Saturday, 3 October 2015

Maalim Seif anguruma huko jimbo la Chumbuni

 Mgombea Urais kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia katika mkutano wa hadhara uwanja wa Masumbani jimbo la Chumbuni jana.
Wanachama na wafuasi wa CUF wakimsikiliza Maalim Seif huko uwanja wa Masumbani jana.
Na Khamis Haji , 

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi CUF, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema akichaguliwa atakuza uwezo wa Serikali kujiongezea mapato na ataongeza kima cha chini cha mshahara hadi kufikia 400,000.Akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni katika uwanja wa Masumbani jimbo la Chumbuni, Maalim Seif amesema Sera ya CUF imeonesha maeneo mengi ya kukuza uchumi na kuziba mianya inayochangia kupotea mapato ya Serikali, hivyo hakuna kitakachozuia Serikali kuwalipa wafanyakazi na wastaafu kiwango cha kuridhisha.Aidha, amesema kwa upande wa askari wa vikosi vya SMZ, majukumu yao ni makubwa na magumu zaidi na kima cha chini watakacholipwa itakuwa ni shilingi 450,000 ambapo kwa upande wa wastaafu pencheni yao itaanzia shilingi 200,000.

Amesema kuwa hivi sasa uwezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kukusanya shilingi bilioni 30 kwa mwezi, lakini kwa mipango ya CUF kikichaguliwa kuongoza Serikali na kwa kutumia ilani yake ya uchaguzi kitaongeza mapato hayo hadi kufikia bilioni 50 kwa kuanzia.

Katika hatua nyengine, Maalim Seif amesema kuwa akichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar, Serikali yake itatoa elimu bure kuanzia msingi hadi Chuo kikuu.

Ameeleza kuwa huduma za afya pia zitatolewa bure katika hospitali na vituo vyote vya afya vya Serikali, ikiwa ni hatua ya kutekeleza malengo ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

“Hivi sasa viongozi waliopo wanasema wanalinda misingi ya Mapinduzi, lakini huduma nyingi wananchi wanalipishwa, mimi ndiye nitakaye vaa viatu vya mzee Karume”, alisema Maalim Seif.    

Mwenyekiti wa timu ya Ushindi wa CUF, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amesema Serikali itakayoundwa na CUF iwapo wananchi watakichagua itaunda Tume Huru ya Mipango itakayokuwa na uwezo mkubwa wa kubuni mipango ya kuiondoa Zanzibar kwenyeb umasikini.

Amesema kuwa miradi mingi inayotekelezwa Zanzibar hivi sasa ni ya kutumia fedha badala ya kuingiza fedha, jambo ambalo linasababisha Serikali kushindwa kukusanya mapato vizuri na kuqweza kuwa na uchumi unaopaaa kwa kasi.   

No comments: