Friday 26 June 2015

Kina Membe wajiandae kuangushwa Z’bar


Mh. Bernard Kamillius Membe alizaliwa tarehe 09 Novemba 1953 katika Kijiji Cha Rondo – Chiponda kilichopo kitika Wilaya ya Lindi Vijijini mkoani Lindi. Alizaliwa kwa mzee Kamillius Antony Ntanchile na mama Cecilia Josha Membe.
Mh. Membe ni mbunge wa Jimbo la Uchaguzi la Mtama kupitia (CCM) toka mwaka 2000 na ni waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa toka mwaka 2007.Nilitulia kumsikiliza Bernard Kamilius Membe akitangaza nia ya kuusaka urais wa Tanzania. Ilikuwa na maana kubwa kwangu kwa sababu kada huyu mwenye nguvu na kachero aliyejijenga nyumbani na ughaibuni, amesimama kama tishio kwa wengine wote.Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ni mbunge wa Mtama, mkoani Lindi, kule kulikojaaliwa raslimali ya kiuchumi ya gesi.Nina rafiki zangu serikalini kama nilivyonao kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM). Wengi wao wamekuwa wakitumia muda mwingi kuniaminisha kuwa Membe anayo nafasi kubwa ya kuteuliwa kuwa mgombea.
Wanasema jina lake litavuka tanuri-moto la Kamati Kuu (CC). Litavuka tanuri-moto la Halmashauri Kuu (NEC) na hivyo kuwa moja ya majina matatu ya mwisho ya kupimwa Mkutano Mkuu. Hapo hutoka mgombea wa CCM.



Na Jabir Idrissa
Na Jabir Idrissa

Wananiambia Membe anaungwa mkono na Rais Jakaya Kikwete, au angalau Mwanamke namba moja, Salma, ambaye kwa ujanajike wake na kule kuwa mke wa kiongozi mkuu wa jamhuri, ana nguvu za kushawishi atakalo liwe.Kwangu mimi, niseme sawasawa Membe. Aungwe mkono na kuridhiwa Ikulu. Lakini katika wasiri wangu haohao, wapo wanaosema mfumo hasa unamuangalia baba mmoja mtulivu, asiyependa makuu (ametosheka na umasikini wake na wa kwao), na mchukia rushwa kihaki lillahi.Lakini muda mfupi kabla ya kutia tamati ya kuandika makala hii, msiri mmoja kanipigia simu akisema mtu mpya ambaye hakuwa machoni pake, ametangaza nia. Anasema huyo akichukua fomu, “atakuwa tishio kwa kila mtu, hata Membe.” Hawa wawili siwataji bado.
Nimelenga makala hii kumjadili Membe. Mbele kidogo, nitamjumuisha Samuel John Sitta ambaye naye amechukua fomu kuomba uteuzi. Juzi tu nimejua kuwa hawa wawili wanakubaliana sasa. Ni kama wametumana katika hili.Ninayaona maskhara makubwa. Naweza kuamini Membe anakubalika Ikulu na kwa wakubwa wa Idara ya Usalama wa Taifa, ambako ndiko “alizaliwa na kukulia” kikazi.
Haki ya Mungu naona kuwa kama imefikiriwa hivyo, basi itakuwa ule ninaoita “mtihani mgumu” kwa CCM katika uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba ni dhahiri. Anguko la kihistoria. Nitafurahi.
Mjadala wangu unabaki kwenye nafasi ya matakwa ya Wazanzibari na Zanzibar yao, kuhusu kurudishiwa mamlaka kamili ya nchi yao ili waijenge kwa mtizamo wao, na sio mtizamo wa kimabavu unaoendelezwa na dola ya CCM.Msimamo wa Wazanzibari walio wengi – na wengi hasa kwa maana ya neno lenyewe, sio kama wanavyojitumainisha wakubwa wa CCM na wahafidhina wanaoandamana nao kuwa CCM ingali na nguvu na inapendwa Zanzibar – ni Muungano wa serikali tatu.Kwa sababu hiyo tu peke yake, lazima wakubwa akiwemo na Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho, wanajua kwa asilimia zote hawatasalimika kukataliwa na Wazanzibari. Wataangushwa tu kama inavyotokea mara zote.
Nieleze kwa lugha nyingine ili iwe rahisi kwenda pamoja. Muungano unabaki kuwa moja ya masuala makuu yatakayoshawishi wananchi kuchagua viongozi katika uchaguzi huu. Ni suala ambalo halijapata kutoka nje ya ajenda kuu za uchaguzi kwa Wazanzibari tangu 1995.
Peke yake inatosha kuamini kuwa mtaka kura yeyote asiyeaminika kuwa ana mchango wa kutoa kuwahakikishia Wazanzibari hao wengi kutimia kwa matakwa yao ya kuipata Zanzibar yenye meno ya kusaidia kuijenga kiuchumi na kuulinda utamaduni wa wenyewe, ataangushwa.Sasa hii maana yake ni moja tu – mgombea yeyote wa CCM na hasa aliyepata kuwa waziri katika Serikali ya Muungano, na pengine akawa ndani ya Kamati Kuu, hachaguliki, kwa sababu haaminiki.Ni bahati kuwa Membe na Sitta, hawaaminiki Zanzibar kwa kuwa wanayo waliyoyatenda yakavuruga umma na kuacha donda ambalo mpaka leo hii, ni bichi halijapona. Haya ndiyo hasa maudhui ya mjadala.Duru za kisiasa ndani ya makundi ya wasaka urais CCM, zimenieleza kuwa hawa wawili wanasema pamoja. Mmoja anamuangalia mwingine kuwa akipenya wanakula wote kimtindo. Wanaita mafanikio baada ya kutafuta vya kusimama dhidi ya kambi kuu ya Edward Lowassa.Katika yote ambayo Membe alinisukuma nimuone kama mwanasiasa asiyetosha kwa urais zama hizi za vijana motomoto na UKAWA – Umoja wa Katiba ya Wananchi – ni alipogusia, maana amegusia tu, kuwa anaupenda muungano na kuahidi kuusimamia uimarike kwa nguvu zote na “sitamvumilia yeyote anayetaka kuuvuruga.”
Nimegundua Membe ambaye ninaamini hajanichukulia kama mmoja wa waandishi wawili wakubwa aliowatangaza ni adui zake, hajasimama vema. Nimecheka kumsikia akitamka maneno ya kuamini katika Muungano songombingo uliopo.Au labda kama Muungano anaouzungumzia ni huuhuu unaozidi kumeng’enywa na CCM, chama anachoamini kitampitisha agombee urais.Sauti kubwa ya Wazanzibari ni kutaka mabadiliko ya mfumo wa Muungano, kama ni ule wa 26 Aprili 1964, uliotengenezwa kijasusi chini ya Marekani na Uingereza.
Kama nionavyo kwa watangaza nia wengine, Membe haaminiki linapokuja suala la kuwahakikishia Wazanzibari muungano wa maridhiano, unaojali hali halisi, unaohitaji kuendeshwa kwa uwazi na ukweli, tena kwa kuzingatia kuwa watu wa nchi hizi mbili walishakuwa na mahusiano ya damu hata kabla ya hiyo 1964.Membe anajulikana kuinyonga Zanzibar kwa kuifutia misaada ya kielimu ya Oman. Alitumia ukuu wake wa wizara anayoongoza akafuta misaada dakika chache kabla ya kusomwa tamko la kiushirikiano kati ya Tanzania na Oman alipokuja kuzuru nchini Waziri wa Elimu ya Juu wa Oman, Dk. Rawiyah Al Busaid, mzaliwa wa Oman kwa baba aliyezaliwa mjini Zanzibar miaka ya 1940.
Lilikuwa tukio baya kwa Waziri Dk. Rawiyah mwenyewe pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Zanzibar, Ali Juma Shamhuna aliyekuwepo Dar es Salaam siku hiyo. Wote waliumia kuona nchi yao inanyimwa msaada unaotoka kwa ndugu zao Oman.Ni ujasiri wa mama Dk. Rawiyah ulioihakikishia Zanzibar kuipata misaada yote kama ilivyopangwa. Aliiona njia ya kufanikisha hilo atakaporudi Muscat. Alhamdulillahi, Oman inatiririsha misaada ikiwemo kudhamini mamia ya watoto wanaoingia chuo kikuu chochote duniani.
Sitta aliwahi kunikatisha tamaa ya Zanzibar kupata mamlaka aliponieleza kwa simu “hayo matumaini yenu ya kuachiwa mpate mamlaka, msahau kabisa, ndio nakueleza na wenzako mnajihangaisha bure. Hatuwezi kuacha mkamleta Sultani kutawala Zanzibar.”Kama simu zinasema zitasema hivihivi. Wakati ule Sitta alikuwa bado amezongwa na pumbao la uenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, ambalo alilitumia kufanya maamuzi yaliyofurahisha wakubwa wenzake katika CCM walioapa piga-ua, ilipo Zanzibar ibakie papo.
Bila aibu, wamewapumbaza wajumbe wa Zanzibar, akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, na mawaziri anaowasimamia, kuwa eti katiba mpya imeipa Zanzibar mamlaka makubwa.
 Chanzo: Mawio

No comments: