Sunday, 22 December 2013

MAALIM SEIF ATAKA MKUTANO WA KITAIFA WA KATIBA

Maalim Seif: 'Asema Tanzania haihitaji Katiba ya Chama fulani bali ya nchi

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutubia wananchi wa Basihaya, Kata ya Bunju jimbo la Kawe, wakati alipofanya ziara ya kutembelea baadhi ya Serikali za mitaa jimboni huo. (Picha na Salmin Said, OMKR).


Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amewatahadharisha wanachama wa chama hicho kuwa macho na wasiwachagua wagombea mamluki wanaoweza kupenyezwa wakati huu wa uchaguzi kwa malengo ya kukivuruga chama.Maalim Seif amesama katika kipindi hichi cha uchaguzi ndani ya chama baadhi ya wapinzani wa CUF wanaweza kuandaa Mapandikizi na kuwapenyeza kugombea nafasi mbali mbali, ili baada ya kushinda waibue migogoro kwa nia ya kukivuruga chama hicho..Alitoa tahadhari hiyo katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama hicho katika jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam, ambapo awali alitembelea baadhi ya Serikali za mitaa na kuzindua miradi ya maendeleo ndani ya jimbo hilo.Amesema migogoro na makundi yanayoendelea kujitokeza miongoni mwa vyama vya siasa haisaidii na badala yake huzorotesha juhudi, mipango na malengo ya vyama hivyo, ambayo kwa upande wa CUF ni kuwaunganisha wananchi wote.Alitoa mfano mgogoro wa uongozi unaokikumba chama cha CHADEMA hivi sasa kuwa hauna faida yoyote, na kwamba yeye binafsi hapendi kuona hali hiyo inaendela. Amezishauri pande zinazo tafautiana kukaa pamoja na kuelewana, ili chama kiweze kuleta ushindani na kuepusha matatizo.

Chama cha CUF hivi sasa kinaendelea na uchaguzi wake wa ndani, ambapo kwa upande wa Zanzibar uchaguzi huo upo katika ngazi ya majimbo na kwa upande wa Tanzania Bara hivi sasa unaendelea katika hatua ya Kata.Akizungumzia maendeleo ya mchakato wa kutafuta katiba mpya, Maalim Seif amesema kutokana na tafauti kubwa iliyojitokeza ikiwemo wanaotaka Serikali ziwe mbili na wale wanaotaka ziwe tatu, ipo haja uitishwe mkutano wa wadau wote wa Katiba kabla ya kuanza Bunge la Katiba kati kati ya mwezi ujao, ili kuweza kufikiwa maelewano.“Kama hatutasikilizana mapema, walio wengi watashinda kwa asilimia ndogo sana, lakini tukumbuke katiba tunayoitaka si ya CCM, CUF wala CAHDEMA ni katiba ya wananchi wote”, amesema Maalim Seif.Amesema jambo la kufanywa ni kuhakikisha inapatikanwa Katiba ambayo Mtanganyika na Mzanzibari ataridhika nayo, katiba ambayo haikupatikana kwa matakwa ya chama fulani au kikundi cha watu wachache. Awali alipotembelea mtaa wa Basihaya, Kata ya Bunju katika jimbo hilo la Kawe wananchi wa eneo hilo walimpa kilio chao cha siku nyingi cha kutaka kuhamishwa katika eneo hilo, bila ya haki zao kuzingatia inavyostahili, kufuatia kuibuka mzozo kati yao na Kiwanda cha Saruji cha Wazo. Katika risala ya wananchi hao iliyosomwa na Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Daniel Aron walisema baada ya mahakama kuamua wahamishwe walifanya mazungumzo na Serikali, ambapo awali iliamualiwa kila atakayehamishwa alipwe shilingi 15,000 kwa kila square mita moja ya eneo lake. Hata hivyo baadaye maamuzi hayo yalitenguliwa na ikaamuliwa watalipwa shilingi 5000, hatua ambayo inapingwa na wananchi wa eneo hilo.Maalim Seif aliwaahidi kuwa CUF itafuatilia mgogoro huo kwa kina na kwa kuanzia chama hicho kitampeleka Kiongozi wa Wabunge wa CUF, Mohammed Habib Mnyaa kusikiliza kilio chao na baadaye kukiwasilisha kwa Waziri Mkuu, ili suala lao liweze kushughulikia ipasavyo.Katika ziara hiyo, Maalim Seif alizindua ofisi ya Serikali ya mtaa wa Ununio, Kata ya Kunduchi pamoja na ofisi ya Serikali ya mtaa wa Basihaya iliyopo Kata ya Bunju.

No comments: