Thursday, 11 February 2016

UJINGA WA UBAGUZI ZANZIBAR LAZIMA UPIGWE VITA

KATIKA makala yangu ya mwisho nilieleza umuhimu wa suala la Zanzibar kushughulikiwa kwa weledi na umahiri mkubwa, na nikasema kwamba hili linamhusu moja kwa moja Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli, na si mtu mwingine.Bila shaka atatakiwa aunganishe juhudi za wengine wengi wanaotaka kuona mgogoro uliotanda katika Visiwa hivyo ukimalizika, na baadhi yao tayari wamekwishakujitokeza. Hawa ni watu wenye nia njema kabisa na ambao wanapata hofu kama ninayopata mimi mwenyewe wakiona hali inazidi kuzorota na kuelekea kwenye hatari.
Lakini, pamoja na nia safi ya hawa wengine wote, hakuna mwenye dhamana ya kuushughulikia mgogoro huo kuliko Rais Magufuli, na hii ni kwa sababu hiyo ni kazi yake, ni jukumu lake, ni dhamana yake. Kikatiba yeye ndiye mkuu wa nchi hii, na ndiye sauti ya mwisho katika uongozi na utawala wa nchi hii. Pia yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa nchi yetu, na inapobidi kukabiliana na janga lolote linaloweza kuihilikisha nchi, yeye ndiye mhusika mkuu.

Na Jenerali Ulimwengu
Na Jenerali Ulimwengu

Najua wapo watu katika Visiwa vya Zanzibar ambao wangependa na wangefurahi kumuona Rais Magufuli akishindwa kupata suluhu ya tatizo la Zanzibar, kwa sababu wanasema, na wangependa iwe hivyo, kwamba “Zanzibar ni Nchi”, na kweli, iwapo Rais wa Jamhuri atashindwa kushughulikia suala hili, kwa nini wasiseme kwamba “Zanzibar ni Nchi”?
Iwapo tumefanya uchaguzi, na kwa upande mmoja wa Muungano uchaguzi huo ukaswihi, matokeo yakatangazwa, wabunge wakaapishwa na serikali ikaundwa, na shughuli za utendaji zikaanza mtindo mmoja, lakini kwa upande wa pili uchaguzi ukafutwa lakini tukaona kwamba tumekamilisha uchaguzi nchini, basi hao wanaosema kwamba “Zanzibar ni Nchi” hawajakosea.

Majuzi, ofisa mmoja alinukuliwa akisema kwamba suala la uchaguzi wa Zanzibar si suala la Rais wa Jamhuri bali ni suala la tume za uchaguzi. Hilo ni kweli. Hata hivyo, masuala ya amani, utangamano na utulivu wa nchi si suala la NEC wala ZEC; ni suala la Rais na wasaidizi wake wote. Yeye ndiye mkuu katika kushughulikia suala hili, na wengine wote wanaohusika nalo hawana budi kuwa chini ya uongozi wake na maelekezo yake. Hiyo ndiyo dhima ya mkuu wa nchi.
Iwapo hali itazidi kuzorota, na iwapo mwishowe kutatokea janga lolote katika Visiwa vya Zanzibar, siyo sisi wenyewe hapa nchini wala jumuiya ya kimataifa, watakaowaza kumuuliza mtu yeyote mwingine kuhusu hili isipokuwa Rais Magufuli.
Kama nilivyosema katika makala ya mwisho, hadi sasa Rais Magufuli hajaanza kufanya kazi ambazo tunaweza kuzihesabu kama kazi zake alizoziombea kura. Ambacho amekuwa akifanya hadi sasa, nilisema wiki mbili zilizopita, ni kusafisha uchafu alioachiwa na wale waliomtangulia ambao walikuwa wamekubali kusimamia serikali mfu, isiyokusanya kodi, isiyojali uaminifu na inayotenda mambo shaghalabaghala.
Ni serikali hiyo marehemu ambayo Magufuli amekuwa akijitahidi kuifufua, na ambayo itampa taabu kubwa kweli. Hii inatokana na kwamba watendaji ambao amewarithi hawakuzoea kutenda kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu, ila kwa utashi wa mkubwa huyu ama yule. Kuihuisha upya mifumo iliyokwisha kufa halitakuwa jambo rahisi, lakini hana budi kuifanya kazi hiyo. Asipoifanya, nani ataifanya?
Katika mambo aliyorithishwa na watangulizi wake ni suala la Zanzibar, nalo hana budi kulishughulikia. Tangu tulipoingia upya katika mfumo wa kisiasa wa ushindani wa vyama, suala la Zanzibar limekuwa mojawapo ya masuala ambayo hayakushughulikiwa ipasavyo. Limekuwa likishughulikiwa kwa mtindo wa zima-moto kila linapojitokeza katika hali moja au nyingine.
Kimsingi, Visiwani Zanzibar hali iliyopo ni hali ya ukinzani mkubwa kati ya watawala waliozoea kuwa madarakani tangu mwaka 1964 hadi leo, ambao wamekuwa wakitafuta kila aina ya visingizio ili waendelee kuwa madarakani. Baadhi ya visingizio wanavyovitumia ni vile tulivyovishuhudia majuzi, ambavyo ni vya kibaguzi moja kwa moja.
Kwamba watu wanaweza kubeba mabango yenye maneno ya kibaguzi na wakapita waziwazi mbele ya vyombo vya dola na wakuu wa nchi bila kukwazwa, si kwamba ni bahati mbaya bali ni kitu kimekuwapo kwa muda mrefu, na hivyo ndivyo wanavyofikiri watawala. Hakuna kazi ya kisiasa iliyofanywa na wale wanaojiita viongozi kuibadilisha hali hiyo na kusaidia kuwafanya Wazanzibari wajitambue kama wamoja.
Lakini ni ujinga kwa Wazanzibari kubaguana kwa misingi ya rangi. Nakumbuka simulizi moja niliyohadithiwa mwaka 1972, baada ya kuuawa muasisi wa Serikali ya Mapinduzi, Abeid Amani Karume. Mwalimu Nyerere aliwatia mbaroni, chini ya kizuizi watu kadhaa wa kutoka Zanzibar na akakataa kuwakabidhi kwa vyombo vya usalama vya Visiwani kwa kuhofia kwamba wangeuawa, kama akina Kassim Hanga walivyokuwa wameuliwa.
Miongoni mwa watu mashuhuri waliokuwa wamezuliwa wakati huo ni Abdulrahman Mohammed ‘Babu’ na Kanali Ali Mahfoudh, wote wakiwa ni ‘machotara’. Katika majadiliano na Mwalimu, mmoja wa wajumbe kutoka Visiwani akamwambia Mwalimu kwamba hana budi kuwaachia watuhumiwa wakahukumiwe Zanzibar.
Jibu la Mwalimu lilikuwa kwamba hawa walikuwa wanatuhumiwa kwa kumuua Rais wa Zanzibar, lakini papo hapo wanatuhumiwa kwa kumuua Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, kwa hiyo ni halali kwao kuhukumiwa Bara. Wakasema, “Lakini Mwalimu wewe huwajui watu hawa. Hawa ni watoto wa Waarabu; ni nyoka.” Jibu la Mwalimu likawa, “Nyoka? Nyoka mnalala nao kitandani?” Kimya!
Kwa nini walikaa kimya baada ya swali hilo? Ni kwa sababu wakuu wengi katika utawala wa Zanzibar walikuwa wameoa wanawake waliokuwa wamechanganya damu, na baadhi yao wakiwa moja kwa moja ni Waarabu, Washirazi au Wahindi. Ndiyo maana ni dalili ya unafiki mkubwa kwa watu kama hao kujifanya wao ni Wazanzibari kuliko hao wanaoitwa “machotara”.
Visiwa vya Zanzibar vimejaliwa kuwa na mchanganyiko wa kila aina ya makabila ya dunia, kutoka Afrika, Asia na Ulaya. Ni visiwa vilivyounganisha tamaduni za kila aina na kutengeneza utamaduni unaoweza kuitwa wa ki-Zanzibari. Huo ni utajiri mkubwa ambao, kwa watu wenye busara, unatakiwa uenziwe, utukuzwe, uendelezwe na utumike kujenga jamii yenye nguvu na yenye dinamiki ya maendeleo.
Lakini ukiachiwa mikononi mwa majuha wasioona mbali zaidi ya urefu wa pua zao, utajiri huo huo unaweza kugeuka laana ya watu kubaguana na kutengana kwa misingi ya rangi zao.
Hivyo ndivyo ninavyoiona Zanzibar na ndivyo ninavyoyaona mabango ya kijinga ambayo wakuu wanaona haya kuyakemea. Wapo watu ambao nimewasikia kwa masikio yangu mwenyewe ambao wanaapizana kwamba haitatokea mtoto wa Mwarabu akawa mkuu wa Zanzibar.
Hii inasemwa leo wakati tukijua kwamba mtoto wa Jaluo kutoka Kenya ndiye anatawala taifa lenye nguvu za kiuchumi na kijeshi kuliko mataifa yote duniani. Mtu akituita majuha, atakuwa ametutukana ama ametueleza jinsi tulivyo?
Mimi sijui ni jinsi gani Rais Magufuli atasaidia kuondoa tatizo hili. Ninachojua ni kwamba anao wananchi wengi wanaomtakia mema, na ambao kama akitaka kuwatumia wanaweza kumsaidia kwa kutoa mawazo yao. Lakini hana budi kuwataka na kuwaleta pamoja na kuwasikiliza. Kazi ninayoiona ni ya masafa marefu, na inahitaji subira, tafakuri na majadiliano ya kina.
Chanzo: Gazeti la Raia Mwema la tarehe 10 Februari 2016


No comments: