Friday, 4 December 2015

Bado Sijamuelewa Mchapakazi Huyu wa hapa kazi tu

 

Maendeleo makubwa, ya maana na endelevu ya nchi, hayawezi kupatikana kwa ufanisi kwa mkakati wa viongozi wa juu kuwavizia-vizia na kuwashitukiza watendaji wa chini, bali yatapatikana kwa mapana zaidi kwa kusimika mifumo endelevu na thabiti kwenye sekta ya utumishi wa umma, yenye uwezo wa kubaini na kudhibiti ufisadi wakati wote na kuwajibisha wasiowajibika wakati wowote.
Ni kweli mkakati wa kuvizia-vizia na kushitukiza umeleta matokeo fulani ya kuvutia na ni kweli matokeo hayo yameshaonekana maeneo mbalimbali kama bandarini. Lakini hii ni nchi, ni kubwa mno na ina mambo mengi mno kwa viongozi wa ngazi ya Rais na Uwaziri kuweza kuyashughulikia yote kwa wakati, kwa njia ya kuvizia-vizia na kushtukiza. Tunahitaji kuweka mifumo inayorahisisha kazi hiyo, vinginevyo itatuchukua muda mrefu mno tena bila uhakika wa kutosha kwa viongozi wetu kuweza kufanya mishtukizo ya kutosha kwenye sekta na ofisi zote za umma, ndipo tupate maendeleo!
Mathalan, kwa mkakati huu wa "Kuvizia-vizia na Kushtukiza", ilimbidi Waziri Mkuu aende bandarini mara mbili ndipo agundue kuwa makontena ambayo hayajalipiwa kodi si yale 349 aliyoyajua mwanzo, bali ni zaidi ya makontena 2,000. Na kama hakuna mfumo thabiti uliowekwa, basi itampasa Waziri Mkuu au Waziri atakayeteuliwa aende tena bandarini kwa mara ya tatu kwa kuvizia-vizia na kushtukiza bandarini, ndipo atakapoweza kugundua kuwa kumbe makontena yasiyolipiwa kodi ni 10,000 na siyo yale 2,000 niliyogundua siku ile!
Kwa mkakati huu wa "Kuvizia-vizia na Kushtukiza" ilimbidi Rais Magufuli na baadaye Katibu Mkuu Kiongozi, Sefue, waende Muhimbili zaidi ya mara moja ndipo wahakikishe mashine ni nzima, mashuka na vitanda vimenunuliwa na huduma zinatolewa vizuri! Na kwa utaratibu huo wa "kuvizia na kushitukiza", itampasa Rais na Sefue wavizie na kuzishtukiza hospitali zote za umma nchini, tena kwa mishitukizo ya kutosha ndipo angalau, vitanda na mashuka viwepo vya kutosha!
Kwa mantiki ya mkakati huu, bado kunahitajika mishitukizo ya kutosha kwenye migodi yote ya madini, uwanja wa ndege, kwenye mbuga zote za wanyama, kwenye mashirika na mamlaka zote za umma, kwenye kila shule ya sekondari na ya msingi, kwenye kila chuo kikuu nchini, kwenye ofisi zote za halmashauri nchini na kila pahali.Tuendelee kuwasifia na kuwatia moyo viongozi wetu kwa dhamira njema wanayotuonyesha ya kusukuma maendeleo, lakini tusije tukawasifia kupitiliza hadi wakawa 'kituko".
Wakiweza kufanya mishitukizo kote huko, wachapakazi wetu watatufurahisha sana kila siku, vyombo vyetu vya habari kila siku vitapata habari moto-moto za mishitukizo, lakini ni ukweli ulio dhahiri kuwa bila kufanyika tathimini ya kina ya utendaji wa sekta zote na hatimaye kuweka au kuimarisha mifumo ya utendaji, uwajibikaji na ya kudhibiti mianya ya ufisadi, basi itatuchukua karne nyingi zaidi tukiwa bado tunayaota "maendeleo". Tunahitaji viongozi wetu si tu wafanye mambo ya kutuvutia (matukio), bali wafanye zaidi yale yenye kuweka misingi endelevu.
Tuendelee kuwasifia na kuwatia moyo viongozi wetu kwa dhamira njema wanayotuonyesha ya kusukuma maendeleo, lakini tusije tukawasifia kupitiliza hadi wakawa 'kituko'. Tuwashauri, wajikite zaidi kwenye kuasisi au kuimarisha mifumo. Mishitukizo isiwe ndio mkakati mkuu wa maendeleo ya nchi hii, bali iwe ni mojawapo ya njia tu za kubaini baadhi ya mapungufu ya kimfumo na hatimaye kuweza kuimarisha mfumo wenyewe.

Wakati wa kampeni karibu kila aliyejisikia kutoa mawazo mazuri alisema "tatizo la nchi hii ni mfumo", au tunataka mabadiliko ya mfumo", "issue hapa ni mfumo tuu". Wiki chache tangu Bwana Mkubwa aingie madarakani, sasa imekuwa vigumu kujua kama kweli sote tulikuwa tunazungumza lugha moja kuhusu dhana ya "mfumo" na kama kweli tulikuwa tuna maana sahihi inayobebwa na neno 'mfumo'. Nina mashaka baada ya kuona hali ya kuridhishwa kwa haraka kwa matukio ya kuvizia-vizia na kushtukiza badala ya kusubiria mabadiliko ya kimfumo tuliyokuwa tukiyasema wakati ule tulipokuwa tunatumia akili nyingi kuchambua udhaifu wa serikali yetu.
Mabadiliko ya kimfumo bado na msingi mkuu wa kutandika bomba la mabadiliko ya kimfumo ni kurudi kwenye mchakato wa kupata Katiba ya Wananchi, kwa kuanzia pale alipoishia Warioba na wenzake. Mchakato huo ukiongezewa na michakato mingine ya kuzifuta au kuzirekebisha sheria nyingi kandamizi na zile zenye kuruhusu mianya ya ufisadi, kupitia na kuimarisha sheria, kanuni na mifumo ya kisasa ya kuchochea uwazi na uwajibikaji wa umma
ikiwemo mifumo ya Tehama, basi nchi hii inaweza kushuhudia mabadiliko mapana, endelevu na ya kasi zaidi ya kimaendeleo, kuliko haya ya kusubiria viongozi wakuu wafanye mishitukizo huku na kule, hapa na pale. Bado sijamuelewa Mchapakazi Huyu!

No comments: