Sunday 9 November 2014

JIMBO LA BALOZI SEIF IDDI LAVAMIWA

Maalim Seif Atembelea Wilaya ya Kaskazini B Unguja.

Na Khamis Haji OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema amesikitishwa na hali ngumu inayowakabili wananchi wa kijiji cha Kiomba Mvua katika jimbo la Kitope kushindwa kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo kikamilifu, baada ya sehemu kubwa ya eneo lao kupewa mwekezaji ambaye amewawekea masharti magumu. 

Maalim Seif amesema hayo jana wakati alipotembelea Shehia hiyo, iliyopo katika jimbo la Kitope, Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja na kupokea malalamiko mengi ya wananchi wa eneo hilo wanayofanyiwa na mwekezaji.
 Wana kijiji wamemweleza Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa hivi sasa wanashindwa kufanya shughuli zao za uvuvi, kilimo na uanikaji wa madagaa kutokana na vikwazo vya mwekezaji anayeshirikiana na  na baadhi ya viongozi Serikalini.

Makamu wa Kwanza wa Rais amesema kwa nchi inayofuata Utawala Bora kama Zanzibar, migogoro ya aina hiyo ingeweza kuepukwa iwapo busara zingetumika kwa kuwakutanisha wawekezaji na wananchi, kabla ya eneo hilo kutolewa kwa uwekezaji.

Maalim Seif amesema azma ya kukaribishwa wawekezaji vitegauchumi hapa Zanzibar haikuwa kuleta vilio na masikitiko kwa wananchi, bali ni kuwawezesha wananchi hao pamoja na Serikali wanufaike na ajira ili waweze kupiga hatua kubwa zaidi katika kujikwamua na umasikini.

Amesema wananchi ndio wenye haki na matumizi ya maliasili na rasilimali katika maeneo yao, ikiwemo ardhi na bahari , hivyo ni lazima washirikishwe kikamilifu katika maamuzi yoyote yale yanayohusu matumizi yake.

Awali katika risala yao kwa Makamu wa Kwanza wa Rais, wanakijiji hao walisema mwekezaji aliyepewa eneo hilo ambaye wanadhani anataka kufanya shughuli zaUutalii, amewazuia wana kijiji kutumia bandari yao ya asili eneo la Nyanjale na sasa wanalazimika kuzunguuka hadi kijiji jirani cha Fujoni wanapotaka kwenda baharini.

Sheha Mstaafu wa Shehia ya Kiomba Mvua, Mwinyishaa Sheha Abdallah amesema hivi sasa wana kijiji hao wanaishi katika hali ngumu katika nchi yao, baada ya mwekezaji huyo kuweka uzio na vizuizi na kuwapiga marufuku wasitumie eneo la bahari na ardhi kwa kilimo.

“Tumelalamika sana kwa viongozi wetu, lakini kubwa lililofanyika walituletea askari na wananchi wengine waliwekwa ndani”, alisema Sheha huyo Mstaafu.

Amesema kuwa kitendo hicho kimewavunja moyo sana wananchi wa Kiomba Mvua na kimewafanya wengi wao wahisi kuwa hawathaminiki na hivyo kuchukua maamuzi ya kujiunga na chama cha upinzani cha CUF, ambacho alisema wana matumaini kuwa viongozi wake wamedhamiria kuwatetea wananchi wa Zanzibar na kuwaondoa katika manyanyaso.

Naye, Bi Rabani Ali Hassan akizungumza kwa uchungu alisema akinamama wa kijiji hicho ambao ndio wanaotoa mchango mkubwa wa kuendesha familia zao, ikiwemo kuwasomesha watoto, hivi sasa hawana la kufanya baada ya kuzuwiwa kwenda katika eneo la baharini ambako walikuwa wakifanya shughuli za upishi na uanikaji wa madagaa.

Alisema hata vijana wengi ambao zamani walikuwa wakijishughulisha na kazi hizo hawana kazi tena na kuna hatari kubwa kwa vijana haoi kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya kutokana na kukosa shughuli za kujipatia rizki walizokuwa wakizifanya.  

Katika hafla hiyo, Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF aliwapokea wanachama 155 waliojiunga na CUF wengi wao kutoka CCM, akiwemo Sheha Mstaafu, Mwinshaa Sheha Abdallah ambaye amejiunga na CUF pamoja na familia zake.

Shehia ya Kiomba Mvua ipo katika jimbo la Kitope, Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, jimbo ambalo Mbunge wake ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi na Mwakilishi wake ni Mhe. Makame Mshimba Mbarouk.

No comments: