Thursday 1 October 2015

CCM YACHOCHEA UDINI KWENYE TAASISI ZA KIISLAMU

Taasisi ya Kiislam yatoa Tamko Dhidi ya Lowassa na Gwajima, Kuhusu Uchaguzi Mkuu 2015

TAMKO LA TAASISI YA KIISLAMU YA IMAM BUKHARY JUU KAULI ZA NDUGU EDWARD LOWASSA NA ASKOFU GWAJIMA WA KANISA LA UFUFUO NA UZIMA

Ndugu Wanahabari,

Assalaam Alaykum,

Hivi karibuni Taifa letu limetikiswa na maneno ya hatari yaliyotoka katika vinywa vya watu wawili mashuhuri hapa nchini. Maneno ambayo endapo yatapuuzwa yatasababisha mpasuko mkubwa wa kijamii na pengine maafa, na hatimaye kubomoa misingi imara ya taifa iliyojengwa na waasisi wa Taifa hili. kauli hizo ni zile zilizotolewa na mgombea urais wa CHADEMA Ndugu Edward Lowassa na kiongozi wa Kanisa la ufufuo na uzima, Askofu Josephat Gwajima.

Mgombea Urais kwa tiketi ya CHADEMA Ndugu Edward Lowassa amenukuliwa akiwa Kanisani Mkoani Tabora akiwaomba Waumini wenzake wa Madhehebu ya Kilutheri kumuombea sana awe Rais wa Taifa letu kwa hoja kuwa nchi hii haijawahi kupata Rais Mlutheri.

Naye Askofu Josephat Gwajima ambaye ni mshirika wa karibu wa Lowassa amenukuliwa pia akielezea ndoto yake ambayo bado haijatimia ya Kuiona Misikiti ya Tanzania ikigeuzwa kuwa “Sunday Schools” za watoto, pamoja na Masheikh na Maimamu kukimbizana kwenda mbele ya msalaba wa Bwana Yesu Kristo (AS).

Maneno haya ya Ndugu Lowassa na yale ya Askofu Gwajima yakitazamwa kwa idadi ni machache sana, lakini kwa uzito wake ni mabaya tena yenye hatari kubwa kwa umoja wetu wa kitaifa.

Maneno hayo yanaweza kulisambaratisha taifa kwa vile yanaonyesha dhamira mbaya waliyo nayo viongozi hao katika kuibomoa misingi ya Utaifa ya umoja na mshikamano, na badala yake kujenga misingi ya udini katika siasa na utawala.

Kadhalika matamshi hayo yanaonyesha dhamira yao ovu ya kujenga utawala wenye kufuata misingi ya ubaguzi wa kidini endapo watafanikiwa kushika uongozi wa nchi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa Uislamu unafutika kabisa katika nchi hii.

Ndugu Wanahabari, tujikumbushe kwamba Edward Lowassa anaomba awe Rais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na mchakato wa kumfikisha huko umeratibiwa na Askofu Gwajima. Kila mmoja kati yao ameweka wazi dhamiri yake.

Wakati Ndugu Lowassa amejikita katika fikra za kupandikiza dhana ya ubaguzi wa kidini kuwa kigezo cha kuchaguliwa katika uongozi wa nchi, mwenzake Askofu Gwajima anatabiri kuwa mara tu baada ya kufanikiwa kushika hatamu za utawala, kitu cha kwanza kitakachotokea ni Misikiti kugeuka kuwa vituo vya kuwafundishia watoto imani ya Kikristo na Masheikh wote watapanga mistari kwenda kubatizwa kuwa Wakristo. Kwa maana nyingine Uislamu utafutika kabisa hapa nchini katika utawala wa Lowassa.

Ndugu wanahabari, Ushirikiano na ukaribu wa Lowassa na Askofu Gwajima si wa kuutazama kwa jicho moja tu. Tukumbuke kwamba ni Askofu Gwajima huyu huyu aliyekerwa kwa kuona Sehemu ya kuswalia Waislamu katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere wakati akieleza porojo zake za dhamira ya kujengwa Msikiti katika ofisi za Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali CAG.

Ni Askofu Gwajima huyu huyu aliyekerwa na mchakato wa Mahakama ya Kadhi hadi akalazimika kutoa lugha zisizo na staha kwa watu wazima wakiwemo viongozi wakuu wa kidini hapa nchini.

kwa upande wake ndugu Lowassa huyu ndiye aliyefanikisha mkataba kati ya Serikali na Makanisa (MoU), mkataba ambao Waislamu tunaulalamikia mpaka leo hii.

Wanaposhirikiana wawili hawa pamoja na historia ya matukio yao hayo ya ‘KIBAGUZI’ kisha kila mmoja akatamka bayana maneno yanayotikisa misingi ya Utanzania na kuweka mbele ajenda zao za udini, si busara kuwanyamazia kwa maslahi ya Umoja wetu wa Kitaifa.

Haiwezi kuwa busara kwa Jamii ya Waislamu na watanzania wanaopenda amani, kukaa kimya wakati viongozi wa kisiasa na kidini kama walivyo Askofu Gwajima na Ndugu Lowassa wanatangaza hadharani nia yao ya kuivunja misingi ya utaifa na pia kukamia kuifuta dini yetu hapa nchini na kuwabatiza Masheikh nchi nzima, na kisha baada ya hapo kuigeuza Misikiti kuwa Sunday Schools za watoto wa kikristo. Hii ni dharau iliyochupa mpaka kwa dini tukufu ya Kiislamu na kwa waislamu wenyewe.

Ndugu Wanahabari, Taasisi yetu ya "Imam Bukhary Islamic Foundation" imekaa kimya kwa muda mrefu ikitafakari matukio hayo mawili ili kuona ni hatua gani stahiki zitachukuliwa kutokana na “cheche” hii ya moto wa hatari wa ubaguzi. Mwishowe tumeona tutahadharishe na kuwakumbusha Waislamu pamoja na Watanzania kwa ujumla yafuatayo:

(1) Kwa sauti ya juu Watanzania wote tumkemee na kumpinga Ndugu Edward Lowassa katika mpango wake wa kuona urais wa Tanzania unastahiki kwa zamu za Madhehebu ya dini, na tumwambie asiwagawe Watanzania kwa misingi ya kiimani

(2) Tuwakumbushe Ndugu Lowassa na Ndugu Gwajima kwamba Waislamu kamwe hawajasahau namna mchakato wa Mahakama ya Kadhi ulivyovurugwa kwa kuwatumia maswahiba wao, ambao leo hii wamejidhihirisha kuwa pamoja kwenye kambi zao za kampeni katika kuutafuta huo urais wa Tanzania, kwa dhana mbaya eti lau mchakato ule ungefanikiwa basi ungembeba mmoja kati ya wagombea wa urais.

(3) Tamko la Gwajima kuwa katika utawala ujao misikiti itageuzwa kuwa Sunday Schools za Watoto na Masheikh watakwenda kubatizwa na hivyo Uislamu kufutika hapa nchini, si tu kwamba ni maneno ya uchochezi, chuki na dharau kwa Waislamu, bali pia ni kipimo tosha kwa watanzania wote kutambua kuwa kundi hili halifai kiuongozi na ni wajibu wa kila mtanzania kumhadharisha mwenzake juu ya kumpigia kura Ndugu Lowassa na kundi lake.

(4) Kila Mtanzania anapaswa kufahamu kuwa, kumpigia kura Lowassa ni hatua moja katika kuvunja misingi ya amani na utangamano wa nchi yetu, kutokana na dhamira yake ya kuutazama uongozi wa nchi katika sura ya udini na umadhehebu. Lakini pia kila Mwislamu atambue kuwa kumpigia kura Lowassa itakuwa ni kuutimiliza utabiri wa Askofu

Gwajima wa kuwabatiza Masheikh wote Tanzania na kuigeuza Misikiti kuwa Sunday Schools kwa watoto wa kikristo.

Ni vizuri sisi Waislamu ambao ni waathirika wa mbinu chafu iliyotumika kuikwamisha Mahakama ya Kadhi, tumuulize Ndugu Lowassa: ameahidi kutatua kero kadhaa akiingia Ikulu, lakini kwanini hajapatapo kuitaja Mahakama ya Kadhi? Je, Lowassa hujui kuwa kutokuwepo kwa Mahakama ya Kadhi ni kero kwa Waislamu?

(5) Tuendelee kuhubiriana udugu wetu wa kitanzania na wale wote wenye nia mbaya tuwakemee na tuwazuwie kufikia kilele cha madaraka kitakachowawezesha kutimiza dhamira zao bila woga ili amani yetu idumu.

(6) Taasisi inajipanga kuandaa Semina maalum kwa Maimamu na baadhi ya Masheikh ili kujadili njia iliyo bora zaidi ya kujikinga na njama za wale wote ambao wanataka kulipasua Taifa letu kwa maslahi yao binafsi, wasifikie kwenye malengo yao hayo maovu.

Na tunawaomba Masheikh na Maimamu wa Misikiti yote Tanzania pamoja na Waislamu wote kushiriki kuwazindua Waumini kila pahala kote nchini kuwazindua Wananchi kwa ujumla juu ya hatari ya kuwaweka juu ya uongozi wa nchi yetu watu wenye dhamira ya kujenga dhambi ya ubaguzi wa kidini ambayo ni kansa itakayokula mwili wa Taifa na hatimaye kuliangamiza kabisa.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Sheikh Khalifa Khamis

MWENYEKITI,
TAASISI YA KIISLAMU YA IMAM BUKHARY
(IMAM BUKHARY ISLAMIC FOUNDATION)

24/09/2015

No comments: