Sunday, 8 November 2009
MAALIM SEIF TUIOKOE ZANZIBAR YETU
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amesisitiza msimamo wa chama chake kumtambua Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume licha ya kauli hiyo kupingwa vikali juzi na wanachama wa chama hicho, kisiwani Unguja.
Katika mkutano wake wa hadhara jana uliofanyika kiwanja cha Masota Mkoa wa Kaskazini Pemba, Maalim Seif alisema kabla ya kutokea Mapinduzi na baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 kumekuwepo na machafuko na misuguano mikubwa miongoni mwa jamii na kusababisha matatizo kwa wananchi kutoishi kwa amani.
Akiwatoa hofu wananchi hao, waliofika kwa wingi katika kiwanja hicho, kwa lengo la kuja kusikiliza kauli ya Maalim Seif aliyoahidi kuitoa mbele ya wanachama wake baada ya kukutana na Rais Karume wiki hii na aliwaambia wasiwe na wasi wasi kwani chama chake kimepewa baraka zote na baraza kuu ambacho ni chombo kikuu cha maamuzi ya chama.
Alisema wamefikia uamuzi huo, baada ya kuona hali ya kisiasa kuzidi kuwa tete huku baadhi mamia ya wananchi wakikosa amani na kwamba kutokana na hali hiyo, maendeleo hayawezi kupatikana na hivyo wanachama wanapaswa kuondokana na fikra mgando ambazo zimekuwa zikipaliliwa na watu wasioitakia heri Zanzibar.
Aliwataka wananchi wote wa Zanzibar kushikamana na kuwa kitu kimoja kwa lengo la kusogeza maendeleo na kuachana na kugombana.
Kumtambua mheshimiwa Karume tutafungua milango ya makubwa zaidi nakuombeni waheshimiwa msije mkakataa hali inavyokwenda tunahitaji sana kukaa pamoja na kushirikiana kwa ajili ya maslahi ya nchi na watu wetu, leo hii tunatangaza rasmi kuwa tumemtambua Mheshimiwa Amani Abeid Karume sawa sawa, alihoji huku akishangiliwa.
Kauli ya Maalim Seif haikuwashangaza wengi kwa kuwa tayari juzi wananchi wa Unguja walikuwa wameshaisikia katika mkutano uliofanyika Kibanda Maiti Mkoa wa Mjini Magharibi, lakini kauli hiyo ilipingwa vikali na wafuasi wa chama hicho kwa madai ya kuwa CCM na serikali zake hawana ukweli katika mazungumzo hayo.
Juzi Katibu Mkuu huyo alitangaza kumtambua Rais Karume jambo ambalo lilizusha tafrani kubwa uwanjani hapo na kusababisha baadhi ya wafusi wa CUF kuondoka mkutanoni na wengi kulia kama vile wako katika matanga wakisema wamechoshwa kunyanyaswa na uongozi wa Rais Karume na hivyo hakuna haja ya kushirikiana naye.
Kufuatia mazungumzo hayo, watu mbalimbali wameyapokea mazungumzo hayo kwa mitazamo tofauti huku wengine wakipongeza na wengine wakiponda kwa madai kwamba mazungumzo hayo, yamekuwa yakifanywa kila inapokaribia uchaguzi jambo ambalo limewaondoshea imani wananchi.
Maalim aliliambia Mwananchi kwamba amepata silaha kubwa na kuitumia baada ya baraza kuu la uongozi wa CUF kuamua kuondosha kipengele cha kumtambua Rais Karume ili viongozi hao waweze kukaa na kupanga jinsi gani wanaweza kuishi kwa amani na utulivu bila ya kusababisha madhara katika jamii.
Silaha yangu ni baraza kuu la uongozi limekubali mimi na Mheshimiwa Karume kukaa pamoja na kuzungumzia maslahi ya umma wa Zanzibar na hivyo nakuombeni na nyinyi mkubali kwani kukutana kwetu kutafungua mambo makubwa ya kimaendeleo tumeshoshwa na matatizo na misuguano ya kila siku hapa kwetu, alisema huku akishangiliwa ya ndio ndio ndio.
Alisema baada ya kurejeshwa mfumo wa vyama vingi huko nyuma kulikuwa na mivutano hadi watu kuuawa na kila unapokaribia uchaguzi watu wanakufa na kuhujumiana huku wengine wakiwa wakiachwa na madhara makubwa mwilini.
Alisema watu wanaumia na kwamba mwaka 1961, watu 68 waliuawa na kutokea ghasia na kukafanyika uchaguzi ambao haukuleta matokeo mazuri jambo ambalo lilisababisha watu kadhaa kupoteza maisha na vitu kuharibiwa huku wengine wakiwa wamekimbia nchi jirani kutafuta hifadhi.
Wiki hii Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume walikutana Ikulu Mjini Zanzibar kwa lengo la kusahau tofauti zao za kisiasa na kujenga mahusiano mema kwa maslahi ya wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba.
Viongozi hao, walifafanua kuwa wananchi wakishirikiana na kujenga nchi kwa pamoja, watapiga hatua kubwa zaidi za maendeleo.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walihusisha umuhimu wa mchakato wa mazungumzo endelevu baina yao na vyama vyao kwa jumla.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment