Thursday, 21 May 2015

Balozi Amina Salum Ali atangaza kuwania Urais Tanzania 2015

5/21/2015 11:54:00 AM
Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika katika Umoja wa Mataifa, Balozi Amina Salum Ali akiwa na Rais Kikwete baada ya kufungua rasmi jengo la ghorofa sita la Ofisi za Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Machi 30, 2015.

Wakati vikao vya maamuzi vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) vikianza kesho, mwanasiasa mkongwe, Amina Salum Ali, amekuwa mwanamke wa kwanza wa daraja lake ndani ya chama hicho kutangaza wazi nia ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu nia yake hiyo, mwanasiasa huyo ambaye pia ni Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa (UN), alisema wanawake wamekuwa wanyonge kugombea nafasi za juu za uongozi kwa kukosa fedha, lakini sasa ni wakati mwafaka kwao kujiamini katika jamii kwani uongozi siyo fedha bali ni uzalendo, kujikubali na kujiamini.

“Nimeona nina uzalendo, ninajiamini na ninaweza kuifikisha nchi yangu katika uchumi wa kwanza kwa kutumia rasilimali zetu zikiwamo gesi, mafuta, kilimo na utalii. Ninajiamini kwamba wakati wangu umefika kuwaongoza Watanzania wenzangu kwa kushika nafasi za juu,” 
alisema mwanasiasa huyo mkongwe.

Amina ambaye aliwahi kushika nafasi za juu za uongozi Zanzibar na Tanzania Bara, ukiwamo uwaziri wa fedha Zanzibar, alisema serikali inatambua mchango wa wanawake katika jamii hivyo kupewa nafasi kubwa kama vile ujaji na uhakimu ili kuongeza zaidi ufanisi wao kiutendaji.

“Wanawake wengi wanaogopa kujitokeza wakihofia kugombea nafasi za juu za uongozi kwamba kunahitaji fedha hivyo wanaishia kuwa wanyonge. Siyo kweli, wajitokeze kwa wingi ili kitimiza ndoto za kuwajibika kwa taifa letu,” 
alisema. 

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, wanawake wamepigana sana dhidi ya mfumo dume na kwamba baada ya miaka 20 ya maazimio ya Mkutano wa Dunia wa Wanawake uliofanyika mjini Beijing, China mwaka 1995, hali kwa sasa imebadilika na wanawake wanapewa nafasi mbalimbali za uongozi.

Alisema sheria hazitoshelezi kumlinda mwanamke, lakini mfumo dume umepungua kwa kiasi kikubwa hata kama haijafikia asilimia 50 kwa 50.

“Jambo kubwa kwa mwanamke ni kujiamini katika mambo yote… wanawake wa Tanzania hatuna utaratibu wa kuchangiana katika harakati za uchaguzi. Utaratibu wa mwanamke kupata fedha za mitaji kwa hapa nchini bado mgumu hasa katika mabenki lakini tusiogope. Mimi nina amini ninaweza kuiongoza jamii yetu,“ 
alisema Balozi Amina.

Balozi Amina ametangaza ni ya kuwania nafasi hiyo kubwa kuliko zote nchini wakati kesho vikao vikao vya juu vya maamuzi vikitarajiwa kuanza kwa ajili ya maandalizi ya mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa udiwani, ubunge na urais Oktoba, mwaka huu.

Vikao hivyo ni Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec). Kesho itaanza CC na kufuatiwa na Nec ambayo inahitimisha mchakato huo Jumapili ijayo.

Baadhi ya makada wameshatangaza nia ya kuwania nafasi hiyo na wengine wanatajwa.

Waliotangaza nia ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba; Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba; Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangallah na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya.

Makada wanaotajwa kugombea nafasi ya hiyo kupitia chama hicho ni Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Steven Wasira; Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli; Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha Rose Migiro na Spika wa Bunge, Anna Makinda.

Wengine ni mawaziri wakuu wastaafu, Fredrick Sumaye na Edward Lowassa; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi. 

Balozi Amina alihitimu Chuo Kikuu cha New Delhi (India) - shahada ya kwanza ya uchumi (B.A), mwaka 1079, amehitimu Institute of Management Pune, India - Diploma ya utawala wa mambo ya fedha na utafiti wa uendeshaji mwaka 1980, pia mwaka 1981 alihitimu Chuo Kikuu cha Pune, India - (Symbiosis College of management) -MBA in Marketing (Masoko) na mwaka 1983 Chuo Kikuu cha Helsinki, Finland - Diploma ya utafiti wa masoko na uuzaji wa bidhaa nje (mafunzo maalum ya PRODEC).

NYADHIFA ALIZOPITIA


Mwaka 1981 hadi 1982 Mchumi Mwandamizi -Tume ya Mipango Zanzibar, mwaka 1982 hadi 1983 Mkurugenzi Biashara za Nje - Wizara ya Biashara ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na mwaka 1983 hadi 984 Katibu Bodi ya Biashara Zanzibar-Wizara ya Biashara Zanzibar.

Nafasi nyingine ni, mwaka 1984 hadi 1985, Mchumi Mwandamizi - Tume ya Mipango, Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar, mwaka 1985 hadi 1990- Mbunge Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, mwaka 1985 hadi 1986- Naibu Waziri wa Fedha Wizara ya Fedha na Mipango Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 1986 hadi 1989- Waziri wa Nchi ,Wizara ya Mambo ya Nje.

Nyingine ni, mwaka 1989 hadi 1990- Waziri wa Nchi Wizara ya Fedha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 1990 hadi 2000 -Mbunge Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Baraza la Wawakilishi Zanzibar, mwaka 2001 hadi 2005- Waziri wa Fedha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , Mjumbe wa Tume ya Mipango Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mwaka 2005 hadi 2006- Mjumbe Baraza la Wawakilishi .

Nyingine ni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mwaka 2006 - Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) kwenye Umoja wa Mataifa.

UZOEFU KATIKA CHAMA

Mwaka 1968 alijiunga na Umoja wa Vijana wa ASP (ASP Youth League) na kuendelea na uanachama hadi kuzaliwa kwa CCM mwaka 1977.

Mwaka 1977 alijiunga na Chama Cha Mapinduzi baada ya kuunganishwa kwa vyama vya ASP na TANU na kuzaliwa CCM, mwaka 2006 alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi hadi alipolazimika kujiuzulu kufuatia kuteuliwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa.

Nafasi nyingine katika chama ni mjumbe wa kamati mbalimbali zilizoundwa na CCM kwa kipindi chote alichokuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na Mlezi wa chama Mkoa Morogoro.

Mlezi wa Jumuia ya Vijana Wilaya ya Mjini mwaka 1992 hadi 2006 na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM hadi alipoteuliwa AU.

No comments: