Tuesday 28 April 2015

Kona ya Julius Mtatiro na uchambuzi wa Wagombea uraisi wa CCM

DK. EMMANUEL JOHN NCHIMBI:  NI NANI URAIS CCM?
HISTORIA YAKE
Dk Emmanuel John Nchimbi alizaliwa Desemba 24, 1971 mkoani Mbeya, (atafikisha miaka 44 Desemba mwaka huu). Elimu yake ya Msingi aliianzia jijini Dar es Salaam katika Shule ya Msingi Oysterbay kati ya mwaka 1980 – 1986. Baba yake mzazi, Mzee John Nchimbi kutoka wilayani Songea ni askari mstaafu wa Jeshi la Polisi na wakati anastaafu alikuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara. Mzee Nchimbi pia amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kwa vipindi viwili kupitia kundi la majeshi na baadaye katibu wa CCM wa mkoa, alikoma kushiriki masuala ya kisiasa mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa.

Dk Nchimbi alijiunga na elimu ya sekondari kwenye Shule ya Sekondari Uru kati ya mwaka 1987 – 1989 (kidato cha I – III) halafu akahamia Shule ya Sekondari Sangu na kukamilisha kidato cha nne mwaka 1989 – 1990.
Nchimbi alisoma Shule ya Sekondari ya Forest Hill, Morogoro, masomo ya kidato cha V na VI mwaka 1991 – 1993. Alijiunga katika Chuo cha IDM Mzumbe (Morogoro) na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Utawala (mwaka 1994 – 1997).
Wakati anahitimu IDM, pia alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mwaka uliofuatia (1998), alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM).
Dk Nchimbi amewahi kuajiriwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kati ya mwaka 1998 – 2003.
Alisoma shahada ya uzamili ya usimamiz wa biashara Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2001 – 2003 akibobea kwenye maeneo ya (benki na fedha).
Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda (mwaka 2003–2005) na (mwaka 2008 – 2011) alisoma na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Dk. Nchimbi amemuoa Jane na wana watoto watatu.
Dk Nchimbi alirudi nyumbani kwao (Songea Mjini) kuanza harakati za ubunge tangu alipokuwa anaongoza UVCCM. Ilipotimu mwaka 2005, aliingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi akakutana na Edson Mbogoro wa Chadema aliyekuwa mpinzani wake mkuu. Dk Nchimbi alisaidiwa na mtandao mkubwa wa CCM na kupata ushindi wa asilimia 67.6 dhidi ya asilimia 30.5 za Mbogoro.
Mara tu baada ya kuwa mbunge, Rais Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, hii ilikuwa Januari 2006, alidumu kwenye wizara hiyo hadi Oktoba 2006 alipohamishiwa kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana – hapa pia alikuwa Naibu Waziri tangu Oktoba 2006 hadi Februari 2008 kisha Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa ambako pia alikuwa Naibu Waziri hadi Novemba 2010.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk Nchimbi alijitosa tena Jimbo la Songea Mjini. Kampeni za 2010 zilimnyima usingizi pamoja na kuwa chama chake kilikuwa kimechukua asilimia zaidi ya 90 ya vijiji, vitongoji na mitaa mwaka 2009.
Kama kawaida, alipambana tena na Mbogoro wa Chadema na kumshinda kwa mara ya pili, japo safari hii Dk Nchimbi akipoteza takriban ushindi wa asilimia 10 ukilinganisha na mwaka 2005. Katika uchaguzi huo, alipata asilimia 59.9 dhidi ya 37.48 za Mbogoro.
Upandaji vyeo wa Nchimbi uliendelea, Rais Kikwete alimpa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo akiwa Waziri kamili, alidumu hapo hadi Mei 2012 alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu Desemba 2013 kwa shinikizo, baada ya ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, iliyoongozwa na Mbunge wa Kahama, James Lembeli juu ya “Oparesheni Tokomeza”.
Wakati watu wengi wanadhani Nchimbi aling’olewa uwaziri kwa shinikizo la Bunge, ukweli ni kuwa aliondoka kwa shinikizo la vikao vya CCM, “party caucas”.
Ripoti ya kamati ya Lembeli ilieleza wazi kuwa anayepaswa kuwajibishwa ni waziri mmoja tu (Dk Mathayo David, aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) lakini “caucas” ya CCM ikawaangushia mzigo wengine watatu akiwamo Dk Nchimbi.
Lembeli aliwahi kukaririwa akisema: “Ripoti ilimtaja Dk Mathayo na sababu tulitoa mle ndani. Hao wengine watatu si kamati, ni mambo ya hukohuko kwenye party caucas. Ndiyo maana mara ya mwisho nilikwenda pale nikasema kuwa (Khamis) Kagasheki (Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, anaonewa.”
MBIO ZA URAIS
Dk Nchimbi alianza mbio za urais tangu alipokuwa naibu waziri kwenye awamu ya kwanza ya uongozi wa Rais Kikwete lakini nimeambiwa kuwa alikuwa anajipanga kistratejia kwa kuzingatia kuwa mbio hizo ndani ya CCM huhitaji fedha nyingi, ambazo hana.
Lakini kwa sababu amekulia ndani ya CCM amekuwa akifahamu kuwa fedha peke yake si kila kitu na kwamba mtu anayejipanga na kuwa chaguo muhimu hufika mbali.
Ndiyo maana ameendelea kuwa mtiifu kwa chama chake hata alipoondoka katika uwaziri kwani anajua kuwa safari za siasa ndani ya CCM huhitaji utulivu ili ufanikiwe.
NGUVU YAKE
Tangu zamani, Dk Nchimbi ni mmoja wa vijana ambao wamekuwa na ushawishi mkubwa ndani ya CCM, unaweza kumfananisha na Amos Makala, Mwigulu Nchemba, January Makamba na Nape Nnauye, japokuwa kila mmoja ana sifa zake binafsi.
Ushawishi wa Nchimbi uliishi hata alipokabidhiwa jukumu la kuongoza UVCCM iliyokuwa maarufu na imara kuliko hii ya sasa. Vijana kadhaa niliozungumza nao ndani ya CCM wanasema Dk Nchimbi anawavutia katika mambo mengi hadi leo.
Jambo jingine linalompa nguvu, ni bahati. Dk Nchimbi ni mtu mwenye bahati. Miaka yote aliyokaa ndani ya CCM amekuwa mtu wa kupanda ngazi tu, kutoka kuongoza UVCCM hadi kuwa mkuu wa wilaya hadi kuwa mbunge hadi kuwa naibu waziri wa wizara mbili tofauti hadi kuwa mbunge kipindi cha pili hadi kuwa waziri kamili katika wizara mbili kabla hajaondolewa.
Ndani ya miaka 14, amepitia nyadhifa nyingi na harakaharaka, ni bahati iliyoje! Dk Nchimbi ni mchapakazi na rafiki. Alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani baadhi ya askari wananiambia kuwa ilikuwa rahisi kuwasiliana naye na kumpa malalamiko yao.
Baadhi ya askari kutoka makao ya polisi wananiambia kuwa pamoja na matatizo makubwa wanayokutana nayo kiutendaji na ambayo Serikali imeshindwa kuyatatua, walau hupata liwazo kutoka kwa watendaji ambao wako karibu yao. Dk Nchimbi aliweza jambo hili.
UDHAIFU WAKE
Moja ya udhaifu wa Dk Nchimbi ni ukaidi. anapoamini jambo lake hakupi nafasi ya kukusikiliza. Mathalan, wakati wa vurugu zilizotokana na sakata la gesi Mtwara, wananchi walipata madhara makubwa kukiwa na ushahidi wa wazi wa ubakaji, kuporwa mali zao, kupigwa na askari bila huruma huku wakiwa hawana silaha, kuteswa katika kambi za jeshi bila kupelekwa polisi na mahakamani.
Dk Nchimbi alipokuwa anapewa malalamiko hayo na wananchi, alikuja juu na kusisitiza kuwa Serikali inatekeleza wajibu wake. Kukaa kwake kimya kunamaanisha kuwa ana uwezo pia wa kufumbia macho mambo ya hatari yanapowakabili wananchi ilimradi tu alinde kazi yake na hata chama anachokitumikia.
Kuna nyakati Dk Nchimbi amekuwa kiongozi asiyeweza kutoa majibu kwa maswali magumu juu ya matukio ya hatari, ya kikatili na kuhuzunisha yaliyotokea wakati yeye ndiye mwenye dhamana. Alipokuwa na dhamana ya ulinzi wa ndani wa nchi kuna matukio mengi makubwa yalijitokeza na hadi leo hakuwahi kuyatolea ufafanuzi na majibu ya kutosha.
Moja ni tukio la utekaji na uteswaji wa Dk Stephen Ulimboka lililotokea usiku wa Juni 26, 2012. Kuuawa kwa Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, tena akiwa kazini na mikononi mwa vyombo vya Dola Septemba 2, 2012 huko Nyololo, Iringa.
Baada ya kifo cha Mwangosi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa ambaye aliingilia majukumu ya kamanda wa polisi wa wilaya kwa kuvamia eneo ambalo Chadema walikuwa wakifungua matawi na kuwa kichocheo cha amri iliyosababisha kuuawa kwa Mwangosi, alipandishwa cheo. Haya yalitokea chini ya uongozi wa Dk Nchimbi.
Pili, ni kupigwa risasi na kuuawa Mwandishi Issa Ngumba (45) wa Radio Kwizera aliyekuwa anafanyia kazi zake katika Wilaya ya Kakonko, Kigoma Januari 2013, katika mazingira ya kutatanisha. Dk Nchimbi akiwa waziri na hadi alipoondoka, tukio hili limebakia tu hewani.
Tatu, tukio la Mwandishi wa Gazeti la Tanzania Daima, Shaaban Matutu kupigwa risasi na polisi akiwa nyumbani kwake Dar es Salaam kwa maelezo kuwa “kimakosa polisi walidhani Matutu ni jambazi”. Pamoja na uzembe huo wa polisi, hakuna hatua zilizochukuliwa.
Nne, siku wa Jumanne ya Machi 5 kuamkia Machi 6, 2013, Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Ltd, ambaye pia Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda alivamiwa na kujeruhiwa vibaya akiwa nje ya lango la kuingilia nyumbani kwake Mbezi Juu, Dar es Salaam.
Kibanda aliumizwa kwa kiwango kikubwa. Alitobolewa jicho la kushoto, akaumizwa vibaya kichwani kiasi cha kusababisha kuvunjika kwa baadhi ya mifupa ya kichwa. Aling’olewa meno mawili na kucha mbili, tena bila ganzi. Watekaji hawa walimkata pingili ya kidole cha pete chini ya kucha na kuondokana nayo.
Hadi Dk Nchimbi anaondoka katika Wizara ya Mambo ya Ndani, masuala yote hayo hayakuwahi kutolewa majibu stahiki na hadi leo watu wanajiuliza nini kilichokuwa kinaendelea. Wakati wa uongozi wake ndipo waandishi wa habari na wanaharakati walipata mateso makubwa.
Pamoja na kuwa Dk Nchimbi hakushiriki kumuua Mwangosi, kumtesa Ulimboka, Kibanda au kuwaua waandishi wengine lakini ilitarajiwa kuwa ataonyesha msimamo imara wa wizara yake dhidi ya wote waliohusika na vitendo hivyo.
Udhaifu huo wa kiusimamizi hauwezi kupita hivihivi bila kuhojiwa na ni moja ya mambo ambayo Watanzania hawana mtu wa kumuuliza, zaidi ya aliyekuwa mlinzi wa usalama wa ndani ya nchi wakati huo, Dk Nchimbi.
NINI KINAWEZA KUMFANYA APITISHWE
Moja ya mambo yanayoweza kumbeba Dk Nchimbi ni kuaminiwa. Taarifa sahihi ndani ya CCM zinathibitisha kuwa yeye ni mmoja kati ya vijana wanaoaminiwa mno na chama hicho “vijana wa chama”, wenye msimamo wa kuitetea CCM muda wote, walio tayari kufanya lolote kwa ajili ya chama chake na waliokulia ndani ya CCM.
Kuaminiwa huku na “mabosi” ndani ya chama, kunamfanya awe na turufu mkononi. Lakini yote haya yanachagizwa na uaminifu wake, katika wizara zote alizopita, hatukuwahi kusikia taarifa zinazothibitishwa kuwa ameshiriki au kukwapua fedha za umma na kuzitumia kwa manufaa yake. Jambo hili linamuinua zaidi.
Pili, dhana ya ujana inambeba. Dk Nchimbi ni mmoja wa vijana ambao wanaonekana kuifahamu CCM na amewahi kuiongoza UVCCM na hivyo anajua mahitaji ya vijana ndani ya CCM na ndani ya nchi. Ukiongezea na sababu kuwa yeye ni kijana, ina maana kuwa yuko kwenye hesabu za CCM ikiwa chama hicho kitahitaji kuwa na mgombea kijana wa kisasa.
Pia, uzoefu unaonyesha kuwa watu wote ambao wamewahi kuongoza nchi hii waliwahi pia kupitishwa kwenye “wizara nyeti”, baadaye imewahi kutokea kuwa wakaingia kwenye rekodi kubwa za uongozi wa nchi.
Wizara hizo mara nyingi huwa ni kama ulinzi wa nchi, mambo ya ndani, mambo ya nje, fedha n.k. Kwa mfano, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Benjamin Mkapa, ambaye alimfuatia aliwahi kuongoza Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje kama ilivyo kwa Rais Kikwete.
Kama hivyo ndivyo, basi fursa aliyoipata Dk Nchimbi kuongoza Wizara ya Mambo ya ndani inamuweka kwenye ulingo sawa na wenzake na jambo hili lisipuuzwe.
NINI KINAWEZA KUMWANGUSHA?
Jambo moja kubwa linaloweza kumuangusha ni nguvu ya makundi ya wasaka urais ndani ya CCM. Kwa bahati mbaya yeye hayumo kwenye makundi makubwa na jambo hilo ni hatari ikiwa makundi hayo yataizidi CCM nguvu.
Pili, sababu za CCM kumuondoa kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kumpumzisha uwaziri wakati ripoti ya Lembeli juu ya Operesheni Tokomeza haikuwa inamtaja, zinaweza pia kurudi katika majadiliano yatakayohusu upitishwaji wake. Kwamba inawezekana CCM inajua vizuri upungufu wa Dk Nchimbi kwenye usimamizi wa ofisi za umma na ndiyo maana ilikuwa tayari kumwajibisha hata kama kamati ya Bunge haikupendeza hivyo.
Mwisho ni rekodi yake ya utendaji katika wizara alizopitia hususan, Mambo ya Ndani. Kwamba ikiwa CCM inajua vizuri upungufu wa wizara hii nyeti wakati inaongozwa na Dk Nchimbi hasa kuhusu matukio makubwa niliyoyataja kwenye kipengele cha udhaifu na ikiwa chama chake kina uthibitisho kuwa hakutimiza wajibu wake ipasavyo, hukumu yake inaweza kutokea pia kwenye eneo hili.
ASIPOPITISHWA (MPANGO B)
Mpango mmoja mkubwa wa Dk Nchimbi ikiwa hatapitishwa kugombea urais itakuwa kurudi Songea Mjini kugombea ubunge kwa mara nyingine. Wasiwasi wangu ni kuwa, Jimbo la Songea Mjini kwa sasa si zuri kisiasa kwa CCM, wananchi wana malalamiko mengi hivyo atahitaji nguvu kubwa kushinda.
Ikitokea ameangushwa kwenye ubunge, bado atakuwa na nafasi ya kushiriki katika siasa za nchi kupitia nyadhifa za kiuongozi au kiuteuzi ikiwa bado CCM itapewa ridhaa.
HITIMISHO
Kwa kiasi kikubwa, Dk Nchimbi ni mmoja wa vijana wa Kitanzania ambao wana uwezo mzuri akipewa nafasi. Nakumbuka wakati anaongoza pale Bunda akiwa mkuu wa wilaya, alihimiza ujenzi wa sekondari 17 na zikafunguliwa zote siku moja. Amewahi pia kuthubutu kuwavua madaraka na kuwasimamisha maofisa waandamizi wanne wa jeshi la polisi kutokana na ukiukwaji wa maadili, hakuna rekodi sahihi kwa mawaziri wengine wa mambo ya ndani kuwahi kuchukua hatua kama hizo.
Historia yake na ukomavu wa uongozi inamtofautisha kabisa na vijana wenzake kama January Makamba, Dk Hamisi Kigwangalla na Lazaro Nyalandu ambao hawakuanza uongozi ngazi za chini kabisa za chama hicho.
Namuona Dk Nchimbi kuwa ni mmoja wa vijana tishio kabisa kwa wazee wa ndani ya CCM wanaosaka uteule katika uchaguzi wa mwaka huu. Wakati ni ukuta na ukifika tutajua, namtakia kila la heri Dk Nchimbi aendelee na safari yake ya kisiasa kwa utulivu.
KUHUSU MCHAMBUZI:
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi na Lugha, Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB) – Anapatikana kupitia +255787536759,(juliusmtatiro@yahoo.com) Uchambuzi na huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi). (Uchambuzi huu umechapishwa na Gazeti la Mwanchi la Jumanne, 28 Aprili 2015).
umechapishwa na Gazeti la Mwanchi la Jumanne, 28 Aprili 2015).

No comments: