Monday, 9 November 2015

ALIYEKUWA KAMISHNA WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA 9MAARUFU KAMA TUME YA WARIOBA) MUHAMMAD YUSSUF ASEMA NI VYEMA SASA USHAHIDI WA JECHA SALIM JECHA KUWEKWA HADHARANI ILI WAPIGA KURA WAPIME

.

Akitoa maoni yake juu ya makala iliochjapishwa na gazeti la Nipashe Jumapili na mwandishi Mwinyi Sadallah ikimkariri mwenyekiti wa kamati ya kampeni za CCM kitaifa upande wa Zanzibar Sief Ali Iddi kwamba suala la marejeo ya uchaguzi halina mjadala na kwamba serikali imeridhia kurudiwa kwa uchaguzi.

Awali ya yote, Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha, alitoa sababu tisa zilizosabisha kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo na kuamua urudiwe, ikiwemo kura katika vituo kupita idadi ya watu waliosajiliwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Sababu nyegine ni kuhamishwa kwa masanduku ya kura na kuhesabiwa nje ya vituo kinyume na taratibu, kupigwa mawakala na kutolewa nje ya vituo, vijana kuvamia vituo na kuanza kupiga watu na kuzuwia watu wasiokua wa vyama vyao kufika katika vituo vya kupiga kura na kupiga kura.

Aidha, alisema walipokea malalamiko mengi kutoka vyama mbalimbali yanayoashiria kutoridhika na mchakato mzima wa upigaji kura, kuhesabu na kutoa matokeo ya uchaguzi huo, pamoja na namba za fomu za matokeo ya vituo vingi vya Pemba kuonekana kufutwa na kuandikwa upya".

MAONI: Ushahidi wa sababu tisa zilizopelekea kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mzima uko wapi? Haitoshi tu kudai kuwa kulikuwa na sababu hizi na zile bila ya kutoa ushahidi kamili hadharani kwa njia ya uwazi kabisa. Tanzania inaishi katika ulimwengu wenye kuheshimu dhana ya uwazi badala ya kukumbatia usiri.

Kwa mfano, Mwenyekiti Jecha anapaswa kutuonyesha hayo malalamiko aliyoyapokea kutoka kwa wawakikishi wa vyama mbali mbali vya siasa yanayoashiria kutoridhika kwao na mchakato mzima wa upigaji wa kura. Kama ushahidi huo upo kweli, sasa Jecha anafichaficha nini? Si autoe tu hadharani kwa kila mtu kujionea.

Isitoshe, Jecha anapaswa kutuambia ni lini hasa amepokea malalamiko hayo; wakati wa upigaji kura au wakati wa uhakiki wa kura baada ya kuhesabiwa?

Nauliza hivi kwa sababu ikiwa kulikuwa na malalamiko hayo, ikiwa ni pamoja na kura katika vituo kupita idadi ya watu waliosajiliwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura; kuhamishwa kwa masanduku ya kura na kuhesabiwa nje ya vituo kinyume na taratibu; kupigwa mawakala na kutolewa nje ya vituo; vijana kuvamia vituo na kuanza kupiga watu na kuzuwia watu wasiokua wa vyama vyao kufika katika vituo vya kupiga kura na kupiga kura; na pamoja na namba za fomu za matokeo ya vituo vingi vya Pemba kuonekana kufutwa na kuandikwa upya.

Kwa kugha nyepesi, ikiwa malalamiko yote hayo ni kweli, kwanini Jecha alisitisha zoezi la kuhakiki matokeo ya uchaguzi katika majimbo ya Unguja baada ya kuhakiki majimbo 31 tu na kubakisha majimbo mengine 5 ya Unguja ambako hakukuwa na 'malalamiko' yoyote yale? Au Jecha anataka kutuambia kuwa hata Unguja nako kulichafuliwa?

Ama kuhusu kauli ya Balozi Seif Ali Iddi inayoashiria kuwa "Serikali imeridhia uamuzi wa Zec kufuta matokeo ya uchaguzi huo", ningelimshauri akafafanua zaidi kauli yake hiyo; ni serikali ipi hiyo iliyofikia uamuzi huo, kwa sababu mara ya mwisho nilipofanya marejeo kuhusu hali hii, nimegundua kuwa mpaka hivi leo hakuna ushahidi wowote ule kuwa Baraza zima la Mapinduzi lenye kujumuisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Ali Mohammed Shein, Makamu wake wote wawili pamoja na mawaziri wote, halijakutana kutathmini hali ya mgogoro wa Zanzibar iliyosababishwa na uamuzi wa kufutwa kwa uchaguzi.

Cha kushangaza zaidi ni kuwa wakati nchi imekumbwa na mgogoro mkubwa wa kikatiba na kisheria, Rais wa Zanzibar, ambaye ndiye mkuu wa nchi, hajatoa kauli yoyote ile kwa wananchi wake kana kwamba hayupo au hahusiki kwa namna yoyote na hali ya kusikitisha inayoikumba Zanzibar hivi sasa! Baadhi yetu tunajiuliza: hivi Zanzibar inaongozwa na nani?

Inashangaza sana!

Chanzo : Muhammad Yussuf

No comments: