Tuesday 2 December 2014

Maalim Seif asema Zanzibar imeathirika sakata la Escrow


Katibu Mkuu wa CUF, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad (katikati), Naibu Katibu Mkuu CUF Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui na Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kaskazini 'A' Bakari Makame akipandisha bendera za CUF wakati wa uzinduzi wa tawi jipya la Tazari.

 Katibu Mkuu wa CUF, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akiweka tofali kusaidia ujenzi wa hodhi la maji safi na salama linalojengwa na wananchi wa kijiji cha Kivunge, Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja.
Wanachama na wafuasi wa CUF wakimsikiliza Katibu Mkuu wao alipokuwa akihutubia kwenye mkutano wa hadhara Mkokotoni. (Picha na Salmin Said, OMKR

Maalim Seif akihutubia katika mkutano wa hadhara huko Mkokotoni.

Na Khamis Haji OMKR
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar imepata athari kubwa kwa kukosa fedha za wafadhili kutokana na wizi wa zaidi ya shilingi bilioni 320 katika akaunti ya Tegeta Escrow uliohusisha baadhi ya viongozi serikalini.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alisema hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CUF katika viwanja vya Mkokotoni, jimbo la Tumbatu mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema miongoni mwa miradi inayotajwa kuathirika kutokana na uamuzi wa wafadhili kusitisha misaada kufuatia kashfa hiyo ni mradi wa Millenium Challenge Corporation unaopata ufadhili kutoka Marekani, ambao unasaidia huduma za umeme pamoja na ujenzi wa barabara kwa uapnde wa Zanzibar.
Alieleza kuwa Zanzibar pia inanufaika na misaada ya kibajeti na ile inayotolewa na Mfuko wa Dunia (Global Fund) maeneo ambayo pia yameathirika kutokana na uamuzi wa wafadhili hao ambao hawakuridhishwa na wizi wa fedha katika sakata hilo la Escrow.
“Zanzibar tumeathirika sana kuna miradi mingi imesitishwa kwa kashfa hiyo ya Escrow, lakini pia hakuna Mzanzibari hata mmoja aliyetajwa kunufaika na fedha hizo, tungekuwa na Mamlaka ya kujiamulia mambo yetu yasingetokea hayo”, alisema Maalim Seif. 
Katika hatua nyengine, Maalim Seif amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa ya kuwatisha wananchi wanaoamua kukihama chama cha Mapinduzi na kujiunga na upinzani.
Akizindua matawi mapya ya CUF, katika vijiji vya Kivunge, Tazari na Nungwi katika Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja amesema amesikitishwa kusikia kuna baadhi ya viongozi wanatoa vitisho hivyo ambavyo ni kinyume na Katiba ya nchi.
Maalim Seif alisema hayo baada ya wanachama wa CUF katika kijiji cha Tazari kusema kwamba wamechukua uamuzi mgumu wa kujiunga na CUF na kufungua tawi katika eneo hilo, kwa sababu kwa miaka mingi wamekuwa wakitishwa na kunyimwa uhuru wa kujiunga na chama zaidi ya CCM.
“Kitendo cha kufungua tawi hapa Tazari ni cha kihistoria, kwa miaka yote haikuwezekana na tumekuwa tukitishwa na tukiaminishwa kuwa chama pekee cha kujiunga ni CCM”, alisema Katibu wa tawi hilo, Simai Uyobi katika risala ya wanachama wa tawi hilo.
Maalim Seif aliwataka wananchi wasiogope kujiunga na CUF na kukihama chama cha CCM kwa sababu kujiunga na chama wanachotaka ni haki yao.
“Hakuna mwenye haki ya kukuzuieni kujiunga na chama mnachokipenda, nasema yoyote atakayekuja kukupeni vitisho niambieni tu nitapambana naye”, alisema Maalim Seif.
Katika kijiji cha Tazani ambacho kwa miaka mingi ni miongoni mwa ngome za chama cha CCM katika mkoa wa Kaskazini Unguja, wanachama wapya 40 walipewa kadi za CUF baada ya kuzirejesha za CCM.
Akihutubia mara baada ya kuzindua tawi la CUF Nungwi, Katibu Mkuu huyo alisema wananchi wa Zanzibar wanapaswa kulinda hadhi na heshima ya Zanzibar na waikatae Katiba inayopendekezwa pale watakapoletewa kwa ajili ya kuipigia kura ya maoni.
“Najua hakuna Mzanzibari asiyeumwa na Zanzibar, haya mambo ya kushabikia sera za vyama na kuididimiza Zanzibar hayana maana, Wazanzibari tuungane tuitetee Zanzibar yetu”, alisema Maalim Seif.
Alisema vyama vya siasa huanzishwa na kufa, lakini nchi ndiyo inayobaki, hivyo ni wajibu wa wananchi bila kujali itikadi zao kulinda heshima ya nchi badala ya kukumbatia vyama.
   
“Vyama vya siasa ni mambo ya kupita hamkumbuki zamani kulikuwa na Afro Shirazi Party, Hizbu, TANU na Umma Party vyama hivyo leo viko wapi, lakini Zanzibar ipo na wala haitakufa”, alisema.
Aidha, aliwataka wanachama wa CUF kujenga matawi na ofisi za kisiasa kwa kile alichoeleza kuwa chama hicho ni kikubwa na kinapaswa kujenga taswira njema kutokana na mipango yake ya maandalizi ya kushika dola katika uchaguzi mkuu ujao.
Katika risala ya wanachama wa CUF jimbo la Tumbatu iliyosomwa kwenye mkutano wa hadhara na Othman Hazir Othman walisema wamesikitishwa na kitendo cha Mbunge wa jimbo la Tumbatu wakati wa vikao vya Bunge Maalum la Katiba alipowasemea kuwa wananchi wa jimbo hilo wanaunga mkono muundo wa Muungano wa Serikali mbili.
Othman alisema wananchi walio wengi katika jimbo hilo wanaelewa kuwa muundo wa Muungano wa Serikali mbili ndicho kitanzi cha Zanzibar, hivyo hawawezi kuuunga mkono na wanataka Zanzibar yenye mamlaka 

No comments: