Tuesday, 23 June 2015

Wazanzibari bila ya kuwa na umoja Urais wa Muungano ni Ndoto

Balozi Ali Aman Abeid Karume akionesha naye mkoba wa wenye fomu za kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 


Muungano wa Jamhuri ya Tanzania hadi kufikia mwaka huu  wa 2015  unafikia miaka takribani 51 tangu kuasisiwa kwake mwaka 1964. Muungano ulijumuisha kuunganishwa kwa nchi mbili huru, yaani Tanganyika na Zanzibar, kwa lengo kubwa la kudumisha udugu wa kihistoria baina ya nchi hizo mbili.

Tangu kuasisiwa kwake, Muungano huu umeshapitiwa na Marais wanne: Nyerere (1964-84), Mwinyi (1985-95), Mkapa (1995 -2005) na Kikwete (2005 – 2015). Mwaka huu, Tanzania itapiga kura tena kumtafuta Rais wa nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Awali, makubaliano ya Muungano baina ya nchi huru mbili yalitegemewa, ingawa haikuandikwa rasmi, kuwa kutakuwa na mzunguko wa mpishano katika nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Yaani ikiwa Rais anayeondoka ni wa Tanganyika, anayekuja sharti awe anatoka Zanzibar.
4
Kwa kuwa Muungano wetu hakuundwa kwa nia njema, kila jambo ambalo lilioneshea kuisimamia na kuisaidia Zanzibar lilikorogwa na kuparaganywa ili lisiwepo na hata likiwepo lisimpe nguvu yeyote Mzanzibari akaweza kupata mamlaka ya kuitetea Zanzibar ambayo kwa malengo ya siri ya Muungano, ililengwa kumezwa na kufutwa kabisa katika ramani ya dunia.

Mambo ya Muungano yaliongezwa maradufu kupita kiasi ili kuizamisha zaidi Zanzibar. Viongozi wa Zanzibar walioonyesha uzalendo wa kuitetea Zanzibar ndani ya Muungano walikumbwa na ‘fyagio la chuma’. Na hadi leo, Mzanzibari yeyote anayejitokeza kuitetea Zanzibar mwisho wake unajulikana wazi wazi na kila mtu hapa nchini.

Ninalotaka kusema, wazo la kuwa Mzanzibari apatiwe zamu ya kuwa Rais wa Muungano lilikuwa na nia njema sana kwa Zanzibar. Lakini kwa kuwa wenzetu wa Tanganyika hawakuwa na nia hiyo, nalo hili likapotezwa kiaina.

Hadi keshokutwa tunafikia awamu hii ya tano na miaka 52, Zanzibar haijawahi kutoa Rais wa Muungano hata mara moja. Wala hakuna dalili hata ndogo kuwa iko siku Mzanzibari atakuwa Rais wa Tanzania kamwe.

Kauli yangu hiyo hapo juu najua itawatatiza wengi walio lishwa unga wa ndere na Bi Kirembwe. Lakini ukweli utabaki kuwa hivyo. Nyeupe itabaki kuwa nyeupe na nyeusi haitabadilika milele. Nasema tena kwa msisitizo; ‘Tangu 1964 Muungano ulipoasisiwa, Zanzibar haijawahi kutoa Rais wa Muungano!’ Full Stop! Wa kunisuta anisute!
Naanza kuhisi wengi wenu mkinong’onezana kuwa nimekosea kusema hivyo. Na wewe hapo unayesoma hivi sasa, nakusikia unasema ‘Ali Hassan Mwinyi Je?’ hakuwa Mzanzibari? Hakika ni sahihi. Ali Hassan Mwinyi, jina lake halisi anaitwa  Ali, Ndunga na hakuwa Mzanzibar. Sijui hivi sasa!

Vijana wengi wa leo hawajui mbinu ambayo CCM wanaitumia Zanzibar kuudumisha Muungano. Basi kwa wale ambao hawakusoma kitabu cha ‘Kwa heri Uhuru Kwa heri Ukoloni’ cha Dokta Harith Ghassany wanisome vizuri hapa.
CCM ni watu wenye akili sana na ujanja zaidi ya sungura. Sijui kama wengi wetu tunawaelewa hivyo. Mbinu yao kubwa wanayoitumia ni ile ya kupandikiza watu kutoka bara wakaja kuishi hapa Zanzibar na kisha kubandikiwa Uzanzibari na kupewa uongozi kwa jina la Uzanzibari. Ndio hawa akina  na Abu Ndunga du Jumbe.

Viongozi kama hawa huandaliwa miaka mingi humu visiwani. Wakishafikia hatua ya kupewa kazi huteuliwa kwa tiketi ya Uzanzibari. Wakafanya kazi ya kuimezesha Zanzibar kwenye Muungano huku CCM bara wakisema maamuzi yote ya Muungano yameidhinishwa na Wazanzibari wenyewe. Rais wao ametia saini hii hapa. 

Ona sasa! Tunaambiwa Rais wetu Wazanzibari wakati wanajua wazi huyo sio Mzanzibari lakini kwa ujuha wetu, hatujui wala hatuamki. Ukitaka kuthibitisha kuwa Viongozi karibu wote wa CCM Zanzibar sio Wazanzibari, mtazame Abudu Jumbe karudi wapi? Yuko kwao mji mwema! Mwinyi na watoto wake, wamejua kwao baada ya kumaliza kazi walizotumwa.

Njia ya pili wanayoitumia CCM ni kuwatumia Wazanzibari halisi lakini wasiosoma wala wasio na maarifa ya kujua haki na batili. Wakishawapata watu hawa huwapa vyeo vikubwa kama vile katibu wa chama, makamo mwenyekiti wa chama Zanzibar na wengineo wengi ambao hawana  kauli ya kuhoji muungano.

Watu hawa huwa hawana sifa za kuajiriwa sehemu nyingi zenye faida na manufaa kutokana na uwezo wao mdogo wa Elimu. Kwa kuwa watu kama hawa huwa wameshakata tamaa na maisha, wakipewa fupa wako tayari kwa lolote lakini lisiwatoke. Ndio hao akina ‘bandu na akina rere’ ambao huapa majukwaani na bungeni kuwa ‘ maadamu walipindua hawatoi kwa kikaratasi cha kura’!

Kwa kuweka viongozi kama hawa, Muungano hufaidika kwa hali mbili. Kwanza, huwa rahisi kwao kujifanyia watakalo kwenye Muungano bila kupingwa wala kuhojiwa. Tuliona walivyokuwa wajumbe wa baraza la wawakilishi kwenye bunge la katiba Dodoma. Walikuwa kimya.

Wakitambua wazi kuwa nafasi na nyadhifa zao walizonazo ni kupewa tu, walinyamaza kimya wakiogopa kumkera bwana mkubwa. Wakaicha Zanzibar  iliyochagua Serikali tatu, ikikaangwa na rasimu ya vijisenti badala ya ile ya Warioba waliyoichagua. Hii ni faida moja.

Faida ya pili waipatayo kwa kuchagua viongozi ‘makanjanja’ wa CCM Zanzibar ni kuwa hata ikija nafasi ya kugombea Uraisi wa Muungano, wengi wa Viongozi wa juu wa Zanzibar hawatatimiza sifa hizo za kuwania uraisi. Na hapo hupatikana kile kisingizio kuwa Zanzibar imeshindwa kutoa mgombea mwenye sifa. Kazi kwisha!

Ukitizama viongozi tulio nao kweli Zanzibar katika CCM wengi wao ni hao hao maji ya kifuu bahari ya chungu. Na wasomi wachache tulio nao kutoka CCM wakishaonekana ni tishio tu hubandikwa vyeo bandia au huondolewa kabisa nje ya nchi hii kwa kupewa kazi nyengine zisizohusiana na Muungano.

Tumeona Dr. Gharib Bilal alipokuwa akilazimisha kuwa Rais muda wote. Kwa kuwa ana uwezo wa kuwa Rais wa Muungano, amepewa umakamo wa Rais ambao kazi yake kubwa ni kutembea na mkasi mkali wa kukatia utepe wa kufungulia majengo ya uma na jembe kwa kuchimba mashimo ya kupanda miti nchi nzima. Hizo ndizo kazi za makamo wa Rais Muungano. Wengine wamepelekwa umoja wa mataifa. Kimya!

Kwa kuwa Zanzibar hatuwi na mgombea mwenye sifa, na kwa bahati wenzetu wa bara wanahitaji wasomi, watamkubali kweli ‘Hajjat  wetu anayeapa viapio kuwa nchi hii hatutoi kwa kikaratasi cha kura’ awe rais wakati wanajua wazi kuwa ni pakiti tupu ya sigara?

 Au kweli watamkubali mwakilishi wetu wa Tumbatu awe raisi wa Muungano ilhali ana elimu ya kidatu cha tatu, cha mipango mipango? Salale wee! Hata siku moja, haitokezei! Wenzetu kwa hakika hawana mambo ya kunga kunga, makuti kuunga unga! Wanataka mtu makini.

Muda mfupi ujao, CCM itatafuta mgombea wa Urais wa Muungano ambaye bila shaka ndiye atakayekuwa Rais wa Tanzania wa awamu ya nne. Hivi sasa kuna mkururo wa majina ya wagombea wapatao thelathini. Nimeona Bi Amina Salim Ali na Dr. Gharib Bilal. kwa mara nyengine tena Ali Karume yumo lakini Dr. Salim Ahmed Salim amejitoa kwa kuchoka kuitwa HIZBU kila akitaka kugombea urais huo,ingawa kuna tetesi hwenda akachukua tena fomu hio,lakini ndio mambo kisebu sebu na kiroho papo.

Kwa kuwa nina uhakika Amina Salim Ali hapiti si kwa kudura wala miujiza, na Dr. Gharib Bilal ni msindikizaji tu, naamini wazi ndoto za Zanzibar siku moja kutoa rais wa Muungano ni sawa na zile za Alinacha. Haziwezi kutimia hata siku moja.

Hazitimii kwa sababu Urais wa muungano ni sehemu ya mkakati maalum wa kumpata Rais sio tu atakayeongoza Tanzania, bali atakayekuwa ‘madhubuti katika kuudumisha Muungano’ kama  wasemavyo wenyewe. Hilo liko wazi na kwa haraka haraka, hakuna Mzanzibari yeyote aliye madhubuti kwa hilo! Akiwa Mzanzibari kweli na sio wakuja!

Kwa hali kama hiyo, hakuna dalili ya kupata Kiongozi wa Muungano kutoka Zanzibar. Kwani nia na malengo ya washirika wetu wa Muungano ni kuwa na Serikali mbili kuelekea moja. Yaani kuwa na Muungano wa nchi moja na nusu. Muungano wa kuifanya Zanzibar mkoa na sehemu ya Jamhuri ya Muungano na sio nchi kama wanavyojidai wenyewe.

Nani anayeweza kufanya hili? Ni Rais makini kutoka kuumeni tu – Tanganyika. Na kama hili ndilo lengo, sioni kuwa kuna siku Mzanzibari atakuwa Rais wa Muungano kwani hata huo Uzanzibari wenyewe umebaki jina tu! ‘Umekwisha! Kwisha kabisa, miguu juu, kifo cha mende,’ chambilecho wana CUF!

No comments: