hong Kong, Taiwan na Macau, visiwa vidogo vya China vilivyosaidia kuibadili China kiuchumi kupitia mitaji yao na umahiri wao kiuchumi. Bahati mbaya Muungano wetu hadi leo unapimwa kwa mezani ya kisiasa na wakati mwingi mezani ambayo tayari imeshatangulizwa mawe ya kasumba za akina Kusupa.
Wengi tuliona kuwa mchakato wa kuanzisha Katiba Mpya ungekuwa nafasi nzuri ya kufanya hayo. Ni bahati mbaya sana kwa kuongozwa na kasumba za watu kama Kasupa na siasa za kale ambao msingi wake umekuwa ule ule wa mmoja kutaka kumdhibiti mwengine, fursa hiyo tumeivuruga.
Hata hivyo, kama kweli pana nia njema basi bado fursa ipo. Marekani na Japan zilikuwa mahasimu wakubwa lakini leo ni washirika wakubwa. China na Japan walikuwa maadui wakubwa lakini leo wanashirikiana. Ujerumani imepigana vita na mataifa mengine ya Ulaya lakini leo wote ni wanachama wa Muungano wa Ulaya (EU). Mifano ya aina hiyo ni mingi. Tanganyika na Zanzibar hazikufikia uhasama kama uliokuwepo katika mifano niliyoitaja. Kuna haja ya kizazi kipya cha
viongozi wa Zanzibar na Tanganyika kukaa pamoja na kuzungumza na kisha kukubaliana mfumo mpya wa Muungano utakaohakikisha haki za washirika wote wawili zinalindwa na pia mfumo utakaohakikisha Zanzibar na Tanganyika zinafaidika kwa pamoja na ushirika wao.
Lakini bahati mbaya Kasumba ya akina Kusupa ndio imeufikisha Muungano hapa ulipo. Unalindwa kwa nguvu za jeshi na sio ridhaa ya watu. Unaekewa mwega kwa kuvunja Katiba, ubabe na kuwaandama wanaoukosoa. Muungano uko mahtuti na kama wataachiwa waganga wa kienyeji akina Kusupa watumie kasumba kuutibu utakufa sawa na ulivyokufa ufalme wa Tsar wa mwisho wa Urusi alipoamua kumtii mganga wake wa kienyeji Ras Putin badala ya washauri wake wa kitaalamu wa kiutawala na wa kijeshi.
HITIMISHO
Ni maoni yangu ya dhati kwamba mahusiano baina ya pande mbili za Muungano hayajaimarishwa kwa misingi ambayo inaufanya Muungano kuwa endelevu na unaoweza kuhimili mabadiliko ya kidunia na ya kisiasa. Sababu kubwa ni kwamba tunatumia mbadala wa uwazi, ukweli, usawa na uadilifu katika kujenga Muungano. Tumesahau kwamba sasa hivi dunia haipo katika vita baridi ya kisiasa ya miaka ya 60, sasa hivi dunia ipo katika vita ya wazi ya kiuchumi; kudhibiti rasilimali, masoko na mitaji. Tanzania ya leo ijengwe katika msingi huo na sio udalali wa kasumba za akina Kusupa.
OTHMAN MASOUD OTHMAN
ADVOCATE AND NOTARY PUBLIC
SIMU: +255777411175
No comments:
Post a Comment