Monday, 15 February 2016

KUMTEUA DK MIGIRO BALOZI, MAGUFULI HUTUTANII KWELI?

NA Maloto LUQMAN

NASUBIRI kauli kwamba uteuzi wa Dk. Asha-Rose Migiro kuwa balozi ilikuwa utani. Naingoja kwa hamu kubwa.

Dk. Migiro awe balozi? Huyuhuyu mama yetu? Ni taarifa za kweli hizi? Mama na wewe umekubali?

Dk. John Pombe Magufuli, wewe ndiye rais wetu. Una mamlaka makubwa hasa, unamteua umtakaye, na kumpumzisha kama siyo kumpiga chini unayemkusudia.

Ni mamlaka yako. Sisi wenyewe Watanzania tumekupa wenyewe rungu, fagio, nyundo, bunduki, bomu, yaani kwa kifupi silaha zote. Unapiga kazi, sawia kabisa na hatuisomi namba! Hapa Kazi Tu!

 Ila kwa hili Dk. Pombe ngoja niongee na wewe! Hujatutania kweli kumteua Migiro kuwa balozi? Nijibu basi mkuu!

Mama ulishirikishwa kwenye uteuzi na ukaridhia kabisa? Yaani umekubali kabisa kucheza mchezo wa kurudi nyuma? Sikuelewi mama, umepatwa na nini?

Mama yangu wewe ulikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, dunia nzima ilikuwa inakuangalia wewe.

Tena mama uliweka rekodi ya kipekee, ukawa mwanamke uliyekamata cheo kikubwa kuliko wengine wote kuwahi kutokea duniani.

Mama wewe ni zaidi ya Sadako Ogata, yule mwanamama mwanadiplomasia mbobezi, aliyepata kuwa Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR). Mwenzako baada kupiga kazi kwa miaka 10, yupo Chuo Kikuu cha Sophia, Japan, anaendeleza taaluma.

Ni sawa kabisa, unapoacha kazi kubwa ni heshima mno kurudi chuo kufundisha ili ukuze watu wa taifa lako. Ufanye tafiti na kuandika vitabu au makala kwenye magazeti na mitandao. Huo ndiyo ustaafu mzuri.

Mama yangu, kweli unataka kumuiga John Quincy Adam, yule Rais wa Sita wa Marekani. Kwa kupenda kwake madaraka bila kujali hadhi, alipomaliza utumishi wake wa urais kwa kipindi cha miaka minne, alikwenda kugombea ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia Jimbo la Massachusetts na akashinda.

Yaani ndiyo kusema, Dk. Jakaya Kikwete, Benjamin Mkapa na Mzee Ruksa, Ali Hassan Mwinyi, nao wawe wabunge. Teh teh teh! Msinivunje mbavu jamani, zinaniuma!

Mama yangu umekuwaje? Hivi unafahamu kuwa wewe una hadhi kubwa kuliko Hillary Clinton?

Unakumbuka alipokuwa anakuja ofisini kwako pale New York, Marekani? Umesahau mara hii? Basi utakuwa unasahau haraka!

Mama wewe ni mkubwa mno. Ni mwanasheria wa kiwango cha juu, shahada yako ya uzamivu (PhD), uliichukulia Ujerumani.

Mama ulikuwa mkuu wa kitengo cha sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ni kwa nini baada ya kumalizana na ajira ya Umoja wa Mataifa hukurudi chuo? Hutaki usumbufu wa wanafunzi eeh! Sawa mama, asante sana!

Miaka yako ya mitano ya utumishi kama Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mbona unaweza kuiweka kwenye maandishi na kuisaidia jamii kwa upana kabisa? Hutaki tuelimike kwa uzoefu wako?

Mama ngoja nikukumbushe, unakumbuka ulipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa? Umesahau kuwa mabalozi wote walikuwa chini yako? Yaani wewe ndiye ulikuwa bosi wao, na waliripoti kwako.

Baadaye ukateuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, yaani ukapiga hatua kubwa mno. Mawaziri wote wa mashauri ya kigeni walikunyenyekea. Marais wa nchi mbalimbali, ukiachana na mabeberu, walikupapatikia.

Leo nikwambie tu ukweli, nilikushangaa mno pale ulipotoka Umoja wa Mataifa, uliporejea nchini ukateuliwa kuwa mbunge, ukakubali, ukapewa uwaziri wa Sheria na Katiba ukasema “asante”. Kweli mama huo ndiyo mwendo wa heshima?

Mama unamuona Dk. Salim Ahmed Salim? Alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), siku hizi unaitwa Umoja wa Afrika (AU). Eti tunakwenda kama wao, Umoja wa Ulaya (EU), tupo vizuri!

Salim ni Afrika tu, wewe dunia nzima. Sasa mpaka hapo hujioni kama hadhi yako ni kubwa kubwa kuliko hata mbobezi wetu huyo?

Sasa jiulize, mbona Salim hawamteui kuwa balozi au vyeo vinginevingine? Thubutu, wataanzaje? Salim ni nguli, anajisimamia, anatambua ukubwa wake. Hawezi kukubali kurudishwa nyuma.

Ila mama yangu wewe unaona sawa kabisa. Ngoja nikwambie kitu mama yangu, usipoweka misimamo kuna siku utateuliwa kuwa mkuu wa mkoa. Na ukizubaa utakuwa mkuu wa wilaya. Hawashindwi mama! Watakuteua tu!

Halafu mama, hao wanaokuteua mbona wewe unawashinda kwa CV kimataifa? Yaani daktari mzima wa falsafa unashindwa kuling’amua hili?

Mama ngoja nikuulize, hivi Dk. Magufuli siku akiondoka Ikulu kisha rais ajaye akamteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu atafurahi? Au hata balozi, je, atachekelea?

Wakati mwingine mama yangu nahisi kama tunakuonea wivu vile kwa CV yako ya UN! Kwa hiyo tunaamua kuichafua kwa kukupa vyeo vidogovidogo ili ionekane pale UN ulifika kwa bahati mbaya, yaani hadhi yako ilikuwa chinichini. Tafadhali mama, onesha ‘usirias’ kidogo basi!

 Ngoja nikwambie, kipindi kile ulipoteuliwa kufanya kazi za chama chako, Chama Cha Mapinduzi (CCM), sikuona ubaya wowote, japo ni ukweli pia uliporomoshwa. CCM walitakiwa kukutumia zaidi kama mshauri, siyo kukupa majukumu yale.

Kutoka UN, mtu nambari mbili kwa cheo mpaka kuwa mjumbe wa sekretarieti ya CCM. Eti Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa. Watu wakiamua kukutania utawaona tu kwa vitendo vyao!

Mama yangu unaanguka! Mbona unachelewa kushtuka? Unataka nani akutunzie heshima yako kama unakubali ichezewe?

Hivi unajua hata Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon anakushangaa? Unamuabisha kabisa. Yaani yeye alikuteua cheo kikubwa mno, wengine wanaamua kukuteua ubalozi. Hebu nuna basi kidogo uoneshe msimamo.

Ndiyo kusema watu wanataka kumfanya Ki-moon ajione alikosea sana kukuteua kwenye ‘licheo’ likubwa la kidunia. Hapana mama, hakukosea, unastahili. Ila wewe mwenyewe unakubali kujiangusha.

Mama yangu wewe uliipa heshima kubwa nchi hii. Mpaka leo hakuna mwanamke duniani amewahi kupata hadhi kubwa kama yako ukiwa Naibu Katibu Mkuu wa UN.

Dk. Pombe, hivi kweli umeridhika mama awe anatoka juu kurudi chini? Tusifanyiane hivyo jamani. Mbona huyu mama alitupa heshima kubwa? Sasa kwa nini unaichakaza? Mnaniumiza moyo mwenzenu!

Mbona ungeweza hata kumfanya mshauri wako wa masuala ya kisheria na kidiplomasia? Uwe naye Magogoni Ikulu, angalau hapo ingeleta maana kidogo.

Kwa mfano, Naibu Katibu Mkuu wa UN kwenda kuwa Balozi wa Tanzania nchini Burundi. Nimesema kwa mfano, teh teh teh! Mbavu zangu zikivunjika nitawashtaki mjue, oohooo!

Haya mambo huwa yanaonekana Tanzania tu. Mtu alikuwa Mnadhimu wa Jeshi la Wananchi, alipostaafu akafanywa balozi wa Tanzana nchini China.

Lazima tuwe na utamaduni wa kuheshimu nafasi za watu. Itakwaje siku mtu anastaafu Ujaji Mkuu kisha kupelekwa kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri? Na ataitwa Mkurugenzi wa Jiji kisha atachekelea, bila kujua wenzake wanamng’ong’a.

Kwa mwendo huu wa Migiro, nahisi itakuja kufika huko. Jamani tafadhalini sana. Huu uteuzi wa Migiro kuwa balozi hapana kabisa. Haujazingatia hadhi yake. Ni kumchoresha tu mama yangu mpenzi kwenye anga za kimataifa.

.

No comments: