Saturday 31 October 2015

CUF:Hatutarudia uchaguzi wa Zanzibar

Hatuwezi kurudia uchaguzi,” alisema Taslima. “Tunachofahamu ni kuwa uchaguzi umefutwa kinyume na sheria, hivyo ZEC ibatilishe uamuzi wake na kuendelea kutangaza matokeo ya majimbo yaliyobaki ili mshindi ajulikane.”
Alisisitiza msimamo wa chama hicho kuwa Jecha alifuta matokeo hayo bila kuwashirikisha makamishna wake kama sheria ya tume hiyo inavyotaka.
“Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ibara ya 119 kifungu kidogo cha 10, inataka vikao vya ZEC kuhudhuriwa na mwenyekiti au makamu mwenyekiti na wajumbe wanne na uamuzi kuungwa mkono na walio wengi,” alisema.
Alisema makamishna wa tume hiyo katika taarifa yao kwa vyombo vya habari wamepinga kuhusika katika uamuzi huo wa kufuta matokeo ya uchaguzi.
Taslima alisema uamuzi huo umetolewa na Jecha mwenyewe kwa kushinikizwa na mamlaka za juu za Serikali.
Aliziomba jumuiya za kimataifa kuzishinikiza serikali za Jamhuri ya Muungano na Zanzibar ili zimalize mgogoro huo na kuiepusha Zanzibar kuingia katika machafuko.
Wakati CUF ikisema hayo, Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) kimetaka kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza jinsi mwenyekiti wa ZEC alivyofikia uamuzi wa kufuta matokeo na akithibitika kuwa alishinikizwa, afukuzwe kazi.
Alisema kwa mujibu wa Ibara ya 119 (1) ya katiba ya Zanzibar ya 1984, tume ni mwenyekiti pamoja na wajumbe sita kama walivyoanishwa na ibara hiyo na kwamba maamuzi yoyote ya Tume, lazima yaungwe mkono na wajumbe walio wengi.
Alisema licha ya utashi huo wa kisheria, wajumbe wawili walieleza hadharani kuwa hawajashirikishwa.
“Taarifa iliyotolewa kwa waandishi na wajumbe wa Tume, Nassor Khamis na Ayoub Bakari, kuwa hakukuwa na kikao chochote kilichofikia uamuzi wa kufuta Uchaguzi wa Zanzibar, haijapingwa mpaka sasa na wajumbe wengine wa Tume. Hii inaleta taswira ya wazi kuwa uamuzi huo haukuwa wa Tume, bali ni wa mtu mmoja ambaye ni mwenyekiti, hivyo kuyafanya kuwa ni batili mbele ya macho ya Sheria,” alisema Said.
Pia walisema kanuni ya 41(1) imeweka wazi utaratibu kufutwa kwa siku ya uchaguzi na kutangazwa siku nyingine na namna uamuzi huo utakavyofikiwa na sio kufuta matokeo ya uchaguzi au uchaguzi wenyewe.
“Ni kwa bahati mbaya sana mwenyekiti katika tamko lake hakueleza kama utaratibu umefuatwa. Huu ni ukiukwaji mkubwa wa Sheria,” aliongeza kiongozi huyo wa ZLS.
Alisema tamko hilo linaweza kuiingiza nchi katika mgogoro mkubwa wa kikatiba kama vile kumalizika kwa muda wa mwishowa utawala wa serikali ya sasa kwa mujibu wa ibara ya 28 (2) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984. Ibara hiyo inaeleza kuwa rais ataacha madaraka yake baada ya kumalizika miaka mitano kuanzia tarehe alipokula kiapo.
Katika hatua nyingine, mgombea urais wa ADC, Hamad Rashid amewaambia waandishi wa habari jana kuwa kwenye ukumbi wa Hoteli ya Grand Malt, Malindi kuwa chama chake kimekosa imani na ZEC kutokana na uendeshaji wake kukosa sifa ya kufuata sheria na kanuni.
Alisema kuwa ili uwazi na uwajibikaji viweze kufikiwa, hakuna budi kwa watendaji wa tume huyo kujiuzulu na badala yake iundwe Tume yenye uwakilishi mpana na usio na mrengo wa kisiasa.
Alisema kuwa hatua hiyo kwa kiasi kikubwa inaweza kufanikisha kufanyika kwa uchaguzi wa amani na utulivu huku demokrasia ikichukua mkondo wake.
Nayo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imemshauri mwenyekiti wa ZEC kutafakari upya uamuzi wake wa kufuta matokeo ya uchaguzi.
Taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa THBUB, Bahame Nyanduga inasema wamepitia sababu za kufuta matokeo zilizotolewa na Jecha na kubaini kuwa zinaweza kutatuliwa iwapo makamishna wa ZEC wataweka tofauti zao pembeni. Nyanduga alisema katika taarifa hiyo kuwa kifungu cha 42(6) cha sheria ya uchaguzi Zanzibar kinaipa ZEC mamlaka ya kushughulikia matatizo ya uchaguzi na kuyapatia ufumbuzi kwa utaratibu ulioanishwa katika kifungu hicho.
Taarifa hiyo ilisema kifungu hicho kinabainisha kwamba ZEC ina mamlaka ya kutangaza matokeo ndani ya siku tatu na endapo kuna matatizo inatakiwa kuyapati

No comments: