Friday, 31 January 2014

WAHAFIDHINA WA ZANZIBAR WANAENDELEA KUJIFICHA KWENYE CHAKA LA MUUNGANO

Inafurahisha CCM Zanzibar inavyojimaliza kwa siasa za ugozi na ubaguzi , na kukifikisha Chama hichi ukingoni wengi wanakokutegemea. Imetegemewa na wengi wiki hii Serkali ya SMZ kuweka Masharti Magumu kuhakikisha inawakomoa Viongozi wa Dini kuwapa masharti magumu ili wasiweze kuayatimiza ili waendeelee kusota gerazani , ni laana ilioje inayotupiwa Viongozi wa Juu wa CCM wa ZNZ kwa kuwanyanyasa Viongozi wa Dini kisa tu walisema wazi hawafurahishwi na muundo wa Muungano wa sasa , Lakini la kufurahisha Chama hichi sasa baada ya kumjeruhi Mtoto wa Mwanasiasa Mwanapinduzi Mwakilishi wa Kiembesamaki MAnsour Yussuf Himidi  , sasa wamemgeukia Mbunge mwenye asili ya uhindi Mbunge wa Uzini Mohammed Raza tayari chungu chake kiko jikoni kinachemka yote hayo pia inaonekana Wahafidhina wana wasi wasi na DR Salim Ahmed Salim kugombea Urais wa Tanzania.
 Kuna mikakati ya kummaliza kabla ya kutangaza nia yake hiyo hasa ukiangalia umaarufu wake huko Bara Salim na Ulimwenguni ni Kiongozi alieheshimika , Kosa la Raza na Salim Ahamed Salim ni kuwa Raza ameweka Wazi kua yeye anaunga mkono serkali tatu na Salim kosalake ni kukubali kuteuliwa kwenye tume ya Katiba amabayo rasimu yake ya pili iliopendekeza serkali tatu imekua mwiba kwa Wahfidhina wa Zanzibar wanaitafuna nchi na kuendelea kujificha kwenye chaka lao maaarufu la Kuulinda Muungano sio kuwaletea maendeleo Wazanzibari bali kulinda matumbo yao.
 .WAHAFIDHINA wa Chama cha Mapinduzi (CCM)/Zanzibar wanatapatapa. Nadhani wameshang’amua kwamba kishada kinawaponyoka na kwa upepo ulivyo karibu kitakwenda arijojo. Wamekwishatanabahi kwamba kila mfumo wa demokrasia unavyozidi kutia mizizi nchini basi uwezekano wa wao kubaki katika madaraka unazidi kufifia.Lakini hawa wahafidhina wetu si wajinga kama wengi wanavyowafikiria na kuwatoa maanani na kuwadharau. Wahafidhina hawa wana mpango. Kweli mpango wao ni muovu lakini lazima tuseme la haki kwamba wamebobea katika upikaji wa majungu. Wanatumia kila aina ya hila, uongo, visingizio na uzandiki ili wapate mradi wao.  Daima huwa wanapiga mbali na wanajua wapi pa kushika na wapi pa kuacha wasije kuzama.
Hiyo ndiyo hofu yao kubwa. Kuzama. Wahafidhina wetu wanachelea kuzama kwa sababu wakizama watapoteza ulwa na madaraka na marupurupu wanayoyapata kutokana na ulwa na madaraka. Ndiyo maana wanafanya kila wawezalo kuyang’anga’nia madaraka na ndiyo maana wakawa pia wanaishikilia ile kaulimbiu ya ‘Mapinduzi Daima.’ Tafsiri moja ya kaulimbiu hiyo ni kwamba waendelee kutawala hata ikiwa kimabavu ilimradi wao tu ndio wawe wanahodhi madaraka.
Hatari ya watu wa aina hii ni kwamba huwa hawajali wanayapataje madaraka. Wanakuwa tayari hata kuiuza nchi madhali maslahi yao ya kibinafsi hayadhuriki. Huu ni uhaini mkubwa.Wahafidhina wamekuwa wakikitumia kisingizio cha kuulinda Muungano kuwa kama chambo cha kuwatia kwenye ndoana na kuwavua papa wa CCM — viongozi wa juu wa chama hicho. Na wanawavua  katika bahari iliyochafuka kwa siasa chafu.Wahafidhina wamekwishatambua kwamba daima hufuzu na huibuka washindi ndani ya CCM wanapokitumia kisingizio cha kuulinda Muungano. Kila wanapokitumia kisingizio hicho huwa wanalipata walitakalo huko Dodoma, kwenye makao makuu ya chama chao.
Walikitumia kisingizio hicho, kwa mfano, kumfukuzisha Mansoor Yusuf Himidi kutoka CCM. Mansoor, aliyekuwa akiliwakilisha jimbo la Kiembesamaki katika Baraza la Wawakilishi, ni mmoja wa kizazi kipya cha wanasiasa wa Zanzibar walioamua kuyaweka mbele maslahi ya Zanzibar badala ya maslahi ya vyama vyao vya siasa.Kilichomponza Mansoor ni msimamo wake wa wazi wa kuitetea Zanzibar na hasa kampeni aliyokuwa akiipiga ya kutaka Katiba mpya ya Tanzania iipe Zanzibar mamlaka yake kamili ya kidola ikiwa ndani ya Muungano wenye muundo mpya.
Msimamo huo haukuwafurahisha wahafidhina wa CCM/Zanzibar kiasi cha kuwafanya wapange njama ya kumla Mansoor mzima mzima ili wammalize kisiasa. Wamefanikiwa kumfukuzisha kutoka CCM lakini wameshindwa kummaliza kwa sababu bado angali akinguruma nje ya CCM akishikilia msimamo wake uleule.Hivi sasa wahafidhina hao wamekwisha andaa njama nyingine kama hiyo kwa kuanza kumkaanga ili waje wamle mwakilishi wao wa Jimbo la Uzini Mohamed Raza Dharamsi. Raza ameshafikishwa mbele ya Kamati ya Siasa ya jimbo la Uzini akitakiwa ajibu hoja 16. Na kamati hiyo tayari imekwishayapeleka juu mapendekezo yake kwenye kamati maalum ya CCM ya Wilaya ya Kati.
Kisingizio wanachokitumia wahafidhina ni kilekile walichokitumia kwa Mansoor.  Wanasema kwamba Raza ameshindwa kuitetea misingi ya Muungano wa Tanzania na amekuwa akiwahamasisha wananchi (wa Zanzibar na Bara) wawachukie viongozi wa Muungano.
Pia wanamtuhumu Raza kuwa anaipinga ilani ya uchaguzi ya chama chao yenye kutaka Muungano uendelee kuwa wa serikali mbili akisema kwamba Muungano aina hiyo mwisho wake ni kisiwa cha Chumbe. Wanaongeza kusema kwamba Raza anataka pawepo Muungano wa serikali tatu.Kadhalika wanamshutumu Raza kuwa aliwahi kusema ya kwamba Watanganyika hawawezi kutawala Zanzibar na wakijaribu watajikuta wanatawala miembe na minazi tu.
Kabla ya kummaliza Raza wahafidhina wameanza kumrukia  Waziri Mkuu wa zamani Dk. Salim Ahmed Salim. Salim, ambaye ni mkereketwa wa CCM, alikuwa mmoja wa Wazanzibari walioteuliwa wajumbe wa Tume ya Katiba chini ya uongozi wa Jaji (mstaafu) Joseph Warioba.
Kuna taarifa kwamba kikao kimoja cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM/Taifa kilichokutana majuzi hapo Kisiwandui kwenye makao makuu ya CCM/Zanzibar kilimshuhudia Salim akikaangwa na kushutumiwa. Inasemekana kwamba shtuma kubwa iliyomwandama ni ile ya kushindwa kuutetea msimamo wa chama chake akiwa mjumbe wa Tume ya Katiba. Kikao hicho kilisahau kwamba Salim hakuteuliwa mjumbe wa Tume hiyo ili kukiwakilisha chama chake.
Yaliyojiri kwenye kikao hicho na yaliyompata Mansoor na Raza yanathibitisha waziwazi kwamba bado wahafidhina wa CCM wanatumia mbinu ileile ya kusakana wapate kulana kwa msingi wa “nani mwenzetu na nani si mwenzetu”. Itakumbukwa kwamba katika mjadala kuhusu suala la Muungano uliofanywa katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi mwanzoni mwa mchakato huu wa Katiba takriban thuluthi mbili ya wawakilishi wa CCM walikuwa na msimamo kama wa Mansoor. Baadaye, ingawaje, walipoanza kutishwatishwa na wahafidhina wakabadili msimamo wao wa hadharani.
Raza na Salim wamekuwa wakiandamwa wakati mchakato wa kuipatia Tanzania Katiba mpya ukiwa unaingia katika kipindi muhimu na kilicho nyeti. Katika kipindi hiki ndipo Rasimu ya Pili ya Mabadiliko ya Katiba iliyopendekezwa na Tume ya Warioba itapokuwa inachambuliwa na kujadiliwa katika Bunge Maalumu la Katiba.
Inavyoonyesha ni kwamba wabunge wa Zanzibar na wawakilishi wataokuwamo katika hilo Bunge la Katiba wanashinikizwa na viongozi wa CCM/Zanzibar wahakikishe kwamba pendekezo la serikali tatu halipiti.
Mmoja wa walio mstari wa mbele kupinga kuwako serikali tatu ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai. Yeye amekwishasema mara kwa mara kwamba hautaki kabisa aina ya Muungano uliopendekezwa na Rasimu ya Pili ya Katiba. Viongozi wa Umoja wa Vijana (UVCCM) huko Zanzibar nao pia ni miongoni mwa wanaopiga kelele kupinga serikali tatu.
Mwengine anayeunga mkono kwa nguvu muundo wa Muungano uendelee kama ulivyo ni Rais Ali Mohamed Shein pamoja na Makamu wake wa Pili, Balozi Seif Ali Idd. Kwa jumla, viongozi wa juu wa CCM/Zanzibar wako upande wa wahafidhina kupinga muundo wa Muungano wa serikali tatu na kupatikana kwa mabadiliko ya maana katika muundo uliopo wa Muungano.
Hali iliyopo CCM/Zanzibar ni tafauti na ile ya huko Bara ambako baadhi ya viongozi wa juu wa CCM/Taifa wamekuwa wakisema wazi kwamba wanapendelea pawepo Muungano wenye muundo wa serikali tatu. Wamekuwa huru kutoa maoni yao bila ya kuangukiwa na shoka shingoni mwao.
Swali ninaloliuliza ni je, hao wahafidhina wa Zanzibar na hao wenye kuwaunga mkono wataweza kweli kuitia shemere CCM/Taifa na kuiburura watakako? Kama wataweza, na kuna uwezekano mkubwa kwamba wakitumia kisingizio cha kuulinda Muungano wataweza, hayo yatatwambia nini kuhusu CCM/Taifa na uongozi wake? Nini utakuwa mustakbali wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao wa 2015?  Na nini utakuwa mustakbali wa Tanzania, na hasa wa Zanzibar, hata kabla ya hapo?

No comments: