Monday, 5 October 2015

SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA MCHUNGAJI CHRISTOPHER MTIKILA KUTOKA KWA MWENYEKITI WA CHADEMA TAIFA


CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa taarifa za kifo cha mwanasiasa mkongwe katika siasa za mageuzi nchini, Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party, Mchungaji Christopher Mtikila kilichotokea leo alfajiri kwa ajali ya gari.

Katika salaam zake za pole kwa familia ya Mchungaji Mtikila, Katibu Mkuu wa DP, viongozi na wanachama wa chama hicho kwa ujumla, Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa kifo cha Mchungaji Mtikila kimeacha pengo kubwa katika siasa za mageuzi nchini hasa katika kupigania Tanganyika na suala la mgombea huru kuwa haki ya kikatiba nchini.

“Mwenyekiti wa DP Mtikila atakumbukwa kwa msimamo wake usioyumba katika katika mambo makubwa mawili, kwanza kwa msimamo wake wa kuipigania Tanganyika kwa muda mrefu bila kuchoka akitumia kila njia na majukwaa mbalimbali kujenga hoja za kudai Tanganyika.

“Suala jingine ambalo nalo pia alilipigania kwa ujasiri kisiasa na kisheria lilikuwa ni agenda ya mgombea huru ili iwe mojawapo ya haki za msingi zinazotambulika katika katiba yetu ya nchi.

“Ni jambo la kusikitisha sana Mchungaji Mtikila ameaga dunia bila kuona mambo hayo makubwa mawili yakitimia akingali hai. Ni imani yangu kuwa kizazi cha sasa ambacho kinapigania mabadiliko katika nchi yetu hasa kupitia uchaguzi huu, kitajifunza mengi kutoka kwa kiongozi huyo wa kisiasa na kuyaenzi yale yote mazuri aliyoyapigania kuhakikisha yanatimia kwa manufaa ya Watanzania,” amesema Mwenyekiti Mbowe na kuongeza;

“Kwa masikitiko na majonzi makubwa natoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki kwa kumpoteza mpendwa wao na moja ya guzo muhimu katika maisha. Mwenyezi Mungu awasimamie na kuwatia nguvu katika wakati huu mgumu wa majonzi katika kuukabili ukweli wa msiba huo mkubwa katika familia.

“Kwa niaba ya viongozi wenzangu wa CHADEMA, wapenzi, wafuasi, mashabiki na wanachama wote kwa ujumla, pia natoa pole na salaam za rambirambi kwa Katibu Mkuu wa DP kwa niaba ya viongozi na wanachama wa chama hicho kwa kuondokewa na kiongozi wao mkuu,” amesema Mwenyekiti Mbowe katika salaam zake.

Imetolewa leo Oktoba 4, 2015 na;

Idara ya Habari na Mawasiliano

CHADEMA

No comments: