Tuesday, 25 March 2014

TUWAKUMBUKE WAPIGANIA UHURU WA TANGANYIKA !FRANK HUMPLICK, MWANAMUZIKI ALIYELETA HAMASA YA UHURU !

“Tanganyika ikichangaruka, Uganda, Kenya na Nyasa zitaumana. Nasikia fununu wanavyoichanachana China, Kitisho! Iam a democrat, I don’t want communism, English, Yes, No I don’t know, Kizungu sikijui. Wanyika msishindane na Watanganyika”. 
Ni moja kati ya Mikutano ya TANU katika harakati za ukombozi wa Tanganyika uliokuwa ukifanyika katika Viwanja vya Mnazi mmoja mbele ya Princess Hotel. Mbele, Kwenye jukwaa lililojengwa kwa miti waliketi wale viongozi wa mstari wa mbele ndani ya TANU – Julius Nyerere rais wa TANU, Sheikh Suleiman Takadir, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU, Bibi Titi Mohamed, Mzee John Rupia na Clement Mtamila. Sahani ya santuri ilikuwa ikipigwa katika gramafoni kupitia kipaza sauti.Na kwa taratibu sauti ya kujiamini yenye kujitambua na kujenga dhamira inasikika vema sauti yenye kuimba mashairi ambayo ni moja ya beti katika wimbo mashuhuri wa “YES” “NO”wa bingwa wa siasa katika sanaa ya muziki wa dansi, mtaalamu wa upigaji wa ala ya muziki, mtunzi na muimbaji, wa miaka ya hamsini aliyeitumia sanaa kuwa moja ya funguo za harakati za kisiasa katika kudai ukombozi wa Tanganyika. Jinale Frank Joseph Humplick.


CHOTARA WA KICHAGA

Ndivyo alivyoumbwa, Huyu alikuwa mwana chotara (Suriama) wa kiswiswi na kitanzania aliyejitoa kwa dhati, Wakati wa harakati za kupambania Uhuru wa Tanganyika Miaka ile ya 50, Hivyo jina lake likatamba sana zama zile katika fani ya muziki. Franz Joseph Humplick lilikuwa jina alilopewa mara baada ya mazazi yake shambani kwa baba yake huko Moshi, Baba yake Frank alikuwa Mhandisi wa Ujenzi ambaye alishiriki katika ujenzi wa reli ya Tanga hadi Arusha. Tarehe 3 April 1927 wakati ule wa Ukoloni ndio siku ambayo Gwiji huyu wa siasa katika muziki, Utunzi wa Mashairi, Uimbaji na kupiga Vyombo alizaliwa.

MSETO WA MAKAKA NA MADADA

“Kijana wa Kichaga” hasa ndivyo alivyojulikana zaidi Miaka ile alipokuwa bado katika rika la Ujana, na alijulikana vema kwa kuwa Mama yake aliyejulikana kwa jina la Odilia Shayo hakuwa mgeni, alitokea pande zile za Kilema katika vitongoji vyaMoshi, mkoani Kilimanjaro. Frank pia alizaliwa na dada zake wawili Thecla clara na Maria Regina ambao hatimae alifanya nao kazi nyingi za muziki, wao wakiwa waimbaji, yeye akitunga, akiimba na kupiga gitaa. Kazi zake zikiwa na ushirika wa mafanikio ya wanawake wawili wa damu yake zilionesha mafanikio makubwa, ambayo yanadhihirisha haki leo ya kumtaja kuwa mmoja ya Watanzania Mashuhuri. Mashairi ya Wimbo huo hapo Juu yamemfanya Frank Humplick kukumbukwa sana kwa mchango wake wa hamasa kwa Jamii. Wimbo Husika ulikuwa umesheheni ujumbe mkali wa kisiasa jambo ambalo liliifanya TANU kuufanya kama vile wimbo wake rasmi kwani ulikuwa ukipigwa katika mikutano yake yote.

KIPAJI KINAMTAJA NA JINA LINADHIHIRI!

Wakati ule akisoma Majengo Middle School ilikuwa ni kawaida kumuona Frank akiendesha Baiskeli yake huku akiwa amefunga Gitaa lake kwenye Baiskeli yake. Lakini siri ya Kipaji cha Frank na dada zake ilifichuka na kudhihirika siku za mwanzoni tu za Ujana wao, wazazi wao kwa kutambua na kuthamini Vipaji hivyo walijaribu kuwapa msaada katika kila hali ili kuviinua zaidi vipaji hivyo. Katika wakati husika fursa za kuvionyesha vipaji vyao kwa jamii ilikuwa ndogo sana, Frank na Dada zake walipata Umashuhuri sana kwa kuimba kwenye Sherehe kama vile Harusi, Ubatizo, Sikukuu na hata kuwaburudisha Marafiki zao tu Mtaani, Burudani ambayo waliitoa haikuwa na kifani na kwa muda mfupi tu wakawa gumzo katika Mitaa yote ya viunga vya mji wa Kilimanjaro.

“KUTOKA” MCHEPUKO WA MAFANIKIO KUKANYAGA KILELE CHA UMASHUHURI

Umaarufu wa kazi za Gwiji huyu wa muziki zilianza kwa kurekodi mnamo 1950, kwenye Bustani iliyokuweko katika ghorofa la KNCU, Moshi Mjini Mkoani Kilimanjaro, alirekodi nyimbo chini ya Lebo ya Kampuni ya Galatone kutoka Afrika ya Kusini. Mgunduzi wa kipaji hiki pekee hakuwa mwingine, vyanzo vya kihistoria vinabaki vikimtaja Peter Colmore ambaye aliweza kugundua vipaji vya wanamuziki wengi kama Edward Masengo, Mathias Mulamba, Esther John kupitia Kampuni yake ya High Fidelity Productions, alianza kuzitangaza kazi za Frank na dada zake akitumia Kampuni yake ya Usambazaji ya “His Masters Voice Blue Label”.Kazi za Ndugu hawa zilipata Umaarufu sana mara tu zilipoanza kusambazwa na kwa miaka zaidi ya kumi sauti ya Frank Humplick na dada zake ilitawala anga za Muziki za Afrika ya Mashariki. Hakuna ambako ungepita ukakosa kusikia akitetwa kwa ubora, akisemwa kwa hoja kuwa kipaji hiki kilikuwa cha kipekee katika taswira ya ukanda huu.Kundi lao lililoitwa Frank na dada zake, hakika waliuletea ulimwengu nyimbo nyingi ambazo mara zote zimekuwa zikitambulishwa kama nyimbo za mwanamuziki mwingine kutoka Kenya marehemu Fundi K.

“VYA KALE DHAHABU” UTUNZI WENYE SHANI KWA HARUSI ZA AFRIKA MASHARIKI

Nyimbo zao nyingi zilipendwa na kuwapa Umashuhuri Mkubwa sana, Lakini wimbo ambao uliwahudumia watu wengi wa Afrika Mashariki na kuwafanya wajizolee sifa zaidi na Mashabiki kila kona ni ule wa “Harusi” ambao watu kwa hiari yao wangeweza kuurasimisha uwe wimbo maalumu, lakini si hivyo tu bali ilifikia uliitwa wimbo wa Taifa wa Harusi wa Afrika ya Mashariki. Mvuto wa Kale uliwagusa wa baada, licha ya zama kuliwa na zama, muziki wa nguli huyu usivyochuja ulikuja kurudiwa tena na bendi ya Afro70, chini ya Patrick Balisidya na pia The Mushrooms wakaurekodi tena na kuupa umaarufu mpya. Hivyo ndio ikawa asbabu ya kuwa moja ya vibao vinavyopigwa hadi leo kwenye sherehe za harusi na hata wao nao kujipatia umaarufu na malipo makubwa japo haukumpa chochote Frank wala ndugu zake.Ndugu watatu mseto wa jinsia, hawakuimba tu nyimbo za kiswahili, bali pia waliimba nyimbo kadhaa za Kichaga, kuna habari inasema Chief Thomas Marealle alimwomba Frank atunge nyimbo za Kichaga kwani wakati huo akina George Sibanda toka Rhodesia ya Kusini (Zimbabwe) na Manhattan Brothers kutoka Afrika ya Kusini waliimba kwa lugha zao za Kishona na Kizulu ambazo zilivutia sana.
Frank alitimiza kazi hiyo kwa kutunga nyimbo kama Wasoro na Kiwaro.

WIMBO WA “YES NO”, KUMBUKUMBU YA THAMANI ILIYOTUPWA

Hakuna usawa usio na kadiri na kwa kadirio la hakika Kati ya nyimbo ambazo zilizostahili na zinazostahili ziwekwe katika kumbukumbu ya Taifa hili ni wimbo “Yes No” (ambao muendelezo wa Mashairi yake umewekwa mwanzoni). Wimbo huu uliotugwa wakati wa mapambano ya kutafuta Uhuru wa Tanganyika. Ni wimbo ambao ulikuwa na mafumbo mengi na ulitumika kabla ya kila mkutano wa TANU na kutumiwa sana na wanasiasa wa wakati huo. Pamoja na kutamba sana kwa wimbo huo na kutokea kupendwa mno na halaiki haikupita muda serikali ya kikoloni ikaelewa ujumbe mzito uliokuwemo katika wimbo huo ambao ilikuwa himizo la harakati likisema Tanganyika itakapoamka, kutakuwa vilevile na mapambano nchini Uganda, Kenya na Nyasaland (Malawi).

Kwa ya Amri ya Gavana Sir Edward Twining, wimbo huo ulizuiwa kusikika tena katika Sauti ya TBC/RTD na msako wa nyumba kwa nyumba ulifanyika kutafuta nakala za wimbo za wimbo huo wa Frank Humplick. Yeye mwenyewe Frank alikamatwa kwa kutunga na kuimba wimbo huo unaohamasisha harakati za Uhuru wa Nchi za Afrika na alitolewa mara baada ya maombi maalum ya Chifu Thomas Itosi Mareale kwa Gavana.

HAZINA ZA MPITO WA KAZI ZAKE

Ukiachilia mbali Nyimbo zake hizo mbili ambazo zilikuwa maarufu zaidi nyimbo zingine za Frank na dada zake zilizotamba sana na zingali zinapigwa hadi leo. katika sehemu mbalimbali ni pamoja na Chaupele Mpenzi, Mwalimu Shekinuru, Sisi kwa sisi, Hodi mimi mgeni, Kichupukizi, Bibi Maria Salome, Shida, Masuti Njiani, Pondamali Hujafa, Mwanangu lala, Wanipenda Juu kwa Juu na Nyoka Kabatini ambayo ilikuwa Maarufu zaidi kwa Watoto. “Nilipokuwa nikifundisha mambo mengi ya elimu, kizungu ndicho kigumu matamshi yalinishinda. Wanafunzi wangu hodari walikitamka kiroja kwenye kabati kuna nyoka na mimi nikifungua. Sir sir there is a snake it will bite u sir. Mnasikia kihoja hichoo, the snake will bite u sir”
Kiliwavutia watoto wengi kibwagizo hicho cha wimbo wa ‘Nyoka Kabatini’.

KILA UA HUCHANUA NA KISHA HUSINYAA BURIANI “MGOSI” FRANK HUMPLICK

Agosti 25, 2007, Ulimwengu ulipaswa kuinamisha kichwa chini, maana sauti yake Frank Humplink ilififia, si kwa muda bali milele, kuashiria kuwa haitasikika tena kwa maana alihudhuria safari yake ya mwisho na kuiaga dunia, hivi leo hatunaye tena kwa takriban miaka saba. Mzee Humplink alifariki dunia huko nyumbani kwake Lushoto, mkoani Tanga, Sehemu ambayo alihamia na kuishi muda mwingi wa salio la maisha yake, tokea miaka ya 60.

Frank aliacha mjane, watoto sita (watatu wa kiume na watatu wa kike), wajukuu kadhaa na kilembwe mmoja. Alizikwa wiki moja tokea kifo chake huko huko Lushoto Mkoani Tanga. Habari za Msiba wake hazikutangaa sana Nje ya Mji wa Lushoto kama zilivyotangaa Nyimbo zake Mashuhuri, Vyombo vya Habari vya wakati huo aidha havikumkumbuka au kumjua kabisa au havikumpa uzito aliostahili kwa Mema yake kwa Taifa hili.Hata hivyo hati ya Haki haifutiki Gazeti moja tu la Serikali liliweka habari ndogo juu ya kifo chake siku kadhaa mara baada ya kufariki. Mzee Ally Kleist Sykes (marehemu nae kwa sasa) ambaye ni mmoja wa Wanamuziki Wakongwe na wa zamani alipokuwa hai muda wote alijivunia kuonesha Picha ambayo alipiga yeye, Joseph Humplick na Peter Colmore wakiwa Mjini Moshi miaka ile ya Mwanzoni mwa 50 kuonyesha namna harakati zao za siasa zilivyosaidiwa naye.

Frank Joseph Humplick amekufa lakini Muziki wake ni wenye kuvutia mpaka leo kwa jamii kusikiliza, Mashairi yake yenye Ujumbe na Mafunzo Maridhwawa ni burudani tosha kwa wasililzaji wake, Upigaji na mirindimo ya Gitaa lake vikiashiria namna alivyokuwa Mwanamuziki kamili kwa Mashairi, Sauti na Vyombo, huku Nyimbo zake na kauli zake za kimafumbo zikichochea na kushajiisha Uchapakazi, Ndoa, Furaha na Upendo.Katika ulimwengu wa muziki Marehemu Frank Humplink anasimama kwenye safu moja na Magwiji wenzie kama Mzee Gabriel Omolo, Marehemu Fadhili William, Marehemu Fundi Konde, Marehemu Ahmed Kipande, Marehemu salum Abdallah na wengine wengi waliovuma katika miaka ya sitini. Ni hoja isiyo na ubishi kwamba majina kama hayo hapo juu ndiyo yanaweza kusemwa kuwa ni msingi wa muziki wa dansi Afrika Mashariki. Shujaa Frank Humplick ameacha watoto saba, wanne wa Kiume na watatu wa kike, mmojawapo ni Mhandisi wa Kitanzania anayetamba katika anga za Kimataifa, Dkt Frannie Leautier.Upumzike baba hata saa ile tunayokutaja, ungali hai katika Sanaa ya Siasa!

Maandishi haya ni kwa Hisani kubwa ya Ndugu Yaqoub Nyembo wa Ujiji, Kigoma. Picha ya Frank Humplick ni kwa hisani ya Mwandishi Mohammed Said Semitungo.

No comments: