KAMPENI za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu zinaanza rasmi mwishoni mwa wiki hii ambapo wagombea wa vyama vikuu vinavyowania nafasi ya urais watazindulia kampeni zao jijini Dar es Salaam.Taarifa ambazo tumezipata kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) zinaeleza kuwa wagombea wawili wanaowania kumrithi Rais Jakaya Kikwete kutoka vyama hivyo wataziweka hadharani ilani za vyama vyao katika siku hiyo. Rais Mwema limeambiwa kwamba mgombea wa CCM, John Magufuli, atazindulia kampeni zake katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam huku yule wa Chadema, Edward Lowassa, akipangwa kuzindua kampeni zake katika Uwanja Mkuu wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Magufuli amepangwa kuzindua kampeni zake hizo siku ya Jumapili ijayo (Agosti 23) huku Lowassa akiwa amepanga kuzindua siku moja kabla, yaani Jumamosi ya Agosti 22.
Hata hivyo, gazeti hili limeambiwa kwamba wakati CCM tayari imekamilisha taratibu zote za kufanya mkutano huo wa Jangwani, mkutano wa Lowassa bado haujathibitishwa kwa sababu taratibu zote hazijakamilika.
Tangu kufunguliwa kwake takribani miaka nane iliyopita, uwanja huo haujawahi kutumika kwa shughuli zozote za kisiasa na Raia Mwema limeambiwa kwamba mamlaka husika zina shaka na namna utakavyoweza kuhimili shughuli za namna hiyo.
Mmoja wa viongozi wa juu ndani ya Umoja wa vyama vinavyodai Katiba ya Wananchi (Ukawa), aliliambia gazeti hili kuwa kama hawatapata kibali cha kufanyia uzinduzi wao kwenye Uwanja wa Taifa, watatafuta sehemu nyingine kwa ajili ya shughuli hiyo.
“Kuna maeneo mengi jijini Dar es Salaam ambako tunaweza kufanya shughuli ya uzinduzi wa kampeni ya Lowassa. Tunaweza kufanya Kawe kwenye viwanja vya Tanganyika Packers au Mwembeyanga wilayani Temeke. Lakini lengo letu ni kufanyia Taifa,” alisema kiongozi huyo kutoka Chadema aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina kwa vile yeye si msemaji wa Ukawa.
CCM inatarajiwa kutoa ratiba kamili ya namna shughuli ya uzinduzi itakavyoedeshwa wakati wowote kuanzia leo lakini zipo taarifa kuwa umepangwa kuwa uzinduzi wa aina yake.
Zaidi ya kuonyeshwa moja kwa moja na vituo mbalimbali vya televisheni na kutangazwa redioni, wananchi wa Tanzania walio mbali na eneo la tukio, ndani na nje ya nchi wataweza pia kuona tukio hilo kwa njia ya mtandao.
Mara baada ya uzinduzi huo wa Dar es Salaam, Lowassa, Magufuli pamoja na wagombea wenza wao; Samia Suluhu Hassan na Juma Duni Haji, wataanza ziara ndefu ya zaidi ya miezi miwili kuzunguka nchi nzima kuomba kura kwa wananchi.
Raia Mwema linafahamu kwamba wapanga mikakati wa CCM na Ukawa tayari wametengeneza timu mbili tofauti; moja kwa ajili ya wagombea urais na nyingine kwa ajili ya wagombea wenza kwa ajili ya mizunguko hiyo ya kuwashawishi wapiga kura zaidi ya milioni 20 wanaotarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo.
Kampeni za mwaka huu zitakuwa za aina yake kwa sababu kwa mara ya kwanza katika historia ya ushindani wa vyama vingi, vyama viwili vikubwa vinavyoshindania nafasi ya urais, vyote vina uwezo wa kirasilimali kushindana.
Chanzo hicho cha habari kutoka Chadema kimelieleza Raia Mwema juzi Jumatatu kwamba Ukawa safari hii haitazidiwa kifedha na CCM kwa sababu wamehakikishiwa kuwa mahitaji yao yote ya kikampeni yatapatikana.
Hakuna hesabu zilizowahi kuwekwa hadharani kuhusu matumizi ya fedha katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2010, lakini Chadema inadaiwa kutumia zaidi ya shilingi bilioni tano kwenye Uchaguzi Mkuu huo; kiasi kinachodaiwa kuzidiwa kwa mbali na kilichotumiwa na chama tawala.
“Kaka, mwaka 2010 tulitumia zaidi kidogo ya shilingi bilioni tano na uliona namna mgombea wetu, Dk. Wilbrod Slaa alivyomtoa jasho Rais Kikwete wakati huo. Hebu fikiria tukiwa na bilioni 20 kwa mfano tutafanya fujo kiasi gani,” alisema kiongozi huyo.
Ilani
Wakati tukienda mitamboni juzi Jumatatu, gazeti hili liliarifiwa kwamba vyama vinavyounda Ukawa tayari vimemaliza kazi ya kuandaa rasimu moja itakayotumiwa na Lowassa.
Ukawa inaundwa na vyama vinne ambavyo ni Chama cha Wananchi (CUF), Chadema, NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD).
Kwa vile vyama hivyo vyote vina mrengo na itikadi tofauti, wataalamu kutoka vyama hivyo walikutana jijini Dar es Salaam kwa takribani wiki kutengeneza ilani moja ambayo ndiyo itakayotumiwa na vyama vyote.
Raia Mwema limefanikiwa kuona nakala nakala ya ilani hiyo lakini imeeleza kuhusu mambo saba muhimu ambayo Watanzania watafaidika nayo endapo watampa ridhaa mgombea wa umoja huo.
Kwanza, gazeti hili limeambiwa kuwa ilani ya Ukawa inazungumzia masuala ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania –jambo ambalo hasa lilisababisha kuanzishwa kwa umoja huo.
Kwenye eneo hilohilo la Katiba, Ilani hiyo, pamoja na muundo huo wa Muungano, ina mapendekezo pia kuhusu masuala ya Utendaji na Uwajibikaji serikalini, vita dhidi ya rushwa
Ilani inapendekeza kuwapo kwa mfumo wa serikali tatu; Tanganyika, Zanzibar na ile ya Muungano, kama ambavyo ilipendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Zaidi ya muundo, ilani ya Ukawa inaeleza pia kuhusu suala zima la elimu. Gazeti hili limeambiwa kuwa Ukawa itaahidi kuwa serikali yake itagharamia elimu na wananchi hawatatozwa gharama kubwa kuipata.
Pia, ilani hiyo inaeleza kwa undani kuhusu namna sekta ya elimu itakavyofanyiwa maboresho kwa kuweka miundombinu ya teknolojia ya mawasiliano na vitendea kazi.
Kwenye eneo la uchumi, ilani ya Ukawa inazungumzia namna ya kuunganisha sekta ya kilimo na viwanda ili kuondoa idadi kubwa ya wakulima kutoka katika umasikini na pia kuongeza ajira.
Miongoni mwa matamko ya msingi ndani ya ilani ya Ukawa litakuwa ni suala la “Mchaka Mchaka wa Maendeleo” ambapo Ukawa inaahidi kuwa idara muhimu kwa maendeleo ya uchumi zitakuwa kazini kwa muda wa saa 24.
Ilani hiyo inaeleza pia kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii ambapo itaahidi wananchi wengi zaidi kufaidika na huduma za afya kupitia bima na taratibu nyingine, ili watu wengi zaidi wapate huduma hiyo muhimu.
Dk. Slaa
Mmoja wa viongozi wa NLD aliyezungumza na gazeti hili Jumapili iliyopita, alisema kwamba wakati wa vikao vya kuandaa ilani ya Ukawa, zilikuwepo taarifa kuwa huenda aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, atarejea wakati wa kampeni.
Slaa ambaye gazeti hili linafahamu kuwa kwa sasa yuko mapumzikoni katika mojawapo ya mbuga za wanyama akipumzika, alitangaza kuachia nafasi zake zote za uongozi ndani ya chama hicho mwishoni mwa mwezi uliopita.
Gazeti dada la hili, Raia Tanzania ndilo lililoandika taarifa hizo kwa mara ya kwanza, likimnukuu yeye mwenyewe akisema kwamba dhamira yake inamsuta kutokana na Ukawa kumpitisha Lowassa kuwa mgombea wake wa urais.
Dk. Slaa ambaye aliwahi kuwa Padri wa Kanisa Katoliki hapa nchini, hakutaka kuingia kwa undani lakini inafahamika kuwa kuna masharti alitaka yafuatwe kabla ya Lowassa kupitishwa lakini hayakufuatwa na akapitishwa kuwania urais.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliwatangazia wanachama wake kuwa Slaa yuko katika “mapumziko ya tafakari” na kwamba atarejea kazini mara atakapojiona yuko tayari kufanya hivyo.
“ Wakati tukiwa kwenye kuandaa ilani kulikuwa na taarifa kuwa Slaa anapumzika na atajitokeza hadharani wakati wa kampeni akiunga mkono Ukawa na mgombea wake, Edward Lowassa. Tuna matumaini hilo litatokea Dar es Salaam wakati wa uzinduzi,” alisema kiongozi huyo wa NLD.
Dk. Slaa ni miongoni mwa viongozi wenye mvuto na ufuasi mkubwa miongoni mwa jamii ya Watanzania na tayari wachambuzi wa siasa za Tanzania wanaamini kuwa uamuzi wowote atakaouchukua; kuhama au kubaki Chadema, utakuwa na athari kwenye uchaguzi wa mwaka huu.
Zanzibar
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kunatarajiwa pia kuwa na upinzani mkali visiwani Zanzibar hususani Pemba ambako chama kipya cha Alliance for Democratic Change (ADC) kinadaiwa kuanza kujitanua.
Chama hicho kimeanzishwa na wafuasi waliokuwa CUF katika miaka ya nyuma, kama Hamad Rashid Mohamed aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Wawi na Said Miraji aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Kampeni wa chama hicho.
Katika uchaguzi wa mwaka huu, ADC imesimamisha wagombea katika takribani majimbo yote visiwani Pemba, huku kikiwa kimefanya hivyo kwa asilimia 75 kisiwani Unguja.
Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita, Hamad Rashid alisema kimsingi wamesimamisha wagombea kwa asilimia 95 kisiwani Pemba na kuweza kuwa chama cha kwanza cha upinzani visiwani humo, ukiondoa CUF, kufanya hivyo.
“ Hii itakuwa ni fursa nzuri kwa Wazanzibari kuwa na chama cha upinzani. Kwa sasa Zanzibar haina chama cha upinzani maana CUF na CCM ndiyo wanaoongoza serikali. Kwa miaka mitano iliyopita, iliyotekelezwa ni ilani ya CCM pekee,” alisema.
Ujio wa Hamad ambaye atawania urais wa Zanzibar na Maalim Seif Shariff Hamad wa CUF katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, unaelezwa kuweza kupunguza idadi ya kura ambazo chama hicho kikuu cha upinzani visiwani humo kitapata.
Kwa kawaida, CUF hupata asilimia takribani 80 ya kura zake kutoka Pemba na kama ADC itakuwa na nguvu inazoelezwa kuwa nazo, kuna uwezekano wa idadi ya kura za CUF kupungua.
Kama ilivyo kwa Maalim Seif, Hamad Rashid na Said Miraji nao pia wanatokea Pemba.
No comments:
Post a Comment