Monday, 5 October 2015

Magufuli anakimbia chama chake au chama kinamkimbia ?

MAGUFULI

KATIKA mazingira ya ukinzani wa kisiasa, kila unapotokea uchaguzi, ukweli huwa unatumika kwa nadra sana, na kila upande unaohusika katika ukinzani huo hujijengea dhana yake ya hicho unachokiita ukweli, lakini ambacho kinaweza kuwa mbali kabisa na ukweli halisia.
Wanafalsafa wa kale walinena kwamba inapofumuka vita katika mazingira yoyote yale, huwa kunatokea waathirika kadhaa, lakini mwathirika wa awali katika vita yoyote huwa ni ukweli. Hii ni kwa sababu kila upande unajaribu kuunda “ukweli’ wake kwa madhumuni ya kuwafanya watu waamini kwamba upande huo ndio wenye kuelekea kwenye ushindi.


Taarifa kama hizo zikitolewa kwa umahiri na watu wanaojua kufanya propaganda za mawasiliano, huwafanya wafuasi wa upande unaozitoa kujenga imani kwamba upande wao ndio unaoongoza, na kuwafanya wafuasi wa upande wa wapinzani wao kufa moyo kwa kuamini kwamba hawana cha kutumai. Ni umuhimu huu wa propaganda katika kampeni za uchaguzi unaovifanya vyama kujali sana namna vinavyoendesha mawasiliano na umma.

 Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu hauwezi na wala hautaweza kuwa tofauti na hayo niliyoyasema hapo juu. Kwa hakika, uchaguzi wa mwaka huu unaonyesha kwamba propaganda inatumika zaidi kuliko ukweli. Ukali wa propaganda ya safari hii ni kwamba uchaguzi wenyewe unaonekana kama wa “kufa na kupona,” ukiwa na viwango vya upinzani ambao labda haujawahi kuonekana hapa nchini.
Kwa hiyo, tunalazimishwa na mazingira ya kampeni hizi kuwa waangalifu ili tuweze kung’amua na kumaizi ni nini kinasemwa na nini hakisemwi ambacho katika kusemwa au kutosemwa kwake kinageuka kuwa propaganda badala ya ukweli. Hebu tuangalie ni jinsi gani kampeni zetu zimekuwa zikienenda, na tuweze kuona ni namna gani propaganda zinatawala na ni kwa kiasi gani ukweli unaachiwa mwanya angalau kwa kiasi fulani.
Jambo la kwanza lililowekwa wazi kupitia kampeni hizi ni kwamba wananchi wanataka mabadiliko, na ndiyo maana wagombea wote wanatangaza kwamba wataleta mabadiliko. Upande wa kwanza kudhihirisha kiu hiyo ya mabadiliko ulikuwa ni ule wa Ukawa, na hali hiyo imetokana na sababu kuu mbili: Moja ni kwamba kaulimbiu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilichochukua mwelekeo huo mpya miaka michache iliyopita pale kilipotangaza vuguvugu jipya la “M4C”, au “Movement For Change”, maana yake, Harakati kwa Mabadiliko.
Ya pili ni kwamba Chadema na vyama vingine vya upinzani vilivyowakilisha ndani ya Bunge Maalumu la Katiba vilikerwa na mienendo ya Bunge hili iliyoonekana kukataa na kutaka kuitupilia mbali misingi ya Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuja kuitwa “Tume ya Warioba.” Samuel Sitta, Andrew Chenge na wenzao walionyesha kutaka kuanzisha mchakato wa kuchukua maoni ya wananchi upya na kuyadharau yale yaliyokwisha kuratibiwa na Tume ya Warioba.
Ni hatua za Sitta, Chenge na wenzao ndizo zilizozaa Ukawa, au Umoja wa Katiba ya Wananchi, na vyama vilivyoungana kwa lengo hilo vikiwa ni Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD. Lengo kuu lilikuwa ni kufanya kazi usiku na mchana ili ipatikane Katiba inayoendana na maoni ya wananchi kama yalivyoratibiwa na kutangazwa na Tume ya Warioba. Huu ndio msingi mkuu wa Ukawa, tukiacha mambo mengine ambayo yanavitofautisha vyama hivyo vilivyojiunga kwa sababu hiyo kuu.
Ni dhahiri, basi, kwamba vyama vya upinzani ndivyo vilivyodhihirisha kwanza kabisa utashi wake wa kuleta mabadiliko ya kina yakisimikwa juu ya “Katiba ya Wananchi.” Lakini ajenda hiyo ya Ukawa imechukuliwa sasa na kampeni ya Magufuli, ambayo hata hivyo haiwi ajenda ya chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM). Inavyoelekea ni kama vile Magufuli anataka kusimamia mabadiliko bila kusaidiwa wala kupitia chama chake.
Nasema hivyo kwa sababu kama ni mabadiliko ya kweli anayoyataka Magufuli, na mabadiliko hayo hayana budi kujengwa juu ya misingi ya kikatiba, hilo halitawezekana chini ya usimamizi wa CCM. CCM imeonyesha wazi kile ambacho Jaji Warioba hakukiona alipokubali uteuzi wa Rais Kikwete kuongoza Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Ingawa Warioba hakuliona hili, ni jambo lililokuwa wazi kabisa.
Baada ya Celina Kombani (sasa marehemu) kutamka kwamba hakukuwa na haja ya kuwa na mabadiliko ya Katiba, tulifanya mdahalo pale Nkrumah Hall, chini ya mwavuli wa Chama cha Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, UDASA, mimi nikichangia jukwaa na Profesa Issa Shviji.
Miongoni mwa maoni niliyoyatoa pale ni kwamba hatuna mazingira ya kutuwezesha kuandika Katiba mpya, na kwamba tulihitaji kwanza kuwa na maridhiano ya kitaifa juu ya misingi ya kisiasa na kifalsafa ndipo tuweze kuandika hiyo Katiba mpya. Hili halikuwezekana kwa sababu wakuu wa CCM hawajazoea mijadala, na jambo lolote lisilozoeleka huogopwa na hao wasio na mazoea nalo.
Matokeo yake ni kwamba Warioba na timu yake wamezunguka kote, wamehangaika na wakati mwingine kukesha bila kulala, wakifanya kazi, lakini wakimfanyia kazi tajiri ambaye hakuwa pamoja nao. Mwisho wake ukaja kuwa ni kazi yao kutupwa, na wajumbe wenyewe kudhalilishwa na kutendewa kama vile walikuwa ni wahalifu: kunyang’anywa magari bila taarifa, kusitishwa ukaazi wao jijini Dar es Salaam na kufungiwa tovuti yao.
Nyanyaso la mwisho lilikuja pale Warioba alipochuuzwa na akakubali kwamba awasilishe rasimu yake mbele ya Bunge kabla ya Rais Kikwete hata hajalizindua Bunge lenyewe, utaratibu ambao sijawahi kuusikia duniani kote. Rais akachukua nafasi hiyo na kuyachanachana na kuyapondaponda yale yote yaliyokua ndani ya Rasimu ya Warioba.
Hapa, Rais Kikwete alikuwa anateua upande wa wana-CCM wenzake, yaani akina Sitta na Chenge, na siyo upande wa Warioba, ambaye pamoja na mapenzi yake makubwa kwa CCM, chama hicho hakina mapenzi yoyote kwake; mapenzi ya CCM ni kwa akina Sitta na Chenge. Waingereza husema, “Birds of a feather flock together”, wakiwa na maana kwamba ndege wanaofanana kwa manyoya yao, huruka pamoja”
Warioba angependa apate manyoya hayo, lakini hakujaliwa kuyapata, na kama angependa wakuu wa chama chake wabadilike na wawe na manyoya yanayofanana na ya kwake, hilo haliwezekani pia. Kimsingi, wakuu wa CCM, wakiwamo akina Sitta na Chenge, wanayaogopa mabadiliko kama ukoma, kwa sababu mabadiliko ya kweli yaliyojengwa juu ya misingi ya kikatiba, yataondoa fursa zao za kujipatia “vijisenti” bila kuzuiwa na katiba wala sheria iliyo wazi.
Sasa, Magufuli amechukua nembo ya Chadema ya M4C, lakini M yake inatokana na jina lake. Hajaona, ama hajali kwamba M ya Chadema haina maana ya Mbowe, Mdee, Mbilinyi wala Myinka; ni “Movement” na wala si jina la mtu mmoja.
Na hiyo ndiyo tofauti kubwa ninayoiona mimi. Magufuli amekuwa akitangaza “mabadiliko” kwa kutumia jina lake mwenyewe. Kila lipokwenda amesikika akisema “Serikali ya Magufuli itakuwa…..”, au “Tanzania ya Magufuli itajenga….,” na kadhalika.
Hii haitokei kwa bahati mbaya, bali imepangwa kwa makusudi mazima. Imekuwa ni lazima kuweka ufa kati ya mgombea John Magufuli na chama chake, kwa sababu anakijua vyema chama chake, na anajua kwamba chama hicho kimejijengea sifa mbaya ndani ya jamii.
Baada ya nusu karne ya kuendesha serikali, ni vigumu kwa yeyote anayekiwakilisha chama hicho kuahidi lolote litakalosikika kama jipya kwa wananchi. Kila ahadi inayoweza kufikirika ilikwisha kutolewa na kutelekezwa; hakuna jipya tena.
Utashi wa kujiweka mbali unaweza kuwa si mkakati wa Magufuli peke yake, bali pia na chama chake, ambacho kingependa kubakia madarakani kwa sababu zinazoelezeka lakini kingependa kuwafanya wananchi waamini kwamba huu ni mwanzo mpya, na Magufuli anaweza kuaminika kuliko chama chake. Ni kama vile, ingewezekana, Magufuli angesimama kama mgombea binafsi, lakini hili lilikwisha kukataliwa na chama chake.
Kwa hiyo imembidi achanganye kidogo kutoka huku na kidogo kutoka kule: upande mmoja ni mgombea wa chama-tawala, lakini kwa upande mwingine ni mgombea nusu-binafsi anayekikosoa chama chake na serikali aliyoifanyia kazi kwa muda wa miaka ishirini sasa. Ni hali isiyoelezeka kirahisi.
Wale wanaokumbuka, tangu siasa za vyama vingii zianze tena nchini, tulizoea kuona mabango ya kampeni za CCM yakisema “CHAGUA CCM, CHAGUA MKAPA” miaka ya 1995 na 2000 na “CHAGUA CCM, CHAGUA KIKWETE” katika miaka ya 2005 na 2010. Leo tunaona mabango yanamuombea kura Magufuli bila kukiombea kura chama chake. Kulikoni? Bila shaka ni ule ufa nilioueleza hapo juu.
Na zipo sababu nyingi za kuielezea hali hii. Mojawapo kubwa ni rekodi ya utendaji wake Magufuli. Kwa mfano, gazeti hili lilipata fursa ya kumhoji siku za hivi karibuni, na akaelekeza apelekewe maswali kabla ya siku ya mahojiano. Pamoja na kupeleka maswali kabla ya mahojiano, alishindwa kujibu maswali aliyoyaona kama nyeti.
Mojawapo ya maswali yaliyomshinda ni lile lililohusu “uuzaji” wa nyumba za serikali (uuzaji ambao kwa kweli haukuwa uuzaji bali ugawaji). Swali hilo lilimshinda kujibu pamoja na kuwa alikuwa amekwisha kupelekewa maswali kabla ya mahojiano. Hili ni suala ambalo nitalirejea wiki ijayo nikiliangalia katika mwanga wa masuala mengine yanayowahusu wagombea wakuu wa urais na wapambe wao, na jinsi kampeni zinavyoendeshwa. Itaendelea
raimwema

No comments: