Monday, 7 December 2015

NAMDURUSU ALI AMEIR UCHAGUZI WA ZANZIBAR 1995 NA JABIR IDRISSA


 Utangulizi

Kwa kawaida na kwa miaka mingi huwa siipiti makala yoyote ya Jabir Idrissa ila nitaisoma. Napenda kusoma makala za Jabir Idrissa kutokana na staili yake ya uandishi. Jabir anaandika kwa upole sana kiasi cha makala nzima kuwa baridi kwa kipimo cha joto lakini ndani yake kila neno kila sentensi, kila mstari na kila paragrafu imesheheni miba na misumari inayochoma na kutoboa kwa ncha kali sana. Lakini juu ya haya yote makala kila ukiirudia ubaridi wake katika hoja, lugha na mantiki inabakia na ubaridi wa kuzizima. Hii ndiyo kalamu ya Jabir Idrissa. Msome Jabir Idrissa anavyoeleza jinsi CCM Zanzibar walivyoshindwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 na nini CCM ilifanya kujipa ‘’ushindi.’’

Jabir Idrissa
Jabir Idrissa
 

Namdurusu Ali Ameir  Uchaguzi wa Zanzibar 1995

Na Jabir Idrissa
(Makala kwa hisani ya Mwandishi na Gazeti la ''Mawio'')

NIMEIKUMBUKA sinema ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka 1995, wa kwanza tangu mfumo wa vyama vingi urudishwe kwa Sheria Na. 5 ya Mwaka 1992, iliyopitishwa na Bunge. Nipo na waandishi wenzangu nje ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) mkabala na sekondari ya Benbella (iliitwa kuheshimu jina la Ahmed Ben Bella, aliyekuwa Rais wa Algeria). Ilikuwa siku ya pili baada ya uchaguzi mkuu 1995, tunasubiri Tume itangaze matokeo ya kura zilizozidi kidogo 300,000. Siku nne haijakamilisha. Sasa wakati tunapiga soga, akatokea Ali Ameir Mohamed, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar. Hakuwa tu mtendaji mkuu kwa Zanzibar, ukweli alikuwa bosi wangu kwani mwajiri wangu wakati ule alikuwa Shirika la Magazeti ya Chama (SMC), moja ya asasi zilizokuwa milki ya CCM.
 
 
 

Ali Ameir, nimuite kwa utambuzi rahisi, ni bwana wa Donge, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambako alipata kuwa Mbunge wa kuchaguliwa. Kiongozi makini katika viongozi wa kisiasa nchini zama zile. Mwerevu na mjuzi, tofauti na wengine. Lakini kama kawaida ya wanasiasa wa nchi zetu za Afrika, alikuwa mjanja wa mambo, mpanga mikakati na msimamizi wa utekelezaji katika kukiimarisha chama chao. Ali Ameir ambaye sasa yu mtu mzima aliyedhoofika afya kutokana na kupatwa na ugonjwa wa kiharusi, alipofika mbele yetu, na kusalimia, alitoa malalamiko CCM imehujumiwa katika uchaguzi. Akasema, “Hatukubali matokeo kwa sababu Tume imekula njama na CUF kutuhujumu.” Kila muandishi alishtuka kumsikia. *******************


Ali Ameir Mohamed

Tulipomuuliza imekuaje Tume na CUF (Chama cha Wananchi) leo vishikamane dhidi ya CCM, wakati ni CCM kilichokuwa kinaongoza dola. Katika kampeni na kabla ya hapo, ni CUF pekee waliolalamika kuhujumiwa. Akaulizwa inakuaje kulalamikia matokeo ya uchaguzi ambayo yalikuwa hayajatangazwa? Akaulizwa tena, “au wewe na CCM wenzako mmeshayajua?” Akajibu, “Sisi ndo tunasema hivo kwamba hatukubali matokeo yatakayotangazwa… tumehujumiwa ili kuwapa ushindi CUF.” Safari hii alipoulizwa kwamba CCM imeshawasilisha malalamiko yake, kama anavyoyaeleza hapo, akasema, “ndio napeleka.” Akaingia ndani ya ofisi za Tume. Niseme kabisa, Tume ilikuwa chini ya Zuberi Juma Mzee, mtumishi wa umma aliyesomea sheria kiwango cha kati.

Hakuna aliyepata uhakika kama ni kweli CCM ililalamika rasmi kwa hayo aliyotuambia Ali Ameir siku ile. Hatukuona barua hiyo wala majibu kama yalikuwepo. Hatukuona. Nilimwambia muandishi rafiki yangu aliyekuwa karibu yangu, “ukiona hivi, ujue CCM inahangaika kutafuta ushindi wa kulazimisha; ishashindwa uchaguzi vituoni.” Hakuamini. Ikaichukua Tume siku mbili zaidi ya pale ndipo ikatangaza matokeo ya urais. Ilikuwa siku ya sita tangu Wazanzibari walipopiga kura kuchagua Rais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani. Nasema tena kura zilizopigwa hazikufika 350,000. Siku sita? Twende tutaona mbele.

Siku ilipofika, tukaona ofisi zimejaa mapolisi kwa idadi iliyozidi kwa sana waandishi tuliokuwepo – kwa kweli tulishachoka – tukisubiri matokeo. (Siku ya nyuma yake, katika njia ya ‘kijasusi’ tulipata karatasi ya matokeo ya majimbo yote iliyokuwa ikionesha kuwa CUF na mgombea wake wa urais, huyuhuyu Maalim Seif Shariff Hamad, ameshinda uchaguzi). Televisheni ya DTV ikayatangaza usiku ule na asubuhi yake. Sisi gazeti la Uhuru hatukutangaza. Sababu ni dhahiri, “tungechinjwa.” Mwalimu wangu Mwadini Hassan nilimuuliza tufanyeje, akaashiria kusema, “Tuachane nayo haitatoka.” Kweli isingetoka.


Tukaona maandalizi ya kutangaza matokeo. Ghafla kundi la polisi limemuweka kati Mwenyekiti Zuberi kuelekea ukumbini. Du askari wengi wale, tena wenye bunduki. Tukafukuzia ukumbini. Nafasi finyu, mwenyekiti kabanwa kila upande. Sasa anasoma kijikaratasi kwa shida, labda alijua amelazimishwa. Kijasho tele. Akasoma na mwisho akamtamka mshindi ni mgombea wa CCM, Dk. Salmin Amour Juma, wakati huu akiitwa Komandoo Dk. Salmin. Matokeo yalimpa ushindi mwembamba – asilimia 50.8 dhidi ya 49.2 wa Maalim Seif – ambao mwenyewe Komandoo Dk. Salmin tulipokutana naye nyumba ya Bosnia, Maisara, aliuita “wa goli moja... lakini ni ushindi.”

Salmin Amour
Usiulize mpaka nikamilishe alichokifanya Ali Ameir baada ya hapo. Alitoka mbio nyingi na kuchupia gari yake na kumuamuru dereva wake aondoshe haraka. Zilikuwa ni mbio kwenda Ofisi Kuu za CCM Kisiwandui, zilipo ofisi za wakubwa wa chama hiki Zanzibar. Nikasema haiwezekani kuandika stori bila ya bosi wangu kusema chochote. Nikatoka na waandishi wawili, mmoja akiwa pia mpigapicha, kumfuata aseme sasa baada ya CCM kutangazwa mshindi. Tuliingia kwa urahisi kwa kuwa nilikuwa naheshima yangu pale. Si muandishi wa Uhuru/Mzalendo, hupati shida kukubalika. Nikaongoza kuuliza “Naibu unasemaje CCM imetangazwa mshindi muda mfupi baada ya malalamiko yenu kuwa mmehujumiwa.” Alijibu hivi: “Sasa ungekuwa wewe Jabir yakhe ungefanya nini, chama changu kimetangazwa mshindi ninafuraha sana, ni sherehe tu sasa.”***********************************************//////

Si uongo ningekuwa pia ningeanza kusherehekea ushindi, japo najua ulitengenezwa mezani kama ilivyokuja kudhihirika. Pata picha ile ya uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi ambao ulikwenda kwa amani kubwa, lakini ukaja kuharibiwa na matokeo ya mwisho yaliyoonesha kupangwa mezani. Unapovuta picha hiyo ya miaka 20 iliyopita, hebu tafakari na kile kilichotokea safari hii katika uchaguzi ambao ulikwenda vizuri kabisa na kusifiwa na asasi za uangalizi zilizoshuhudia kinagaubaga vituoni na tangu wakati wa kampeni. Maalim Seif hakulalamika Oktoba 26 alipokutana na waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya CUF Mtendeni mjini Zanzibar. Hakulalamika. Alitaja takwimu za kura kama alivyokabidhiwa na wasaidizi wake katika chama, zikionesha alikuwa ana asilimia 52.87 (kura 200,077) dhidi ya 47.13 (kura 178,368) za Dk. Ali Mohamed Shein. Tofauti ya kura ni 21,714.

Mpaka hapo, Tume ilikuwa imehakiki kura za majimbo 40, ikiwa na maana majimbo 14 tu yalibakia kuhakikiwa. Lakini mpaka asubuhi ile ya Press Conferece ya Maalim Seif, Tume ilikuwa imetangaza matokeo ya majimbo manne tu. Ni Kiembesamaki (CCM 4,413 v CUF 2,989); Fuoni (CCM 889 v CUF 429); Malindi (CCM 2,334 v CUF 5,697) na Kwahani (CCM 5,960 v CUF 2,879). Mpaka Jecha Salim Jecha, mwenyekiti wa Tume, anatoa tangazo la kufuta uchaguzi mchana wa Oktoba 28, alikuwa ameshatangaza matokeo ya majimbo 31, akibakisha 21 kukamilisha.



Mpaka hapo hakukuwa na malalamiko yoyote rasmi ya chochote kilichotokea si vituoni wakati wa kupigakura wala kuhesabu kura. Tukiwa ukumbi wa Hoteli ya Bwawani, kituo cha kutangazia matokeo, tulisikia CCM walipeleka barua Oktoba 27 kulalamika. Tafadhalini, asasi za waangalizi zilishatoa ripoti za awali za kusifia uchaguzi, zikisema ulisimamiwa vizuri zaidi ya ilivyokuwa 2010. Kisheria, malalamiko ya vituoni huwasilishwa kupitia fomu maalum kwa wasimamizi. Haikuwepo hata moja.  Kwa hivyo basi, fikiria unapoambiwa uchaguzi umefutwa wote, wakati mwenyekiti mwenyewe alishatangaza asilimia 70 hivi ya majimbo, unaendelea kuuliza kulitokea nini? Usijisumbue akili, njama za CCM kulazimisha watakavyo si kwa vile walivyoamua wapigakura. Tena isitoshe, unaposikia wasomi na makada wanavimbisha mishipa ya shingo na kutetea uamuzi wa Jecha, na huku wakivizonga vifungu vya sheria kuhalalisha walichotumwa kufanya, ujue tatizo ni moja tu – demokrasia ya kweli haijapewa nafasi na hawa CCM.

No comments: