Sunday, 19 October 2014

MAALIM SEIF AIMALIZA RASIMU YA CHENGE KISIWANI PEMBA

KATIBA INAYOPENDEKEZWA NI KOTI LINALOZIDI KUIBANA ZANZIBAR - MAALIM SEIF
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Katiba inayopendekezwa ni koti linalozidi kuibana Zanzibar, badala ya kuipa nafuu na kamwe Wazanzibari hawawezi kuikubali. Maalim Seif ameyasema hayo wakati alipokuwa akihutubia katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika kiwanja cha Gombani ya Kale, Chake chake Pemba.
Alisema Katiba hiyo ina mambo mengi ambayo yanainyang’anya Mamlaka yake Zanzibar, na wale wanaopita kusema kuwa Zanzibar imepata kila inachokitaka kwenye Katiba hiyo ni waongo.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alisema Katiba hiyo imekiuka hata ile misingi mikuu ya mkataba wa Muungano ambayo inatambua Mamlaka ya Zanzibar ndani ya Muungano. Akitoa mfano, Maalim Seif alisema CCM anapita na kusema kuwa Katiba hiyo imeyatoa mafuta na gesi asilia sasa kuwa ya Muungano, jambo hilo ni sawa na kuipaka mafuta Zanzibar, kwa sababu ardhi sasa imefanywa ni jambo la Muungano.
Alisema sheria za Zanzibar ziko wazi kabisa juu ya ardhi kumilikiwa na Wazanzibari, lakini kwenye Katiba inayopendekezwa suala hilo sasa ni la Muungano, licha ya kuwa ardhi ya Zanzibar ni ndogo sana na haitoshi hata kwa Wazanzibari wenyewe.

Maalim Seif alisema kuwa si kweli kwamba kuna msururu wa makampuni ya kuchimba mafuta na gesi asilia, baada ya kusikia sekta hiyo imetolewa kwenye Muungano.
Alisema kwamba Zanzibar haiwezi kuruhusu kuchimbwa mafuta na gesi asilia, kabla kwanza haijawa na sheria na Sera juu ya mafuta hayo ambazo ni nzuri zinazotamka wazi wazi ni vipi Wazanzibari watanufaika na mafuta na gesi hiyo.
“Lazima tuwe na chombo chetu wenyewe Wazanzibari cha kushughulikia uchimbaji wa mafuta, ambacho kitakuwa na usimamizi mzuri utakaohakikisha kila Mzanzibari ananufaika na mafuta na gesi, ikiwemo suala la ajira”, alisema Maalim Seif.
Katika hatua nyengine, Maalim Seif alisema katika uchaguzi mkuu ujao mwakani hakuna wa kukizuia chama cha Wananchi CUF kushinda na kuingia Ikulu ya Zanzibar.
Alisema kwamba matukio yaliyojiri Dodoma juu ya mchakato wa Katiba yatawafanya Wazanzibari kushikamana na kuitetea Zanzibar, jambo ambalo wanajua litaweza kufanikiwa iwapo chama cha CUF kitakamata Serikali.
“Hawa wameshamalizika, wameshamalizika kabisa namwambia rafiki yangu Rais Kikwete wasiwaletee Katiba hiyo Wazanzibari wataikataa”, alisema.
Katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jusa Ladhu amewapongeza wananchi wa kisiwa cha Pemba kwa kuwa imara miaka yote na kuonesha ukomavu mkubwa na msimamo isio yumba katika kuhakikisha hadhi ya Zanzibar ina baki na wao wamekuwa ngome imara ya kuitetea Zanzibar na maslahi yake.
Alisema kwa wananchi wa Pemba hakuna kituko au kitimbi ambacho hawajafanyiwa, lakini hilo kamwe halikuwatoa kwenye mstari na wameweza kuhimili dhoruba hizo na hivi sasa kuna kila dalili chama cha CUF kitashika serikali katika uchaguzi mkuu hapo mwakani.
“Hakuna wa kuzuia wakati, wakati ni ukuta. Wakati sasa umefika, kila wanalolifanya CCM hivi sasa linawageukia wenyewe, na Inshallah ushindi wa CUF mwakani hauna mjadala na Maalim Seif anaingia Ikulu ya Zanzibar”, alisema Jusa.
Alieleza kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa upande wa Zanzibar utakuwa ni kati ya wanaotaka Mamlaka kamili na wale madalali wa Zanzibar waliokwenda kuiuza Dodoma.
Jusa alisema kuwa katika hali hiyo upande unaotaka Mamlaka kamili lazima utashinda kwa sababu unaungwa mkono na Wazanzibari walio wengi, wakiwemo viongozi mashuhuri ambao baadhi yao ni viongozi mashuhuri wa CCM.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amesema mambo yaliyokuwa yakifanyika Dodoma si mambo ya kufanywa na watu waungwana, hasa kitendo cha baadhi ya wajumbe kuuza nchi yao ya Zanzibar kwa kujali maslahi yao wachache.
Alieleza kuwa Wazanzibari wanachotaka sasa ni kuwa na Mamlaka ya kujiamulia mambo yao katika kuimarisha uchumi na hali za wananchi, na wala hawataki kuona baadhi ya wachache wakipigania matumbo yao na kuwaacha wananchi walio wengi wakisumbuliwa na hali ngumu ya maisha.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Salum Bimani amesema dalili ya kuwa katiba iliyopendekezwa Dodoma haina maslahi kwa Zanzibar, wajumbe wengi waliohusika kuipitisha hivi sasa wanaona shida kutembea Zanzibar kutokana na usaliti walioufanya.
Mkutano huo uliofanyika Gombani ya Kale Pemba ni wa pili mkubwa kufanywa na CUF tangu Bunge Maalum kutoa Katiba inayipendekezwa na kukabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar huko Dodoma.
Mkutano wa kwanza ambao pia ulihutubiwa na Maalim Seif na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wanachama, wafuasi na wananchi mbali mbali wa Zanzibar ulifanyika Oktoba 16 katika viwanja vya Kibandamaiti.

No comments: