Na Enzi T. Aboud
KAMA aliyoyasema Balozi Seif Ali Iddi, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa kampeni wa CCM Zanzibar, yalitoka moyoni mwake kuwa viongozi wa CUF na UKAWA kupitia cha CHADEMA, Edward Lowassa na Maalim Seif Shariff Hamad ni wabaguzi wenye uchu wa madaraka na nia chafu, basi yumkin Balozi amejidhalilisha.
Balozi Seif itakuwa anasumbuliwa na msongo wa mawazo kutokana na woga wa mabadiliko endapo CCM ikishindwa katika uchaguzi huu, atakosa wadhifa unaompa kiburi.
Bila shaka Balozi hajiangalii. Amejaa uchu wa madaraka kiasi cha kujiona anafaa kuwa Rais uchaguzi wa miaka mitano ijayo na kutarajia adumishe Muungano wa Serikali mbili ambao ni kinyume na fikra mbadala za Maalim Seif ambaye ni Makamo wa Kwanza wa Rais na Katibu Mkuu wa CUF.
Maalim Seif amekuwa akishikilia katika kampeni yake kuwa Muungano kwa mfumo uliopo haukubaliki tena kwa Wazanzibari, na akichaguliwa kuongoza Zanzibar, atashirikiana na Lowassa kutimiza ndoto za wananchi.
Na huo ndio utashi wa wananchi wengi wa pande zote mbili za muungano kama walivyoonesha katika rasimu ya katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Balozi Seif ameonesha uhafidhina kama walivyoonesha wajumbe wenzake wa kamati ya kampeni ya Dk. Shein ambao ni Shamsi Vuai Nahodha, Waziri Kiongozi mstaafu, na Hamza Hassan Juma, aliyekuwa waziri wa nchi wakati huo.
Watatu hawa wameshuhudiwa wakitoa kauli za ovyo kwenye majukwaa ya kampeni wakihusisha Uhizbu, chama kilichokufa cha (ZNP), na Usultani usiokuwepo tangu ulipong’olewa kwa mapinduzi ya 1964.
Wakati CCM kikitafuta mgombea kwa uchaguzi mkuu wa 2005, viongozi wahafidhina kutoka Zanzibar, walitumia chuki za Uwarabu, Uhizbu na Usultani kumhujumu Dk. Salim Ahmed Salim asipate nafasi ya kuteuliwa.
Lilikuwa rungu kubwa dhidi ya matumaini ya Dk. Salim ambao walijikuta waizuiwa na makada Tanzania Bara na viongozi wahafidhina wa Zanzibar waliobeza mchango wake katika kutumikia Taifa kwa heshma, utu na uadilifu uliotukuka nje na ndani ya nchi. Alipata kuwa waziri mkuu chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere.
Wahafidhina haohao wanachekelea Dk. Karume kutukanwa na kubezwa kama wamesahau mchango aliotoa kujenga siasa za maridhiano pamoja na Maalim Seif ambazo zimeleta utulivu uliopo sasa.
Siasa walizotandika ndizo zilizotuliza uhasama kwani muundo wa serikali ya umoja wa kitaifa (SUK) umekuja. Lakini unapita majaribuni kutokana na kuendelea kwa fitna na uhasama.
Kinachotisha katika kadhia hii ni ukweli kwamba CCM inaendekeza siasa hizi za ubaguzi kwa kuwa Shamsi na Hamza hawakuona enzi za chuki ziso tija kwa wananchi Unguja na Pemba. Kuzirejesha leo majukwaani ni kupandikiza ujinga akilini mwa vijana wanaotaka matumaini.
Hamza na Shamsi wanafanana. Hamza ni fundi wa charahani wa zamani kupitia maskani ya CCM Muembekisonge, akabahatika kuingia Baraza la Wawakilishi na kuteuliwa waziri na Dk. Karume.
Shamsi alikuwa Afisa wa Habari serikalini na baada ya kuingia baraza la wawakilishi, akateuliwa waziri kiongozi. Ndio maana leo husemwa wazi kuwa “aliokotwa” akiwa na madole matatu ya ndizi akienda nyumbani kwake na kujulishwa kuwa anaitwa Ikulu.
Karume alimteua Shamsi akiwa mwanagenzi katika siasa na uongozi, tofauti na walivyokuwa Maalim Seif aliyeteuliwa mwaka 1984 na mze Ali Hassan Mwinyi na baadaye Dk. Idris Abdulwakil. Hata madktari Omar Ali Juma na Mohamed Gharib Bilali walijiweza.
Hii ndio CCM ya Rais Jakaya Kikwete na Dk. Ali Mohamed Shein ambayo kwa kweli haina shukrani kwa Lowassa, waziri mkuu aliyejizulu na kumkingia kifua Rais Kikwete ambaye serikali yake ilikuwa nchani kuanguka kufuatia kashfa ya mkataba wa umeme wa Richmond.
CCM Zanzibar haina shukrani kwa Maalim Seif ambaye anatukanwa na kusimangwa na wanamaskani wa Muembekisonge kupitia ubao wa matangazo unaoandikwa unaoeneza kauli za uchochezi dhidi ya Wapemba.
Huu ni ukichaa wakati Dk. Shein ni mzaliwa wa Pemba na ni Rais wa Zanzibar mwenye uwezo wa hata kuibomoa maskani hiyo na kwamba hakemei kwa sababu tu ya maslahi ya kisiasa.
Lakini kilichoandikwa karibuni kwenye ubao huo ndio udhibitisho hasa wa fikra mgando zilizoko akilini kwa baadhi ya viongozi na makada mamluki wa propaganda za kishetani zinazochochea ugonvi, chuki na fujo.
Maskani ya Muembekisonge inabebwa kuvunja sheria za nchi, inaiaibisha SMZ inayojigamba kuheshimu utawala wa sheria, kulinda amani na utulivu huku ikisambaza askari wenye bunduki kila kona kulinda amani, lakini inashindwa kuwakamata wachochezi wa kisiasa na kuwafikisha mahakamani.
Bila ya kumtaja kwa jina maskani ya kisonge imeandika maneno yanayomlenga Dk. Karume ambaye ni mwana wa Rais wa Kwanza baada ya mapinduzi, Abeid Amani Karume.
Kwa kumshambilia na kumtukana Dk. Karume, CCM wanathibitisha wasivyo na staha hata kwa Mzee Karume, na kwa hivyo ni waongo wanaposema wanaenzi Mapinduzi wakati wanamkandamiza aliyeongoza serikali yake.
Ndipo nikasema CCM hawana shukurani kwani chama cha Hizbu kilikuwa na uhasama na ASP miaka ya 1950 na 1960 na kutokana na uhasama huo kila mwananchi anayekuwa na mawazo mbadala ya kuleta mabadiliko, anahusishwa na ZNP.
Ni tabia inayoendelezwa wakati Zanzibar imepiga hatua kwa siasa za uvumilivu, lakini ni watu wachache wanapalilia mbegu za siasa chafu kwa lengo la kuleta mifarakano.
Propaganda zinazotolewa na makada wa CCM kulenga wagombea wawili wanaoungwa mkono na UKAWA zinaibua ugomvi na fujo na kujenga chuki kwa wafuasi wa CCM na CUF na Ukawa.
Matokeo ya siasa chafu tayari yameshuhudiwa. Kijana anaesadikiwa kuwa mfuasi wa CCM alipigwa na kuumizwa vibaya alipotuhumiwa kuchana picha za Maalim Seif zilizobandikwa ukutani kufanya kampeni.
Ni hivyo hivyo pia mtu mmoja aliyedhaniwa ni mfuasi wa CUF alipigwa na vijana wa CCM kwa tuhuma hiyohiyo kuchana picha za mgombea wa CCM, Dk. Shein.
Vitendo hivi vinaendelea kufanyika na katika jimbo la Kiembesamaki vibanda kadhaa vya biashara vimevunjwa na watu wasiojulikana vikihusishwa na uhasama huohuo.
Kibaya zaidi ni pale Jeshi la Polisi linaponyamazia kwa kuwa hakuna mtu aliyekamatwa. Hili ni tatizo kubwa Polisi wanalea hujuma huku wakisema hakuna mtu aliyeripoti kituoni.
Hali inatisha. Uhalifu ulianza mapema mwaka huu na waliohusika wakaachwa ingawa wanajulikana ni makada wa CCM. Ni uchokozi unaoweza kuwa na matokeo mabaya uchaguzi unapokaribia.
Zanzibar imegubikwa na wingu la shari za kisiasa na wakati wowote linaweza kutokea lolote, pamoja na wito wa kila mara wa Rais kulinda amani na utulivu kwa nguvu zote, tamko hilo linatolewa geresaha.
Wafuasi wa vyama wamecharukwa wanapokea maelekezo na kuwasikia wakubwa zao kama Balozi Seif wanapiga vijembe wepinzani wao huku wakishadidia kuwa Zanzibar haiwezi kutawaliwa na wapinzani.
Chanzo: Mawio
No comments:
Post a Comment