Sunday 20 April 2014

MSIKILIZE MWANASHERIA MKUU WA ZANZIBAR


MSIKILIZE MWINGULU NCHEMBA !
Dodoma. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amesema Rais Jakaya Kikwete hana uwezo kisheria wa kuwafukuza au kutengua uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.Jaji Werema alisema Sheria namba 8 ya Mabadiliko ya Katiba ya 2011, ipo kimya kuhusu suala hilo na kwamba kwa maana hiyo Rais hana mamlaka ya kutengua hata ubunge wa wale aliowateua kupitia kundi la wajumbe 201.“Umesoma Sheria ya Mabadiliko ya Katiba? Kaisome maana ili mtu afukuzwe ubunge lazima apungukiwe sifa za nafasi hiyo, lakini kama sheria iko kimya maana yake ni kwamba hana (Rais) uwezo wa kuwafukuza,” alisema Jaji Werema.

Jaji Werema alikuwa akijibu maswali ya gazeti hili kuhusu hatima ya wajumbe ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao Jumatano jioni waliondoka bungeni kwa madai ya kutoridhishwa na uendeshaji wa Bunge Maalumu.Wajumbe waliotoka nje ni wanaotokana na vyama vya CUF, Chadema, NCCR Mageuzi, NRA, NLD na baadhi kutoka kundi la 201. Alhamisi asubuhi, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta alisema utafiti liofanywa na ofisi yake ulibaini kuwa katika kundi la 201, ni wajumbe 25 tu ambao walitoka nje pamoja na Ukawa.Baada ya wajumbe hao kutoka nje, Mjumbe wa Bunge hilo, Mwigulu Nchemba ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, aliomba mwongozo akihoji iwapo Ofisi ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu haiwezi kumwandikia Rais Kikwete ili ateungue uteuzi wa wajumbe katika kundi la 201 ambao waliungana na Ukawa kususia vikao.
“Ningependa Rais atengue hadhi zao ili kuingiza watu wengine ambao wako tayari kufanya kazi hata bure, sisi tunalipwa fedha nyingi, lakini tunaleta mzaha, watu hawana maji, dawa, madawati, ada za elimu ya juu watu wamekosa, hizi fedha zingetumika huko,” alisema Nchemba mwenye wadhifa mwingine wa Naibu Waziri wa Fedha.
Matakwa ya Sheria
Jaji Werema alisema: “Ili mtu aondolewe katika nafasi yake ni lazima akose sifa za kuwa mjumbe, mathalan kuugua ugonjwa wa akili au kichaa, kuumwa muda mrefu kiasi cha kushindwa kutimiza majukumu yake na kadhalika, lakini sifa hizo kama hazipo kwenye sheria sasa unaanzia wapi?”Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2011 pamoja na marekebisho yake ya 2012 na 2013 inawataja Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa mujibu wa nafasi zao.Kadhalika sheria hiyo inampa Rais mamlaka ya kufanya uteuzi wa wajumbe 201 kutoka makundi mbalimbali, lakini haitaji sifa wanazopaswa kuwa nazo wajumbe hao.Jaji Werema alisema hata kama sheria ingekuwa inaruhusu kufukuzwa au kusitishwa kwa ujumbe wa wabunge hao, hakuna sababu ya msingi ya kuwachukulia hatua hiyo.
“Pia wakati huu kupendekeza kwamba wafukuzwe hata kama sheria ingekuwa inaruhusu, it is very unfair (siyo haki), wafukuzwe kwa kosa gani? It is very clear (ni wazi tu ) kwamba wameshindwa kuvumilia waliyoyasikia humo ndani na wameamua kutoka nje,” alisema Werema.Hata hivyo, alisema wajumbe wote wanapaswa kuwa wavumilivu na kushindana kwa hoja badala ya kuwa na jazba, hasira na kutoa kauli zisizo na staha.“Kila mtu anaweza kufanya uamuzi anaodhani unamfaa kwa manufaa yake, lakini si kwa hawa. Hawa walitakiwa kuwa wavumilivu, kila kinachoendelea ndani ya Bunge wangekuwa wavumilivu, inasikitisha wamekosa uvumilivu,” alisema na kuongeza:“Nimeshangazwa na Bunge kujaa mipasho, wajumbe wanatukanana matusi ya waziwazi, matusi ya nguoni, kuna watu na heshima zao humu, kuna watu wamekuja kufanya kazi ya Katiba, lakini inasikitisha haya yanayotokea.”Aliendelea: “Wajumbe wa CCM Zanzibar na CUF Zanzibar wanatukanana waziwazi, na wengine wanaingia humo, sikutarajia kabisa…sikutarajia, kwa kweli kunahitajika uvumilivu wa hali ya juu. Tunu na maadili ya taifa yamepotea kabisa.”Jaji Werema alikataa kuzungumzia hali itakuwaje endapo wataendelea kugoma na kusema: “Wacha tuone maana Bunge limeahirishwa hadi Jumanne na tuone, kama wataendelea kususia, tutaanzia hapo,” alisisitiza.
Awashangaa Lipumba, Lissu
Jaji Werema pia alielezea masikitiko yake kuhusu kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba kuwaita wajumbe wa Bunge la Katiba kuwa ni Interahamwe.“Hawa jamaa wa Interahamwe, walihusishwa sana na mauaji ya kimbari kule Rwanda, sasa kusema CCM na wajumbe wengine Interahamwe sijui alikuwa na maana gani, kwa kweli sijamwelewa Profesa Lipumba,” alisema.Kwa upande mwingine, Jaji Werema alisema anamshangaa Mjumbe wa Bunge la Katiba, Tundu Lissu kuingia katika kundi la waliogoma wakati alishiriki katika kutengeneza kanuni za kuendesha Bunge hilo.“Hatukulala, Lissu tulitengeneza kanuni za kuendesha Bunge, pamoja na wajumbe wengine, alifanya kazi nzuri, kanuni zikatimia, lakini hiki alichoshiriki kutoka nje, kimenisikitisha, sijui, lakini ninaamini hawakutoka nje ya Bunge kwa sababu ya matusi, isipokuwa walishapanga mapema…,” alisema Jaji Werema. From mwananchi

No comments: