Saturday 3 May 2014

LIPUMBA AFUNGUA KIAKO CHA BARAZA KUU LA CUF BUGURUNI LEO



Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba, akiongozana na Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, kuelekea ukumbi wa mikutano katika ofisi kuu za Chama hicho, Buguruni Dar es Salaam.

 Baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi CUF Taifa, wakifuatilia kikao hicho kinachofanyika Ofisi Kuu za CUF Buguruni Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba, akifungua kikao cha siku tatu cha Baraza Kuu la Uongozi CUF Taifa, katika ofisi kuu za Chama hicho, Buguruni Dar es Salaam. (Picha na Salmin Said, OMKR)
 
Na: Hassan Hamad (OMKR).
 
Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Haruna Lipumba ameweka bayana kuwa Chama chake pamoja na washirika wenzao wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), hawatorejea kwenye Bunge maalum la katiba mpaka wahakikishe kuwa kinachojadiliwa ni rasimu ya katiba inayotokana na mawazo ya wananchi ambayo roho yake ni sura ya sita inayoelezea muundo wa Muungano wa Serikali tatu.
 
Amesema kamwe hawatokuwa sehemu ya kujadili na kupitisha rasimu inayokiuka misingi ya mawazo ya wananchi na kufuata matakwa ya Chama Cha Mapinduzi ambacho kimeigeuza rasimu hiyo kuwa ya kwao.
 
Prof. Lipumba ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha kawaida cha siku tatu cha Baraza Kuu la Uongozi la CUF, kinachofanyika Ofisi kuu za Chama hicho Buguruni Dar es Salaam.
 
Amefahamisha kuwa mpango wa kulivuruga Bunge hilo Maalum la Katiba ulianza zamani baada Mwenyekiti wa Bunge hilo Samuel Sita kuanza kupindisha kanuni kwa kumruhusu Rais Jakaya Kikwete kuzindua bunge hilo mwisho, sambamba na njama za kutaka kumpa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba muda mfupi wa kuwasilisha Rasimu ya Tume hiyo.
 
Ameelezea kusikitishwa na kitendo cha kubezwa kwa rasimu ya katiba iliyowahusisha watu wazito ambao wengi wao ni kutoka Chama cha Mapinduzi na kuhoji hali ingekuwaje kama yeye ndio angekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo.
 
“Ni jambo la kusikitisha kweli kuona mapendekezo ya Tume ya Katiba yanapuuzwa wakati tume hii ilikuwa na watu wazito wanaoaminika sana wakiwemo Jaji Mstaafu Warioba, Mhe. Salim Ahmed Salim, Augostino Ramadhan na wangine wazito kutoka CCM, sijui kama Mwenyekiti ningekuwa mimi Prof. Lipumba kutoka upinzani hali ingekuwaje?’ alihoji Lipumba.
 
Prof. Lipumba ametumia fursa hiyo pia kutoa ufafanuzi kuwa vitendo vilivyofanywa na kundi la  “Interahamwe” vilianzia na lugha za kibaguzi na uchochezi ambazo hazikukemewa, na hatimaye kusababisha mauwaji ya halaiki nchini Rwanda.
 
“Inakuwaje leo kiongozi wa nchi anakuwa mstari wa mbele kuhamasisha lugha za kibaguzi na uchochezi, huku viongozi wengine wakifurahia jambo hilo, tunaelekea wapi?” aliendelea kuhoji Prof. Lipumba.
 
Aidha ameelezea hatua ya Serikali ya kuifunga Tovuti ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na kukiita kitendo hicho kuwa ni cha ‘kihuni’, kwani wananchi wengi walikuwa wakipata taarifa za tume kupitia tovuti hiyo.

Amewaasa wajumbe wa kikao hicho kuwa wana kazi kubwa ya kutathmini hali ya kisiasa na kuweka mikakati imara ya kukabiliana na kile anachokiita  “Ombwe” la uongozi  ndani ya Chama cha Mapinduzi.
 
Mapema akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, amesema malengo makuu ya kikao hicho ni pamoja na kufanya uteuzi wa mwisho kwa wagombea wa nafasi za ukatibu na uwenyeviti katika ngazi za Wilaya, pamoja na kuandaa na kupitisha Mkutano Mkuu wa Taifa.
 
“Kikao hiki kilikuwa ni cha siku mbili, lakini kutokana na uzito wa ajenda hizi imetubidi tukifanye kwa siku tatu ili kuweka mambo sawa”, alifahamisha Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
 

No comments: