Tuesday 19 May 2015

CUF kufanya kura ya maoni Dar kesho

Makada wa CUF wanaowania tiketi ya kugombea ubunge katika majimbo ya Dar es Salaam, kesho watakuwa na wakati mgumu wa kusubiri mustakabali wao wakati wa Kura ya Maoni, huku wingu zito likiendelea kufunika mchakato wa uachianaji majimbo ndani ya Ukawa.
Wagombea wa CUF watakaopatikana katika majimbo sita watatoa mwelekeo wa kinyang’anyiro cha Ukawa hapo baadaye wakati wa kuamua ni mwanasiasa yupi kati ya watakaowania katika vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF, awakilishe umoja huo hapo Oktoba.
Jiji la Dar es Salaam, lina majimbo ambayo yamebaki kuwa mwiba mchungu kwa mikakati ya umoja wa vyama hivyo, huku majimbo ya Segerea na Ukonga yakiwa na mchecheto zaidi.
Katibu wa CUF wilaya ya Ilala Omary Muarabu, alisema jana kuwa katika Jimbo la Segerea, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, Julius Mtatiro anachuana na Mjumbe wa Baraza la Uongozi Taifa, Ashura Mustapha.

Ashura mbali na kuchuana na Mtatiro, pia ndiye mgombea pekee wa viti maalumu, hivyo kuwa na njia nyeupe iwapo atadondoka katika Kura ya Maoni inayotarajiwa kufanyika Gongo la Mboto.
Mgombea wa CUF atakayepatikana kesho ataendeleza sitofahamu ya kuachiana jimbo hilo na Chadema ambao wana watia nia wawili mashuhuri ambao ni Fred Mpendazoe na Hebron Mwakagenda.
Muarabu alisema katika uchaguzi huo watahakikisha uwazi na haki vinatendeka .
“Tumewaagiza Makatibu wa kata wawaruhusu Wajumbe wa Mkutano Mkuu kupata habari za mgombea na sera kwa uwazi. Pia, tumewapatia semina watia nia  kutambua kuwa mtu akikosa nafasi, ajue ni utaratibu wa chama na atakayepita hajashinda bali amepata nafasi ya heshima,” alisema.
Katika jimbo la Ukonga, Muarabu alisema Mngwali Mngwali atapambana na makada wenzie Homeni Abdul, Colman Obote na Mziwanda Rashid huku Safina Mgumba akisubiri baraka za kupitishwa kuwania nafasi ya viti maalumu.
Kama ilivyo Segerea, jimbo la Ukonga lipo katika mvutano mzito ndani ya Ukawa kutokana na Chadema kulitolea macho kiasi cha uamuzi wa kuachiana kuwekwa kiporo hadi uongozi wa umoja utakapokamilisha shughuli hiyo.
Mkutano Mkuu wa CUF katika wilaya ya Ilala, unatarajia kumpitisha Jamal Mucadamu ambaye amekosa upinzani, hivyo kusubiri mchujo ndani ya Ukawa kabla ya Uchaguzi Mkuu.
Katibu wa chama hicho wilaya ya Temeke, Kaisi Kaisi alisema watahakikisha kura hizo zinapigwa kwa uhuru na haki kwa sababu hakuna haja ya kufanya upendeleo.
Kaisi alisema katika Jimbo la Temeke, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF Abdallah Mtolea atachuana na Mjumbe wa Baraza la Uongozi Taifa Kaswaka Kaswaka na kada Hafidh Fakh. Nafasi ya viti maalumu inawaniwa na Zainabu Mndolwa na Salome Masoud ambaye pia ni diwani wa Viti Maalumu.
Kigamboni mjumbe wa Baraza la Uongozi Taifa, Juma Mkumbi atasubiri kesho kupatiwa baraka za kupeperusha bendera ya chama hicho kinachoongozwa na Prof Ibrahim Lipumba.
Katika jimbo la Kawe, licha ya sasa kufahamika kuwa lipo chini ya Halima Mdee (Chadema), Katibu wa CUF, Kinondoni Mohammed Mkandu alisema Mohammed Mtandu anasubiri kupitishwa na Mkutano Mkuu...  “Kinondoni tuna wagombea watano ambao ni Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Abdul Kambaya, Naibu Katibu Mtendaji Jumuiya ya Vijana, (JUVICUF) Maulid Said, Msanii Karama Masoud maarufu Karapina, Faraji rangi na Chambo Chambo.”
CHANZO: MWANANCHI

No comments: