Saturday, 8 August 2015

Kwaheri Profesa Lipumba! Lakini kwa nini leo?


8/07/2015 07:27:00 PM
Profesa Lipumba
Profesa Lipumba
Hadi asubuhi hii imeshasemwa ama kuandikwa na wengi kuwa CUF ni taasisi na inafanya kazi zake ki taasisi. Mimi nasema ni Taasisi Imara iliyojengwa kwa misingi imara ya kitaasisi.

Nilipokuwa University miaka ya mwanzoni mwa 1990 nilisoma somo la Organizational Behavior. Kitu kimoja nilichojifunza humo, na hupenda kukitumia mara kwa mara, ni kuwa Office (Cheo) sio mtu binafsi, ingawa ni lazima iwe na mtu. Office itabaki kuwa ipo hata kama ofisa husika hayupo, ameondoka, amekufa, au ameshindwa kwa njia moja au nyengine. kuna njia kadhaa za ofisi kuendelea na kazi zake hata kaa mwenye jina hayupo. Office itabaki kuwa office na jina la mtu ni kwa ajili ya utendaji.

Akiondoka Rais nchi haiondoki wala cheo cha urais hakifutwi, ila hupatikana anaekaimu urais kama ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Jaji Mkuu au mwengine yeyote kwa mujibu wa Katiba ya nchi husika. Saini zinawekwa, maamuzi yanafanywa, na hatua zinachukuliwa.

Profesa ameondoka katika nafasi hiyo kubwa ambayo wananchi wa Tanzania, na wanachama wa CUF khasa, walimtunuku kwa heshima kubwa. Sote tunajua kuwa amekuwa na mchango mkubwa katika kukikuza na kukieneza Chama Tanzania, hasa bara. Pamoja na kuwa mfinyo wa CCM ulijitahidi sana kukiumiza na kutaka kukiondoa Chama hichi katika picha. Matokeo yake hadi uchaguzi wa 2010 chama kilishuka sana katika kura, na idadi ya wabunge wa kuchaguliwa ilikuwa ni 2 tu.

Mohammed Nur
Mohammed Nur
Mimi binafsi nilitembea nchi nzima na Profesa. Nikamuona jitihada zake kubwa. Mote tulimopita wananchi walimpa imani yao na waliweka matumaini na mategemeo yao makubwa kwake. Lakini je wananchi hawakujua kuwa huyu ni binaadamu? Walitambua! Hawakujitayarisha? Kama walijua walijitayarisha (kisaikologia). Ndio! huwezi kumchukulia dhamana binaadamu. Kuna maradhi, kuna kifo na mengi mengineyo. Hili lililotokea ni moja.

Wananchi wa Tanzania, wana-UKAWA, na wanaCUF khususia, hawatokata tamaa ya mageuzi kwa kuondoka Profesa katika nafasi ya Mwenyekiti wa CUF. Tukio hili linawakumbusha ubinadamu na uwepo tayari wa kukamiliana na kila aina ya mikiki. Iwe ya ndani ama iwe ya nje.

Wananchi wamejitokeza kwa wingi kuonesha kuwa wanamheshimu sana Prof na mchango wake, wanaheshimu maamuzi yake ya kikatiba, wanampongeza kwa kufanya maamuzi anayoyaamini. Lakini wengine wanajiuliza kwanini leo? LEO? WAKATI HUU WA SAFARI NZITO KWENYE MAWIMBI MAKUBWA?

Hata hivyo wanaCUF tunamtakia maisha mema na kazi njema na shughuli njema anazoziendea. Tunategemea tutapata papers nzuri za kiuchumi ambazo zitaweza kubadilisha maisha ya wananchi masikini sana waliodhalilishwa kwa kipindi kirefu na serikali ya CCM na watangulizi wake. Pamoja na kuwa kuna mamilioni ya papers ambazo zimeshachapishwa.

Mapambano yanaendelea. Watanzania watakomboka kwa umoja na imani yao. Kila aliesaidia katika safari hii, ikiwa ni pamoja na Profesa Lipumba, watakumbukwa kwa mchango wao. Wapiganaji wapya watatokea na MAPAMBANO YA KISIASA YATAENDELEA HADI MASLAHI YA WANANCHI YAPATIKANE.

Mungu Ibariki CUF, WABARIKI WANANCHI WA TANZANIA, NA IBARIKI TANZANIA YETU.

Mohammed Nur


No comments: