Thursday 30 April 2015

TAARIFA YA UKAWA LEO TAARIFA KWA UMMA, DAR ES SALAAM, ALHAMIS, 30 APRIL 2015 UCHAGUZI MKUU OKTOBA 2015 LAZIMA, KIKWETE ASIONGEZEWE MUDA, KURA YA MAONI BAADAE



MOJA WA KATIBA YA WANANCHI (UKAWA),
DAR ES SALAAM,
TANZANIA.

TAARIFA KWA UMMA,
DAR ES SALAAM, ALHAMIS, 30 APRIL 2015


UCHAGUZI MKUU OKTOBA 2015 LAZIMA, KIKWETE ASIONGEZEWE MUDA, KURA YA MAONI BAADAE


V
yama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) leo vimetoa msimamo wao juu ya njama za kuahirisha Uchaguzi Mkuu unaotakiwa kufanyika Oktoba mwaka huu. UKAWA imesisitiza kwamba kuahirisha Uchaguzi Mkuu huo ni sawa na kumuongezea Rais Jakaya Kikwete na Chama chake cha Mapinduzi muda wa kuendelea kutawala Tanzania. UKAWA imesema jaribio lolote la kuahirisha Uchaguzi Mkuu kwa kisingizio chochote kile litakuwa kinyume na Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na litahesabika kuwa ni sawa na mapinduzi dhidi ya Katiba (constitutional coup d’etat). Msimamo wa UKAWA unafuatia kumalizika kwa Kikao cha Viongozi Wakuu wa Vyama vinavyounda UKAWA (UKAWA Summit) kilichofanyika katika Makao Makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), jijini Dar es Salaam kati ya tarehe 28 na 29 Aprili mwaka huu.

Akielezea msimamo wa UKAWA juu ya suala hili, mwenyeji wa Kikao hicho na Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba alisema kwamba kuna dalili za kuonyesha kwamba zipo njama za kuahirisha Uchaguzi Mkuu na kumuongezea Rais Kikwete na CCM muda wa kutawala. “Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijaanza maandalizi yoyote kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu licha ya kwamba imebaki miezi sita tu Uchaguzi huo ufanyike kwa mujibu wa Katiba. Shughuli zinazohusiana na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu na vifaa vinavyotumika kwa ajili yake ambavyo kwa taratibu za miaka yote huanza kufanyika angalau mwaka mmoja na nusu kabla ya Siku ya Uchaguzi hazijaanza kufanyika, vifaa vinavyohitajika havijanunuliwa na fedha kwa ajili hiyo hazijatengwa hadi sasa.”

Profesa Lipumba aliongeza kwamba jambo hili limefanyika kwa makusudi kwa sababu vyama vya UKAWA vimekuwa vinapigia kelele suala la maandalizi ya Uchaguzi Mkuu tangu mwaka 2012. “Licha ya madai ya muda mrefu ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 imevurugwa kwa makusudi kwa kutokutenga fedha kwa ajili hiyo katika bajeti ya Serikali tangu mwaka 2012, Serikali hii ya CCM haijatoa fedha kwa NEC kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu. Badala yake, NEC imeendelea kutangaza kwamba inafanya maandalizi kwa ajili ya Kura ya Maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa ambayo imepitwa na muda kisheria na haiwezi kufanyika tena bila kwanza kufanyika kwa marekebisho katika Sheria ya Kura ya Maoni (the Referendum Act) ya mwaka 2013.”

Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, Kura ya Maoni ilitakiwa ifanyike ndani ya siku 124 kutoka tarehe Rais Kikwete alipotoa Tangazo la Kura ya Maoni na kutamka kuwa Kura hiyo itafanyika tarehe 30 Aprili, 2015, yaani leo. Profesa Lipumba alisema: “Kwa Sheria ya Kura ya Maoni ilivyo kwa sasa, hakuna uwezekano wa Kura ya Maoni kufanyika tena bila kwanza kufanya marekebisho ya Sheria hiyo. Kila hatua inayotakiwa kuchukuliwa chini ya Sheria hiyo imewekewa muda wake na muda huo haubadiliki. Tangazo la Kura ya Maoni likishatolewa na tarehe kutangazwa haibadilishwi kwa sababu yoyote ile. Hakuna namna yoyote ya kuahirisha Kura ya Maoni na kuifanya tarehe nyingine yoyote.”

Profesa Lipumba aliongeza: “Haya ndio masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni. Yasipofuatwa hakuna namna ya kuyarekebisha bila kwanza kurekebisha Sheria yenyewe. Na hadi sasa Serikali hii ya CCM haijapeleka Muswada wa Sheria kuirekebisha Sheria hiyo ili kuwezesha Kura ya Maoni kufanyika kwa tarehe nyingine. Tunashangazwa na Tume inayoongozwa na aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ambayo ndio mahakama ya juu kabisa katika nchi yetu, na Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye ni Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali, kuendelea kutangaza kwamba Kura ya Maoni itafanyika kwa terehe itakayotangazwa baadae wakati Tume inafahamu kwamba jambo hilo haliwezekani kisheria. Kama bado CCM na washirika wake wanataka Katiba Inayopendekezwa ipigiwe Kura ya Maoni na Watanzania ni lazima wapeleke Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kura ya Maoni Bungeni. Vinginevyo itakuwa na ubatilifu mtupu kama tuliouona wakati wa Bunge Maalum.”

Aidha, UKAWA imesema haiko na haitakuwa tayari kuunga mkono jitihada zozote za kumuongezea Rais Kikwete na CCM muda wa kutawala kwa kuahirisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Kwa mujibu wa Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Mheshimiwa James Mbatia, haijawahi kutokea Uchaguzi Mkuu ukaahirishwa kwa sababu yoyote tangu mwaka 1960 tulipofanya Uchaguzi Mkuu uliotupatia Serikali ya Madaraka ya Ndani hadi sasa.
Mheshimiwa Mbatia alisema: “Watu hawa wanafahamu kuwa tumekuwa tukifanya Uchaguzi Mkuu kila baada ya miaka mitano tangu mwaka 1960. Hata mwaka 1980, miezi michache baada ya kutoka vitani dhidi ya nduli Iddi Amin wa Uganda na licha ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kutangaza miezi 18 ya kujifunga mikanda kwa sababu ya hali mbaya ya uchumi iliyosababishwa na Vita ya Uganda, hatukuahirisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo. Watu hawa wanafahamu kwamba Katiba yetu hairuhusu Uchaguzi Mkuu kuahirishwa kwa sababu yoyote ile. 

Wanafahamu kwamba tangu mwaka 1985, Rais anatakiwa atumikie vipindi viwili tu vya miaka mitano mitano. Wanafahamu kwamba maisha ya Bunge ni miezi sitini au miaka mitano kuanzia tarehe ya Uchaguzi Mkuu na haiwezekani kwa maisha hayo kuongezewa muda kikatiba bila ya kufanyika Uchaguzi Mkuu. Na wanafahamu kwamba Rais Kikwete anakamilisha kipindi chake cha pili mwezi Oktoba mwaka huu na maisha ya Bunge la Kumi yanamalizika mwezi huo. Kuruhusu Uchaguzi Mkuu uahirishwe kwa kisingizio chochote kile ni kuwazawadia wazembe na kuwaongezea mafisadi wanaolimaliza taifa letu kwa ufisadi muda wa kuendelea na ufisadi huo. UKAWA haitakubali kuruhusu jambo hilo litokee.”

Aidha, UKAWA imesisitiza kwamba haitakubali na haitaunga mkono jaribio lolote la kufanya marekebisho katika Katiba ya sasa kwa lengo la kumuongezea Kikwete, chama chake na Serikali muda wa kutawala. Akielezea msimamo huo, Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA na Mwenyekiti wa chama cha National League for Democracy (NLD) Dkt. Emmanuel Makaidi amesisitiza kwamba suala la vipindi viwili vya miaka mitano mitano kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ni nguzo kuu muhimu ya Katiba ya sasa na UKAWA haitakubali nguzo hiyo iguswe au kufumuliwa kwa sababu au kisingizio chochote kile. Dkt. Makaidi alisema: “Kubadilisha Katiba ya sasa kwa lengo la kuahirisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka sio tu kutaathiri misingi muhimu ya Katiba ya sasa, bali pia kutahatarisha amani ya nchi yetu. Tumeona kinachoendelea Burundi baada ya Rais Pierre Nkurunzinza na chama chake kuamua kujiongezea muda wa kutawala nchi hiyo. Tumeona yanaoendelea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) baada ya Joseph Kabila kutaka kufanya hivyo hivyo. Kikwete na wanaCCM wenzake wasitake kuiingiza nchi yetu katika majanga yasiyokuwa na sababu.”

Kwa upande mwingine, UKAWA imeitaka NEC kuhakikisha kwamba wananchi wote wenye sifa ya kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wanaandikishwa kwenye Daftari hilo. Katika Mkutano wake na vyama vya siasa uliofanyika Dar es Salaam tarehe 9 Julai mwaka jana, Mwenyekiti wa Tume Jaji Damian Lubuva alisisitiza kwamba NEC ilikuwa na uwezo na vifaa vya kuandikisha takriban wapiga kura milioni 24 katika vituo vya kuandikishia 40,000 nchi nzima kwa muda wa siku 14 katika kila kituo cha kuandikishia. Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA na Mwenyekiti wa CHADEMA Mheshimiwa Freeman Mbowe alieleza kushangazwa kwa UKAWA na matamko ya Tume kwamba sasa Tume itaandikisha wapiga kura kwa muda wa siku saba katika kila kituo.

Mwenyekiti Mbowe alisema: “Tume iliwaahidi Watanzania kwamba watu wote wenye sifa wataandikishwa katika Daftari la Wapiga Kura. Sisi wa UKAWA tulishauri muda wa kuandikisha uongezwe hadi angalau siku 28 kama ilivyokuwa kwa Uchaguzi Mkuu uliopita lakini Tume iling’ang’ania kwamba muda wa siku 14 unatosha. Leo Tume inapunguza muda huo wakati tunafahamu kwamba Tume ina vifaa pungufu vya kuandikishia wapiga kura kuliko ilivyoomba kupatiwa na Serikali hii ya CCM. Hii ni njama ya Tume na ya Serikali hii ya CCM kuhakikisha wapiga kura wengi hawaandikishwi. Sisi UKAWA hatutakubali jambo hilo litokee.”

Wakati huo huo, Viongozi Wakuu wa UKAWA wameeleza kushangazwa na taarifa zilizosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini kwamba Chama cha NCCR-Mageuzi kimejitoa au kimeandika barua ya kuomba kujitoa kwenye UKAWA. Viongozi hao wamesema kwamba taarifa hizo ni uzushi mtupu unaosambazwa na wapiga ramli na wanajimu wa kiama cha UKAWA kwa lengo la kuipatia CCM na vyama vibaraka wake ahueni ya kisiasa. Akikanusha taarifa hizo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Mheshimiwa Mbatia amesema kwamba yeye mwenyewe na Katibu Mkuu wake Mosena Nyambabe pamoja na maafisa wa chama chake wamekuwa katika hatua zote za vikao vya UKAWA kuanzia Kamati ya Ufundi na ile ya Wataalam hadi Kikao cha Viongozi Wakuu kilichomalizika jana.

Mheshimiwa Mbatia alisisitiza: “Tangu juzi tupo hapa tukijadiliana namna ya kupata wagombea wa UKAWA wa ngazi zote kuanzia Urais, Ubunge hadi Udiwani. Kwa kiasi kikubwa tumeshakamilisha kazi ya kupata wagombea Ubunge wa UKAWA. Tumeshapata muafaka kwa zaidi ya asilimia 95 ya majimbo yote ya Uchaguzi Tanzania, na majimbo 12 yaliyobakia tunaendelea kuyashughulikia na tutayapatia ufumbuzi muda si mrefu. Tunaendelea na majadiliano juu kupata Mgombea Urais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano atakayepeperusha bendera ya UKAWA. Tumeshakamilisha kazi hiyo kwa upande wa Zanzibar na tutaikamilisha kwa upande wa Jamhuri ya Muungano katika muda muafaka. UKAWA iko imara sasa kuliko kipindi kingine chochote tangu Bunge Maalum mwaka jana. Hao wanaosambaza uzushi kwamba tumefarakana na kwamba sisi NCCR tumejitoa au tunataka kujitoa watafute hoja nyingine. Hii imebuma.”

Mungu Ibariki Tanzania!
Imetolewa na;


---------------------------------------
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba,
Mwenyekiti – CUF – Chama Cha Wananchi,


-----------------------------------
Mh.Freeman Mbowe (MB),
Mwenyekiti - CHADEMA


--------------------------------------
Mh.James Francis Mbatia(MB),
Mwenyekiti – NCCR MAGEUZI.


--------------------------------------
Mh. Dkt. Emmanuel Makaidi

Mwenyekiti – NLD.


No comments: