Monday, 9 November 2015

NAUNGA MKONO UAMUZI WA MAGUFULI, LAKINI NATOA ANGALIZO!!

Na. Mtatiro J,

Naunga mkono asilimia 100 uamuzi wa KUFUTA SAFARI ZA NJE YA NCHI hadi kuwepo Kibali cha Rais au Katibu Mkuu Kiongozi.

Hata kama bado pana mvutano wa ndani kati ya UKAWA na CCM juu ya ushindi na Urais wa Magufuli ambao najua mwisho wa siku utakamilika kwa UKAWA kusamehe na kujipanga (mtizamo binafsi), ukweli unabaki kuwa, UFUTWAJI WA SAFARI HIZO "is a popular decision" (ni uamuzi unaoungwa mkono na wengi) bila kuhusisha ishu ya kujadili URAIS wa Magufuli na Ushindi wa CCM.

Ni kwa sababu hiyo mimi binafsi naliona jambo hilo kama tija muhimu kwa taifa. Hakika Serikali ya KIKWETE na CCM ilivuruga kabisa uchumi wa nchi kwa matumizi mabovu, ya anasa na safari zisizokwisha. Kwa JK, masuala ya kufanywa na balozi yalimpeleka yeye mwenyewe nje na mara chache waziri wake wa mambo ya nje.

Hata alipotunukiwa shahada za uzamivu za pongezi na vyuo vikuu vya nje bado alisafiri yeye na wasaidizi kibao ili kuhudhuria UTUNUKIWAJI husika, na kumbe balozi wake mmoja alitosha kupokea tuzo hizo kwa niaba yake. Kwa vyovyote vile bila kujali itikadi zetu, huu ni uamuzi bora kabisa kufanywa na mtu aliyekabidhiwa ofisi ya juu ya nchi kikatiba.

TAHADHARI,
Watanzania wanapaswa kupongeza ufutwaji wa safari za nje kwa tahadhari maalum sana. Uamuzi huo umefanywa na mtu mmoja (Rais) lakini haupo kisheria wala kiutamaduni.

Najaribu kufikiri tu, ni vipi Rais wa sasa na aliyefanya uamuzi huu akashindwa kuongoza nchi kwa sababu za kikatiba (kujiuzulu, kifo, kuondolewa na bunge n.k.), akiachiwa nchi makamu wake au akichaguliwa Rais mwingine atakuja kuendeleza utaratibu huo? Jibu ni HAPANA, kiuzoefu anaweza kuja mtu mwingine ambaye atazirudisha safari kwa asilimia 1000.

NINI KIFANYIKE?
Kuna mambo mawili makubwa;
1. Serikali iandae muswada wa sheria na kuupeleka bungeni, muswada unaweza kuitwa "Sheria ya Safari za Nje ya mwaka 2016". Muswada huu;

(a) uweke vigezo vya safari zote za nje ya nchi,

(b) muswada umuelekeze hadi Rais ni safari zipi anaweza kwenda na zipi atume wawakilishi, muswada uweke wazi kila mhimili wa dola utafanya safari kiasi gani kwa mwaka na kwa vigezo vipi (Bunge, Mahana na Serikali)

(c) Muswada uelekeze ni mambo yapi lazima yashughulikiwe na mabalozi nje ya nchi na wao watoe taarifa kwa serikali,

(d) Muswada uoneshe adhabu kwa watumishi wa umma na viongozi ambao watafanya safari nje ya nchi kinyume na utaratibu uliowekwa na sheria.

(e) Muswada uainishe masuala mengine yote muhimu yanayohusu safari za nje na kuyawekea utaratibu wa kisheria ambao ni BINDING.

2. Kama serikali haileti muswada huu bungeni,mbunge mmoja apewe ushirikiano na wenzake awasilishe muswada binafsi juu ya jambo hili, kwa vyovyote vile jambo hili litaungwa mkono (Kama ningekuwa mbunge jambo hili lingekuwa kipaumbele kikubwa sana).

SIKILIZENI;
Pamoja na kuwa nchi yetu imekuwa na sheria nyingi nzuri ambazo hazifuatwi wala kusimamiwa na serikali, bado kuna haja ya kushughulikia masuala magumu kisheria zaidi kuliko kuyaacha yaelee kwa amri ya mtu mmoja ambaye anaweza asiwepo madarakani kesho.

Yes, safari za nje zimelifilisi Taifa na walioongoza safari hizo ni CCM na serikali yake, kama wanazifuta hebu wafanye hivyo kisheria na kwa dhati. Afrika ina tatizo la asili kwenye utendaji, KUJENGA WATU BADALA YA KUJENGA MIFUMO IMARA. Leo Rais Magufuli anapiga marufuku safari za nje kwa mdomo na kwa kusimamia yeye mwenyewe, kesho asipokuwepo??

Nasisitiza kuwa mfumo wa uongozi wa nchi yetu ni mbovu na tunapaswa kuujenga kisheria na kuurasimisha kiusimamizi. Sikubaliani na ujenzi wa mfumo bora kwa mdomo au kwa kutumia Presidential orders ambazo ni rahisi kufutwa na Rais anayefuata.

Jambo hili ni SERIOUS na lishughulikwe SERIOUSLY!

Mtatiro J,
Dar Es Salaam.

No comments: