Saturday, 8 August 2015

Huu ndio Mwisho wa CCM ?
NILIKUSUDIA kuendeleza mjadala kuhusu madai kwamba Edward Lowassa hakutendewa haki katika michakato ya CCM mjini Dodoma, lakini taarifa mpya za masuala ya kisiasa zimenilazimisha nibadilishe kidogo mwelekeo wa makala ya wiki hii ili niweze kuendana na hali ilivyobadilika.

Hatua ya Edward Lowassa kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imekuja baada ya tetesi za muda mrefu kwamba mbunge huyo wa Monduli angekihama chama chake klichomlea kwa sababu kimemtosa katika mchakato wake wa kupata mgombea urais.

 Sasa imekuwa kweli: Edward Ngoyayi Lowassa ameamua kuhamia upinzani na amekubali kupeperusha bendera ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Bila shaka hili ni tetemeko la ardhi kisiasa ambalo linaweza kubadilisha mambo mengi nchini na kuacha alama za kihistoria ambazo hazitasahaulika.

 Kuhama kwa Lowassa kunafungua milango mipana kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hatimaye kuondoka madarakani baada ya kuwa kimeiendesha nchi hii (vizuri na vibaya) tangu tupate Uhuru mwaka 1961. Leo hii kinajikuta kikiwa kichovu hadi kinaona uwezekano wa kubomolewa na mmoja wa makada wake waandamizi.

Nimejaribu kuwahoji watu walio karibu na uongozi wa Chadema kuhusu hatua hii isiyokuwa ya kawaida ni kwa nini wamemkubali (au wamemtaka) mtu ambaye wao wenyewe walikwisha kumuorodhesha kama mmojawapo wa ile “Orodha ya Fedheha” katika ule mkutano maarufu wa Mwembe-Yanga, jijini Dar es Salaam. Maelezo niliyopata ni kwamba hatua yao hiyo imetokana na matakwa ya kisiasa kwa wakati huu. Wanaitambua nguvu ya Lowassa katika jamii ya Watanzania, na wanaamini kwamba nguvu hiyo ikiunganishwa na nguvu waliyonayo wapinzani tayari, njia ya kuiondoa CCM madarakani inakuwa wazi zaidi. Kuhusu tuhuma za ufisadi, nimeambiwa kwamba wapinzani wanadhani kwamba Lowassa amekuwa akifanywa kuwa “kondoo wa kafara” na wakuu wa CCM, ambao wanataka wananchi waamini kwamba fisadi peke yake ni Lowassa, na wengine wote ni safi, ambao ni uongo na mbinu za kuendelea kuitafuna nchi huku akilaumiwa mtu mmoja peke yake. Mmoja wao aliongeza: “Ukiangalia kashfa zote zilizopita, unaweza kusema kwamba ni za Lowassa? Hata kama tukisema alihusika na Richmond, ingawa nayo imegubikwa na utata, unaweza kusema alihusika na EPA au Tegeta Escrow au Deep Green?” Kada huyo wa Chadema anasema kwamba chama chao, na pia Ukawa, wameona fursa ya kuimaliza CCM, hatua ambayo itakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wote, ni bora watumie rungu ambalo liko tayari na limeonyesha uzito wake miongoni mwa wananchi. Lowassa alihudhuria kikao cha kamati kuu ya Chadema kilichofanyika Jumapili usiku, na ndipo uamuzi wa nini kifanyike ulipohitimishwa. Atakuwa mgombea wa Chadema wa urais, lakini wakati muafaka utakapowadia atajiunga na nguvu pana zaidi ya Ukawa na kuwa mgombea wa muungano huo unaodai Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano, dawa ambayo CCM imeshindwa kuiheshimu. Mojawapo ya makubaliano yalifiyofikiwa kati ya uongozi wa Chadema na Lowassa ni umuhimu wa kuharakisha upatikanaji wa Katiba hiyo iliyomshinda Rais anayemaliza muda wake, Jakaya Kikwete.

Kada mwandamizi wa Chadema anadhani kwamba kwa Lowassa kuingia Chadema ishara za mageuzi ya kweli na ya kina zinajionyesha waziwazi. Hii itakuwa sio mara ya kwanza kwa mitafaruku ndani ya CCM kuunufaisha upinzani tangu siasa za ushindani zilivyoanza katika miaka ya 1990. Augustine Lyatonga Mrema alikuwa mwanasiasa aliyejipatia umaarufu mkubwa wa kisiasa alipokuwa waziri wa mambo ya ndani ya nchi. Alitaka kuutumia umaarufu huo kugombea urais kupitia CCM, lakini wenzake ndani ya chama hicho wakamzibia njia kwa kuweka kigezo cha mgombea kuwa na shahada ya chuo kikuu, ambayo Mrema hakuwa nayo. Mrema alipohamia chama kidogo cha NCCR-Mageuzi ghafla kikaumuka, kikapata nishati ya ajabu, kikaikumba nchi nzima, na CCM na mgombea wake Benjamin Mkapa wakanusurika kwa sababu tu Mwalimu Julius Nyerere alifanya kazi kubwa ya kampeni kwa niaba ya mgombea wa CCM. Mwaka huo huo, CCM ilikataa kumuidhinisha Dk. Wilbroad Slaa kuwa mgombea ubunge wa Karatu na badala yake ikamsimamisha rafiki yake Mkapa aliyekuwa ameshindwa na Slaa katika kura za maoni ndani ya chama. Slaa alipohamia Chadema akasababisha changamoto nzito ambazo zinaisumbua CCM hadi leo. Sasa ni Lowassa.

Nguvu aliyoikusanya Lowassa kwa muda wote huu tangu ajiuzulu uwaziri mkuu miaka minane iliyopita ni kubwa mno. Alionyesha katika hatua mbalimbali za mchakato wa kuwania kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM. Naamini kwamba nguvu hiyo iliwatisha wakuu wa chama hicho kiasi cha kuamua kutumia mbinu zilizofichika kuhakikisha hapenyi hadi halmashauri kuu. Kuhama kwa Lowassa kutavuruga mambo mengi yaliyokuwa yameanza kutulia. Nategemea kwamba baadhi ya makada wa CCM waliokuwa na Lowassa hadi anaenguliwa mjini Dodoma watamfuata huko alikohamia. Kama kawaida yetu, kuhama huko hakutashinikizwa na mitazamo ya kiitikadi, bali itatokana na ile ari ambayo wafuasi wake (Team Lowassa na Friends of Lowassa) wamekuwa wakionyesha kwa muda mrefu. Lakini vile vile, safari hii, alama kwamba ushindi unaweza kwenda kwa wapinzani zinaonekana kwa uangavu mkubwa zaidi. Itakumbukwa kwamba katika uchaguzi wa mwaka 2010, Slaa, aliyekuwa mgombea wa Chadema aliweza kufanya vizuri mno katika kura za urais, na upinzani ukapata viti vingi vya ubunge, hasa katika maeneo ya miji mikubwa. Mwaka jana, wakuu wa serikali walifanya hadaa kwa kutoa kauli zilizoelekea kusema kwamba hakungekuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa. Baadaye walishitukiza uchaguzi huo wakiamini kwamba wapinzani wangejikuta hawako tayari.

Lakini matokeo yake yalikuja kuonyesha kwamba upinzani ulipata ushindi mkubwa katika vijiji na vitongoji vilivyokuwa vimeshikiliwa na CCM. Sasa hivi tunakabiliwa na hali mpya ambayo inatoa taswira mpya ambayo inaweza kubadilisha kabisa mwelekeo wa nchi hii. Kuna makutano ya mambo kama matatu ambayo yamesadifu: muungano wa vyama vya siasa ambavyo vimekuwa vikijaribu kila kitu kuiondoa CCM madarakani bila mafanikio; mwanasiasa aliyeshabikiwa na watu wengi ndani ya chama chake lakini chama chake kikamkataa; wananchi waliosubiri kwa muda mrefu kuona mabadiliko katika maisha yao, lakini wakakatishwa tamaa. Makutano ya nguvu zote hizo yanaweza yakawa ndio mwanzo wa kile kifo cha CCM kilichobashiriwa mara kwa mara.


No comments: