Sunday 8 November 2015

AZIMIO LA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA LA CUF KUHUSIANA NA UCHAGUZI MKUU WA ZANZIBAR WA TAREHE 25 OKTOBA, 2015


Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la THE CIVIC UNITED FRONT (CUF - Chama Cha Wananchi) limekutana katika kikao cha dharura leo hii tarehe 7 Novemba, 2015, mjini Zanzibar kuzungumzia hali ya kisiasa hapa nchini kufuatia Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015.


KILICHOJIRI KUHUSIANA NA UCHAGUZI MKUU WA ZANZIBAR:
Baraza Kuu limeridhika kwamba Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015 ulikwenda vizuri na kuwapa nafasi wananchi wa Zanzibar walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kuchagua viongozi wanaowataka kuwaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Baada ya upigaji kura kumalizika, kazi ya kuhesabu kura nayo ilikwenda vizuri na fomu za matokeo ya uchaguzi kwa kila kituturi cha kupigia kura zilikamilika. Baada ya hatua hiyo ilifuata hatua ya majumuisho katika ngazi ya majimbo ambayo nayo ilikwenda vizuri na kukamilishwa bila ya kuwepo malalamiko yoyote kutoka chama chochote kilichokuwa kinashiriki uchaguzi huo.
Ni kutokana na kukamilika kwa hatua zote hizo bila ya kuwepo malalamiko yoyote, na kwa kufuata masharti ya kifungu cha 88 cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 11 ya
1984, ndipo Wasimamizi wa Uchaguzi wa majimbo yote ya Unguja na Pemba wakawatangaza washindi wa nafasi za Uwakilishi na Udiwani na pia kuwapa taarifa za maandishi wagombea walioshinda.
Kifungu hicho cha 88 cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar kinaeleza mamlaka na uwezo wa Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo kama ifuatavyo:
"88. Baada ya matokeo ya uchaguzi unaogombewa kuthibitishwa, Msimamizi wa
                 Uchaguzi atafanya yafuatayo:-

(a) haraka atamtangaza mgombea aliyepata wingi wa kura halali zilizopigwa
     kuwa amechaguliwa; na


(b) atapeleka taarifa ya maandishi kwa mgombea aliyeshinda; na
(c) atatoa taarifa ya matokeo ya uchaguzi kwa Tume ambayo itapeleka
     matokeo hayo, pamoja na idadi ya kura alizopata kila mgombea katika  
     kila jimbo kutangazwa katika Gazeti Rasmi."

Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, uchaguzi wa Wawakilishi na Madiwani ulikuwa umeshakamilika na washindi kutangazwa kwa majimbo na wadi zote za Unguja na Pemba. Wagombea walioshinda kutoka vyama vyote walishapewa hati za uthibitisho rasmi wa kuchaguliwa na Wasimamizi wa Uchaguzi wa majimbo.
Hatua hizo pia zilifanyika kwa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar ambapo majumuisho yalishakamilika mpaka ngazi ya jimbo kwa majimbo yote 54 na matokeo ya kila jimbo kubandikwa nje ya vituo vya majumuisho baada ya kukamilisha masharti ya kifungu cha 42(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar. Hatua zote hizi zilishakamilika ilipofika asubuhi ya tarehe 26 Oktoba, 2015. Baada ya hapo, kazi iliyobaki ilikuwa ni ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kupitia kituo kikuu cha majumuisho kuhakiki matokeo hayo iliyoyapokea kutoka kwa Wasimamizi wa Uchaguzi wa Majimbo na baada ya kuyathibitisha kuyatangaza. Kazi hii nayo ilikuwa inaendelea vizuri na matokeo ya majimbo 31 ya Unguja yalikuwa yamehakikiwa na kuthibitishwa na Tume na kutangazwa. Matokeo ya majimbo mengine matano (5) yaliyobakia kwa kisiwa cha Unguja na manne (4) kati ya 18 ya kisiwa cha Pemba nayo yalihakikiwa na yakawa yanasubiri kutiwa saini na Mwenyekiti wa Tume na kutangazwa.
Ilikuwa ni katika hatua hii, ndipo katika hali iliyowashtua na kuwashangaza wananchi wengi pamoja na waangalizi wote wa uchaguzi wa ndani na nje, tarehe 28 Oktoba, 2015 zikiwa ni siku tatu tokea siku ya uchaguzi na siku mbili tokea kura kumaliza kuhesabiwa na kujumuishwa katika majimbo yote 54 ya Unguja na Pemba, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, aliandaliwa mkutano na waandishi wa TBC na ZBC pekee na kurikodi tamko la kwamba eti Tume imeufuta uchaguzi wote wa Zanzibar. Jecha alifanya hivyo bila ya kutaja kifungu chochote cha Katiba ya Zanzibar ya 1984 au Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 11 ya 1984 kinachotoa uwezo wa kufuta uchaguzi wa wananchi wa Zanzibar iwe ni kwa Mwenyekiti au hata kwa Tume kwa ujumla wake.
Mamlaka pekee iliyo nayo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa mujibu wa kifungu cha 74 cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar tena kwa kupitia Msimamizi wa Kituo ni ya kuahirisha shughuli ya upigaji kura katika kituo husika hadi siku inayofuata "endapo taratibu za uchaguzi katika kituo chochote cha upigaji kura zimeingiliwa au zimezuilika kutokana na fujo au utumiaji nguvu." Hili halikutokea katika kituo chochote na ndiyo maana uchaguzi uliendelea hadi hatua ya kuhesabu kura na kufanya majumuisho majimboni.
Ni vyema tuseme kwamba hakukuwa na malalamiko yoyote kutoka chama chochote kinachoshiriki uchaguzi katika siku ya upigaji kura si kati katika vituo vya kupigia kura, vituo vya kuhesabu kura wala katika vituo vya majumuisho ya kura vya majimbo. Kwa msingi huo, ndiyo maana taratibu ziliendelea na hazikuzuiwa.
Ni kutokana na ukweli huu ndiyo maana waangalizi wa uchaguzi wakiwemo wa Jumuiya ya Madola (The Commonwealth), Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Ulaya (EU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na TEMCO wote wametoa taarifa zao wakieleza kuwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar ulikwenda vizuri, ulikuwa huru na wa haki na uliofanyika kwa amani. Hata Mwenyekiti wa ZEC naye alitangaza kuwa Uchaguzi ulikwenda vizuri, ulikuwa wa wazi, haki na huru.
Tokea kutolewa kwa tamko la Mwenyekiti wa Tume, Jecha Salim Jecha, Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejikuta imeingizwa katika taharuki na wasiwasi na kupelekea hofu kubwa kuhusiana na hali ya kisiasa na kiusalama ya Zanzibar.
Katika hali isiyotarajiwa na isiyo ya kiungwana katika nchi inayofuata Katiba na Sheria na inayozingatia misingi ya utawala wa sheria, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jaji Abdulhakim Muhsin Ameir, alishuhudiwa na hata waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa akiwa anachukuliwa kwa nguvu na vyombo vya ulinzi na usalama kutoka katika eneo la Hoteli ya Bwawan ambako ndiko kulipokuwa na kituo kikuu cha majumuisho ya kura na utangazaji wa matokeo ya uchaguzi.
Baada ya hatua hiyo, kumeripotiwa matukio mengi ya uvunjwaji wa haki za binadamu ambapo raia wasio na hatia wamepigwa na kujeruhiwa vibaya, nyumba kuchomwa moto na nyengine kuvunjwa. Matukio haya mengi yamefanywa na kikundi kidogo cha askari wa Vikosi vya SMZ ambacho kinaonekana kimeandaliwa maalum kwa ajili ya kuwahujumu raia.
Matukio yote haya yametia dosari kubwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika jumuiya ya kimataifa na kupelekea nchi yetu kuonekana haina tofauti na nchi nyengine zinazokandamiza demokrasia na haki za binadamu na kutofuata Katiba na Sheria za nchi.
Kwa upande mwengine hali hiyo inaonekana kuvuruga misingi ya maridhiano na umoja wa kitaifa tuliyokuwa tumeanza kuijenga Zanzibar tokea mwaka 2009. Hali ya uhasama na chuki inarudishwa kwa nguvu na kikundi kidogo cha watu ambao wameamua kwamba maslahi yao binafsi na familia zao ni muhimu zaidi kuliko maslahi makubwa ya nchi yetu na watu wake.

ATHARI ZA KUFUTA UCHAGUZI MKUU WA ZANZIBAR KWA UCHAGUZI WA JAMHURI YA MUUNGANO:
Jambo moja ambalo linaonekana halikuzingatiwa na Jecha Salim Jecha na wale waliomsukuma kutoa tangazo lake ni athari ya kufuta uchaguzi mkuu wa Zanzibar kwa uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wabunge kwa upande wa Zanzibar.
Kwa taratibu za uendeshaji wa chaguzi zilivyo kwa upande wa Zanzibar, chaguzi mbili hizi (ule wa Zanzibar na ule wa Muungano) huwa zinafanyika siku ile ile, katika vituo vile vile, kwa kutumia Daftari la Wapiga Kura lile lile (ukiondoa wapiga kura wachache ambao si Wazanzibari na ambao huandikishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano tu kwa upande wa Zanzibar) na pia wasimamizi wake wa uchaguzi wa NEC na ZEC huwa wanashirikiana katika kusimamia chaguzi hizo.
Kwa hivyo, ni kituko na jambo la ajabu kusema matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Wabunge kwa upande wa Zanzibar ambapo kura zake zilipigwa katika vituo vile vile na wapiga kura wale wale katika siku na wakati ule ule yawe ni halali na yanakubalika na kutangazwa lakini eti matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, Wawakilishi na Madiwani yawe ni batili na yasiyokubalika na hivyo kufutwa.
Kwa ufupi, kuendelea kushikilia msimamo uliotolewa na Jecha Salim Jecha, ni kutia walakini katika matokeo ya uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande wa Zanzibar. Hii si taswira nzuri na hatupaswi kuiacha iendelee.

MGOGORO WA KIKATIBA KUHUSU UONGOZI WA NCHI:
Tamko la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, limeiingiza Zanzibar katika mgogoro mkubwa wa kikatiba ambao hauna sababu ya kuwepo.
Kifungu cha 28(1)(a) cha Katiba ya Zanzibar kinaeleza kwamba mtu ataendelea kuwa Rais mpaka Rais anayefuata ale kiapo cha kuwa Rais. Kifungu hichi kimetumiwa na baadhi ya watu kudai kwamba Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein ataendelea kuwa Rais halali mpaka hapo Rais anayefuata atakapokula kiapo.
Hata hivyo, ili kukifahamu kifungu cha 28(1), mtu inabidi pia asome pamoja na kifungu cha 28(2). Kifungu cha 28(2)(a) kinaeleza kwamba:
"28(2). Kufuatana na maelezo ya kijifungu cha (1) cha kifungu hiki, Rais ataacha   madaraka yake baada ya kumalizika miaka mitano kuanzia tarehe, ambapo:
(a) kama yeye ni mtu ambaye ndiye mara ya kwanza amechaguliwa kuwa Rais     chini ya Katiba hii alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa Rais"
Kwa maana hiyo, kifungu hichi kinaeleza kwamba kipindi cha Rais aliyechaguliwa ni miaka mitano tokea siku alipoapishwa. Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein aliapishwa tarehe 3 Novemba, 2010 na hivyo kipindi chake cha Urais kimemalizika tarehe 2 Novemba, 2015.
Kwa upande mwengine, kuna suala la kuvunjwa Baraza la Wawakilishi ili kupisha uchaguzi kufanyika na pia kuitishwa kwa Baraza la Wawakilishi jipya baada ya uchaguzi.
Kifungu cha 90(1) cha Katiba ya Zanzibar ya 1984 kinaeleza kwamba:
"90.(1)  Wakati Baraza litakapovunjwa, Uchaguzi Mkuu wa Wajumbe wa Baraza la  Wawakilishi utafanywa na mkutano wa mwanzo wa Baraza jipya utafanywa si  zaidi ya siku tisini toka kuvunjwa kwa Baraza."
Baraza la Wawakilishi lililopita lilivunjwa tarehe 13 Agosti, 2015. Kwa maana hiyo, kwa mujibu wa kifungu cha 90(1) cha Katiba ya Zanzibar, Baraza jipya linapaswa kuitishwa si zaidi ya tarehe 12 Novemba, 2015. Kwa mujibu wa kifungu cha 29 na 92(2) cha Katiba hiyo, Baraza la Wawakilishi linaweza tu kuongezewa muda iwapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakapokuwa kwenye vita.
Kwa msingi huo, sasa hivi hakuna Baraza la Wawakilishi ambalo ndiyo chombo cha wananchi wa Zanzibar kinachoisimamia Serikali yao, na Baraza jipya linapaswa kuitishwa si zaidi ya siku tisini tokea Baraza lililopita lilipovunjwa. Kwa maana hiyo, ifikapo tarehe 12 Novemba, 2015 ni lazima Baraza jipya lililochaguliwa tarehe 25 Oktoba, 2015 liitishwe na lisipoitishwa, nchi yetu itaendelea kutumbukia kwenye mgogoro mkubwa zaidi wa kikatiba na kiutawala. Hatupaswi kufika huko na hatuna sababu ya kufika huko.

UFUMBUZI:
Marafiki wa Tanzania zikiwemo nchi za Marekani, Uingereza, nchi za Umoja wa Ulaya (EU), na jumuiya za kimataifa na kikanda ambazo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanachama zikiwemo Jumuiya ya Madola (The Commonwealth), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zimetoa wito kutaka hali hii ipatiwe ufumbuzi kwa kukamilishwa hatua za majumuisho ya hesabu za kura na kutangaza matokeo ya uchaguzi wa nafasi ya Urais wa Zanzibar. Nchi na jumuiya hizo zimesema kwamba baada ya hapo uongozi wa kisiasa wa vyama vya CUF na CCM unapaswa kukaa pamoja kuzungumza jinsi ya uundwaji na uendeshaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kama yalivyo matakwa ya Katiba ya Zanzibar na kuhakikisha kuwa demokrasia, haki za binadamu na amani vinaenziwa, kulindwa na kutunzwa.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF linapongeza msimamo huo uliooneshwa na marafiki wa Tanzania na jumuiya za kikanda na kimataifa na linauunga mkono. Baraza limetiwa moyo sana na hatua ya jumuiya ya nchi za Kiafrika na kikanda zikiwemo AU, SADC na EAC kutoka waziwazi na kutetea haki za wananchi wa Zanzibar na maamuzi yao waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015. Hii ni dalili njema ya jinsi gani Bara la Afrika linavyosonga mbele katika kutambua umuhimu wa ujenzi na ulinzi wa misingi ya demokrasia na haja ya kuheshimu maamuzi ya watu katika kuchagua viongozi wanaowataka na kuwaweka madarakani kupitia sanduku la kura.

AZIMIO LA BARAZA KUU:
Baada ya mjadala wa kina wa suala hili, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF limefikia maazimio yafuatayo:
1. KWAMBA Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) itengue uamuzi wa Mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha, wa kufuta uchaguzi mkuu wa Zanzibar, jambo ambalo hana mamlaka na uwezo nalo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi Nam. 11 ya 1984.
2. KWAMBA Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar irudi kukamilisha hatua zilizobaki za uhakiki na majumuisho ya matokeo ya uchaguzi ya majimbo 14 ya Pemba na kisha iyatangaze matokeo ya majimbo hayo 14 pamoja na majimbo mengine 9 (5 ya Unguja na 4 ya Pemba) ambayo tayari ilikamilisha uhakiki na majumuisho lakini ikawa haijayatangaza. Baraza Kuu linasisitiza kwamba halitakubaliana kwa namna yoyote ile na hatua ya kufanya uchaguzi wa marudio ikizingatiwa kwamba uchaguzi ulishafanyika na kazi ya kuhesabu kura kumalizika.
3. KWAMBA baada ya matokeo kutangazwa, mshindi wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar akutane na viongozi wa vyama vya CUF na CCM vilivyopata Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika uchaguzi mkuu uliopita na kukubaliana namna bora ya uundwaji na uendeshwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na kuendeleza maridhiano, umoja wa kitaifa na amani ya nchi yetu.
4. KWAMBA linatoa wito kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli, kuchukua hatua za kuona suala hili linapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa haki unaozingatia matakwa ya Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar ya 1984. Baraza Kuu linamhakikishia na kumuahidi Rais Magufuli kwamba litampa kila ushirikiano yeye na viongozi wengine katika hatua atakazochukua ili kuona nchi yetu inaondokana na mkwamo huu na tunasonga mbele kwa pamoja kama Taifa.
5. KWAMBA linatoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha kuwa nchi yetu inabaki katika hali ya amani na utulivu kwa kuepuka kujiingiza katika vitendo vinavyoashiria vitisho na kuvunja haki za binadamu. Baraza Kuu linamuomba Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama kuchukua hatua za kuondosha vikosi na vifaa vizito vya kijeshi mitaani ili kuwajengea imani wananchi kuhusu usalama wao wakati huu wanaposubiri suluhisho la amani la hali iliyojitokeza.
6. KWAMBA linawaomba wananchi wa Zanzibar kuendelea kuwa watulivu na kutunza amani ya nchi yetu na kutoa fursa kwa viongozi wetu kuendeleza juhudi za kulipatia ufumbuzi wa haki suala hili na kukamilisha hatua zilizobaki za kukamilisha majumuisho ya kura na kutangaza matokeo.
7. KWAMBA linawahakikishia wananchi wa Zanzibar kwamba Baraza Kuu liko imara na litatetea haki yao ya kidemokrasia na chaguo lao walilolifanya tarehe 25 Oktoba, 2015.

Limetolewa na:
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, tarehe 7 Novemba, 2015, mjini ZANZIBAR.

No comments: